Monday, August 15, 2011

MAFUTA Kupanda Bei Tena Wiki 2 Zijazo!



Niliposoma hii taarifa hapa chini nilijiuliza maswali mengi sana ikiwa ni pamoja na: 


  • Ni Nani anayewajibika kudhibiti kupanda na kushuka kwa thamani ya Shilingi?
  • Ile Stoke ya Mafuta iliyodaiwa na Ngeleja kwamba inaweza kudumu kwa Siku 60 imeisha lini, mbona Mafuta yamepanda ghafla?
  • Ina maana Serikali iliposema itapunguza bei ya Mafuta kwa mwaka huu wa fedha ILIKUWA INADANGANYA ili kuwezesha kupitishwa kwa bajeti yake? 
  • Hivi wanaofanya haya MAAMUZI YA KIPUMBAVU wanadhani kwamba Taifa hili limejawa na Watu wapumbavu tu?....
Maelezo na Visingizio vilivyotolewa na EWURA jana vinaonesha Wazi kuwa WIKI MBILI ZIJAZO Mafuta yatapanda bei tena, kwa sababu hakuna dalili zozote zinazoonesha kwamba Shilingi itapanda thamani wala kwamba mafuta yatashuka bei kwenye soko la dunia!

Taifa hili limebaki kama yatima!

Meneja Biashara wa Mamlaka ya Udhibiti wa

 Huduma za Nishati (EWURA)
Mhandisi Godwin Samweli 


SERIKALI YASEMA NI SABABU YA KUANGUKA KWA SHILINGI NA BEI KATIKA SOKO LA DUNIA 
Fidelis Butahe
SIKU kumi na moja baada ya kutangaza kushusha bei ya mafuta nchini, hatua ambayo ilisababisha mgogoro mkubwa uliotishia uchumi wa nchi, jana Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeongeza tena bei ya nishati hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Meneja Biashara wa Ewura, Godwin Samwel alisema petroli imepanda kwa Sh 100.34 sawa na asilimia 5.51, dizeli kwa Sh 120.47 sawa na asilimia 6.30 na mafuta ya taa kwa Sh 100.87 sawa na asilimia 5.30 na kwamba bei hizo zitaanza kutumika kuanzia leo.

Alisema bei hizo mpya zimetokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, ikilinganishwa na Dola ya Marekani.

Hatua hiyo ya Ewura imekuja siku moja baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12.

Agosti 3, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alitangaza bei elekezi iliyoshusha bei ya nishati hiyo ili kumpunguzia makali mwananchi wa kawaida na kusema kwamba petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita sawa na asimilia 9.17, dizeli Sh173.49 sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa kwa Sh 181.37, sawa na asilimia 8.70.....
Soma hii habari ya Mwananchi kwa ukamilifu kupitia http://www.mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/14505-serikali-yapandisha-tena-bei-ya-mafuta.html

Friday, August 12, 2011

Shy-Rose Bhanji
"Dear Mr. President HE Jakaya Kikwete: In 2005 we gave you a victory of over 80% because we had high expectations of your performance.


By 2010 your popularity had slipped to just over 60% and it seems your popularity is taking a further deep due to various reasons including vacuum on the leadership direction... as a CCM cadre and a passionate citizen, I feel a sense of big letdown after some seven years of your leadership.


What answers do you offer in order to put to rest your peoples outcries?." Shy-Rose Bhanji, (FACEBOOK), August 12th 2011.

BUNGE: Tamako la MNYIKA dhidi NAIBU SPIKA


Leo tarehe 11 Agosti 2011 katika kikao cha 48 cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi nilitaka kuomba muongozo wa Spika kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la 2007 ) kifungu cha 68 (7) kuhusu maswali na majibu ya Waziri Mkuu na nikarejea pia kanuni ya 133 (1).

Hata hivyo, kabla hata ya kutoa maelezo kamili ya kuomba muongozo wa Spika nilizuiwa na Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai (Mb) bila hata ya kusikilizwa muongozo ambao nilitaka kuomba kinyume na kanuni ya 5 (1) inayotaka Spika kuongoza Bunge kwa kuzingatia kanuni na pale ambapo kanuni hazijatoa muongozo Spika anapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali na desturi za kibunge.

Naomba kutoa taarifa kwa umma kwamba sijaridhika na uamuzi uliofanywa na Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai hivyo nawajulisha kwamba ninakusudia kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu 5 (4) na 7 (3) mara baada ya kupata nakala ya kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) ya kikao husika.

Mara baada ya kunukuu kanuni husika nilipoanza tu kuzungumza kwamba katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekuwa akitoa majibu yenye upotoshaji yasiyokuwa ya kweli; baada ya kauli hiyo kabla hata ya kumaliza maelezo niweze kuomba muongozo kwa Spika; Naibu Spika alinikatisha na kuninyima fursa ya kuomba muongozo kinyume na kifungu 68 (7) na 5 (1).

Naomba umma uelewe kwamba nilikuwa naelewa kwa kina mahitaji ya kanuni za bunge kifungu cha 133 na vipengele vyake kuanzia cha kwanza mpaka cha sita; ndio maana katika kuanza kuomba muongozo nikasoma kifungu cha 133(1).

Napenda umma ufahamu kwamba muongozo ambao nilitaka kuomba kwa Spika ni kwamba kumekuwa na kawaida ya Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoa maelezo yasiyokuwa ya kweli yenye upotoshaji ambayo ni kinyume cha katiba ya nchi, sheria mbalimbali pamoja na kanuni ikiwemo kanuni za bunge hivyo nilitaka Spika atoe muongozo wenye kumpa nafasi nyingine Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi wa kweli kuhusu masuala husika ili kuepusha uwezekano wa wabunge kupoteza imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu cha 133.

Katika maelezo yangu ya kuomba muongozo huo nilikusudia kutaja mifano miwili mikubwa ya majibu ya Waziri Mkuu kwenye maswali ya papo kwa papo yasiyokuwa ya kweli yenye upotoshaji kuhusu kashfa ya Meremeta na kuhusu mgogoro katika Manispaa ya Arusha.

Ikumbukwe kwamba tarehe 14 Aprili 2011 wakati wa kikao cha saba cha mkutano wa tatu wa Bunge la Tanzania wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, nilimuuliza Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa “Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye vile vile ni Mwenyekiti wa CCM amenukuliwa akizungumzia kuhusu haja ya Chama kinachotawala kujivua gamba. Kati ya mambo aliyoyazungumza ni pamoja na kuondokana na watuhumiwa wa ufisadi.  

Mheshimiwa Mkuu uliwahi kulieleza  Bunge hili tukufu kwamba usingetaka kabisa kuzungumzia masuala ya Meremeta kwa sababu ni siri za Jeshi. Baada ya kauli hii ya Rais na dhamira hii ya kujivua gamba kuhusiana na masuala ya ufisadi. Je, uko tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu kutaja wahusika wa Kampuni ya Meremeta na kuelekeza Serikali kuchukua hatua zinazostahili kuhusiana na tuhuma hizo? . Waziri Mkuu katika majibu yake Mheshimiwa Mizengo Pinda hakuitumia nafasi hiyo kurekebisha kauli zake zisizokuwa za kweli zenye upotoshaji alizozitoa kwa nyakati mbalimbali katika Bunge la Tisa kuhusu kashfa ya Meremeta.

Ikumbukwe pia kwamba tarehe 10 Februari 2011 katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la kumi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa papo ya Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb) kuhusu matukio yaliyojitokeza Arusha wakati na baada ya uchaguzi batili wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha. 

Tarehe 11 Agosti 2011 katika kipindi cha Maswali ya papo kwa papo ya Waziri Mkuu kuliulizwa maswali kuhusu maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA ya tarehe 6 na 7 Agosti 2011 kwa kurejea pia mazungumzo baina ya Waziri Mkuu na viongozi wa taifa CHADEMA kuhusu muafaka batili juu ya mgogoro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na uamuzi wa kuwafukuza uanachama madiwani watano kutokana na kukiuka maagizo ya kamati kuu. 

Badala ya Waziri Mkuu kuitumia nafasi hiyo kutoa majibu yenye kulenga kutoa ufafanuzi wa kurekebisha upotoshaji uliofanyika awali Waziri Mkuu Mizengo Pinda akatoa majibu mengine yasiyokuwa ya kweli kuhusu mazungumzo yake na viongozi wa CHADEMA pamoja na uamuzi wa chama wa kuwafukuza uanachama madiwani waliokiuka maamuzi ya kamati kuu ya chama.

Majibu ya Waziri Mkuu kuhusu ufisadi wa Meremeta, matukio katika halmashauri ya Jiji la Arusha na masuala mengine ya kitaifa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo yenye uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu yaliyoanishwa katika ibara ya 52 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yana mwelekeo wa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sheria nyingine za nchi yetu pamoja na misingi muhimu ya utawala bora kama ambavyo nitafafanua katika hatua zinazofuata. 

Naomba umma upuuze upotoshaji uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai kuhusu muongozo nilioomba mpaka pale maamuzi yatakapofanywa na Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mujibu wa kifungu 5(5) na Bunge kujulishwa.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
11/08/2011

Wednesday, August 10, 2011

KIKWETE: Rais Mwanafunzi au Rais Mtendaji?



Labda hata 'wenzetu' wanamuona ni Mwanafunzi Zaidi
(Discalimer: Uandishi wa Makala Hii haukulenga kwa namna yoyote kuvunja sheria au katiba ya Nchi au chombo kingine chochote halali nchini. Kama mojawapo ya hayo limetokea, sio kwa makusudi, na linaombewa msamaha tangu mwanzo).

Wakati nilipoenda field nikiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, nilipokelewa na Bw. Andrew Mushi katika Shirika la TANGO (Tanzania Association of NGOs) (kwa sasa ni mwanabidii pia). Ukweli ni kwamba siku za mwanzo za kuwepo kwangu zilikuwa ngumu kidogo, kutokana na ukweli kwamba nilikuwa sijawahi kuwa na uzoefu wowote wa kufanya kazi katika ofisi.

Moja ya changamoto ambazo nilikabiliana nazo ilikuwa ni kutokuelewa kitu chochote ambacho nilitakiwa kukifanya au kile ambacho kila mtu ofisini alitarajia nikifanye katika nafasi niliyokuwa nayo. Kutokujua huko kulinifanya nitumie muda mwingi kujisomea vitabu, taarifa na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kujiongezea ufahamu – hata wakati nilipokuwa natakiwa katika kutekeleza majukumu yangu kwa vitendo, nilijikuta nikitumia muda mwingi kusoma!

Hali hii iliendelea hadi siku Ndg. Mushi alipoiniambia: “We umekuja hapa Kusoma au Kufanya Kazi? Kama bado hujajua cha kufanya rudi shule ukasome, ukishajua unachotakiwa kukifanya ndipo uje ufanye kazi!” Maneno yale yalikuwa mazito sana kwangu, na sijayasahau na sitayasahau katika muda wote nifanyapo kazi!

Hivi karibuni, katika kufuatilia matangazo ya TBC1, nilikutana na kipindi cha “Makala yangu”. Katika makala ile, mtangazaji alikuwa akielezea taarifa mbalimbali kuhusiana na safari ya Rais Jakaya Kikwete kwenye nchi moja ya visiwani, hapa hapa Afrika. Moja ya mambo niliyoya-note yaliyokuwa yakijitokeza mara nyingi katika majibu aliyokuwa akiyatoa Kikwete kwenye mahojiano aliyoyafanya, alikuwa akisisitiza muda wote kwamba amejifunza mambo mengi, na atawatuma wataalam wa kitanzania kwenda kujifunza zaidi huko!

Nimejifunza… Nimejifunza… nimejifunza… Yalikuwa ni maneno yaliyokuwa yanajirudia mara nyingi sana, yakiambatana na msisitizo wa kutumwa kwa wataalam wa kitanzania kwenda “kujifunza”… Nikayakumbuka tena maneno ya ndugu Mushi wa TANGO, “kama bado unataka kujifunza Rudi Shule, ukishaelewa cha kufanya, Njoo Ufanye kazi”.

Nikajiuliza, hivi kwa taifa lililobado nyuma sana kimaendeleo kama Tanzania, linahitaji kuwa na Rais “anayejifunza” au anyefanya kazi? Je, taifa kama hili linahitaji kuwa na wataalamu wanazunguka duniani “kujifunza” au ni kuwa na wataalam wanaofanya kazi?
Hapa akiwa anaendelea "kujifunza" kwa kusoma kitabu,
huku kushoto kwake Waziri wa Nishati Ngeleja
akiwa ANACHAPA LEPE LA USINGIZI!

Hoja yangu inatokana na ukweli kwamba Tanzania ni mojawapo ya mataifa duniani ambayo yanasifiwa kwa kuwa na sera, sheria na mipango mingi mizuri sana – ikilinganishwa na mataifa mengi sana ya kiafrika na hata duniani kwa ujumla miongoni mwa nchi maskini na zinazoendela. Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika masuala mengi ya kisera na mipango hata na kuyapita baadhi ya mataifa yaliyoendelea kuliko Tanzania. Mipango kama Dira ya 2025, MKUKUTA, MKURABITA, Programu za Maboresho za Kisekta kama ASDP, LSRP, WSDP, ESDP n.k. ni moja ya mipango bora kabisa kuwahi kupatikana katika mataifa maskini.

Pamoja na mipango hiyo mizuri na sera, bado taifa letu ni moja ya mataifa yenye raia maskini kabisa duniani! Changamoto kubwa ambayo, pamoja na mambo mengine, imechangia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha huu umaskini hapa nchini, ni taifa kutokuwa na watu wanaoweza kusimamia utekelezaji wa sera na mipango na kuhakikisha kuwa matokeo na shabaha zote za malengo na mipango hiyo vinafikiwa.

Taifa kama hili, katika hali hii tuliyonayo, linahitaji kwa kiasi kikubwa sana kuwa na watu wenye uwezo wa kiufundi na kiutaalam wa kuweza kuliongoza taifa katika utekelezaji wa mipango na sera iliyopo. SIO WATU WANAOSHIKA MADARAKA ILI WAJIFUNZE! Uzuri wa sera, mipango na programu za taifa hautakuwa na manufaa yoyote kwa taifa na raia wake ikiwa haitatekelezwa. Mipango yetu mizuri haitatekelezwa na WANAFUNZI bali WATENDAJI!

Swali la msingi la kujiuliza kwa hapa Tanzania ni Je, taifa hili linaowataalam wanaoweza kuliongoza taifa kwenye kutekeleza mipango iliyopo, au wataalam tulionao bado ni wale wanaohitaji kukaa na kusoma vitabu maofisini au kwa kufanya ziara za kujifunza? Je, wataalam walio kwenye nafasi mbali mbali za utendaji hapa nchini, kama Rais, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi n.k. ni watu wenye uwezo wa kutenda kile wanachotakiwa kukitenda au ni watu ambao hawana hata uwezo wa kufanya hayo madogo yanayotakiwa kulitoa taifa “maskini” kama Tanzania hapa lilipo na kulipeleka hatua nyingine?

Makusudi ya tafakari yangu hii ya leo SIO kueleza kwamba mtu akishakuwa na nafasi ya uongozi/utendaji hatakiwi kuhitaji kujifunza, HAPANA. Ninachopenda kieleweke hapa ni kwamba kila mtu anayepewa nafasi fulani ya uongozi/utendaji anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya kazi za msingi katika nafsi hiyo.

Hutomlaumu kwa kutozunguka duniani na kukutana
na watu tofauti (wengine sijui hata kama wana TIJA
kwa taifa letu)!
Kwa mfano, mtu anapoajiriwa kuwa mhasibu, hatutarajii kwamba baada ya kusaini mkataba, mhasibu huyu aombe kwenda kozi ya book-keeping au basic accounting! Hatutarajii kwamba mtu akiajiriwa kuwa CEO wa kampuni ya ndege, baada ya kusaini mkataba wa kazi aanze kuzunguka duniani kufanya “study-tour” ya namna ya kuendesha kampuni ya ndege!

Tunatarajia kwamba mtu anapopewa nafasi kama hiyo, hususan ya juu ya utendaji, mtu awe tayari na uelewa wa kitu gani anapaswa kukifanya katika nafasi hiyo. Tunatarajia kuwa hadi mtu anapopewa nafasi ya juu ya uongozi (kama ya kisiasa) au utendaji tayari, awe na dira na uelewa wa kile anachotakiwa au kutarajiwa kukifanya.

Ziara za “kujifunza” zinatarajiwa zianze baada ya mtu kutekeleza yale masuala ya msingi aliyopaswa kuyatimiza katika nafasi yake. Ziara za kujifunza hazipaswi kuwa suala la kuanza nalo kazini, au kufanywa kama sehemu ya kazi alizoajiriwa kuzifanya mtu. Mtu asifanye ziara “za kujifunza” kama sehemu ya ajira yake, bali liwe ni suala litakalojitokeza mara moja au mbili na hiyo iwe ni baada ya taathimini ya muda mrefu ya kubaini uhitaji wa hizo “ziara”.

Miaka SITA ya Kikwete kuwepo Madarakani bado taifa linakabiliwa na changamoto nyingi sana. Katika changamoto hizi, nyingi ni ndogondogo, ila zinapokuwa nyingi mno, zinafika mahali zinaonekana kuwa kubwa sana. Ufisadi, matumizi mabaya ya mali ya umma, kutokuwajibika kwa watumishi wa umma na serikali kwa umma, kutokuwajibika kwenye matumizi ya fedha na mali za umma, huduma mbovu za umma, Mgao wa Umeme tangu aingie madarakani hadi leo, njaa katika baadhi ya sehemu za nchi wakati vyakula vikiharibika sehemu nyingine n.k. Kero hizi zimeendelea kudumu hapa nchini na zimetoka katika hatua mbaya (bad) kuwa mbaya zaidi (worse) kila siku, kila mwezi na kila mwaka.

Lakini, tangu mwanzoni kabisa mwa utawala wa Kikwete, ZIARA zimekuwa nyingi utadhani ni sehemu ya majukumu yake ya kila siku. Sina uhakika ni kwa kiasi gani hizo ziara zina tija au zinalenga kwa vitendo kumaliza hizi kero za watanzania. Ni kwa kiasi gani ziara hizi zinaongeza matumizi bora ya fedha za umma, ni kwa kiasi gani ziara hizi zimesaidia kupunguza au kudhibiti ufisadi, kumaliza mgao wa umeme n.k.? Je ziara za Kikwete “kujifunza“ zimepunguza ufisadi nchini? Zimemaliza mgao wa umeme? Zimemaliza ufujaji wa mali ya umma kwenye wizara, Idara na Serikali za Mitaa? Zimeongeza uwajibikaji serikalini? n.k. Kuna wengine watadai kwamba safari hizo zimeongeza misaada (kama ambavyo Kikwete mwenyewe hudai), lakini TAIFA HILI HALIHITAJI MISAADA!

Zaidi ya hapo, iwapo kuna huo ulazima wa hizo ziara, basi nadhani kuna haja ya taifa kujiridhisha kwamba ni kweli RAIS WETU HAJUI JAMBO HILI NA HILI NA HIVYO TUMTUME AKAJIFUNZE MALAWI, BURUNDI AU KWINGINEKO. Ni muhimu tukajiridhisha kama taifa kwamba Rais wetu hajui abcd na taifa letu tunahitaji abcd, hivyo tukubaliane kumtuma akajifunze! Isije ikawa anasema kwenda kujifunza, aidha mambo ambayo taifa haliyahitaji au kumbe ni mambo ambayo tayari alikuwa anayafahamu! Au labda, TAIFA TUELEWE KWAMBA TUNA RAIS AMBAYE HAELEWI MAJUKUMU YAKE ALIYOOMBA NA KUAHIDI KUYAFANYA HIVYO TUMLIPIE ADA AU GHARAMA YA KWENDA KUJIFUNZA au TUAMUE VINGINEVYO!

Sijui kama kweli ndio maneno aliyokuwa anayatamka,
lakini pozi linaonesha alikuwa haelewi vizuri kinachosemwa!

Ukweli unabaki kuwa ‘mafunzo kazini’ ni sehemu ya muhimu katika kuboresha uwezo wa mtu kutekeleza majukumu yake. Lakini mafunzo kazini hayapaswi kuwa ndiyo kazi kuu ya mfanyakazi! Inapaswa kufanyika pale tu taathimini inapoonesha kuwa na haja ya hayo mafunzo, na pia kuwe na makubaliano ya uelewa gani ambao mtendaji anahitaji kuupata kwa kwenda kujifunza kwa wengine. Kwa kuwa safari za nje ya nchi huwa zinaambatana na posho nyingi na zilizonona, isijekuwa safari hizo ni njia zak ujipatia posho nyingi halali kwa kisingizio cha kwenda kujifunza!

Mwisho: Hutomlaum kwa kutokucheka
hata pale alipotakiwa kuwa serious!


Na hii ndiyo tafakari yangu ya leo!

Wasaalam, mwana wenyu
…mussa

UDA KUCHUNGUZWA NA BUNGE: Taarifa ya Zitto Kabwe


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
9/08/2011
BUNGE KUCHUNGUZA UFISADI UDA
Ndugu Wanahabari, Suala la Ubinafsishaji wa Shirika la UDA limeibua hisia kali miongoni mwa Wabunge, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla. Suala hili limekuwa tata na kuzusha kila aina ya maneno. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma imeona ipo haja ya msingi ya suala hili kuchunguzwa kwa kina na mhimili wa Bunge. 

Kwa hiyo, imemuandikia barua Spika wa Bunge, ikimuomba aridhie mapendekezo ya wabunge watakaoundakamati ndogo ya Bunge chini ya Kamati hii ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ili ichunguze sakata zima la uuzwaji wa Shirika la UDA.

Uchunguzi huu umependekezwa kufuatia hisia kwamba taratibu za kuuza Shirika hili pamoja na mali zake hazikuzingatia Sheria za nchi na hivyo kupelekea Taifa kuwa katika hatari ya kupoteza mali.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Toleo la mwaka 2007, nyongeza ya sita kifungu cha 13(e), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ina jukumu la kufuatilia ‘Utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma’ na kanuni ya 13(d) ‘kufanya tathmini ya ufanisi wa Mashirika ya Umma’. Ili kutekeleza majukumu haya, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma imemuomba Mhe. Spika aridhie kuundwa kwa kamati ndogo ili kufanya uchunguzi wa suala la Shirika la UDA.

Hadidu Rejea

Hadidu rejea za Kamati ndogo ya uchunguzi inayopendekezwa ni kama ifuatavyo:
i. Kuchunguza kama katika zoezi la kubinafsisha Shirika la UDA taratibu zote za Sheria zilifuatwa.
ii. Kuchunguza kama Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) walitimiza wajibu wao ipasavyo katika zoezi zima la ubinafsishaji wa Shirika la UDA.
iii. Kuchunguza kama Bodi ya Shirika la UDA ilifuata sheria na kanuni katika kuuza hisa zilizouzwa za Shirika la UDA na kama walikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo bila kuhusisha wana hisa. Pia kuchunguza nafasi ya Bodi kwa umoja wake na mjumbe mmoja mmoja wa Bodi katika zoezi zima husika.
iv. Kuchunguza nafasi (role) ya wana hisa (Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali) katika zoezi zima la kuuzwa kwa hisa (unalloted shares) za UDA kwa Kampuni ya Simon Group.
v. Kuwaita mbele ya Kamati wadau wote wa suala la UDA hususani Bodi ya UDA iliyokuwepo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UDA, Mmiliki wa Kampuni ya Simon Group ltd, Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa CHC, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na mtu mwingine yeyote yule itakavyoonekana inafaa. vi. Kufanya tathmini ya Shirika la UDA katika mazingira ya sasa ya biashara ya usafirishaji Jijini Dar es Salaam.
vii. Kutoa Mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuwa na makosa katika zoezi zima la Ubinafsishaji wa Shirika la UDA.
viii. Kupendekeza namna bora ya kuendesha Shirika la UDA.
Ukomo
Kwa kuwa mamlaka nyingine za Uchunguzi zinaendelea na uchunguzi wake, Kamati hiyo ya Bunge itajikita katika maeneo yaliyoainishwa hapo juu tu na haitahusika na suala kama la rushwa au Mahesabu ambayo yanashughulikiwa na TAKUKURU na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. 

Isipokuwa Kamati inaweza kuhitaji msaada wa Taasisi hizi katika kutimiza wajibu wake wa uchunguzi wa kibunge. Bunge, kwa namna yoyote ile, halitazuiwa kuendelea na uchunguzi wake wakati Serikali (Executive) ikitimiza wajibu wake. Izingatiwe kuwa uchunguzi huu pia unahusisha Taasisi za Serikali zenye mamlaka ya masuala ya Ubinafsishaji na utunzaji wa Mali ya Umma (hivyo Serikali pia inachunguzwa).

Muda wa Uchunguzi

Nimependekeza kuwa uchunguzi huu uchukue jumla ya Siku 14 (kumi na nne tu) na kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma na kisha kwa Spika ambaye ataelekeza hatua zitakazofuatia.

Wajumbe wa Kamati Ndogo ya Uchunguzi.

Kwa kuwa Uchunguzi huu unahusisha mambo mengi, nimependekeza kamati hiyo ndogo ihusishe Wabunge wengine katika uchunguzi huu badala ya wajumbe wa Kamati ya Mashirika ya Umma peke yake.

Wajumbe wafuatao wanapendekezwa kuunda Kamati ndogo.
1. Mhe. Murtaza Mangungu, Kilwa Kaskazini (Kamati ya POAC) – Mwenyekiti
2. Mhe. Esther Bulaya, Viti Maalum (Kamati ya POAC)
3. Mhe. Amina Mwidau, Viti Maalumu (Kamati ya POAC)
4. Mhe. David Kafulila, Kigoma Kusini (Kamati ya LAAC)
5. Mhe. Angellah Kairuki, Viti Maalumu (Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala)
6. Mhe. Herbert Mtangi, Muheza (Kamati ya Miundombinu)
7. Mhe. John Mnyika, Ubungo (Mwakilishi Wabunge wa Dar es Salaam)
Katibu wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma na Katibu wa Kamati ya Sheria ndogo wanapendekezwa kuwa Makatibu wa Kamati ndogo ya Uchunguzi wa Ubinafsishaji wa Shirika la UDA.
Ni matarajio yangu na ya wenzangu kuwa Spika wa Bunge, Mhe.Anne Makinda ataridhia kuundwa kwa Kamati hiyo, ili Bunge liweze kuchukua wajibu wake wa kiuchunguzi na wa kuisimamia Serikali. Ninaamini, uchunguzi huo ndio utakaokata mzizi wa fitina kuhusu nani amehusika na achukuliwe hatua gani zichukuliwe kwa maslahi ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Taifa zima kwa ujumla.

Nashukuru kwa kunisikiliza.

Kabwe Zuberi Zitto (Mbunge)
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma