Monday, November 21, 2011

HOTUBA YA KIKWETE Juzi



Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,

Mstahiki Meya,

Viongozi wa Serikali,

Wazee wangu,

Ndugu Wananchi,

 Nakushukuru Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuniandalia fursa hii ya kukutana na Wazee wa Dar es Salaam.  Nawashukuru sana wazee wangu kwa kuitikia wito wangu huu wa kukutana nanyi.  Nimefarijika sana kwa mahudhurio yenu makubwa pamoja na taarifa kuwa ya muda mfupi.

Nimewaiteni wazee wangu nizungumze nanyi na kupitia kwenu nizungumze na wananchi wote wa Tanzania.  Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kufanya hivyo kupitia utaratibu wetu wa kawaida kwa sababu nilikuwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola nchini Australia.  Mwisho wa Mwezi  huu nitakuwa Bujumbura kuhudhuria  Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hivyo sitaweza kuongea na wananchi wakati huo. Lakini, yapo masuala kadhaa ambayo ni muhimu watu kupata ufafanuzi kutoka kwangu.  Kwa ajili hiyo nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi siku ya leo.   Leo nataka kuzungumzia hali ya uchumi na mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Hali ya Uchumi

Ndugu Wananchi;

          Katika kuelezea hali uchumi nchini, naomba nianze kwa kuelezea hali ya uchumi duniani kwani yanayotokea nchini yana uhusiano mkubwa na yanayotokea duniani.  Hali ya uchumi duniani siyo shwari.  Ukweli ni kwamba hali katika uchumi wa mataifa ya Marekani, Ulaya Magharibi na Japan haijatengemaa kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa miaka miwili iliyopita.  Hivi sasa uchumi wa mataifa tajiri ya Ulaya , wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa wanachama wa Umoja wa Sarafu ya Euro unapita katika kipindi kigumu na mashaka.  Thamani ya sarafu hiyo inashuka na hata kuaminika kwake ni kwa mashaka. Mfumuko wa bei umepanda, ukosefu wa ajira umeongezeka na ipo hofu kubwa ya uchumi wa nchi hizo kudorora tena.  Lakini nchi hizi ndiyo masoko makubwa ya bidhaa zetu, watalii na bidhaa za viwandani.  Hivyo, athari zao zinatugusa na sisi.  Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kunaongeza bei ya bidhaa tunazonunua kutoka kwao.  Aidha, kutetereka kwa uchumi wao nako kumepunguza masoko ya bidhaa zetu.

Lakini kulegalega kwa sarafu ya Euro kumesaidia kuimarika kwa sarafu ya dola ambayo kabla ya hapo ilikuwa imepungua nguvu.  Kwa sababu hiyo thamani ya sarafu ya dola imepanda duniani ikilinganishwa karibu na sarafu nyingine zote pamoja na yetu.  Wakati huo huo bei ya mafuta imeendelea kupanda duniani kutoka dola 76.1 kwa pipa Septemba,, 2010 hadi dola 100.5 Septemba, 2011.  Jumla ya yote haya ni kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 4.2 Oktoba, 2010 hadi asilimia 17.9 Oktoba, 2011.

Ndugu Wananchi;

Serikali na vyombo husika vimekuwa vinachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matatizo ya kushuka kwa thamani ya shilingi, bei ya mafuta, bei ya sukari na matatizo ya umeme.  Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua zilizopo ndani ya mamlaka yake hususan kubana ulanguzi wa fedha za kigeni, kudhibiti matumizi ya fedha kigeni kufanyia malipo hapa nchini na kuongeza fedha za kigeni katika masoko ya fedha.  Kwa kweli uwezo wao una ukomo.  Jawabu la uhakika lipo kwenye uchumi wa mataifa makubwa kuchukua hatua thabiti kuimarisha uchumi wao ili thamani ya dola irejee mahali pake stahiki na bidhaa zetu zipate masoko ya uhakika na bei nzuri ili mapato yetu ya fedha za kigeni yaongezeke.

Kwa upande wa mfumuko wa bei, ni vyema tukatambua kuwa Asilimia 75 ya ongezeko hili imetokana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.   Asilimia 25 iliyobaki imechangiwa na sera za fedha.  Kwa upande wa mafuta, tunaamini utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja utasaidia kudhibiti bei za ndani za bidhaa hiyo.  Aidha, itsaidia kupunguza makali ya athari ya bei za dunia zinazopanda.  Kwa upande wa bei za vyakula, tatizo kubwa ni uhaba wa chakula katika nchi jirani unaosababisha wote kututegema sisi na hivyo kupandisha bei nchini.  Tunaendelea kudhibiti magendo ya chakula na wakati huo kutengeneza taratibu rasmi za kuziuzia chakula nchi jirani.

Kwa upande wa sukari tumeamua kuruhusu tani 120,000 ziagizwe ili kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo na kushusha bei yake.

Hatuko Peke Yetu

Ndugu Wananchi;

          Ni vizuri tukafahamu kuwa, matatizo ya mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha yetu siyo yetu peke yetu.  Nchi zote za Afrika Mashariki zinakabiliana na matatizo haya.  Kwa mfano, mfumuko  wa bei  kwetu ni asilimia 17.9, Kenya wako asilimia 18.9 na Uganda asilimia 30.5.  Wakati mwaka wa jana sote tulikuwa kwa watani karibu asilimia 5.  Kwa upande wa kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola sote tumeathirika.  Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 9.4, Kenya kwa asilimia 6.8 na Uganda kwaasilimia 17.4.  Randi ya Afrika Kusini kwa asilimia 18.7, Rupia ya India kwa asilimia 9.8, Pauni ya Uingereza kwa asilimia 6.6. na Euro kwa asilimia 9.7. 

Ndugu Wananchi;

          Katika kukabiliana na tatizo la umeme, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa dharura wa kuongeza uzalishaji wa umeme.  Serikali imewawezesha TANESCO kukodi mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwenye makampuni ya Symbion (112 MW) na Aggreko (100 MW) na kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL (100 MW).

Napenda niwahakikishie wananchi kuwa, ifikapo Desemba, 2011 hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa nzuri na mgao utapungua sana baada ya kufunga mitambo mingine mipya ya kuzalisha umeme ya TANESCO (160 MW) na Symbion (60 MW).  Mikakati tuliyonayo ya muda mrefu ni kuongeza mitambo zaidi na kuongeza upatikanaji wa gesi ya kuendeshea mitambo kwa kujenga bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Mchakato wa Katiba

Ndugu Wananchi;

Kama mtakavyokumbuka tarehe 31 Desemba 2010 katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 nilizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011.  Miongoni mwa mambo ambayo niliyataja kuwa tutayafanya katika kusherehekea siku hiyo adhimu ilikuwa ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa nia ya kuihuisha ili hatimaye tuwe na Katiba mpya.

Nilifafanua siku ile kwamba tunataka kufanya hivyo si kwa sababu Katiba yetu ya sasa ni mbaya, la hasha!  Nilieleza kwamba Katiba yetu ya sasa ni nzuri na imelilea vyema taifa letu.  Tuna nchi yenye amani, utulivu na umoja pamoja na watu wake kuwa wa rangi, makabila, dini na itikadi mbalimbali za kisiasa.  Tunayo nchi ambayo imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 50 iliyopita.  Pamoja na hayo tunataka kuihuisha Katiba yetu ili tuwe na Katiba inayoendana na Tanzania ya miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara, Tanzania ya miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Tanzania ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa ajili hiyo nilielezea dhamira  yangu ya kuunda Tume Maalum ya Katiba yaani Constitutional Review Commissionitakayojumuisha Watanzania wa makundi mbalimbali katika jamii yetu na kutoka pande zetu mbili za Muungano.  Aidha, nilifafanua kuwa jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato wa kupata maoni ya Watanzania kuhusu nini wanachokitaka kiwemo katika Katiba yao.

Tume itasikiliza maoni hayo na baadaye kutengeneza rasimu ya Katiba mpya ambayo baada ya kukubaliwa na Bunge itafikishwa kwa wananchi kutoa ridhaa yao kwa kupiga kura.  Nilisisitiza kuwa mchakato huo utawahusisha Watanzania wote wa ngazi zote na popote walipo mijini na vijijini.  Hapatakuwa na aina yoyote ya  kuwabagua watu kwa itikadi zao za siasa, shughuli wazifanyazo, dini zao, rangi zao au jinsia zao.

Ndugu Wananchi;

Nilifarijika sana na kauli za pongezi kwangu na kwa Serikali kwa uamuzi wa kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya.  Miongoni mwa waliotoa pongezi alikuwa Ndugu Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa CHADEMA  ambaye wakati akichangia hotuba yangu ya kufungua Bunge Jipya, tarehe 11 Februari, 2011; nanukuu Hansad ya Bunge aliposema “Mheshimiwa Spika, ninapenda kwenye hili, nimpongeze Rais kwa kuwa msikivu, na Rais anapofanya jema tutampongeza, Serikali yake inapofanya jema tutaipongeza na Chama chochote kitakapofanya jambo jema kwa Taifa letu, tutakipongeza.  Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu moja ya msingi sana, kuridhia mabadiliko au kuitafuta upya Katiba ya nchi yetu.”  mwisho wa kunukuu.    Lakini siku chache baadaye Chama chake kikaja na msimamo tofauti, wakawa wanalalamikia kunyang’anywa hoja yao na kukataa Rais asiunde Tume ya Katiba na wala asihusike kabisa na mchakato huu.  Tangu wakati huo wameendesha kampeni kubwa ya kutaka Rais asihusishwe kwenye mchakato wa kubadili Katiba

Kwa kweli watu wengi wanaoitakia mema nchi yetu walishangazwa na madai hayo na vitendo vya ndugu zetu hao.  Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba au hata kuandika upya Katiba tangu Uhuru na Muungano.  Mara zote hizo iliundwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ambayo iliundwa na Rais.  Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere,  Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa tatu Mzee Benjamin Mkapa.  Mwalimu Julius Nyerere alifanya hivyo mara tatu.  Mara ya kwanza mwaka 1963 wakati wa kubadilisha mfumo wa vyama vingi kwenda Chama kimoja, Rais aliunda Tume ya Mheshimiwa Rashid Kawawa, Amon Nsekela.  Mara ya pili wakati wa kutengeneza  Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 aliunda Tume ya Mzee Sheikh Thabit Kombo.

Mwaka 1984 Mabadiliko ya Katiba ya 1977 yaliyoweka ukomo wa Urais na kuingiza katika Katiba Haki za Binadamu, yaliyotokana na mchakato uliokuwa ni wa Kichama, ambapo CCM ilikusanya maoni kupitia mtandao wa kichama kuanzia Matawi hadi kufikia Makao Makuu.  Wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, kulikuwa na Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali iliyotuletea mabadiliko  ya nane ya Katiba yaliyoruhusu vyama vingi vya siasa.  Wakati wa Rais wa Awamu ya Tatu, mzee Benjamin Mkapa kuliundwa Tume ya Jaji Kisanga iliyoleta mabadiliko ya 13 na 14 ya Katiba ya nchi.

Hivyo la ajabu lipi kwa Rais wa sasa kuunda Tume ya Katiba?  Amepungukiwa nini Kikatiba na Kisheria ambacho Marais wenzake walikuwa nacho katika madaraka yao?  Hakipo hata kimoja!  Madaraka waliyokuwa nayo Marais waliomtangulia ndiyo aliyonayo Rais wa sasa.  Hajapungukiwa chochote kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.  Kwa kweli hakuna hoja yoyote ya msingi ya kumuengua Rais katika mchakato wa kutengeneza Katiba ya nchi.  Haipo hoja ya Kikatiba wala ya Kisheria.  Hivi Rais asipounda Tume, nani aiunde Tume hiyo?  Na huyo atakayeunda atapatikanaje?

Juzi Bungeni msemaji wa kambi ya upinzani, katika mjadala wa Muswada wa Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni alisema Rais ni dikteta.  Ama kweli “akutukanae hakuchagulii tusi” kama ulivyo msemo wa Kiswahili.  Hivi mimi kweli ni dikteta?  Kwa jambo lipi?  Hivi ndugu zangu Rais dikteta anatoa uhuru mkubwa kama uliopo sasa wa vyombo vya habari na wa watu kutoa maoni yao?  Kama mimi ningekuwa dikteta kweli nina hakika hata yeye asingethubutu kusema hivyo na kama angethubutu basi mpaka sasa asingekuwa anatembea kwa uhuru.  Mimi ninachofahamu ni kuwa nasemwa kwa kuwapa watu, vyama vya siasa na vyombo vya habari uhuru mkubwa mno ambao watu wanaona unatumika vibaya kusema maneno yasiyokuwa na staha au hata matusi, fitina na kupandikiza chuki katika jamii.  Labda, nijaribu kuwa dikteta kidogo watu waone tofauti yake.  Naamini kungekuwa na malalamiko makubwa zaidi ya haya.

Ndugu Wananchi;

Mimi na wenzangu Serikalini tumefanya yote ambayo Katiba ya nchi na Sheria vinaruhusu.  Ndivyo Marais walionitangulia na Serikali zao walivyofanya tena sisi tumefanya zaidi ya wao.  Wote waliunda Tume za kukusanya maoni ya Katiba na wakati wa Mwalimu Julius Nyerere liliundwa Bunge Maalum la Katiba lililojumuisha Wabunge na wananchi wengine kama tulivyoamua kufanya sisi.  Ilifanyika hivyo wakati wa kutengeneza Katiba ya Tanganyika kuwa Jamhuri na Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.  Sisi tulichofanya cha ziada ni kulihusisha Bunge kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya kusimamia mchakato wa Katiba mpya na vile vile kuwapa wananchi wote ridhaa ya kuamua kwa kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.  Ni kutokana na nyongeza hii ndipo tukaona busara ya kuwepo kwa Sheria maalum ya kuongoza mchakato wa kupata Katiba mpya.  Tumepanua demokrasia na kuwahusisha wananchi wenyewe siyo tu katika kutoa maoni bali pia kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba ya nchi yao, badala ya kuwaachia Wabunge na viongozi wengine Serikalini peke yao.  Kwa kweli tunastahili pongezi badala ya shutuma na lawama zisizokuwa na msingi.

Pia inasikitisha kuona au kuwasikia watu wanaojua wakijifanya ukweli huu hawaoni au  hawajui.  Baya zaidi ni pale wanapojihusisha na kupotosha ukweli na kuipaka sura isiyokuwa ya kweli kuhusu kinachofanywa na Serikali.  Mimi hujiuliza kwa nini wanafanya hivi.  Kwa nini wanafanya hiyana ya upotoshaji wote huu?  Kwa kweli sipati majibu ya uhakika.  Labda ndiyo ile dhamira ya kutaka nchi isitawalike.  Au ndiyo pengine ni ile nia ya kutaka kwenda Ikulu kwa njia ya mkato.  Ati kwa kutumia nguvu ya umma.  Basi hata hiyo nguvu unaitumia bila ya kuwa na hoja za kweli?

Ndugu Wananchi;

Nayasema haya kwa sababu kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa jambo hili tangu baada ya hotuba yangu ya tarehe 31 Desemba, 2010 mpaka wakati wa kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria wa Kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba uliomalizika leo Bungeni.  Upotoshaji wa kwanza ulikuwa ni ule wa kujenga dhana kana kwamba Serikali imewasilisha Muswada wenyewe wa Katiba mpya.  Wapo watu wamefanywa waamini hivyo wakati si kweli hata kidogo.  Huu ni Muswada ambao ukipitishwa, itaundwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu nini wanachokitaka kijumuishwe katika Katiba yao mpya.  Kwa maneno mengine, maoni yenu mtakayoyatoa wananchi kwa Tume ndiyo yatakayotumika kutengeneza Katiba mpya.

Ndugu Wananchi;

Katika Muswada huu kuna mambo tuliyotaja kuwa ni ya msingi ambayo yamewekewa wigo wa kuhakikisha yanalindwa.  Mambo hayo ni yale ambayo yanalitambulisha taifa letu na tunu zake kuu.  Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:  Kuwepo kwa nchi yetu na mipaka yake; kuwepo kwa Serikali, Bunge na Mahakama; kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; umoja wetu, mshikamano wetu na usalama wetu; Mfumo wa uchaguzi kwa kura unaotoa fursa kwa wote; Hifadhi ya haki za Binadamu; Haki za watu; Usawa mbele ya sheria na haki; Uhuru wa kuabudu na kuvumiliana kwa imani zetu.

Kumekuwepo na upotoshaji ati huko ni kuwaziba watu midomo.  Siyo hivyo hata kidogo.  Mambo hayo yanajadiliwa, lakini siyo kwa nia ya kuyaondoa bali kuboresha.  Kwa mfano, kuhusu Muungano,  tunachosema ni kwamba hatujadili kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali namna bora ya kuendesha shughuli za Muungano wetu.  Lakini, tulichokifanya siyo kitu kigeni, hata Rais wa kwanza alifanya hivyo mwaka 1963 alipounda Tume ya Mfumo wa Chama Kimoja cha Siasa iliyoongozwa na Mheshimiwa Rashid Kawawa.  Alitoa mwongozo na aliyataja mambo ya kulinda.  Sisi tulichokifanya ni kuyataja kwenye sheria badala ya kuwa Mwongozo wa Rais.

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;

Kwani Katiba ya Nchi ni kitu gani.  Katiba hutaja nchi na mipaka yake.  Kwetu sisi nchi yenyewe ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na kuungana kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.  Pili, Katiba inaelezea jinsi nchi hiyo itakavyoendeshwa kwa maana ya mihimili mikuu mitatu ya dola ya Utawala/Serikali, Bunge na Mahakama.  Katiba inafafanua jinsi Serikali inavyopatikana, muundo wake na inavyofanya kazi.

Aidha, inaeleza jinsi Bunge linavyopatikana, jinsi linavyofanya kazi ya kutunga sheria na mahusiano yake na mihimili mingine.  Vile vile, Katiba inaeleza jinsi Mahakama inavyofanya kazi ya kutoa haki, muundo wake na jinsi Majaji na Mahakimu wanavyofanya kazi.  Kwa kweli mchakato wote huu unahusu hayo.  Tunatakiwa kutoa maoni juu ya namna gani bora zaidi na ikiwezekana namna mpya ya kuendesha shughuli za Muungano wetu na jinsi mihimili yetu inavyopatikana na kufanya shughuli zake.

Ndugu Wananchi;

Jambo lingine lililopotoshwa ni dhana ya muswada kusomwa mara ya kwanza.  Kwa mujibu wa utaratibu wa kutunga sheria, Miswada, husomwa mara tatu Bungeni.  Muswada kusomwa mara ya kwanza ni pale unapogawiwa kwa Wabunge baada ya kuchapishwa katika gazeti la Serikali siku 21 kabla ya kuwasilishwa Bungeni.  Baada ya kuchapishwa, hugawiwa kwa Wabunge.  Muswada husomwa mara ya kwanza Bungeni ili kutoa fursa kwa Mheshimiwa Spika kuwasilisha Muswada huo kwenye Kamati iuchunguze na kuutolea maoni.  Mheshimiwa Spika anaweza pia kuielekeza Kamati kutafuta maoni ya wananchi.

Baada ya Kamati kukamilisha kazi yake, Muswada husomwa mara ya pilli ambapo Muwasilishaji atatoa hoja kwamba Bunge liujadili Muswada pamoja na kutoa maelezo ya Muswada.  Mjadala huanza kwa Kamati ya   Bunge kutoa maoni yake ikifuatiwa na maoni ya Kambi ya Upinzani.  Wakati Kamati ya Bunge inapojadili Muswada, Waziri mhusika huwepo na mara nyingi maoni ya Kamati ya Wabunge na wadau hujumuishwa wakati Waziri anapowasilisha hoja Bungeni ya Muswada unaposomwa mara ya pili.  Baada ya mjadala, Bunge hukaa kama Kamati ya Bunge zima ambapo hupitia Muswada kifungu kwa kifungu.

Katika hatua hii Wabunge huweza kupendekeza mabadiliko mahsusi kwenye kila kifungu.  Aidha, Waziri nae anaweza kutetea marekebisho ya Muswada.  Baadaye Bunge hurejea, taarifa ya Kamati ya Bunge zima hutolewa kwamba Muswada umepitiwa kifungu kwa kifungu na kukubaliwa.  Kisha Muswada husomwa mara ya tatu kuashiria kwamba Muswada umepitishwa.  Mara nyingi Muswada hutokana na majadiliano katika hatua hizi zote, mabadiliko hufanywa na wakati mwingine mabadiliko  huwa makubwa kiasi kwamba kufanya  Muswada uliochapishwa na kusomwa mara ya kwanza na ule uliokubaliwa mwishoni uwe tofauti kabisa.

Ndugu Wananchi;

Muswada huu ulisomwa mara ya kwanza mwezi Aprili na kupelekwa kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi Aprili, 2011.  Tangu wakati huo Kamati imekuwa ikiufanyia uchunguzi Muswada huo na kukusanya maoni ya wadau.  Walisikiliza wadau Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na kufuatilia maoni ya makongamano, magazetini na kwenye mitandao.  Kisha Kamati ikayajadili na kutoa mapendekezo yake ambayo Serikali iliyasikiliza na kuyajumuisha wakati uliposomwa mara ya pili.  Muswada huu haukuwahi kuondolewa Bungeni.  Kwa sababu hiyo, hakuna sababu ya kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za kuendesha Bunge.

Tukumbuke kwamba baadhi yao waliahidi kwamba wangetoa Katiba Mpya katika siku mia moja tu.  Serikali imechukua miezi kumi na mmoja na wanalaumu kwamba eti inawahisha mchakato!!  Hiyo Katiba ya siku mia moja sijui wangeipataje bila kuwashirikisha wananchi?

Ndugu Wananchi;

          Ni kutokana na hoja hizo Spika akaamua Muswada uendelee kujadiliwa na Bunge na leo Bunge limeupitisha Muswada huo.  Baadae Muswada utaletwa kwangu kwa ajili ya kutiwa saini uwe Sheria.  Baada ya hapo itabakia kazi yangu na Rais wa Zanzibar kuunda hiyo Tume ili mapema mwakani kazi ya kukusanya maoni ya wananchi ianze.  Lengo letu ni kuwa ifikapo mwaka 2014 zoezi zima liwe limekamilika ili mwaka 2015 tufanye uchaguzi tukiwa na Katiba mpya.  Itapendeza tukisherehekea miaka 50 ya Muungano na Katiba mpya.  Ni matumaini yangu kwamba wananchi wote watashiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yao kwa Tume hiyo.

Ndugu Wananchi;   

Nimechukua muda wenu mwingi kuyafafanua masuala haya kwa umuhimu wake.  Nia ni kutaka watu waelewe maoni ya upande wa Serikali.  Matatizo ya kiuchumi yanayotukabili tunaendelea kuyashughulikia.  Yale yaliyo kwenye uwezo wetu tutayamaliza na yale yaliyo nje ya uwezo wetu tutaendelea kuchukua hatua za kupunguza makali.  Aidha, tutaendelea kutoa wito kwa mataifa husika kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo yao kwani tunaoumia ni wengi.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa mchakato wa kupata Katiba mpya nawasihi Watanzania tujiandae kwa maoni ya kutoa kwenye Tume ya Katiba mara itakapoanza kazi.  Kwa wale ambao hawatapata walichokitaka nawaomba warudi kundini, sote tuungane kwa hatua inayofuata.  Najua wanayo maoni mengi mazuri wayatayarishe na kuyawasilisha kwa Tume itakayoundwa.  Njia ya maandamano na vurugu si ya busara kufuata.  Haijengi bali inabomoa, haina faida bali hasara nyingi, haina faraja bali machungu kwa pande zote.  Busara ituongoze sote kuchagua njia inayojenga, yenye faida, furaha na faraja kwa wote.  Tutofautiane bila kupigana.  Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu.

Mwisho

Ndugu Wananchi,

Naomba nimalizie kwa kuwashukuru wananchi kwa kuwa na subira kwa kipindi chote hiki toka tutangaze nia yetu ya kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya.  Kwa mara nyingine tena nawaomba mjiandae kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba mpya mara utakapoanza ili tuendelee kuijenga na kuiendeleza nchi yetu na vile vile tuendelee kuithamini na kuitunza amani ya nchi yetu.

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni sana kwa kunisikiliza

KATIBA MPYA: Maamuzi ya KAMATI KUU YA CHADEMA


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)


MAAMUZI YA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA.
Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao chake maalum kilichofanyika siku ya Jumapili, tarehe 20 Novemba 2011 katika Ukumbi wa Hoteli ya Mbezi Garden, Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kimepokea na kujadili kwa kina taarifa ya majadiliano na kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Aidha, Kamati Kuu imejadili kwa kina hatua za kuchukua baada ya Serikali, kupitia wabunge wa CCM, kulazimisha kupitishwa bungeni kwa Sheria hiyo bila kuzingatia maoni ya Wananchi na wadau wengine mbalimbali. Baada ya kuyatafakari mambo haya kwa kina, Kamati Kuu imeazimia yafuatayo:
1. 
1. Kamati Kuu imewapongeza wabunge wote wa CHADEMA kwa hatua thabiti na sahihi walizochukua, kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, kupinga Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa Bungeni bila ya wananchi kushirikishwa kwa ukamilifu kutoa maoni yao na muswada kuboreshwa kwa kuzingatia muafaka wa kitaifa. Kamati Kuu imewapongeza wabunge wa CHADEMA na wale NCCR Mageuzi kwa kususia vikao vya Bunge vilivyojadili na kupitisha Sheria hiyo kwani kushiriki kwao kungeipa uhalali wa kisiasa na kijamii Sheria ambayo haikuzingatia nia na haja ya dhati ya kuweka utaratibu wa kisheria utakaoiwezesha nchi yetu kupata Katiba Mpya yenye kuzingatia na kukidhi matakwa ya umma wa Watanzania;

2. Kamati Kuu imezingatia kuwa Sheria iliyopitishwa na Bunge ina mapungufu mengi na ya kimsingi ambayo hayatajenga muafaka wa kitaifa juu ya Katiba Mpya na hayataleta mabadiliko yoyote ya kimsingi ya Katiba:

a) Mchakato wa kuipitisha Sheria ndani ya Bunge ulikiuka Kanuni za Kudumu za Bunge kwani Muswada uliosomwa mara ya kwanza Bungeni sio ulioletwa Bungeni kusomwa mara ya pili na baadae kupitishwa; Kamati ilizuiliwa kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa na maeneo mbali mbali; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano aliingilia kazi na majukumu ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe na baadhi ya wajumbe wa CCM kukusanya maoni nje ya utaratibu wa Kamati na baadae kuingiza wajumbe wengine wa CCM na CUF kwa lengo la kupitisha matakwa ya CCM na Serikali ndani ya Kamati bila kuushirikisha wananchi kwa ukamilifu;
b) Sheria inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mamlaka makubwa ya kuunda Tume ya Katiba na Sekretarieti yake ambayo sio tu itakusanya maoni ya wananchi na kuandaa ripoti, bali pia ndiyo itakayoandaa na kuandika Rasimu ya Katiba Mpya na kusimamia mchakato wote wa wananchi kuijadili na kuipitisha katika Bunge la Katiba;

c) Sheria inampa Rais na Mwenyekiti wa CCM mamlaka makubwa sio tu ya kupokea ripoti ya Tume ya Katiba bali pia ya kuifanyia mabadiliko ambayo yeye na Serikali yake wataona yanafaa kwa kutumia taratibu za kiserikali za kutunga sheria;

d) Sheria inampa Rais na Mwenyekiti wa CCM mamlaka makubwa ya kuliitisha tena Bunge la Katiba kwa lengo la kufanya mabadiliko kwenye Katiba Mpya endapo litapitisha Katiba Mpya ambayo yeye Rais, au Serikali yake, au chama chake wataona hailindi maslahi yao;

e) Sheria inaunda Bunge la Katiba ambalo litakuwa na Wajumbe hadi 400 wa CCM kati ya wajumbe 545 wa Bunge la Katiba. Idadi hii ya wajumbe itaiwezesha CCM kupata theluthi mbili ya wajumbe wanaohitajika chini ya Sheria hii ili kupitisha jambo lolote katika Bunge la Katiba na kwa hiyo Katiba Mpya itakuwa ni ile inayolingana na matakwa na maslahi ya CCM na itakuwa mpya kwa jina tu;

f) Sheria inatoa nafasi kubwa kwa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM na vyombo vya uwakilishi vya Zanzibar kushiriki kutunga Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na Katiba ya sasa ambayo imevipa mamlaka ya kutunga Katiba ya Jamhuri ya Muungano vyombo vya Muungano kama Serikali na Bunge ambako Zanzibar ina uwakilishi wa kutosha;

g) Sheria inahakikisha kwamba muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali hautaguswa bali utadumishwa na kutiliwa nguvu licha ya madai ya miaka mingi ya wananchi na mapendekezo ya Tume za Kiserikali kwamba muundo wa Muungano uwe ni wa Serikali tatu;

h)Sheria inaipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoteuliwa na Rais na Mwenyekiti wa CCM mamlaka ya kusimamia mchakato mzima wa kura ya maoni ya kuipa Katiba Mpya uhai wa kisheria. Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina uhuru na imeshindwa mara nyingi kusimamia chaguzi huru na haki katika nchi yetu na haiwezi kusimamia kura ya maoni kwa uhuru unaohitajika;
3. Kamati Kuu ya CHADEMA imesisitiza siku zote kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya unahitaji mwafaka wa kitaifa ambao utazingatia maoni mapana ya makundi mbalimbali ya kijamii. Kamati Kuu inasikitishwa na hatua za makusudi za kufifisha juhudi zote zilizofanyika na wadau mbalimbali katika kufikia mwafaka wa kitaifa juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na upotoshaji wa makusudi wa hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni uliofanywa na wabunge wa CCM na CUF, wakiongozwa na Spika wa Bunge, Anna Makinda, kuhusu msimamo wa CHADEMA juu ya Muungano;

4. Kamati Kuu inasisitiza kwamba njia pekee ya kuunusuru Muungano wetu ni kwa wananchi wa pande zote mbili kupiga kura ya maoni kuamua kwamba wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu ni ndio, muundo gani wa Muungano huo wanaoutaka. Aidha, Kamati Kuu inarudia msimamo wa CHADEMA kwamba ili kuondoa kero na malalamiko ambayo yameuandama Muungano wetu tangu kuzaliwa kwake, muundo unaofaa ni wa Serikali tatu kama ilivyopendekezwa pia na Tume ya Nyalali mwaka 1991 na Tume ya Kisanga mwaka 1998;


5. Kamati Kuu inaamini kuwa pamoja na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kupitishwa, bado kuna fursa za kisiasa na kijamii katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya haja, nia, mchakato na misingi ya Katiba Mpya. Hata hivyo, Kamati Kuu imeshangazwa na kusikitishwa na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kutozitumia fursa hizo na badala yake kujiingiza katika jalala la taka za upotoshaji uliofanywa na Wabunge wa chama chake juu ya misingi na maudhui ya Sheria hiyo. Kamati Kuu inaamini kwamba badala ya kuwaunganisha Watanzania na kujenga muafaka unaohitajika katika mchakato wa Katiba Mpya, hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa CCM wa Dar es Salaam imezidi kuwagawa Watanzania kwa misingi ya ushabiki wa vyama badala ya kuwaunganisha kwa misingi ya utaifa;

6. Baada ya kutafakuri mambo yote haya, Kamati Kuu imeazimia yafuatayo:


a) CHADEMA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki;

b) Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo;

7. Kamati Kuu inawaagiza wabunge na viongozi wote wa chama katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi;


8. Kamati Kuu inaamini kwamba uamuzi wa Serikali ya CCM kulitumia Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga mchakato uliopitishwa kuwa Sheria sio tu ni kwenda kinyume na haki za kimsingi za kikatiba bali pia unahatarisha moja kwa moja amani, utulivu na umoja wa nchi yetu. Kamati Kuu inasikitishwa na msimamo huu wa Serikali ya CCM kwani unashindwa kutambua ukweli kuwa matumizi ya nguvu za dola hayajawahi kuokoa serikali za kidikteta kuondolewa madarakani na Katiba Mpya kupatikana katika nchi mbali mbali duniani na katika Bara la Afrika;

9. Kamati Kuu inasisitiza kwamba CHADEMA itaendelea kutumia njia zote za amani, ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano kama ilivyoainishwa na Katiba na sheria husika za nchi yetu kuunganisha nguvu ya umma kupinga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mchakato wake utakaopelekea Tanzania kutopata Katiba Mpya na bora; 



.................................................. ...........................................

Freeman A. Mbowe (MB)
MWENYEKITI WA TAIFA
Novemba 21, 2011

Tuesday, November 15, 2011

KATIBA MPYA: Tamko la TUNDU LISSU, Msemaji wa Upinzani

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA

SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)KUHUSU
MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011
(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI



Mheshimiwa Spika,


Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika Gazeti la Serikali la tarehe hiyo. Muswada huo ulipelekwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa dhidi ya Muswada huo kujitokeza karibu nchi nzima, Bunge lililazimika kuondoa Hati ya Dharura na hivyo kufanya Muswada kushughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa kutunga sheria uliowekwa na kanuni za 80, 83 na 84 za Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, 2007. Katika kufanya hivyo, Bunge – kwa kupitia Spika - liliiagiza Serikali kufanya mambo yafuatayo kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano Katika Bunge (Hansard) ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa Tatu cha tarehe 15 Aprili 2011:


(a) “Muda zaidi utolewe kwa Kamati na wananchi kuufikiria Muswada huu. Katika kufanikisha hili, “... iandae Muswada huu kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wenyewe waweze kusoma yaliyomo kwenye Muswada huo badala ya kupewa tafsiri tu na watu wengine;


(b) “Muswada uchapishwe kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi wengi kuuelewa na kuutolea maoni;


(c) “Utangulizi wa Muswada huu uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe madhumuni ya Muswada huu, kwani imeonekana wazi wananchi wengi wanadhani tayari tumeanza kuandika Katiba, kumbe lengo la Muswada huu ni kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni tu.” (uk. 31-32)

Mheshimiwa Spika, 
Katika kutoa maagizo haya, Bunge lilisitiza kwamba “... Muswada huu uko ndani ya Bunge, hauko serikalini.” (uk. 33) Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Bunge, Muswada ulikwishasomwa kwa mara ya kwanza na kupelekwa kwenye Kamati inayohusika kwa ajili ya kuanza kujadiliwa. Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 84(2) Kamati ilikwishaanza kupokea maoni ya wadau “... kwa lengo la kuisaidia katika uchambuzi wa Muswada huo.” Kazi iliyokuwa imebaki kwa Kamati ilikuwa ni kutumia mamlaka yake chini ya kanuni ya 84(3) “... kufanya marekebisho katika Muswada wa Sheria kwa kumshauri Waziri ... anayehusika na Muswada huo kufanya mabadiliko....” Ni baada tu ya kupata ushauri wa Kamati kuhusu mabadiliko ndio Serikali ingeweza kuleta Jedwali la Mabadiliko kwa lengo la kufanya mabadiliko katika hatua hii kabla Muswada haujaletwa Bungeni kwa ajili ya kusomwa mara ya pili na kwa mjadala wa Bunge zima. 

Mheshimiwa Spika, 
Hakuna hata moja ya maagizo haya ya Bunge ambalo limetekelezwa na Serikali. Tafsiri ya Kiswahili ambayo imeletwa Bungeni – pamoja na kuonyesha imesainiwa tarehe 8 Machi 2011 sawa na Muswada wa Zamani uliopigiwa kelele sana na wananchi – ililetwa kwenye Kamati wiki mbili zilizopita, ikiwa ni wiki moja baada ya Kamati kukataa kuujadili Muswada Mpya kwa vile ulifanyiwa mabadiliko na Serikali bila kupata ushauri wa Kamati kama inavyotakiwa na kanuni ya 83(4) ya Kanuni za Bunge. Badala ya kutekeleza maagizo ya Bunge, Serikali imeleta Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ambao ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 14 Oktoba 2011. 

Muswada huu mpya una tofauti kubwa na za kimsingi na Muswada wa Zamani kama nitakavyoonyesha hapa. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mabadiliko makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada wa Zamani yalihitaji na bado yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi kama ambavyo wengi wamedai katika mijadala inayoendelea nchi nzima. Aidha, Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado linahitaji, muda zaidi wa kuyatafakari mabadiliko haya makubwa nay a kimsingi katika Muswada wa Zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini ni busara na ni sound policy kwa Muswada huu Mpya kusomwa mara ya Kwanza ili kuruhusu mjadala unaohitajika kufanyika.

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA

Mheshimiwa Spika, 
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, Muswada huu unapendekeza kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa mujibu wa Utangulizi wa Muswada, itawajibika “... kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba (na) kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi....” Kwa mujibu wa ibara ya 5, Tume hii itaundwa na Rais “kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar....” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais atateua wajumbe wa Tume “... kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar....” 

Ibara ya 6(2) inapendekeza kwamba “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Pendekezo hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi, msimamo wa ibara ya 6(2) ya Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi kwamba idadi ya wajumbe wa Tume itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano! Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, ibara ya 7(2) ya Muswada inapendekeza kwamba “uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.” 

Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na Katibu. (ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo atateuliwa na Rais “baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.” Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na Waziri “kwa makubaliano na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.” 

Muswada unapendekeza kumpa Rais - baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya kutoa hadidu za rejea za Tume na muda wa kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(1) Na kama hali itahitaji kufanya hivyo, Rais – “kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar” – anaweza kuongeza muda usiozidi miezi mitatu ili kuwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(2) Hadidu za rejea, kwa mujibu wa ibara ya 8(3), “... zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo Tume itaizingatia katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake kwa mujibu wa Sheria hii.” 

Mheshimiwa Spika, 
Ibara ya 9(1) ya Muswada inaelezea kazi za Tume kuwa ni pamoja na:
(a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
(b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora;
(c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na 
(d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti.
Ijapokuwa haijaanishwa hivyo, ni wazi - kwa mujibu wa wa ibara ya 17(1)(d) na (2) ya Muswada - kwamba moja ya kazi za Tume ni kuandaa Rasimu ya Muswada wa Katiba mpya. Mapendekezo ya Muswada kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni muhimu na yanazua maswali mengi yanayohitaji mjadala wa kitaifa na maamuzi ya wananchi. Maeneo haya muhimu ni pamoja na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mchakato mzima wa kutengeneza Katiba Mpya. 

MAMLAKA YA RAIS 

Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge hili, kwa muda wote wa uhai wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo kuu ya Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana ya kiutendaji na ya kiutungaji sheria. Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha kikatiba juu ya mahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Urais wa Kifalme ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote za serikali na ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha ambao umefanywa kuwa ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali. 



Sio vibaya, katika kuthibitisha jambo hili, kurudia maneno ya ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977: “... Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote....” Na kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye mahojiano ya mwaka 1978 na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kama Rais wa Tanzania alikuwa na mamlaka – kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu – ya kuwa dikteta!

Muswada unaendeleza kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama Rais alivyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji wa katiba ya kidemokrasia. Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume yanayopendekezwa na Muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na Rais Ali Mohamed Shein, Makamu wake na pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi vile vile kwamba watu watakaoteuliwa na Marais hawa ni watu wasiokuwa tishio kwa status quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM! 

Mheshimiwa Spika, 
Hali ni hiyo hiyo kwa Sekretarieti ya Tume ambayo ndio chombo cha kiutendaji na moyo wa Tume yenyewe. Kama Katibu, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Tume ni mteuliwa wa Rais na ni mtumishi wa Serikali; kama watendaji wengine wa Tume ni watumishi wa serikali walioteuliwa wa Waziri ambaye naye ni mteuliwa wa Rais baada ya kukubaliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar; na kama watumishi wengine wa Tume nao ni watumishi wa Serikali kama inavyopendekezwa na ibara ya 13 ya Muswada Mpya, ni wazi, kwa hiyo, kwamba mapendekezo haya yote ya uteuzi wa wajumbe, watendaji na watumishi wengine wa Tume yana lengo moja tu: kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM. 

Mheshimiwa Spika, 
Badala ya mapendekezo haya ya Muswada Mpya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza utaratibu wa kidemokrasia zaidi katika uteuzi wa Tume. Kwanza, badala ya Tume hiyo kuwa ‘Tume ya Rais’ kama inavyopendekezwa katika Muswada, tunapendekeza iwe ‘Tume ya Vyama’ (multiparty Commission) kwa maana moja kubwa: wajumbe wa Tume wateuliwe kufuatana na mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, vyama vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini. Hii haina maana kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawatatakiwa kuwa na sifa zilizoainishwa katika ibara ya 6(3) ya Muswada Mpya. La hasha! Wajumbe wa Tume ya Vyama watatakiwa kuwa na sifa zozote za kitaaluma zinazotakiwa ili kuwawezesha kufanya kazi ya kitaalamu kama inavyopendekezwa na 
Muswada Mpya. 

Pili, baada ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Vyama, inapendekezwa kwamba wajumbe walioteuliwa kwa mashauriano na makubaliano kama tunavyopendekeza watatakiwa wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pendekezo hili litahakikisha kwamba wajumbe wa Tume wanakuwa vetted na chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Hili litajenga kuaminiana baina ya Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini na litaipa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uhalali mkubwa wa kisiasa, kitu ambacho ni muhimu katika mazingira ya sasa ya kisiasa.

Mheshimiwa Spika, 
Tofauti pekee na muhimu kati ya pendekezo la Muswada Mpya na pendekezo letu kuhusu mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ni locus ya uwajibikaji wao. Wajumbe wanaoteuliwa na Rais wanakuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha Rais au chama chake. Wajumbe wanaotokana na mapendekezo na makubaliano ya wadau wengi na wanaothibitishwa na chombo cha uwakilishi cha wananchi kama tunavyopendekeza hawawezi kuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha mmojawapo wa wadau hao. Faida kubwa na ya wazi ya Tume ya Vyama ni kwamba matokeo ya kazi yake yana nafasi kubwa zaidi ya kukubaliwa, kuheshimiwa na kutekelezwa na wadau mbali mbali kuliko matokeo ya kazi ya Tume ya Rais. Kwa lugha nyingine, kazi ya Tume ya Vyama itakuwa na uhalali wa kisiasa (political legitimacy) mkubwa zaidi kuliko Tume ya Rais. 


Pendekezo hili linawahusu Katibu, watendaji na watumishi wengine wa Tume vile vile. Kutokana na uzoefu uliotokana na historia yetu na mfumo wetu wa kiutawala na kikatiba, watumishi wa serikali wamekuwa hawana uhuru wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia utashi wao na uadilifu wa kitaaluma bali hufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya mabosi wao wa kisiasa. Hii ni kwa sababu, kisheria na hata kivitendo, watendaji na watumishi karibu wote wa umma hujiona wanawajibika kwa mamlaka zao za uteuzi, yaani Rais na/au Waziri. Aidha, watendaji na watumishi hawa wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali ambao nao ni wateuliwa wa Rais na kwa hiyo wanakuwa na woga wa kufanya maamuzi yanayoweza kuhatarisha maslahi ya kisiasa ya Rais na chama tawala. 

Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa watendaji na watumishi wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wawe huru dhidi ya mashinikizo yoyote ya kisiasa kutoka kwa Rais na Serikali yake na chama chake. Ili Tume iwe na mamlaka na uhuru unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na ili isiingiliwe kweli na mtu au mamlaka yoyote kama inavyosema ibara ya 10 ya Muswada, inabidi mamlaka ya uteuzi yaondolewe katika mikono ya Rais na/au Waziri ambaye ni mdau mmojawapo tu wa wadau wengi wa mchakato wa Katiba Mpya. Na namna ya pili ya kuhakikisha uhuru huu unakuwepo ni kuweka utaratibu wa kuwapata watendaji na watumishi hawa nje kabisa ya utumishi wa serikali kwa kuweka masharti ya kuwataka waombe kazi, kufanyiwa usaili na kuteuliwa na jopo la wataalamu walio huru. 

Mheshimiwa Spika, 
Namna ya tatu ya kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ni kuhakikisha wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao (security of tenure) sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya Tanzania ili kuzuia uwezekano wa wajumbe kuondolewa kwa sababu zisizotokana na utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili. Kwa maana hiyo, mapendekezo ya ibara ya 10 Muswada Mpya juu ya uhuru wa Tume hayatoshelezi hata kidogo. Hii ni kwa sababu ibara ya 12 ya Muswada Mpya, ambayo inazungumzia ukomo wa ujumbe wa Tume, haijaweka utaratibu wowote wa namna ya kushughulikia nidhamu ya wajumbe pale kunapokuwepo tuhuma za ukiukaji wa Kanuni za Maadili zinazopendekezwa katika ibara ya 12(2) na Jedwali la Pili la Muswada. Kutokuweka utaratibu huu kuna hatari kubwa kwani, kisheria, mamlaka ya uteuzi huwa ndio mamlaka ya nidhamu pale ambapo sheria haijaweka utaratibu tofauti wa nidhamu. Hii ina maana kwamba bila kuweka utaratibu wa kisheria wa nidhamu ya wajumbe wa Tume, Rais ndiye atakuwa na uwezo wa kuwaondoa madarakani kwa sababu yeye ndiye aliyewateua! 

Mheshimiwa Spika, 
Pendekezo letu la tatu linahusu hadidu za rejea. Hapa kuna hoja za aina mbili. Kwanza, sambamba na pendekezo la kutompa Rais madaraka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume, Rais asipewe mamlaka ya kutoa hadidu za rejea kwa Tume. Pili, kwa vile – kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya – hadidu za rejea ni hati ya kisheria inayotakiwa kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu yake, ni muhimu hati hii iwekwe wazi katika sheria yenyewe badala ya kubakia kuwa siri ya Rais. Watanzania lazima wajue Tume inapewa majukumu gani ya kisheria. Aidha, wajumbe wa Tume wenyewe lazima wafahamu wanapewa majukumu gani ya kisheria na wafahamu kwamba wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria na sio maelekezo ya mtu mmoja hata kama ni Rais wa Kifalme. Hii itasaidia uwajibikaji wa Tume kwa wananchi kwani itakuwa rahisi kupima matokeo ya kazi ya Tume kwa hadidu za rejea zilizowekwa wazi katika sheria. 


Ukweli ni kwamba badala ya kumsubiri Rais kutoa hadidu za rejea, tayari ibara za 9 na 16 za Muswada Mpya zimeshafanya hivyo kwa kuainisha kazi za Tume, mipaka ya Tume katika utekelezaji wa kazi hizo na utaratibu wa namna ya kuzifanya. Kwa ajili hiyo, zaidi ya kutaka kuonyesha kwamba Rais ana mamlaka makubwa katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya, mapendekezo ya ibara ya 8 hayana maana wala sababu yoyote na yanaweza kuondolewa bila kuathiri maudhui ya Muswada. Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya ibara ya 9, haijulikani Rais atatoa maelekezo gani ya ziada yanayohusu kazi za Tume na namna ya kuzitekeleza. Kwa upande mwingine, mapendekezo ya ibara ya 8 yanaweza kuleta mkanganyiko na mgogoro wa kisiasa na kisheria usiokuwa wa lazima endapo Rais atatoa hadidu za rejea zinazotofautiana na matakwa ya kisheria kama yanavyopendekezwa na ibara 9 ya Muswada Mpya. Pendekezo letu, kwa hiyo, ni kwamba ibara ya 8 ifutwe yote na ibara za 9 na 16 zifafanuliwe vizuri ili kuweka wazi zaidi hadidu za rejea za Tume na namna ya kuzitekeleza.

Mheshimiwa Spika, 
Kuna mapendekezo mengine yaliyoko kwenye Muswada yanayoonyesha hatari za Urais wa Kifalme. Kama tulivyoona, Tume inatakiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kwa Rais wa Zanzibar. Baada ya hapo, kwa mujibu wa ibara ya 18(2) ya Muswada, “baada ya mashauriano na makubaliano na Rais wa Zanzibar na baada ya kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera, Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kupitishwa kwa vifungu vya Katiba.” 

Pendekezo hili ni la hatari kubwa. Kwanza, ‘kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera’ maana yake ni baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kawaida wa kiserikali unaohusu utungaji sera na sheria. Chini ya utaratibu huu, rasimu ya muswada hupelekwa kwanza kwenye Kamati ya Watalaam ya Baraza la Mawaziri (Inter Ministerial Technical Committee of the Cabinet) kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho na Makatibu Wakuu kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa maamuzi ya mwisho. Baada ya maamuzi ya mwisho ya Baraza la Mawaziri, rasimu ya muswada hurudishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuandikwa upya ndipo upelekwe Bungeni la Katiba. 

Katika hatua zote hizi, muswada wa sheria huweza kufanyiwa marekebisho makubwa. Kwa maana hiyo, pendekezo la kuuwasilisha Muswada wa Katiba Mpya katika Bunge la Katiba baada ya kuupitisha kwanza kwa Makatibu Wakuu ambao wote ni wateuliwa wa Rais, na kwenye Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake wote (ukiacha Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar) ni wateuliwa wa Rais ni kutengeneza mazingira ya kisheria yatakayoruhusu uchakachuaji wa Muswada huo kwa lengo la kuhakikisha matokeo yake ya mwisho, yaani Katiba Mpya, yanakidhi maslahi ya Rais na chama chake cha CCM. Kwa vyovyote vile, pendekezo hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. 

SIFA ZA WAJUMBE 

Mheshimiwa Spika, 
Muswada Mpya unapendekeza sifa zifuatazo wanazotakiwa kuwa nazo wajumbe wa Tume: 
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya jamii;
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(c) Maslahi ya umma;
(d) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii; na 
(e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa. (ibara ya 6(3)
Zaidi ya sifa zilizotajwa, ibara ya 6(4) inakataza watu wenye sifa zifuatazo kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume:
(a) Wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote kuanzia Wilaya hadi Taifa;
(b) Watumishi wa vyombo vya usalama;
(c) Watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au wanaotuhumiwa mahakamani kwa mashtaka ya kukosa uaminifu au uadilifu;
(d) Watu wasiokuwa raia wa Tanzania. 

Mapendekezo haya yana athari kubwa kwa mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Kwanza, kwa kukataza viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa kuteuliwa wajumbe wa Tume kunaondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya kundi kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala mbali mbali ya kisiasa, kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha na kisayansi jamii. Vile vile, viongozi wa vyama vya siasa wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye mtawanyiko wa watu na wa kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wanawakilisha watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya. 

Aidha, kwa kuwa maneno ‘maslahi ya umma’ hayajafafanuliwa katika Muswada, hakuna anayeweza kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria baada ya kutimiza masharti yote husika ya kisheria, na ambao wanaungwa mkono na mamilioni ya wananchi wa Tanzania kwa kupewa nafasi za uwakilishi katika taasisi za uwakilishi za umma kama Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri za Serikali za Mitaa hawajui wala hawazingatii maslahi ya umma na kwa hiyo hawafai kuwakilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba! Kama ingekuwa hivyo, Rais – ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na kwa hiyo kiongozi wa chama cha siasa – naye pia atakuwa hana sifa za kuteua Tume! Na wakati haja ya kutoshirikisha watumishi wa taasisi za ulinzi na usalama katika mchakato wenye ubishani wa kisiasa kama utungaji wa Katiba Mpya inaeleweka, ni matusi kwa watu waliochaguliwa na wananchi kuwa Wabunge, Wawakilishi au Madiwani au viongozi wa vyama vya siasa vilivyowapendekeza watu hao, kuwekwa pamoja na wahalifu na kutamkwa kuwa hawana sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba!

Inaelekea lengo kuu la pendekezo hili ni kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani, hasa hasa CHADEMA, vyenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Bunge havipati fursa ya kuamua muundo na maudhui ya Katiba Mpya hasa katika hatua muhimu za uundaji wake. Pili, lengo kuu vile vile ni kuhakikisha kuwa Rais, na kwa hiyo chama chake cha CCM, wanadhibiti mchakato wa Katiba Mpya katika hatua muhimu ya uundaji wake. Endapo watafanikiwa katika hili, Rais na chama chake cha CCM watakuwa na nafasi kubwa ya kuamua aina ya Katiba Mpya itakayotokana na mchakato walioudhibiti kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya. Hii ni kwa sababu, kwa kutumia uzoefu wa Tume nyingine zilizopata kuteuliwa miaka ya nyuma, wajumbe wengi huwa ni watumishi au waliopata kuwa watumishi wa Serikali na/au taasisi zake. Wajumbe wa aina hii wamekuwa hawana uthubutu wa kupendekeza mabadiliko makubwa yanayohitajika katika mfumo wa utawala wa nchi yetu. 

Mheshimiwa Spika, 
Badala ya kukataza viongozi wa vyama vya siasa kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya, na kwa kuzingatia nafasi ya vyama vya siasa katika historia yetu na mfumo wetu wa utawala, na kwa lengo la kuhakikisha Tume inakuwa na utaalamu, uzoefu na uhalali wa kisiasa unaohitajika, watu wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume wawe ni wale wenye sifa zinazopendekezwa na ibara ya 6(3)(a), (b), (c) na (d) ya Muswada. Kwa sababu hiyo, hakutakiwi kuwa na vigezo vingine visivyojulikana wazi kwa wananchi. Kwa maneno mengine, pendekezo la kuwa na ‘vigezo vingine ambavyo Rais ataona inafaa’ halikubaliki kwani linampa Rais mwanya wa kuteua marafiki zake au watu ambao hawana sifa zinazojulikana. Kwa maoni yetu vile vile, badala ya kuwa sababu ya disqualification, uongozi wa kuchaguliwa na wananchi katika taasisi za uwakilishi au katika vyama vya siasa unatakiwa kuwa an added advantage pale ambapo kiongozi husika ana sifa za kitaaluma zinazotakiwa! 

MISINGI MIKUU YA KITAIFA

Mheshimiwa Spika, 
Muswada unapendekeza kuwepo kwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ambayo Tume inatakiwa kuizingatia kwa lengo la kuihifadhi na kuidumisha. Misingi mikuu inayopendekezwa ni:
(a) Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) Uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) Mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) Umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(e) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
(f) Ukuzaji na na uhifadhi wa haki za binadamu;
(g) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
(h) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine. (ibara ya 9(2)
Kifungu hiki kimefanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno ‘Tume itahakikisha ... kutokugusika na utakatifu (inviolability and sanctity) wa mambo yafuatayo’ yaliyokuwa katika Muswada wa Zamani, na badala yake yamewekwa maneno mapya ‘... kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo....’ Mabadiliko haya yamefanywa ili kujaribu kuondoa hofu iliyojitokeza wakati wa mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kwamba lengo la pendekezo hilo lilikuwa kuzuia mjadala juu ya masuala ya kikatiba yenye utata mkubwa kama vile suala la Muungano. Hata hivyo, hatari ya kuzuiliwa kwa mjadala juu ya misingi mikuu ya kitaifa bado haijaondolewa kwani, kwa mujibu wa ibara mpya ya 9(3), “... Tume itatoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.” Tafsiri halisi ya maneno haya ni kwamba mjadala pekee utakaoruhusiwa juu ya ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni ule ambao lengo lake ni ‘kuendeleza na kuboresha masuala hayo.’ 

Kwa maoni yetu, lengo kuu la pendekezo linalohusu kuendeleza na kuboresha ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni kuzuia mjadala wenye kuhoji ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ ili kuendeleza mfumo wa sasa wa Muungano wenye Serikali mbili. Hii ni kwa sababu katika mambo yote yanayopendekezwa kuwa misingi mikuu ya kitaifa, ni ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ yenye Serikali mbili ndio ambayo imekuwa na mgogoro mkubwa kwa muda wote wa maisha ya Jamhuri ya Muungano. Ukiacha ‘ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu’ ambalo lilikataliwa na Serikali ya Mwalimu Nyerere kwa miaka yote ya utawala wake, mambo mengine yote yanayotajwa kuwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ hayajawahi kubishaniwa kwa miaka yote ya uhai wa Jamhuri ya Muungano. 

Mheshimiwa Spika, 
Pendekezo la ‘misingi mikuu ya kitaifa’ linastaajabisha sana kwani, kwa mujibu wa ibara ya 98(1)(b) ya Katiba ya sasa, ‘kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Kamhuri ya Muungano, kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Zanzibar, Orodha ya Mambo ya Muungano na idadi ya Wabunge kutoka Zanzibar’ ni mambo yanayoweza kubadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ili mradi tu mabadiliko hayo yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa kutoka Tanzania Bara na wa Tanzania Zanzibar. Kwa sababu hiyo, pendekezo la ibara ya 9(3) ya Muswada kwamba ‘misingi mikuu ya kitaifa’ izungumzwe kwa lengo la kuiendeleza na kuidumisha tu halikubaliki kwa sababu linazuia uhuru wa kuhoji na/au kupinga mambo ambayo kwa Katiba ya sasa ni ruhusa kuyahoji, kuyapinga na/au hata kuyabadilisha! Tunapendekeza ibara ya 9(2) na (3) za Muswada zifutwe kabisa ili kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kwa kupinga au kuunga mkono, kila jambo linalohusika na Katiba Mpya. 

NAFASI YA ZANZIBAR 

Mheshimiwa Spika, 
Pengine mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Muswada ni mapendekezo yanayohusu nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Itakumbukwa kwamba moja ya masuala yaliyozua tafrani kubwa katika mchakato wa kukusanya maoni juu ya Muswada wa Zamani hasa katika kituo cha Zanzibar ni kuwepo hisia kwamba nafasi ya Zanzibar ilikuwa imepuuzwa katika Muswada huo. Muswada sio tu kwamba umetekeleza matakwa yote ya ushirikishwaji wa Zanzibar, bali umekwenda mbali zaidi kwa kuifanya Zanzibar mwamuzi wa mustakbala wote wa kikatiba wa Tanzania. Hii imefanyika kwa njia mbili: kwanza, kwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa mshirika sawa wa kikatiba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; na pili, kwa kuipa Zanzibar nafasi kubwa ya uwakilishi katika mchakato mzima wa Katiba Mpya. 

NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika, 
Muswada unapendekeza kwamba utekelezaji wa mamlaka yote ya Rais, Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano lazima ufanyike kwa ‘mashauriano na makubaliano’ na Rais, Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kwa mfano, ibara ya 5 inayohusu kuundwa kwa Tume inamtaka Rais ‘kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar na kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Vile vile, ibara ya 6(1) inayohusu uteuzi wa wajumbe wa Tume; ibara ya 8(1) na (2) inayohusu hadidu za rejea na kuongeza muda wa Tume; na ibara ya 13(2) inayohusu uteuzi wa Katibu wa Tume, zote zinataka kuwepo na makubaliano na Rais wa Zanzibar. Aidha, ibara ya 13(5) inayohusu uteuzi wa watendaji wengine wa Tume inalazimu makubaliano kati ya Waziri na Waziri mwenzake wa Zanzibar ambao nao ni wateuliwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.

 
Mamlaka ya Rais wa Zanzibar hayaishii tu kwenye uteuzi wa wajumbe na watendaji wa Tume, bali pia yanaingia hata katika uwasilishaji wa ripoti ya Tume. Kwa mujibu wa ibara 18(1) ya Muswada, mara baada ya kumaliza kazi yake, Tume itawasilisha ripoti yake kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 18(2), mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais, ‘baada ya kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar, “... atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba.” Kwa mapendekezo haya pia, Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya turufu katika mchakato wa Katiba Mpya. Maana yake ni kwamba Rais wa Zanzibar asipopatiwa nakala ya ripoti ya Tume au asipokubaliana na Rais wa Muungano, basi Muswada wa Katiba hautawasilishwa kwenye Bunge la Katiba! 

Mheshimiwa Spika, 
Mapendekezo haya yanaashiria kuwepo kwa mtazamo ambao chanzo chake ni Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ya tarehe 25 Aprili 1964. Kwa mtazamo huo, Zanzibar ni nchi huru kama ilivyokuwa mwaka 1964 na kwa hiyo ni lazima sio tu ishirikishwe kwa usawa, bali pia lazima ikubaliane na mabadiliko yoyote ya kikatiba yanayopendekezwa na Muswada. Kama Profesa Palamagamba Kabudi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alivyosema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika tarehe 12 Novemba 2011: ‘Katika kuandika katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.’ 


Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mtazamo huu sio sahihi. Kwanza kabisa, Zanzibar sio nchi huru tena kama ilivyokuwa mwaka 1964, kama ambavyo hakuna tena nchi inayoitwa Tanganyika wala serikali yake. Hii ni kwa sababu tangu kusainiwa kwa Hati za Muungano mwaka 1964, na kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ya Katiba ya sasa, masuala yote yanayohusu Muungano kama vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambayo pia imekasimiwa mamlaka juu ya masuala ya iliyokuwa Tanganyika. Masuala haya ya Muungano hayawezi kujadiliwa upya na kwa usawa kati ya nchi hizi mbili kwa vile moja kati ya nchi hizo haipo tena na iliyobaki imepoteza sehemu ya uhuru wake kutokana na Muungano huo! Hii ndio kusema hakuwezi tena kuwa na wabia wa Muungano bila kwanza kuirudisha Tanganyika kama nchi na bila kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kama iliyokuwa nayo kabla ya Muungano!

Pili, kuna dhana kwamba Rais wa Zanzibar hakushirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya Muswada wa Zamani. Dhana hii vile vile ni potofu. Kwanza, Rais Ali Mohamed Shein mwenyewe ametamka wazi kwa waandishi wa habari kwamba alishiriki katika hatua zote za maamuzi kwenye Baraza la Mapinduzi. Pili, mujibu wa ibara ya 54(1) ya Katiba ya sasa, Rais wa Zanzibar ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni mshiriki wa maamuzi yote ya Serikali hiyo. Kwa maana hiyo, maslahi ya Zanzibar yanawakilishwa ndani ya ‘chombo kikuu cha kumshauri Rais’ katika Jamhuri ya Muungano. (ibara ya 54(3) Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mlolongo wa madaraka uliopo katika ibara ya 54(2), Rais wa Zanzibar sio mmoja wa wajumbe wanaoweza kuongoza mikutano ya Baraza hilo. 

Aidha, ndani ya Baraza la Mawaziri, Zanzibar inawakilishwa pia na Makamu wa Rais ambaye – kwa mujibu wa ibara ya 47(1) ya Katiba ya sasa – “... ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano....” Kwa maana hiyo, mapendekezo ya Muswada yanayomfanya Rais wa Zanzibar kuwa sio tu mshiriki sawa lakini pia mwamuzi wa mustakbala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaenda kinyume sio tu na Katiba ya sasa bali pia na Hati za Muungano wenyewe. Kwa mapendekezo haya, endapo Rais wa Zanzibar hatakubaliana na uteuzi wowote wa wajumbe wa Tume au Katibu wake au watendaji wake wengine, anaweza kusimamisha mchakato mzima wa kikatiba hata kama unahusu masuala ya Tanzania Bara yasiyo ya Muungano! 

UWAKILISHI WA ZANZIBAR 

Mheshimiwa Spika, 
Ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake. Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vya maamuzi vinavyopendekezwa na Muswada. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 6(2), “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Hii ina maana kwamba wajumbe wa Tume na Sekretarieti yake wanatakiwa wawe sawa kwa sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Ikumbukwe kwamba Tume hii inatengeneza Katiba inayohusu masuala ya Muungano, ambayo ni haki kwa Zanzibar kushirikishwa kwa usawa kabisa, na vile vile masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo Zanzibar haina haki ya kushiriki. 

BUNGE LA KATIBA 

Mheshimiwa Spika, 
Eneo la pili ambalo Zanzibar ina ushawishi mkubwa kutokana na uwakilishi wake ni katika Bunge la Katiba linalopendekezwa katika Sehemu ya Tano ya Muswada. Kwa mujibu wa ibara ya 20(2), wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar; mawaziri wa katiba na sheria wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; na wajumbe mia moja kumi na sita wakaoteuliwa kutoka asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii. Inaelekea kwamba, kwa mujibu wa ibara ya 20(4), wajumbe wasiokuwa wabunge ama wawakilishi nao pia watateuliwa na Rais licha ya kutoka nje ya mfumo wa kiserikali!

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(a) ya Katiba ya sasa ya Muungano, wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni pamoja na wabunge wa majimbo ya uchaguzi. Kwa composition ya sasa ya Bunge, kuna jumla ya majimbo ya uchaguzi 239 ambayo kati yao majimbo ya Zanzibar ni hamsini. Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(c) ya Katiba, Baraza la Wawakilishi Zanzibar linawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, kama inavyotakiwa na ibara ya 66(1)(b), kuna wabunge wanawake mia moja na mbili wanaojulikana kama ‘wabunge wa viti maalum.’ Kwa mgawanyo wa sasa wa wabunge hawa, idadi ya wanaotoka Zanzibar ni ishirini na tano kwa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni. Na mwisho, kuna wabunge wasiozidi 10 wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(e). Hadi sasa, Rais ameshateua wabunge watatu ambao wote ni wa kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, katika Bunge la sasa lenye wabunge 353, wabunge wanaowakilisha Zanzibar ni themanini na tatu au karibu 23.5% ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. 

Kwa mujibu wa Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na wawakilishi wa majimbo hamsini ya uchaguzi, wawakilishi kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na wawakilishi ishirini wa viti maalum na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa hiyo, jumla ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sasa ni themanini na moja. Kwa maana nyingine ni kwamba endapo mapendekezo ya ibara ya 20(1)(b), (c) na (d) ya Muswada yatakubaliwa, idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Zanzibar itaongezeka hadi kufikia mia moja sitini na nne kati ya wajumbe 545 wa Baraza hilo kwa mujibu wa ibara ya 20(2). Idadi hii ni sawa na 30% ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba. 


Idadi hiyo ya uwakilishi wa Zanzibar bado haitakidhi matakwa ya Muswada kwani ibara ya 20(3) inapendekeza kwamba “... idadi ya wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar ... haitapungua theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba”! Theluthi moja ya wajumbe wa Bunge la Katiba ni wajumbe 182. Kwa hiyo ili kukidhi matakwa ya Muswada kuhusu uwakilishi wa Zanzibar, itabidi wajumbe 18 kati ya 116 waliotajwa na ibara ya 20(2)(e) watoke Zanzibar ili kufikisha idadi ya wajumbe 182 ambayo ndio theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba. 

Mheshimiwa Spika, 
Kuna maeneo mengine ya Muswada ambayo pia yanazua maswali mengi juu ya nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Kwa mfano, wakati ibara ya 21(1) inapendekeza kwamba Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba wachaguliwe kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, ibara ya 21(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Naibu wake lazima atoke upande mwingine. Sambamba na pendekezo hili, ibara ya 22(1) inapendekeza Makatibu wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar watakuwa ndio Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba. Aidha, sawa na ibara ya 21(2), ibara ya 22(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Katibu wa Bunge la Katiba lazima atoke upande mwingine. 

Mapendekezo haya yanaonyesha sio tu nafasi na ushawishi mkubwa wa Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya, bali pia ni mwendelezo wa dhana potofu kwamba Zanzibar ni mshirika sawa wa Jamhuri ya Muungano. Hii inathibitishwa pia na pendekezo la ibara ya 24(3) ya Muswada inayotaka Katiba Mpya ikubaliwe na theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Tanzania Bara na vile vile theluthi mbili ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba iwe ni kwa masuala ya Muungano yanayoihusu Zanzibar pia, au kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo hayaihusu, Zanzibar itakuwa na kura ya turufu kwa mujibu wa mapendekezo ya Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, 
Uwakilishi mkubwa wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano umetumika kihistoria kwa lengo la kuwatuliza Wazanzibari wakati Serikali ya Mwalimu Nyerere ilipokuwa inamomonyoa uhuru wa Zanzibar kwa kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwenye Katiba ya Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni mashuhuri wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu amemnukuu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati Sheikh Abedi Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume juu ya nafasi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe na wasi wasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwakilishwa katika Baraza letu la Mapinduzi’”!


Mheshimiwa Spika, Sababu nyingine inatokana na kuongezeka kwa ushawishi na nafasi ya Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika mazingira haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia CCM anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro hicho. Kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwenyewe katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, “sababu moja kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ... ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia.” Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hofu hii ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano - juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010.


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba upendeleo wa Zanzibar unaopendekezwa katika Muswada huu kuhusiana na uwakilishi katika Bunge la Katiba na katika vyombo vingine vya maamuzi juu ya mchakato wa Katiba Mpya sio wa haki na haukubaliki tena. Kwanza, ibara ya 64(2) ya Katiba ya sasa inaweka wazi kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina mamlaka ya kutunga sheria katika Zanzibar ‘... juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano....’ Hii pia ndio lugha ya ibara ya 78(1) ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka jana. ‘Katiba ya Tanzania’ ni jambo la kwanza katika orodha ya Mambo ya Muungano iliyoko kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa Muswada Mpya kupendekeza kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar liwe sehemu ya Bunge la Katiba ni kukiuka wazi wazi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ya Katiba ya Zanzibar. Ni ajabu iliyoje kwamba wale wanaojifanya ni machampioni wa Muungano wanaweza kunyamazia ukiukaji huu wa Katiba!


Mheshimiwa Spika, Thomas Paine, mwandishi maarufu wa Marekani ya wakati wa Mapinduzi ya mwaka 1776, aliwahi kuandika kijitabu alichokiita Common Sense juu ya uhalali wa Uingereza kutawala Bara la Amerika ya Kaskazini ambako alisema: ‘... [T]here is something very absurd in supposing a continent to be perpetually governed by an island [for] in no instance hath nature made the satellite larger than its primary planet...’! Yaani, ni ujinga kudhani kwamba bara linaweza kutawaliwa milele na kisiwa kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya kitegemezi kuwa kikubwa kuliko sayari yake ya msingi. Hata kama ni kweli kwamba Tanganyika sio bara kama ilivyokuwa Marekani ya Kaskazini, bado tunakubaliana na Tom Paine kwamba ni ujinga kudhani kwamba Visiwa vya Zanzibar vitaendelea kuwa na maamuzi na ushawishi mkubwa katika masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya maslahi ya Visiwa hivyo kuwa bora zaidi ya maslahi ya Tanganyika! 


Kwa maoni yetu, wakati umefika kwa Muungano kuwekwa kwenye msingi wa usawa na imara zaidi. Msingi huo unahitaji kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika ambayo ndio ilikuwa – pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – mbia mkuu wa Muungano wa mwaka 1964. Kurudishwa huko kwa Tanganyika kutaiwezesha Zanzibar kujadiliana nayo kwa usawa juu ya masuala yote yanayohusu Muungano. Haya yote yanawezekana tu endapo Muungano huu utawekwa mbele ya wananchi ili waamue – kwa kura ya maoni - kama wanataka kuendelea nao au la; na kama wanataka kuendelea nao ni muundo gani wa Muungano wanaoutaka. 

Mheshimiwa Spika, 
Mapendekezo ya kurudishwa kwa Tanganyika na Serikali yake sio mapya. Miaka ishirini iliyopita, Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali) ilipendekeza hivyo hivyo. Miaka saba baadae, Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper Na. 1 ya 1998 (Tume ya Kisanga) nayo ilipendekeza hivyo hivyo. Kuendelea kupuuza mapendekezo haya wakati Zanzibar inavunja Katiba ya sasa ya Muungano; kuendelea kukaa kimya kwa hofu ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ wakati wao wanajitwalia uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe huku wakiendelea kushiriki katika maamuzi ya mambo ya Tanganyika yasiyokuwa ya Muungano; kuendeleza kile alichokiita Mwalimu Nyerere falsafa ya ‘changu ni changu, chako ni chetu’ katika mahusiano ya Zanzibar na Tanzania Bara, ni kutulazimisha tuipinge dhana nzima ya Muungano kati ya nchi zetu mbili kitu kinachoweza kupelekea kuvunjika kwa Muungano wenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni isingependa tufike huko lakini ndoa hii ya kulazimishana haiwezi ikadumu muda mrefu kwa taratibu za aina hii.

UDHOOFISHAJI WA UPINZANI

Mheshimiwa Spika, 
Mapendekezo ya Muswada juu ya uwakilishi katika Bunge la Katiba yana athari nyingine kubwa katika majadiliano na maamuzi ndani ya Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa G. Shivji kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, endapo mapendekezo ya ibara ya 20(2) ya Muswada yatapitishwa, CCM itakuwa na kati ya wajumbe 350 hadi 400 katika Bunge la Katiba ambalo lina wajumbe 545. Kwa upande mwingine Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina Wawakilishi 29 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kitakuwa na wajumbe 65 katika Bunge la Katiba. Kwa maana ya uwakilishi katika Bunge la Katiba, CUF itakuwa ndio chama cha pili kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge hilo, licha ya kuwa na wabunge wawili tu wa kuchaguliwa kwa upande wa Tanzania Bara na licha ya kupata kura chache sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. 

Na kama inavyojulikana, tangu Muafaka wa Kisiasa Zanzibar kati ya CCM na CUF wa mwaka 2010 na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, upinzani wa kisiasa Zanzibar umekufa na kwa upande wa Tanzania Bara, na hasa Bungeni na kwenye chaguzi ndogo kama ule wa Igunga, CUF imekuwa ikishirikiana na CCM kuipinga CHADEMA. Kwa mapendekezo haya, kambi ya CCM na CUF katika Bunge la Katiba inaweza kufika hata zaidi ya wajumbe 465 katika ya wajumbe 545 wa Bunge hilo! CHADEMA ambayo kwa sasa ndio chama kinachoongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, itabakia na Wabunge wake 48 na vyama vya kibunge vilivyobaki, yaani NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vitabaki na jumla ya Wabunge sita. Kwa hiyo, CHADEMA itakuwa chama cha tatu kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge la Katiba licha ya kuwa ni chama kikuu cha upinzani chenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini! 

Kwa maana nyingine, iwe ni kwa makusudi au bila ya kujua au kwa kunuia, athari mojawapo kubwa ya mapendekezo ya Muswada kuhusu uwakilishi katika Bunge la Katiba itakuwa ni kuiongezea nguvu zaidi kambi ya CCM/CUF na kupunguza nguvu na ushawishi wa CHADEMA ambayo ndio chama pekee kinachobeba matarajio na matamanio ya Watanzania wengi wanaotaka mabadiliko ya kimsingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Haihitaji kuwa na shahada ya uzamivu kujua kwamba Bunge la Katiba lenye uwakilishi wa aina hii litapitisha Katiba Mpya ambayo pengine itatofautiana na Katiba ya sasa kwa jina tu! Na wala haihitaji kisomo kikubwa kujua kwamba Bunge la Katiba la aina hii halitagusa ‘msingi mkuu’ uliobaki wa Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali mbili. Hapa pia ni wazi kuwa lengo halisi la mapendekezo haya ni kuhakikisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya utazaa matunda yasiyokuwa tofauti sana na ya Katiba ya sasa!

‘UWAKILISHI’ WA BUNGE LA KATIBA 

Mheshimiwa Spika,
Sio Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wala Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye mamlaka kikatiba na kisiasa ya kutunga Katiba Mpya ya Tanzania. Hii ni kwa sababu sisi wote tulioko humu ndani tulichaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa na mamlaka yetu yote yako ndani ya kona nne za Katiba hiyo. Kama ni kweli, kama anavyodai Profesa Kabudi, kwamba kitendo cha kutunga Katiba Mpya vile vile ni kitendo cha kuua Katiba ya Zamani, basi sisi Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar hatuna mamlaka ya kuiua Katiba ya sasa kwa sababu sisi wote tulikula kiapo cha kuilinda, kuihifandhi na kuitetea. 

Pili, sisi sote ni Wabunge na Wawakilishi wa vyama vya siasa kwa sababu, kwa mujibu wa Katiba ya sasa sheria zote husika, tumechaguliwa kwa sifa kuu ya kuwa wanachama wa, na tuliopendekezwa na, vyama vya siasa. Kuligeuza Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa Bunge la Katiba ni sawa na kusema kwamba wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa hawana haki ya kushiriki katika kutunga Katiba Mpya kwa sababu ya kuwa na kilema cha kisheria kinachowakataza kuchaguliwa kuwa Wabunge na Wawakilishi! Ibara ya 20(4) ya Katiba ya sasa inatamka wazi kwamba “... ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote....” Sio kosa, kwa hiyo, kwa mamilioni ya Watanzania ambao wameamua kwa hiari zao kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani, na haiwezi kukubali, ubaguzi wa aina hii dhidi ya Watanzania walioamua kutumia haki zao za kikatiba ya kutokujiunga na chama chochote cha siasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitakubali Watanzania hao waadhibiwe kwa kunyimwa kushiriki katika Bunge la Katiba kwa sababu tu ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Tatu, wajumbe 116 wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais. Pili, Bunge la Katiba ni chombo cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi na kwa mila na desturi zinazokubalika na kutumika kimataifa, wajumbe wa Bunge la Katiba huchaguliwa moja kwa moja na wananchi bila ya kujali vyama vya siasa na huwa na kazi moja tu: kutunga Katiba Mpya. Kwa sababu zote hizi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wajumbe wa Bunge la Katiba wachaguliwe moja kwa moja na wananchi na kusiwe na masharti yoyote kuhusu uanachama wa vyama vya siasa.

UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA

Mheshimiwa Spika, 
Muswada una mapendekezo ambayo yanaashiria kuachana na utaratibu wa kihistoria wa utungaji wa Katiba ambao umewaweka wananchi kando katika michakato wa kikatiba tangu miaka ya mwanzo ya uhuru. Kwa mujibu wa ibara ya 27(1), kutakuwa na kura ya maoni kwa lengo la kuihalalisha Katiba Mpya. Kwa mujibu wa ibara ya 30, watu wote walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, watakuwa na haki ya kupiga kura katika kura hiyo ya maoni. Aidha, kufuatana na ibara ya 32(2), matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa zaidi ya 50% ya kura zote zilizopigwa Tanzania Bara na kiasi hicho hicho kwa Zanzibar. 

Mapendekezo ya ushirikishwaji wa wananchi katika kuipa Katiba uhai wa kisheria ni jambo la maana sana na linaonyesha kuwa tumeanza kuachana na urithi wa kikatiba wa kikoloni ulioanza na Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961. Hata hivyo, mapendekezo haya yamejaa mitego na vichaka vingi vya hatari. Kwanza, ibara ya 27 inapendekeza kwamba kura ya maoni itaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili – kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar - ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni. (ibara ya 28(1) na (2) Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 31, utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika chaguzi za kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, 
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli yake ndani ya Bunge hili wakati wa kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 24 Agosti, 2011: “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani, sio tu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bali pia na mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi unaoendesha chaguzi za nchi yetu. Mfumo huu na watendaji wake wameonyesha wazi kutokuwa huru na kutumiwa na Chama cha Mapinduzi kuchakachua matokeo ya chaguzi mbali mbali hapa nchini. Kwa maana hiyo, Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na ile ya Zanzibar, haiwezi kuachiwa jukumu kubwa la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali ilete bungeni muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba na ya sheria husika za uchaguzi kwa lengo la kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha inasimamia zoezi la kura ya maoni kwa uhuru na bila upendeleo kwa chama tawala.” 

Kuna maeneo mengine ambayo nayo yanaonyesha kwamba lengo halisi la Muswada huu ni kupata Katiba ambayo haitabadilisha mambo ya msingi ila itakuwa mpya kwa jina tu. Kwanza, ibara ya 26(2) inapendekeza kumpa Rais mamlaka ya “kuliitisha tena Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale siku zijazo kwa ajili ya kutunga masharti ya katiba kabla ya kuizindua Katiba inayopendekezwa kwa lengo la kurekebisha masharti yaliyomo kwenye Katiba iliyopendekezwa.” Maana halisi ya maneno haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama chake hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na wananchi! Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya kupingana na kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba. 

Pili, wakati ibara ya 32(3) inapendekeza kurudiwa kwa kura ya maoni endapo kura za ‘NDIYO’ na ‘HAPANA’ zitalingana, ibara ya 32(4) inaelekeza kwamba “endapo wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘HAPANA’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.” Endapo pendekezo hili litapitishwa na kuwa sheria, hii itakuwa ni kualika maasi kwa vile, kwa vyovyote vile, wananchi wa Tanzania – baada ya kupitia mchakato mrefu wa kutengeneza Katiba Mpya – hawatakubali tena kuvishwa minyororo ya Katiba ya sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba badala ya kurudi kwenye status quo ante kama inavyopendekezwa, mchakato wa Katiba Mpya uanze tena hadi hapo utakapopatikana muafaka wa kitaifa wa katiba. 

HITIMISHO 

Mheshimiwa Spika, 
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 ni Muswada muhimu kuliko pengine miswada yote ambayo Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili na kuipitisha. Ni muswada wa kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na tangu Muungano miaka karibu arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi kupata fursa ya kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa utaratibu kama unaopendekezwa katika Muswada huu. Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo Muswada huu ulivyoandaliwa na kwa maudhui yake na kwa jinsi ulivyoletwa Bungeni kwa kukiuka makusudi Kanuni za Bunge, ni wazi – kama utapitishwa jinsi ulivyo – Watanzania tutakuwa tumekosa fursa ya kuamua mustakbala wa taifa letu kwa njia ya amani na maridhiano. 



Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo Bunge hili tukufu litaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali sana. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa kama yanayopendekezwa na Muswada huu bila kwanza wananchi wa Tanzania na Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote kwa uzito unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara. 

Kwa sababu hizi zote, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja chini ya kanuni ya 86(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili tukufu kwamba Bunge hili likatae Muswada huu Kusomwa Mara ya Pili kwa sababu Serikali imeleta Muswada Mpya na wenye mabadiliko makubwa na ya msingi bila kufuata masharti ya kanuni ya 84(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge; na pia kwa sababu Serikali haijatekeleza maagizo ya Bunge hili tukufu kuhusu kutoa muda zaidi kwa Kamati na wananchi kuufikiria, kuuelewa na kuutolea maoni Muswada huu kinyume na matakwa ya ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano juu ya uhuru wa wananchi kutoa maoni yao; ibara ya 21(1) na (2) juu ya haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan chi, na haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayowahusu wananchi, maisha yao au yanayolihusu Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI& WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA