Friday, January 27, 2012

SALAAM Kutoka Davos, Uswiss!

Salaam ndugu zangu Waafrika. Mimi ni rais wa nchi mojawapo maskini barani Afrika – Jamuhuri ya Muungano wa Gambia, huko Afrika Magharibi. Kwa sasa nipo hapa Davos, Uswiss kuhudhuria mkutano wa mwaka – ambao kimsingi ni wa Nchi na Makampuni tajiri duniani. Nchi yangu ni maskini na inaishi kwa kutegemea misaada kwa zaidi ya 40% ya mahitaji yake kila mwaka – hivyo naamini wengi wenu mnashangaa nimefuata nini huku.

Ukweli ni kwamba Davos ni pazuri jama – tuache utani. Kuna hoteli kali sijawahi ona, pamoja na kuwa na baridi kali na barafu imefunika mji,  lakini uzuri sisi viongozi tunapita kwenye barabara ambazo zimesafishwa, magari yetu yana heater na muda wote tunakaa mahali penye joto – barafu tunaiangalia kwenye TV tu kama nyie mlioko huko kwenye joto.

Hakuna foleni kama huko mliko nyie, na hapa sina cha msafara wala nini, sitanguliwi na ving’ora wala Polisi maana hata Rais wa hapa hajui kama nimekuja. Niliomba viza ya mtalii maana ningeomba viza kama Rais wangenikatia kwa sababu siko kwenye ratiba yoyote wala sijaalikwa. NInatumia kigari fulani cha kukodi walichonikodia CIA wa nchini kwangu, hamuwezi amini hiki ki gali nakilipia dola 5,000 kwa siku kukikodi - ila kizuri kusema ukweli.

Kwa sababu natokea nchi maskini, kimsingi sihitajiki wala sihitajiwi na mtu yeyote mimi kuwepo hapa – infact kuna hata baadhi ya viongozi waliopo hapa hawajui kama mimi na marais wenzagu wa Afrika tumekuja pia – mmoja nilimsikia jana akijishangaa tumekuja kufanya nini? Mzungu haelewi kinachotuketa sisi.

Ratiba yangu
Kwa sasa ninapo watumia hizi salaam nimekaa kwenye restaurant moja hapa karibu na mlango wa kutokea kwenye ukumbi wa mkutano walimo kina Obama. Nimemaliza kunywa chai na mapochopocho mengine. Niko na marafiki zangu marais wengine kutoka Afrika. Tunakaa hapa mlangoni ili kusubiri wanaohusika na huu mkutano wakimaliza tuwaombe kupiga nao picha.

Idadi ya Marais kutoka Afrika tulioko hapa ni wengi kuliko wale tunaohudhuriaga mkutano wa Umoja wa Afrika. Mi nashauri mkutano wa AU tuwe tunaufanyia huku huku Davos, tutapata washiriki wengi zaidi kuliko kuufanyia Uganda.

Picha hizi kama mnavyojua huwa zinatusaidia sana kuuzia sura huko Afrika tunapozisambaza kwenye mitandao Kama Facebook. Na hata kwenye kampeni huwa zinatusaidia kuonesha kwamba na sisi tunafahamiana na viongozi maarufu.

Kuuza Sura CNN
Jambo lingine la muhimu ambalo mimi binafsi na wenzangu wa Afrika huwa linatuvutia sana kuzamia mikutano kama hii (tunazamia kwa sababu sisi ambao kwetu Afrika tunaitwa viongozi huwa hatualikwi kwa maana wanaogopa tutakuja kuwaomba-omba misaada) huwa ni kupata nafasi ya kuonekana kwenye vyombo vikubwa vya habari kama CNN, Al-jazeera, BBC, CCTV, RT, Sky News, Fox News n.k.

Kwa kawaida vyombo hivi huwa haviwezi kuja hata nchini kwangu kunihoji nikiwa Ikulu, japo nilishawaalika mara nyingi, nikawaahidi kuwapa vyumba vya kulala pale pale ikulu na kuwalipa Allowance kama ya mimi Rais lakini walisema sina jambo la maana la kuwaambia – jama huwa wananidharau sana.

Lakini nikiwepo hapa, huwa wanaweza kunionesha – hata kama ni kwa bahati mbaya – nikiwa nasalimia na mtu kama Bill Gates, Obama, Sarcozy, M-Kameron n.k. Kuna wakati pia mida kama hii tunapokunywa chai kwa sababu waandishi hawa wanakuwa hawana kazi – wakisubiri mkutano uishe ili wapewe tamko la mkutano – huwa wanaweza kutuhoji kimtindo wakati wanapoteza-poteza muda kusubiri habari zenyewe.

Mwaka juzi nakumbuka niliwahi kuhojiwa hivi-hivi kwa bahati mbaya huko Ufaransa nikachapia kwamba sijui kwa nini Nchi yangu ni maskini. Ilikuwa soo kishenzi huko nyumbani Gambia, lakini niliporudi nikasambaza picha zangu nilizopiga na Bill Gates, Sarcozy na 50 Cent zikasaidia kupoteza soo nzima. 

Nikawaambia pia 50 Cent amesema atakuja kuwekeza Gambia wananchi wakufurahi kishenzi na ile soo ikaisha. 50 Cent kumbe hata namba yangu ya simu hakui-save, nilimpigia siku nyingine akapokea Secretary wake, alipomuuliza kama anamjua rais wa Gambia akakana kujua hata kama hiyo nchi ipo duniani!

Nasikia jirani zangu Senegal wameondolewa kwenye michuano ya Afrika, huku mechi za Afrika wala hawajui kama zipo – hivyo hazioneshwi. 

Gambia nasikia madktari nao wameamua kugoma. Jana shemeji yangu alinipigia simu kaniambia madaktari wamegoma na wagonjwa wanazidi kufa. Mke wake alikuwa ana upele nimeagiza Wizara ya Afya impele India akachekiwe afya yake. Kusema kweli mimi siwaelewi hao Madaktari, na ninaamini lengo lao tu niahirishe safari yangu na mishe mishe zangu Ulaya ili kuja kuwasikiliza.

Kwa taarifa yenu madaktari SIRUDI hadi nimalize ratiba zangu, nikitoka hapa natembelea nchi nyingine za Ulaya kwa ajili ya “kuimarisha mahusiano” halafu ndo narudi Bongo. Nawaahidi nikifika kabla hamjamaliza mgomo wenu nitaunda tume kuchunguza chanzo cha mgomo wenu na itanipa maepndekezo ya nini cha kufanya….

Ninamengi ya kuwaelezea ila naona mwandishi wa CNN anakuja kuelekea nilipokaa nadhani anataka kunifanyia intavyuu, ngoja nikae mkao wa kuhojiwa, nitaendelea kesho…. Ila kwa ufupi huku maisha matamu, Allowance inatumika vilivyo, ila kwa jinsi maisha yalivyo ghali, nadhani inabidi ofisi iniandalia Bonus ili kujazia pesa zangu nilizotumia…. 

NITARUDI kwetu Gambia mwezi ujao, Niombeeni Rais niendelee kuwa na Afya huku Ughaibuni!

Friday, January 20, 2012

USALAMA: Tanzania Hatarini Zaidi Kuvamiwa!


Katika hotuba za bungeni za kila mwaka za Waziri wa Ulinza na zile za Waziri wa Mambo ya ndani huwa zimejaa maelezo mengi ambayo hulenga kuwapa uhakika wananchi kuwa nchi yao iko salama, mipaka yake inalindwa na wananchi waishi kwa amani na salama bila wasi wasi wowote. Maelezo hayo hayo huwa yanatolewa mara nyingi sana pia na Waziri wa Utalii katika kuwavutia watalii na kuwahakikishia kuwa Tanzania ni eneo salama.

HALI SIO SALAMA
Hata hivyo, uchunguzi wangu binafsi umenibainishia kuwa Tanzania kama taifa tuko katika hali ya hatari sana kuweza kuvamiwa na magaidi au makundi mengine ya kihalifu yasiyo na nia nzuri na nchi yetu. Ukweli ni kwamba Tanzania haiko salama kama wanasiasa na viongozi wetu wanavyodai, na wala sidhani kama wananchi tuna sababu ya kuwa na "starehe" kama ambayo viongozi wetu hutuamisha tuwe nayo.

NINA USHAHIDI

Taarifa za Chama Tawala CCM
Wakati wa Uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka jana, kulikuwa na Taarifa mbili Nyeti sana za Kiusalama hapa Nchini. ZOTE zilitolewa na Chama Tawala - CCM.

Ya Kwanza, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Wilson Mukama alieleza kuwa Chama chake kina Taarifa na Ushahidi kuwa CHADEMA imeingiza Kikosi cha Makomandoo / Magaidi 33 kutoka nje ya nchi na tayari walikuwa wako Igunga na CCM ilifahamu mgawanyo wao katika Kata za huko Igunga ulikuwa kama ifuatavyo: Itobo (4), Burede (5), Isakamaliwa (9) Bukene (9) pamoja na Chamacholo (6).
Katibu Mkuu wa CCM alithibitisha Uwepo wa MAKOMANDOO
Kutoka Pakistani, Libya na Israel
 Katibu Mkuu wa CCM ambaye kabla ya kushika nafasi hiyo alishawahi kushika nafasi nyingine nyeti na za juu hapa nchini alieleza kuwa makomandoo hao walipata mafunzo ya ukomandoo katika nchi za za Libya, Israel na Pakstani.

Ya Pili, Kwamba CHADEMA kilikuwa kimeingiza Majangiri wa kundi la Mungiki (kundi linaloongoza kwa mauaji ya kikatili nchini Kenya) wapatao 40 na kuwafikisha Igunga. 

Akithibitisha taarifa hizo za Chama Tawala CCM, Mbunge wa Nzega (CCM), Hamis Kigwangalla ambaye naye kwa wakati huo alikuwa huko Igunga kwenye kampeni alisema kwenye mtandao mmoja kuwa "kuna Mkenya mmoja tumemkimbiza huku Choma, na sasa tunamuwinda mpaka tumkamate labda hapo tutaelewana! Mkakati gani huu wa kutuletea Mungiki Igunga jamani? Na sisi tuko sawa, tutawakamata na kuwapeleka polisi wenyewe kwa mikono yetu!"
Hamis Kigwangall, Mbunge wa Nzega CCM alithibitisha Uwepo
wa Mungiki Kutoka Kenya huko Igunga
 Ebu fikiria, "madaidi"  yanapenya kwenye mipaka ya Nchi na kuingia hadi katikati ya nchi kama Igunga ndipo Chama tawala kinayabaini. Wakati huo huo, kamanda wa Polisi huko Nzega alipoulizwa alisema yeye hajui kama kuna magaidi hao wakati Jemedari Mkuu wa Majeshi na mwenyekiti wa CCM anafahamu!

Wakati mtu akitafakari hizo taarifa na kujaribu kuziona kuwa na za kisiasa, ni muhimu kuzingatia kuwa mwenyekiti wa Chama hizcho kilichotoa hizo Taarifa ndiye Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiye Mkuu wa Majeshi na Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama wa Taifa. Siamini kwamba Rais anaweza akatoa Taarifa za UONGO kuhusiana na hali ya usalama wa Taifa kupitia Chama chake.

Taarifa za POLISI (1)
Mwezi wa kwanza nilikuwa Jijini mbeya kwa mapumziko ya mwisho/mwanzo wa mwaka ambapo nilipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba kuna Maiti za Wahamiaji Haramu zimeokotwa mkoani Morogoro. Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro alithibitisha kuwa maiti hizo zilikuwa ni za Wasomali walioingia nchini Bila Vyombo vya Ulinzi na Usalama mipakani kutambua, hadi walikamatwa Morogoro!

Katika taarifa iliyonishtua zaidi, kamanda huyo alisema kwa mwezi mmoja tu, Polisi Morogoro walikuwa wamekamata wahamiaji haramu 200 (mia mbili) kutoka Somalia ambao walipita katika Mipaka ya Tanzania ambayo tunahakikishiwa inalindwa salama na hadi wakafika Morogoro. [Kumbuka mkoa wa Morogoro uko katikati ya nchi na hivyo haupakani na nchi yoyote ya jirani. Maana yake ni kwamba Wahamiaji hao hupitia katika mipaka yetu na kuingia hadi ndani ya nchi].

Katika mahojiano na BBC, kamanda huyo wa Mkoa alionekana wazi kuvilaumu vikosi vya ulinzi vilivyoko mipakani kwa kutokujali kazi zao na kuruhusu wahamiaji haramu kuingia.

N.B: Ni muhimu kufahamu na kuzingatia kuwa Somalia ni eneo lililojawa na Magaidi na Maharamia kuliko maeneo mengine ya Afrika kutokana na kutokuwapo kwa Serikali imara kwa zaidi ya miongo miwili sana.

Taarifa za POLISI (2)
Katika juma hili hili nilikuwa naangalia TBC1 walipoonesha kuwa Mkoani Mbeya, wamekamatwa wahamiaji Haramu kutoa Ethiopia wakiwa kwenye nyumba ya mkazi wa Mbeya. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya alipoulizwa alisema kwa Mwaka 2010, jumla ya wahamiaji haramu wa namna hiyo (wanaotoka Ethiopia na Somalia) waliokamatwa mkoani Mbeya walikuwa 710. Mwaka 2011 walikuwa 450 (Jumla = Zaidi ya 1100 kwa miaka miwili tu).

Ni muhimu kufahamu na kuzingatia kuwa Wahamiaji hao huingilia katika mikoa ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga na huweza kupenya hadi kufikia Mbeya (wanai-cross nchi) wakiwa katika safari zao za kuelekea Afrika ya Kusini.

ULINZI NA USALAMA UKO WAPI?
Maswali ambayo yanaacha hali ya kuogopesha na kutia hofu kwa kila mtanzania anayebaini udhaifu huu mkubwa katika mipaka yetu ni kwamba iwapo wahamiaji hao haramu - ambao mara nyingi huwa katika safari zao tu za kuekea Afrika ya Kusini wanaweza kuingia kwa urahisi na kusafiri masafa marefu ndani ya nchi, je, ni kwa kiasi mtu mwingine yeyote anaweza akafanya hivyo hivyo?
Majeshi yetu hufahamika na kusifiwa sana kwa Uwezo wao
wa Kuwapiga Wanafunzi na Wananchi katika Maandamano ya Amani,
Kulinda Mipaka ya Nchi Je?
Iwapo hao wahamiaji wasio na mafunzo ya kijeshi, kigaidi au kijasusi (wakisaidiwa na mawakala wao) wanaweza kujipenyeza na kui-cross nchi kwa maelfu-elfu yao, Je, Ni nani tuliye naye hapa Tanzania anayeweza kuwazuia Magaidi au Majasusi wanaoweza kupanga kujipenyeza na kuingia hapa nchini kwa nia Mbaya?

Iwapo Magaidi yaliyopewa Mafunzo Libya, Israel na Pakistani yanaweza kuingia hadi kufika Igunga wakati wa Uchaguzi mdogo wa jimbo Moja, je ni magaidi mangapi yanaweza kuingia Tanzania na kuwawinda wagombeaji kama yatakavy wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge na Madiwani wa Nchi nzima?
Jeshi letu lina uwezo wa kufanya mambo mengi sana....
Hata kuvunja Tofali kadhaa kwa Ngumi Moja
Je, ni kweli kwamba amani na utulivu tulionao kwa sasa ni matokeo ya ulinzi "thabiti" wa mipaka yetu (kama tunavyoshawishiwa kuamini na wanasiasa wetu) au ni kwa sababu tu hakuna waovu ambao wameshakusudia kuingia kigaidi katika nchi yetu na "kutuliza"?

Je, mipaka yetu imeandaliwa kwa ajili ya ukagusi wa kina wa vyombo vya usafiri ambavyo mara nyingi ndivyo hupenyeza watu "kinyemela" kama wale wanaopakiwa kwenye chemba za mafuta kwenye malori makubwaya mafuta?

Binafsi nina mashaka na wasiwasi na hali ya Ulinzi na Usalama wa taifa letu, siamini kuwa usalama tulio nao ni matokeo ya ulinzi bora - zaidi tu kwamba "tunaishi hivi kwa neema ya Mungu" - sijui. Tuache kutiana moyo kisiasa wakati taarifa za kila siku zinaashiria hatuko salama, tuyakabili masuala kama yalivyo, tuyafanyie kazi kabla hatujaja kuumizwa ndipo tuanze kutafuta mchawi....

N.B: Makala isichukuliwe kama tangazo la hali ya hatariau dharura kwa taifa - maana hali hiyo huweza kutangazwa na taasisi husika tu.

Thursday, January 19, 2012

MBUNGE mwingine AFARIKI, Ni Wa Arumeru!


Aliyewahi kuwa naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa sasa wa Arumeru Mashariki, -CCM - Amefariki dunia Usiku wa Kuamkia leo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa. Marehem,u alikuwa anaumwa Kansa ya Kichwa/Ubongo.

Mbunge huyu amekuwa ni wa Pili kufariki ndani ya Wiki moja baada ya Marehemu Regia kufariki wiki iliyopita na kuzikwa Juzi kwao Ifakara, Morogoro.

Wednesday, January 18, 2012

MAREHEMU Regia: PICHA za KUAGA MWILI Wake, DSM na Ifakara!

Kutoka ulikohidhiwa Mwili...



Wageni mbalimbali waliwasili....

Mwili ukapelekwa eneo husika......


Viongozi wengi walikuwepo....



 Hotuba kutoka Chama na Serikali zikatolewa....


Ndipo tulianza kuaga.......



Mzee wa Vijisurufu tulikuwa naye.... nilipenda Pozi lake la Kumwangalizia makamu wa Rais....




Kule Ifakara Mwili Ulipokelewa na Mamia ya Watu waliojawa na Hisia za Uchungu.....





R.I.P REGIA



UDINI TANZANIA: Wanafunzi WAISLAMU Kuandamana Kesho Kutwa!



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
NDUGU WANAHABARI
Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mola wa viumbewote. Pili tuna kushukuruni kwa kuitikia wito wetu licha ya kuwa namajukumu mengi ya kutoa taarifa kwa wananchi.Kwa mara ya kwanza tumeamua kukutana nanyi. Nasi tunatoa taarifa yetu hii kwenu ilimuifikishe kwa Watanzania na wapenda amani wote duniani. Tunakuusienijuu ya ukweli na uaminifu katika kuripoti taarifa hii. Tuna kuusieni tena kuripoti taarifa hii bila ya kupotosha maana iliyokusudiwa.Kutakuwa na nafasi ya maswali ili kuuliza ikiwa kunasehemu ambayohaikueleweka.

NDUGU WANAHABARI
Tuliowaita ni viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi na Vijana wa KiislamuTanzania yaani Tanzania Muslim Students & Youth Association (TAMSYA).Jumuiya yetu inatambulika kisheria na inafanya kazi zake kwa kufuatasheria za nchi.

NDUGU WANAHABARI
Jumuiya yetu kama inavyojieleza inashughulika na malezi ya wanafunziwafuasi wa dini ya kiislamu waliopo katika shule, vyuo vya kati navyuo vikuu na vijana wa kiislamu kwa ujumla. Jumuiya hii inawalingania waishi kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Uislamu.

NDUGU WANAHABARI
Tumeamua kukutana nanyi ili kuzungumzia mambo ambayo yanawapatawanafunzi waislamu waliopo kwenye shule na vyuo vya serikali kwa mudamrefu. Wanafunzi waislamu wamekuwa wakinyanyaswa na kuwekewa vipingamizi vya makusudi ambavyo vinasababisha kufanya vibaya katikamasomo yao pindi wakiwapo shuleni.

NDUGU WANAHABARI
Sheria ya nchi inaruhusu uhuru wa kuabudu na kuchagua dini. Kwa mujibuwa dini yetu ya uislamu ibada haimaliziki kwa kuingia msikitini nakuswali tu bali Uislamu wenyewe ni mfumo kamili wa maisha. Ibada nikila jambo analolifanya muislamu na linaloridhiwa na Mwenyezi Mungulikiwa katika muundo wa vitendo au kauli za dhahiri na kificho.

NDUGU WANAHABARI
Tumepata malalamiko kutoka kwa wanafunzi waislamu wakikatazwa kuvaa HIJABU shuleni, Tumepata mashitaka kutoka kwa wanafunzi waislamu wakinyimwa sehemu zakusalia/kufanya ibada ya sala katika mazingira ya shule na vyuo.Tumepata mashitaka juu ya kupangwa makusudi matukio mbali mbali ya shule katika nyakati za sala za waislamu. Mfano sherehe za Mahafalizinapangwa kufanyika siku za Ijumaa muda wa sala, Ratiba za mitihanivyuo vikuu hazizingatii muda wa swala ya Ijumaa .kurefusha muda wa kusimama mstarini (Parade) mpaka muda wa swala unapita.Wanafunzi waislamu wamekuwa wakikatazwa kuvaa kofia au kanzu baada yamuda wa masomo katika shule za bweni huku wakristo wakiwa wanashinda na Rozari masaa 24. Waalimu wanaofundisha somo la maarifa ya uislamu wanawekewa vikwazo mbalimbali wakati wachungaji wanapishana katika shule bila vikwazo kwenda kufundisha baibal knowledge. Vipindi vya dini vinawekwa katika ratiba za shule muda wa saa saba mchana siku ya ijumaa wakati ambao wanafunzi wa kiislam wanapaswa kuenda msikitini kwa ajili ya swala ijumaa.

NDUGU WANAHABARI
Tutatoa mifano kadhaa katika maeneo tofauti ambayo wanafunzi waislamwamefanyiwa madhila, manyanyaso na udhalilishwaji ikiwa ni pamoja na kutukaniwa Mungu wao,mtume wao na kitabu chao (Quran tukufu) na TAMSYA imefuatilia bila ya mafanikio.

SHULE YA SEKONDARI KIZUNGUZI WILAYANI KILOSA –MOROGORO
Mwanafunzi wa kidato cha nne, Frank Thobias Cosmas, aliandika waraka ulioukashifu uislamu, Qurani tukufu na Mtume Muhammad Sallalahu alaihi wasallam.Wakati wanafunzi wakristo wakiwa wanaubandika katika mbao za matangazo shuleni hapo na kusambaziana waraka huo Tarehe 13/05/2011 mwanafunzi muislamu Saidi Suleiman aliupata na kuufikisha kwa viongozi wa wanafunzi waislamu na hatimaye malalamiko hayo yalifika kwa mkuu wa shule.Mkuu wa shule alimpa Adhabu Yule mwanafunzi aliye peleka taarifa na viongozi wa wanafunzi waislamu walisimamaishwa shule kwa muda wa siku 21, na Yule aliyendika waraka huo alibakishwa kufanya kazi za shule.Tukio hili liliripotiwa kwa Mkuu wa polisi Morogoro, Afisa Elimu Mkoa Morogoro na ofisi ya mkuu wa wilaya ambao walipuuza. Hatua hiyo ilisababisha waislamu wa Mkoa wa Morogoro kuandamana kwa amani siku ya Ijumaa tarehe 5 Agosti, 2011.

PIA SHULE YA SEKONDARI ULONGONI – DAR ES SALAAM
Siku ya Alhamisi,tarehe 27/01/2011Mkuu wa shule hiyo aliwalazimisha wanafunzi wa kike wa shule hiyo kuvua Hijabu wakati wa zoezi la kupiga picha kwa ajili ya Mtihani wa kidato cha nne.Alifanya hivyo kwa chuki za udini kwa sababu waraka wa baraza la mitihani unaotoa maelekezo ya namna na utaratibu wa kupiga picha kila mkuu wa shule amepatiwa na haukuagiza hivyo.

SHULE YA SEKONDARI ENGUSERO KIBAYA –KITETO
Mkuu wa shule hiyo kwa kushirikiana na Kaimu katibu Mkuu wa mkoa wa Manyara kwa barua yake ya Kumb.Na.FA.58/347/01/27 aliwaamrisha wanafunzi wavunje msikiti uliopo hapo shuleni kwa madai ya kwamba katika shule za serikali hairuhusiwi kujengwa nyumba ya ibaada. Lakini sikweli kwa kuwa zipo shule nyingi za serikali zilizo na nyumba za ibada makanisa tena makubwa sana. Mfano Shule ya sekondari Ndanda, Shule ya sekondari Umbwe, Lyamungo Sekondari, Pugu Sekondari Dar es salam na karibu shule zote kubwa za Serikali nchini. Huu ndio udini na mfumo kristo unaolalamikiwa na unaoliyumbisha taifa.

SHULE YA SEKONDARI ALDERSGATE BABATI MANYARA
Mkuu wa shule hiyo aliwanyima wanafunzi waislamu darasa kwa ajili ya kusomea somo la maarifa ya uislamu na kuwaambia kama wanataka kusoma somo la dini wachanganyike na wakristo ambao wamepewa chumba cha kusomea shuleni hapo, Jambo ambalo ni kinyume na sheria na kanuni za nchi.aidha alipiga marufuku uvaaji wa hijabu shuleni hapo kwa taarifa tuliyo letewa ya 17/03/2011.

SHULE YA SEKONDARI LUGOBA
Mwalimu aliwataka wanafunzi waislamu washerehekee Krismas walipokataa akawaambia tutaweka Taarabu maana waislamu mnapenda sana taarabu.Siku ya 21/01/2011 kwa makusudi Makamu Mkuu wa shule hiyo aliingia na viatu katika eneo la chumba wanachotumia waislamu kuswalia na kuwaamuru watoke katika chumba hicho wakati wa swala.Makamu Mkuu huyo alikwenda tena siku ya tarehe 31/01/2011 kwa hasira na kundi kubwa lililo sheheni wanafunzi wakristo kwa ajili ya kuwafanyia fujo waislamu waliokuwa wakiswali.  Jambo ambalo lileta tafrani kubwa shuleni hapo cha kusikitisha ni kuwa ukweli ulipotoshwa na hatimaye wanafunzi waislamu walionekana ndio chanzo cha tatizo.

SHULE YA SEKONDARI ILBORU ARUSHA
Mwanafunzi Juma Hassan alifukuzwa shule 13/01/ 2006 ikiwa ni wiki tatu kabla ya kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita. Sababu ya kufukuzwa shule ilidaiwa alimsukuma Mama Mkwizu mwalimu sheleni hapo alipotaka kuingia msikitini.

SHULE YA UFUNDI TANGA JIJINI TANGA
Mwaka 2006 Mkuu wa shule hiyo bwana T. Z. Kinala amekuwa na tabia ya Kutoa salamu ya HALELUYAH mstarini wakati wa PAREDI huku akijua kwamba wanafunzi walio mbele yake ni mchanganyiko wa waislamu,wakristo na watu wa dini nyingine.Lakini si hivyo tu, Tarehe 24/7/2006 mkuu wa shule alileta kikundi cha kwaya cha kanisa wakati PAREDI na kuimba nyimbo za ibada ya kikristo. Wakati alipo kuwa akiongea na wanafunzi wa, katika hafla fupi ya kuwakaribisha kidato cha tano mnamo tarehe 28/4/2006 Pia alitamka wazi wazi kuwaambia wanafunzi waislamu kuwa hapa shuleni hakuna kuswali swala tano kwani hii siyo seminari.Mnamo tarehe 18/06/2006 aliwaambia wanafunzi wa kiislamu wanaovaa mavazi yanayotambulisha uislamu wao, kama Kofia, Kanzu na Kilemba lau kama angeliwajua asingewachagua kujiunga na shule yake. Mnamo tarehe 02/08/2006 aliwaita waislamu wanaovaa mavazi ya kiislamu kama kanzu kuwa ni Mashoga.

NDUGU WANAHABARI CHUO KIKUU CHA DODOMA (UDOM)
Madhila haya na manyanyaso hayawasibu wanafunzi wa kiislam waliopo mashule tu lakini hata wale waliopo vyuo na vyuo vikuu pia hawajasalimika hapa tutatoa mfano wa chuo kimoja tu cha Dodoma (UDOM) ambako wanafunzi wa kiislam chuoni hapo wamekuwa wakidhalilishwa, kwa kutukaniwa dini yao na mtume wao mfano wa haya ni mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi wa serikali ya wanafunzi ambapo yalibandikwa matangazo yenye ujumbe unaowatukana na kukejeri uislam na waislam kuwa ni watu wasioweza na wasiostahiki kuongoza,jambo ambalo liliwafanya wanafunzi wakiislam chuoni hapo kuripoti katika uongozi wa chuo na vyombo vya usalama bila ya kupewa msada, hatimae waislam waliamua kujitowa katika mchakato huo wa kampeni na uchaguzi wakiwa na nia njema ya kujiepusha na uadui na uhasma baina yao na wanafunzi wa dini zingine, lakini hata hivyo baada ya uchaguzi walitukanwa na kukashifiwa wazi wazi na wakirsto wakishangilia kwa kusema Yesu ameshinda na Mohammad ameshindwa katika kona zote za chuo, bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria na mamlaka husika za chuo na serikali.

NDUGU WANAHABARI
Tukio kubwa na la kusikitisha kwa wakati huu ni hili la shule ya sekondari NDANDA iliyopo mkoa wa MTWARA wilaya ya Masasi tarafa ya Chikundi kata Mwena kijiji cha Ndanda. Mpaka hivi sasa tunapozungumza nanyi wanafunzi ishirini (20) wa kiislamu wamefukuzwa shule watano (5) wakiwa ni kidato cha tano na kumi na tano ni kidato cha sita ambao wanatarajiwa kufanya mtihani wa mwisho mwanzoni mwa mwezi wa pili.Aidha wengine waliosalimika kufukuzwa shule wamewekewa masharti magumu ya kusaini ikiwa wanataka kuendelea na shule hiyo ya serikali.Miongon mwa masharti hayo ni kutojihusisha na dini yao wakiwa shuleni sharti ambalo linapora haki ya kikatiba ya kuabudu.Sababu na kosa la kufukuzwa wanafunzi hao wa kiislam likiwa ni kuuomba uongozi wa shule uwape eneo maalumu la kufanyia ibada (Msikiti) kama vile walivyotengenezewa wanafunzi wakirsto kanisa kubwa shuleni hapo,kulalamika lugha za kashfa na dharau ambazo zinatolewa na mkuu wa shule dhidi ya wanafunzi wa kiislamu uislamu shuleni hapo.

Kilichowaponza wanafunzi waislamu ni kupinga udini wa mkuu wa shule na upendeleo kwa wanafunzi wakristo, mfano kitendo cha mkuu wa shule kuteua viongozi wa serikali ya wanafunzi kiholela na kiupendeleo kwa wakirsto huku wakitoka nje ya shule wakishangilia na kusema Muhammad ameshindwa katika uchaguzi mwache bwana Yesu atawale shule!!! Haya yamefanyika mkuu wa shule akiyaona bila ya hata kukemea na kuwaadabisha wanafunzi wahusika jambo ambalo linaonesha wazi wazi kuwa ni mpango maalum ulio sanifiwa kwa mfumo maalum.

NDUGU WANAHABARI
TAMSYA mikoa, wilaya na matawi, shule na vyuo kwa muda mrefu imefanya jitihada mbalimbali za kuonana na wakuu wa shule na watendaji husikaNkatika kadhia hizi na kuishia kupuuzwa bali na kupewa majibu ya kejeli na jeuri. Na baadhi ya wakuu wa shule kuomba msamaha na kuahidikutorudia tena, lakini baada ya muda mfupi hurejea na kuendeleza dhulma na madhila kwa wanafunzi wakiislam kwa kasi ya ajabu.

Pia walimu walezi wa wanafunzi wa kiislamu au hata walimu waislamu wanao thubutu kuhoji juu ya ubaguzi wa kidini pia huonekana vioja huku wakichekwa na hatimae kupewa adhabu ya kuhamishwa kituo cha kazi kiholela mfano dhahiri ni walimu wawili pekee wakiislam wa Ndanda Sekondari ambao wamefungashiwa virago vyao na kupelekwa vijiji vya mbali kosa lao likiwa ni kutaka haki itendeke baina ya wanafunzi wote,na wakati mwingine walimu waislam hujikuta wakiambulia vichapo na vipigo kama alivyofanyiwa mwalim Halima wa Ifunda sekondari pale alipopinga dhulma, uonevu na udhalilishwaji dhidi ya wanafunzi waislam shuleni hapo mwaka 2009 akajikuta anaambulia kipigo kutoka kwa mwalim wa kikristo.

NDUGU WANAHABARI
Hapa tumeonesha sehemu ndogo ya madhila yanayowasibu wanafunzi wa kiislam nchini kama mifano tu. kwani ni vigumu kueleza madhila ya kila shule au chuo kwa njia hii. Jambo la faraja ni kuwa kila mtanzania anajua haya hata watu wa kawaida pia Kwa kuwa tatizo hili ni la muda mrefu na baadhi ya viongozi wa serikali mfano Rais mstaafu wa awamu ya Tatu Mh. Benjamin Mkapa alipoulizwa juu ya hali ya uwiano wa waislamu na wasiokuwa waislam katika sekta ya elimu alikiri kuwepo matatizo na uduni kwa upande wa waislam na matatizo mengi huku akisema kuwa si kosa la serikali bali ni tatizo la kihistoria.

Sisi wanafunzi wa kiislam Tanzania tunasema wazi na tunao ushahidi kuwa hili si tatizo la kihistoria bali ni mpango maalum uliosanifiwa na serikali ya awamu ya kwanza kwa lengo la kuwadhulumu na kuwakandamiza waislam kielimu kwa mbinu mbalimali kama hizi zilizotumiwa na uongozi wa shule ya sekondari Ndanda na wanaharakati wengine wa mfumo kiristo katika sekta zote za elimu nchini.Wanafunzi wa kiislamu Tanzania tunajua kuwa kitendo kilichokifanywa na mkuu wa shule ya Ndanda na Bodi ya shule pamoja na maafisa elimu cha kuwafukuza shule wanafunzi ishirini (20) wa kiislam na wengine kuwekewa masharti magumu ya kuacha wito wa dini yao ili waruhusiwe kurudi shuleni si kitendo kipya bali ni muendelezo wa dhulma ambayo walifanyiwa babu na baba zetu ambapo walilazimishwa wachague aidha kuacha dini au kusoma, Alhamdul llah tunashukuru kwa kiasi Fulani walifanya maamuzi magumu ya kulazimika kuacha kusoma na kubaki na dini yao kwani kama wangechagua la pili basi huenda nasi leo tusingekuwa katika dini ya haki ya uislam. Ama leo hii sisi wanafunzi wa kiislamu Tunasema kusoma ni sehemu ya dini yetu kama tulivyoamrishwa na Allah (sw) Quran (96:1-5) kwa hiyo hatutokubali tena kuacha wito wa dini yetu kwa kutenganisha dini na elimu kwani ikiwa tutafanya hivyo basi itakuwa tumefanya dhulma kubwa kabisa. Hapa tunawapongeza wanafunzi wa kiislam wa Ndanda sekondari kwa kujitambua na kujua haki zao za kiiman na kikatiba kwa kutoutii uongozi wa kidhulma wa shule ya ndanda pale ulipowalazimisha kuacha wito wa dini yao ili wasome, wanafunzi wa Ndanda wamefanya jambo tukufu linalopaswa kuungwa mkono na kuigwa na kila mtu mwema. Na napenda kutoa wito kwa wanafunzi wakiislam nchini kote ya kuwa wanapaswa kuwaiga na kuungana na ndugu zao zao wa Ndanda sekondari kwa kutokubali dhulma ya namna yoyote ile.

NDUGU WANAHABARI
Kadhia ya Ndanda ni mzito sana ambayo imegusa hisia ya kila muislam na kila mtanzania mpenda amani na haki, ukweli wa hili unathibitika wazi wazi kwa kila mwenye uhuru wa kufikiri kwani vijana wale wa kidato cha sita waliofukuzwa ni nguvu kazi muhimu sana kwa ujenzi wa taifa ambao tayari kusoma kwao wangeweza kuiokomboa jamii na taifa kiujumla.Lakini jambo la kusikitisha ni kuona viongozi wenye dhamana katika wizara ya elimu wakilichukulia swala hili kisiasa kinyume na uhalisia wake. Kwa kufanya ziada na uchunguzi wa kubahatisha bila umakini hatimae kutoa taarifa zilizojaa usiasa ndani yake, kuwa eti maamuzi ya bodi ya kuwafukuza wanafunzi (20) wa kiislam ni sahihi huku akieleza kuwa amefika Mtwara na kuongea na Bodi ya shule, mkuu wa shule, walimu na serikali ya wanafunzi hatimae wanafunzi wote Paredi bila ya kuwaruhusu kuuliza maswali au kutoa maoni yao hatimae kutoa hukumu.Hukumu hii haiwezi kuwa sahihi kwani hajawashirikisha wahusika wa upande wa pili wa mgogoro ambao ni wanafunzi wa kiislam kwa kuwasikiliza hoja zao madai yao ya msingi, huku ni kuisaliti katiba ambayo wameapa kuilinda ambayo inarususu uhuru wa kutoa mawazo na kila mmoja kuheshimiwa kwa nafasi yake. Jambo zito zaidi ni kuona naibu waziri anaungana na watu madhalimu waliovunja katiba ya nchi kwa kuwalazimisha wanafunzi kuacha wito wa dini yao ili warudi shule sharti hili linavunja katiba Ibara ya (19:1-2) kinachozungumzia uhuru wa imani na kuabudu.Kutokana na uzito na unyeti wa kadhia hii na madhila haya yanayoendelea kufanywa dhidi ya wanafunzi wa kiislam nchini leo hii tunapenda tuutangazie uma kuwa sasa basi hatutaki kuendelea tena kudhulumiwa na kunyanyaswa, sisi ni watanzania na tuna haki zote kama wanajamii wengine.Kwahiyo tumeitaka serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kufanya mambo yafuatayo;

  •   Tunaitaka wizara ya elimu kuwarejesha wanafunzi wote walofukuzwa na wengine bila masharti yeyote ndani ya siku tano (5) kuanzia tarehe 13/01/2012.
  • Tunaitaka serikali kuunda Tume huru itakayo chunguza kero wanazopata wanafunzi waislamu katika shule za serikali nchi nzima.
  • Tunaitaka serikali kuwawajibisha watendaji wa sekta ya elimu wanaoendekeza udini ubaguzi na unyanyasaji kwa wanafunzi wa kiislamu.
  • Tunaitaka serikali ithibitishe au ikanushe juu ya madai ya mkuu wa shule Ndanda na badhi ya viongozi wa serikali kuwa mashule yaliyotaifishwa na serikali, serikali inamiliki majengo tu ama ardhi na mamlaka ya matumizi yake yako chini ya Taasisi zake za asili.
  • Shule zote za serikali zitenge maeneo malum ya kufanyia ibada kwa ajili ya watu wa dini zote.
  •  Asilimia kubwa ya wakuu washule za sekondari za serikali ni wakristo, hivyo basi tunaomba serikali iweke mgawanyo sawa wa nafasi hizo.


Kila jambo linapaswa kuwa na mwisho, hatuwezi kuendelelea kuvumilia uonevu wa wazi wazi siku zote.Hatuwezi tena kuendelea kuishi kama wanafunzi daraja la pili katika nchi yetu.Lazima haki sawa na uhuru upatikane kwa wanafunzi wa dini zote na sio kukandamiza waislamu. Hivyo basi tunalazimika kupaza sauti zetu kwaNkuingia barabarani kuonesha hisia zetu katika hali ya unyonge wetu

NDUGU WANAHABARI
Tunakusudia kufanya maandamano ya amani nchi nzima 20 Januari 2012 ambayo yatapeleka ujumbe kwa kila kiongozi wa Elimu katika mkoa yaani Afisa Elimu Mkoa na waislam wa Mkoa wa Dar es salaam watapeleka ujumbe moja kwa moja kwa waziri wa elimu.Kwa lengo la kutaka azingatie madai yetu ya kutonyanyaswa na kubaguliwa katika shule ya serikali.Lakini hatutoishia katika maandamano iwapo hali ya ubaguzi haitokoma. Tutatumia njia nyingine za kujikomboa katika madhila haya. Tunasema“tumenyanyaswa,tumedhaliliswa, tumebaguliwa kwa miaka 50 ya uhuru na tukavumilia na kusubiri vyakutosha leo tunasema inatosha na tumechoka tunaitaka serikali itambue haki,heshima na utu wetu kama wanavyoheshimiwa wanafunzi wa dini zingine mashuleni na mavyuoni.”Tunataka tuheshimiwe kama wanaadamu, kama wanatanzania huru, wanafunzi halali mashuleni na vyuoni kama wananyoheshimiwa wanafunzi wa dini zingine. Tumeanza muda mrefu kudai haki zetu kwa njia za kidiplomasia lakini hatujasikilizwa na leo tunatumia njia nyingine ya kidiplomasia na kikatiba ambayo ni MAANDAMANO ya amani huenda kwa njia hii serikali na jamii itasikia kilio chetu.

ACHENI KUTUDHALILISHA NA KUTUNYANYASA WANAFUNZI WA KIISLAM MASHULENI NA MAVYUONI SASA BASI INATOSHA TUNAOMBA WAISLAM WOTE NA WAPENDA AMANI WOTE MTUUNGE MKONO KATIKA MAANDAMANO HAYA YA AMANI.
Ahsanteni. JAFARI SAIDI MNEKE RAISI WA JUMUIYA YA WANAFUNZI NA VIJANA
WA KIISLAMU TANZANIA (TAMSYA)