Tuesday, May 29, 2012
Zanzibar: KANISA Lininge LACHOMWA MOTO!
BAADA ya Kanisa la Assemblies of God kuchomwa moto katika vurugu zilizoanza mwishoni mwa wiki iliyopita, jana Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae nalo limechomwa moto.
Akizungumzia hali hiyo jana, kiongozi wa Kanisa hilo, Ambaros Mkenda, alidai kwamba Kanisa hilo lilichomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha uharibifu mkubwa.
Alidai Kanisa hilo lilichomwa moto jana saa 8.30 mchana na watu wanaohisiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, waliokuwa wakitoka katika Mahakama ya Mwanakwerekwe kusikiliza kesi ya wenzao waliokamatwa juzi.
Mkenda alidai kuwa watu hao waliwazidi nguvu walinzi wawili wa Kanisa hilo na kuvunja lango kuu la kuingilia ndani ya Kanisa na kuchoma moto na waliharibu madirisha na vifaa kadhaa vyenye thamani ya Sh milioni 20.
“Tunasikitika sana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika Kanisa letu ambalo lilikuwa tegemeo kubwa kwa wafuasi wapatao 2,000 wa eneo la Parokia ya Mpendae na jirani,” alisema Mkenda.
Mkenda alidai kuanzia juzi, viongozi wa makanisa mbalimbali waliwasilisha maombi yao Polisi kuhusu kupewa ulinzi katika nyumba za ibada, baada ya kupokea vitisho. Hata hivyo, Mkenda alidai ombi lao hilo halikutekelezwa na Polisi na uharibifu mkubwa ukatokea katika Kanisa la Assemblies of God la Kariakoo.
Wafuasi na waumini wa Kanisa hilo walikusanyika nje ya jengo hilo, huku vijana wakishikwa na hasira wakitaka kwenda kulipiza kisasi katika maeneo ya jirani wakidai wanawatambua vijana waliofanya vitendo hivyo.
Mmoja wa waumini wa Kanisa hilo ambaye ni mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Susan Kunambi alilazimika kuwatuliza wafuasi vijana wa Kanisa hilo waliopandwa na jazba wakitaka kulipa kisasi.
“Hakuna sababu ya kupandisha jazba na kutaka kufanya vitendo ambavyo vitasababisha hasara na uharibifu ... Kanisa siku zote linahimiza amani na upendo na si chuki,” alisema Kunambi.
Polisi walifika haraka katika eneo la tukio na kurusha mabomu ya machozi ili kutawanya makundi ya vijana waliojikusanya na wengine kurusha mawe.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alithibitisha kuchomwa moto Kanisa hilo na kusema ulinzi umeimarishwa katika baadhi ya maeneo ya nyumba za ibada yakiwamo makanisa. Baadhi ya mitaa ya Jang’ombe na Mwanakwerekwe njia zimewekwa mawe na vikundi vya vijana waliochoma mipira ya gari na kusababisha moshi mkubwa.
Vikundi marufuku Wakati huo huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepiga marufuku maandamano, mihadhara ya kidini na mikusanyiko isiyo na kibali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema hayo wakati akitoa taarifa rasmi ya SMZ baada ya vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Uamsho baada ya kukamatwa kwa viongozi wao wa kidini.
Aboud alisema Serikali haitakubali kuona kikundi cha watu wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kuvuruga utulivu wa nchi kwa kisingizio cha kudai mabadiliko ya Katiba na imani ya dini.
“Wapo watu wanataka kuona tunarudi nyuma katika kipindi cha fujo na vurugu za kisiasa...wakati huo umepita,” alisema Aboud. Kutokana na hatua hiyo ya Serikali, mihadhara na maandamano kuanzia sasa italazimika kupata kibali kutoka taasisi husika ikiwamo Polisi. Alitaka wazazi wakataze watoto wao kujishughulisha na ushawishi wa kufanya vitendo vitakavyohatarisha amani na utulivu wa nchi.
Utulivu wajirudia mjini Jana hali ya utulivu ilirejea kisiwani hapa ikiwamo Mji Mkongwe na sehemu za mitaa ya Ng’ambo, huku wananchi wakifanya shughuli zao za maendeleo na biashara bila matatizo.
Maduka na huduma za usafiri viliendelea kama kawaida huku wafanyakazi wa Manispaa wakifanya usafi ikiwa ni pamoja na kuondoa matairi ya magari yaliyochomwa barabarani katika vurugu za juzi.
“Tunasafisha barabara zilizoharibiwa na waandamanaji kwa kuchoma moto mipira ya magari,” alisema Ali Juma mfanyakazi wa Manispaa ya Mji wa Unguja. Kamishna Mussa alisema Polisi waliendelea kuweka doria katika maeneo mbalimbali ya mji kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ.
“Tutaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ikiwamo nyumba za ibada ili kuhakikisha hakuna vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema Mussa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alionya kuwa suala la amani na ulinzi wa raia na mali zao halina mjadala na kuvihadharisha vikundi vinavyohatarisha amani, kwamba vitapambana na mkono wa Dola.
Dk Nchimbi aliyekuja hapa ili kukutana na viongozi wa vikundi vya dini na mihadhara na Polisi, alisema athari ya kuvunja amani na utulivu ni kubwa na wananchi wa Zanzibar wanafahamu vizuri mazingira yalivyokuwa miaka ya nyuma.
Alitaka viongozi wa dini wajifunze sheria za nchi na kuzifuata na kuwataka wasihusishe Uislamu na vurugu na fujo kiasi cha kuhatarisha amani ya nchi.
Pia alitaka wananchi walioharibiwa mali zao kwenye vurugu na fujo kutoa taarifa Polisi kwa hatua zaidi.
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, alisema Polisi itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya nchi.
Watu 30 wakiwamo wafuasi wa Uamsho walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe kujibu mashitaka yakiwamo ya kuandamana kinyume cha sheria na ukorofi wa kuwashambulia polisi kwa mawe.
Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka katika makundi matatu tofauti; kundi la kwanza likiwa la viongozi wawili wa jumuiya hiyo; Mussa Juma Issa (57) na Mbarouk Said Khalfan (45). Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mohamed Ali Sheni ya kujikusanya kinyume cha sheria na kufanya maandamano ambayo yalianzia Uwanja wa Lumumba kupitia Msikiti wa Kwabiziredi na kumalizia uwanjani hapo.
Watuhumiwa hao walikana mashitaka na kupewa dhamana ya masharti ya Sh 300,000 kila mmoja kwa kiasi hicho hicho; walitimiza masharti na wako nje kwa dhamana hadi Juni 11 kesi yao itakapotajwa. Kundi la pili la watuhumiwa wengine sita walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Janet Sekihola ambayo ni ya uzembe, ukorofi na kushambulia polisi waliokuwa doria.
Watuhumiwa hao ni Abdulrahman Simai Khatib, Hashim Juma Issa, Martar Said Ramadhan, Mbwana Hamad Juma, Masoud Hamad Mohamed na Mohamed Juma Salum.
Kesi ya watuhumiwa hao iliahirishwa hadi Juni 11 itapotajwa huku baadhi yao wakitafuta wadhamini na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja kwa Sh 500,000.
Maimamu wawakana Jumuiya ya Maimamu na Mihadhara ya Jumaza, imesema waliofanya fujo na vurugu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi si wafuasi wao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Muhidin Zubeir Muhidin ambayo pamoja na jumuiya hiyo ndizo taasisi zinazojishughulisha na mihadhara ya dini ya Kiislamu ambayo hutoa elimu kuhusu marekebisho ya Katiba.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Shehe Zubeir alisema jumuiya hiyo haijatuma watu kufanya fujo, kwa sababu katika dini hiyo ni makosa mtu kuharibu mali ya mwenzake. “Tunataka Waislamu wote na wafuasi wa Jumaza na Uamsho kuacha fujo na kurudi nyumbani kusubiri hatma ya viongozi wao,” alisema Shehe Zubeir.
Serikali ya Marekani imesema matukio yaliyotokea kwa siku mbili Zanzibar yanaweza kuchafua taswira nzuri iliyowekwa na visiwa hivyo, katika uchaguzi mkuu uliosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutokana na ghasia zilizotokea visiwani humo na kusababisha Kanisa na gari la kiongozi wa Kanisa kuchomwa moto.
“Kudumisha mazingira ya amani visiwani Zanzibar ambayo yanaruhusu utalii na maendeleo kuna maslahi kwa Wazanzibari wote na hata wageni waingiao visiwani humo,” alisema Balozi Lenhardt katika taarifa yake iliyotolewa jana Dar es Salaam.
Alisema ni muhimu kwa kila mtu kujizuia na kulinda maisha na mali za watu wasio na hatia na aliunga mkono waliozitaka pande zinazozozana kushirikiana kuleta amani na utulivu katika visiwa hivyo.
“Tunatambua umuhimu wa mjadala wa kisiasa unaoendelea lakini tunavitaka vyama vyote kuendelea kuufanya kwa njia ya amani na kidemokrasia zaidi,” alisema Balozi huyo.
Aliongeza kuwa anakubaliana na anaunga mkono hatua za haraka zilizochukuliwa na viongozi waandamizi wa kisiasa waliojitokeza kushughulikia masuala yaliyosababisha matukio hayo ya kusikitisha.
Selasini (CHADEMA): Mazishi ya Mama Yake Kesho!
Naendelea
kuwashukuru Makamanda na Ndugu zangu wote mnaoniombea mimi na familia
yangu kuweza kuvuka katika kipindi hiki kigumu tunachokipitia kwa
majonzi na maumivu makubwa!... AHSANTENI SANA!...
Kesho
tutafanya maziko ya Marehemu Mama yangu ambapo itatanguliwa na ibada ya
mazishi kwenye Kanisa Katoliki Mkuu kuanzia saa sita mchana na baadaye
kuzikwa nyumbani Kata ya Makiidi...
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA.. Jina la Bwana lihimidiwe!..
R.I.P my Mom!.
Joseph Selasini
Mb. Rombo (CHADEMA)
Monday, May 28, 2012
Muungano: TUUZUNGUMZE au TUUVUNJE!
Ni hivi majuzi tu mwezi uliopita Muungano wetu umetimiza miaka 48, kama kawaida tulifanya Sherehe. Lakini ukweli ni kwamba kwa Sasa Muungano wetu unahitaji kuadhimishwa kwa kitu kingine zaidi ya Maonesho kwenye viwanja vya mipira, magwaride ya majeshi na hotuba zilizojaa nukuu za Nyerere na za Karume.
![]() |
| Kuzaliwa kwa Muungano |
Muungano wetu umedumu kwa miaka yote hii katika mazingira ya usiri na ulinzi mkuwa mkubwa wa "mada" hiyo. Lakini ukweli ni kwamba, zama hizo zimepita.
Maswali kuhusu Muungano
![]() |
| Sheikh Karume |
Muungano huu ni wa nchi mbili ambazo kabla ya kuungana zilikuwa huru. Katika mazingira ambayo hayafahamiki vizuri kwa Watu wa Nchi hizi mbili mpaka sasa - hususan vijana - nchi hizi ziliungana na kuunda Nchi Moja iliyokuja kuitwa Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania. Maswali mengi yaliyobaki tangu kuundwa kwa Muungano huu hadi leo ni pamoja na:
- Majadiliano baina ya Nchi hizi mbili ili ziungane yalifanyika wakati gani na kwa muda gani?
- Ni wajumbe wapi na wapi walioziwakilisha nchi hizi mbili katika majadiliano hayo?
- Ni yapi yaliyokuwa makubaliano ya mwisho baina ya pande hizi mbili?
- Makubaliano ya majadiliano ya pande hizo mbili yalijadiliwa na Wananchi wa Nchi husika (moja kwa moja au kupitia mabunge yao) na kuridhia kuunganishwa kwa Nchi zao?
- Nakala ya Mkataba/Makubaliano baina ya nchi hizi mbili yalifikishwa kwa wananchi na kusambazwa kwa uwazi ili waelewe misingi ya kuunganishwa kwa nchi zao?
- Nani anayenufaika Zaidi na Nani anayepoteza Zaidi kwenye huu Muungano?
Maswali haya yote - pamoja na mengine mengi - inawezekana katika nchi hii kuna watu wana majibu yake, lakini ukweli unabakia kuwa walio na hayo majibu ni wachache (kama wapo kweli). Kwa misingi hiyo Muungano tangu zama hizo mpaka leo umebakia ni kama kitendawili ambacho wananchi wengi hawawezi kukitegua. Na wengine wamefikia hatua ya kuamini kuwa Siri ya Muungano alikuwa nayo Nyerere na Karume (ambao walikuwa marais wa Tanganyika na Zanzibar kwa wakati huo) na sio Watanzania wote!
Mwisho wa Zama Umefika
Wanasiasa na viongozi wa Serikali kwa ujumla walijitihidi sana kwa miaka kuutunza, kuudumisha na kuulinda Muungano kwa njia mbali - kubwa ikiwa ni kutoruhusu ujadiliwe - na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini ni wazi kwamba Zama hizo za "Giza" kuuhusu Muungano zinapita kwa kasi - kama sio kwamba zimeshapita kabisa mpaka sasa!
| Zanzibar: Wanawake Barabarani kutaka Muungano Upigiwe Kura! |
Zama za kuulinda na Kuudumisha Muungano kwa kutumia mbinu ya kuuficha usijadiliwe waziwazi zimefikia mwisho wake sasa.
Mapinduzi ya Uarabuni Yamewaamsha Watanzania!
Watanzani wa leo - hususan baada ya kushuhudia "Mapinduzi ya Umma" katika nchi kadhaa za Kaskazini mwa Afrika na Uarabuni - leo hii wengi wao nao wanaamini kwamba jambo lolote linawezekana kwa nguvu za Umma, hata hapa Tanzania - NA INAWEZEKANA WAKO SAHIHI! Na huu ni ukweli usiopingika kwamba Hakuna Nguvu Duniani hapa inayoweza kuishinda Nguvu ya Umma - hata Serikali na Majeshi haziwezi kuzima nguvu ya Umma - Umma uliojiunga na Kusimama pamoja!
![]() |
| Mubaraka: nguvu ya Umma ilimng'oa |
Ukiwa unaongoza watu kama hao, ni wazi kwamba unapaswa kuwa makini sana na mambo ambayo wao wanayataka au kuyaona ni ya kipaumbele na kuyapatia nafasi stahiki - badala ya kudhani unaweza kuwanyamazisha kwa "kujifanya" unashughulikia mambo mengine ambayo kwako ndiyo ya muhimu zaidi - UTAKUWA UNAJIDANGANYA!
Maswali yanayobaki
Utaratibu huu wa sasa wa "kuulinda na kuudumisha" Muungano unaweza kudumu iwapo tu Nchi ingeendelea kutawaliwa na CCM kwa Asilimia 100 siku zote (kutokana na sababu zinazojulikana). Lakini hilo kwa sasa hilo halipo tena! CCM Inazidi kupoteza majimbo na Ushawishi miongoni mwa raia kwa kasi kubwa kila kunapokucha. Vyama vyenye Upinzani vilivyojawa na hamu ya kuhoji kila Sera ya CCM ndivyo vinazidi kupata mvuto na kusikilizwa zaidi Nchini!
![]() |
| Sera za CHADEMA zinamaswali mengi kuhusu Muungano! |
MOJA: Kwa Mfano, Iwapo CHADEMA Itachukua dola mwaka 2015 na ikaamua kuigawa nchi katika Majimbo kama sera yake inavyoelekeza kwa sasa, ZANZIBAR Itakuwa katika jimbo Lipi? Je, Itabakia ba hadhi yake ya Sasa ambayo hata hivyo haijulikani Vizuri - au kutakuwa na Badiliko?
PILI: Iwapo Jumuiya ya Afrika Mshariki Itaanzisha Shirikisho la Kisiasa (kuwa na rais Mmoja wa AM), Zanzibar itakuwa mgeni wa Nani chini ya huo Mfumo? (maana muundo wa Muungano wa Sasa hauko wazi katika hilo pia)!... na mengine mengi!
Dalili kutoka Zanzibar
| Zanzibar Leo! - Tatizo ni Muungano! |
Mambo yanayoendelea kwa sasa visiwani Zanzibar - kwa hakika ni ishara kubwa sana kwamba zama za kuulinda na kuudumisha Muungano kwa mbinu ya Ukimya imepitwa na wakati. Vurugu zinazoendelea kwa sasa huko Zanzibar - hususan zinapoanza kuhusisha hisia za Ubaguzi dhidi ya "wabara", ni wazi kwamba Siku sio nyingi zitaweza kuigia bara, na kundi la kwanza kutafutwa wanaweza kuwa Makamu wa Rais na Mawaziri kutoka Zanzibar - kabla ya kuingia mitaani na kuwageukia wapenmba waliojazana kwenye miji ya Tanganyika!
Katiba Mpya SIO Jibu!
Wakati vuguvugu la kudai katiba mpya lilipoanza kushika kasi mwishoni mwa mwaka juzi (wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu) na hatimaye Serikali ikazidiwa nguvu na Upinzani na kukubali Madai ya CHADEMA ya kuundwa kwa katiba mpya (ikumbukwe CCM haikuwa na Mpango wa Kuunda Katiba Mpya Tanzania wakati wa Awamu ya Pili ya Kikwete Madarakani), binafsi nilidhani kwamba hii ndiyo ingekuwa fursa muhimu sana kwa Serikali "kujivua lawama" za usiri na tatizo la Muungano kwa kuruhusu wananchi waujadili Muungano huu wakati wanajadili katiba mpya na kuutolea majibu! HAIKU WA HIVYO!
Uundaji wa Sheria ya Katiba Mpya bado ulighubikwa na "WOGA" ule ule wa miaka neda rudi, na hatimaye Suala la Muungano kuondolewa kwenye masuala yatakayojadiliwa! Ukweli ni kwamba hili NI KOSA, na kuna "mtu" atalilipia hili kosa!
Nini Kifanyike?
Ushauri wangu kwa Rais Kikwete na Serikali kwa ujumla ni kutambua na kufanya yafuatayo:
- Kwanza, ni muhimu kwa Kikwete na Serikali yetu ya leo kutambua kwamba Watanzania wa leo sio wa miaka ile ya Uhuru - au enzi za Nyerere! Watanzania wa leo sio watu unaoweza kuwaridhisha kwa "maneno mepesi" huku ukikwepa kujibu maswali yao Magumu? Watanzania wengi wanataka waelezwe - kabla hawajashawishiwa kuendelea nao au kuuvunja - ni nani anayenufaika zaidi na huu Muungano na Nani anayepunjwa zaidi kwenye huu Muungano. Hili ni swali gumu ambalo linahitaji majibu magumu, zaidi ya zile hotuba ambazo tumezoea kuzisikia za kuuremba na kuupamba Muungano pasipo takwimu na Vielelezo!
- Serikali itafute njia nzuri ya kulileta Suala la Muungano katika mjadala wa Wazi wa Kitaifa. Kama nilivyosema hapo juu - Fursa kubwa ya kufanya hivyo ilikuwa ni Mjadala wa Katiba. Ninaposema "njia nzuri" ninamaanisha kwamba iwapo Serikali tayari ina mtazamo wake ambao isingependa ubadilishwe - hata na "wenye nchi" wenyewe (wananchi), basi ijipange kuuleta huu mjadala kwa namna ambayo itawavuta Watanzania wengi kuunga mkono matakwa ya Serikali ya kuudumisha!
Kinyume cha Hapo, kuendelea kuuficha-ficha na kuutetea Muungano kwenye Hotuba pasipo kujibu maswali ya Msingi ya Wananchi, kutazidi kuongeza idadi ya watu wanaotaka kujua kiini hasa cha "Usiri"huo, na hapo ndipo tatizo litakuwa kubwa zaidi hata ya hapa lilipo leo!
![]() |
| Watanzania kwa Sasa wanahitaji Majibu magumu Zaidi |
Kuendelea kukwepa kuujadili Muungano SIO kuulinda wala kuudumisha kama ambavyo wanasiasa wetu wengi wanaweza kuwa wanajidanganya kwa sasa. Kitendo hicho ni kuzidi kuongeza watu wanaouhoji na wale wanaotaka majibu mazidi. Kwa kadri idadi ya watu wanaouhoji na kuutilia mashaka Muungano itakavyoongezeka ndivyo Uwezekano wa Kuwapa Majibu Sahihi na kuwaridhisha utakavyozidi kuwa mgumu - NA HUO NDIO UTAKUWA MWISHO WA MUUNGANO!
The Union: It's Now or Never!
"UGAIDI" Zanzibar: Tamko la Waislam!
![]() |
THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION
P. O. BOX: 1266
Tel: +255-777-419473 / 434145-
FAX +255-024-2250022
E-Mail: jumiki@hotmail.com
MKUNAZINI ZANZIBAR
Tarehe 27MAY2012
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika Uislamu.
Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila
kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala zisiharibiwe.
Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali, mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.
Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.
Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil ya kulinda haki za wengine.
Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu kwa watu wote.
WABILLLAH TAWFIQ
Zanzibar: UDINI, UGAIDI Usipenyezwe kwenye Muungano!
| Nembo ya JUMIKI, Zanzibar |
Taarifa zilizotoka Zanzibar zimewashtua na kuwahuzunisha watu wengi - hususan kitendo cha Watu kuvamia Kanisa, Kulibomoa na Kulichoma moto - katika harakati zao za Kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar!
![]() |
| Kanisa lililochomwa Zanzibar |
Japo ni kweli kwamba kuna haja ya Suala la Muungano kuwekwa wazi machoni pa Watanzania wote, kujadiliwa hadharani na hatimaye kufanyiwa maamuzi ya wazi - lakini ni lazima tuelewe kwamba kwanza kuna njia sahihi za kuweza kufanya hivyo, na Pili na MUHIMU ZAIDI, tuwe makini na watu wanaotaka na wanaoweza kupenyeza Ajenda zao za Siri na za Uovu katika mchakato huo.
Ni ukweli usiopingika kwamba kanisa la TAG Tanzania halikuhusika katika kuuanzisha Muungano, sina uhakika kama lina sera ya kuuimarisha na au kuudumisha Muungano, lakini muhimu zaidi, halina sera ya kupinga kujadiliwa au kupigiwa kura ya maoni suala la Muungano. Suala la Kushambuliwa kwa kanisa hilo ni dalili ya wazi kwamba KUNA WATU WAOVU ZANZIBAR - wenye Dhamira na Malendo ya Kigaidi - ambao wanataka kutumia vurugu zinazoendelea Visiwani humo kutekeleza uovu wa kidini na kigaidi!
| Zanzibar! |
Kushambuliwa kwa kanisa hili na watu wanaodhaniwa kuwa katika harakati za kudai Kura ya maoni kuhusu Muungano ni wazi kwamba harakati hizo zinaanza (kama sio kwamba tayari) zimekwisha kuingiliwa na WATU WAOVU, ambao wanataka kutumia mwanya wa kuwepo kwa vuguvugu na harakati hizi kutekeleza uovu wao ambao aidha uko katika misingi ya kidini tu au umechanganyikana na dhamira ya UGAIDI ndani yake!
| Katibu wa JUMIKI - anatafutwa na Polisi Zanzibar! |
Napenda kutoa tahadhari hii kwa taifa letu hili kwamba tusifanye kosa la kufumbia macho uovu huu unaoanza kama vile unafanywa na makundi ya watu wahuni, maana madhara yake hakika yatakuja kuwa makubwa kupita tunavyoweza kufikiria kwa sasa.
Uzoefu wa Nigeria!
Nchini Nigeria, wakati kundi la Boko al Haram lilipoanzishwa mwishoni mwa miaka ya 90, lilidhaniwa na kuchukuliwa tu kama kundi la kidini la Waislam ambalo lilikuwa linapenda na kuhamasisha elimu ya kiislam. Lakini ukweli ni kwamba malengo ya kundi hilo tokea mwanzoni yalionesha dalili za wazi kuwa iwapo litaachwa na kuendelea kukua na kujipanua, litakuja kuwa kundi la hatari sana nchini humo.
![]() |
| Kiongozi wa BOKO Haram, Aliua wengi kabla hajauawa! |
Miaka 10 baadaye, ni kundi kubwa zaidi la Ugaidi nchini humo ambalo sio tu linataka kulazimisha watu wote kuwa Waislamu (KWA LAZIMA) bali linaitumia nafasi hiyo kufanya Vitendo vya Kishetani vya Mauaji ya Kikatili dhidi ya raia wa Wasio na hatia - Ambao linadai ndio linataka wawe Waislamu!
Mbaya zaidi - lifanya Ushetani na Uovu huo wote CHINI YA KIVULI CHA DINI - uislamu - jambo ambalo linakisaidia kikundi hicho kujipatia wafuasi wengi wa dini ya kiislamu ambao hudanganyika kwa kudhani linatetea maslahi yao (japo kwa njia ambazo sio za kidini kabisa)!
![]() |
| Shambulio la Boko Haram kwenye kanisa, Nigeria! |
Kikundi hiki kilichoanza kama vuguvugu la kutaka Nchi Nzima Nigeria iwe ya Kiislamu na kufuata Sharia, kwa sasa limejikita zaidi katika kushambulia Makanisa na kufanya mauaji ya wakristo kila linapopata nafasi ya kufanya hivyo. Kitendo hiki ni cha Kisenzi na Kishetani ambacho hakiungwi mkono na Dini yoyote - hata Uislamu wenyewe - ambao Waovu wanaohusika wanadai wanaupigania na kuueneza!
Wito wangu kwa taifa!
Wito wangu kwa taifa tangu sasa Serikali iwe ya kwanza kujitokeza hadharani na KULAANI kitendo hicho cha Zanzibar na kuwatafuta na kuwafikisha wahusika wote mbele ya Sheria - bila kujali Imani zao za Kidini au dhamira zao katika kufanya Uovu huo!
![]() |
| Kanisa la TAG, limechomwa moto Zanzibar |
LAKINI kwa upande mwingine, ni muhimu Serikali ikajifunza kusikiliza na kuelewa matakwa ya Umma na kukubali kuusikiliza umma na kufanyia kazi mawazo yao. Sio wakati wa Serikali kuendelea kudhani kwamba zitaendelea kuwatawala wananchi wake kama mabubu na mbumbumbu ambao wako tayari mara zote kunyamazishwa na Serikali na kuzuiliwa kuyazungumzia masuala ya nchi yao - ETI kwa sababu tu Serikali na au Chama kilichoko madarakani hakijisikii vizuri kulizungumzia suala husika!
| Hii SIO Zinjibar, Yemen, NI Zanzibar, Tanzania! |
Serikali yetu isijidanganye kwamba Watanzania (wa bara na visiwani) wataendelea milele na milele kukaa kimya kuhusu Muungano. Jitihada za serikali kukwepa kuliweka suala la muungano huu tata hadharani ili ujadiliwe na kufanyiwa maamuzi na hazitadumu siku zote. Ukweli utabakia kwamba kukataa kuuzungumza Muungano kwa sasa SIO kuuimarisha BALI ni kuchelewesha kuvunjika kwake!
| Mabomu na Risasi Haviwezi Kudumisha Muungano Siku Zote |
Subscribe to:
Posts (Atom)












