Kuna msemao usemao “Hata Mbuyu Ulianza kama Mchicha”. Msemo huu hufahamika na kutumiwa na watu wengi sana kama njia ya kujipatia hamasa katika masuala mbalimbali wanayotaka kuyafanya au wanayoanza kuyafanya. Zaidi sana, msemo huu hutumiwa na watu ambao huanza shughuli fulani na mawazo madogo sana huku wakiamini na kutarajia kwamba siku moja yatakuja kuwa makubwa sana tofauti na yanavyoonekana wakati wanaanza.
Wakati ukweli ni kwamba jambo la mtu kujitia moyo na kujifariji ni la muhimu sana pale unapoanza safari yoyote katika maisha, ni muhimu sana pia kuelewa ni kitu gani ambacho huwa kinawatofautisha wale ambao huwa wanafika mbali sana na wale ambao hawafiki mbali. Kwa kuutumia mfano huu huu wa mchicha na mbuyu, tunabaini msingi wa tofauti.
Tofauti kubwa kati ya mbuyu na mchicha SIO unaanzaje bali ni kiini cha hiyo mbegu yenyewe inayoanza!!. Ukweli ni kwamba, japo mbuyu na mchicha huweza kuanza kwa namna inayofanana, na hata wakati mwingine mtu asiweze kutofautisha kati ya mchicha na mbuyu pale mimea hii inapokuwa na urefu wa robo au nusu futi, lakini tofauti huwa ipo NA TOFAUTI HII HUWA NDANI – KATIKA KIINI!Kiini kinachokuwa katika mchicha ndicho huamua mchicha huu unaweza ukakua na kufikia wapi, kiini hicho ndicho huamua huu mchicha utaweza kuishi kwa muda gani, Mchicha huu unaweza kuwa Imara namna gani n.k. Sio mazingira ya nje ya mchicha wala hamu inayokuwa ndani ya mpandaji ambayo huwa na nafasi ya kwanza ya kuamua Sifa hizo za Baadaye za Mchicha NI KIINI kinachokuwa ndani ya Ule Mchicha wenyewe! Kiini hiki ndicho huamua mchicha huu utaishia wapi – hata kama watu wengi wanaouzunguka wanaweza kuwa wanaunenea maneno mazuri kwamba na wenyewe unaweza kuwa kama mbuyu siku moja – siyo maneno, dua wala matamanio – ni kiini!
Vivyo hivyo kwa mbuyu, japo unaweza kuanza “kama mchicha”, ndani ya mbuyu huwa kuna kiini, ambacho huukumbusha ule mbuyu mara zote kuwa japo kwa sasa unaweza kuonekana kama mchicha, lakini unaweza kwenda mbali zaidi na kuwa mmea mkubwa zaidi katika nyika yote.Tukirudi katika hali ya maisha ambamo mtu unaweza kuwa unautumia huu msemo kwa ajili ya kujitia moyo na kujifariji kuhusiana na uwezekano wa kuweza kukua na kuwa “kama mbuyu” siku moja, japo mawazo na vitendo vyako kwa sasa vinaonekana ni vidogo, ni muhimu kujiuliza kwanza swali moja kubwa, kabla ya kujiaminisha kwamba faraja yako inaweza ikazaa matunda: Je, kiini cha wazo, shughuli, biashara au jambo hili linalotaka kulifanya ni kama cha mbuyu au ni kama cha mchicha?
Ni muhimu sana tangu katika hatua za awali kabisa za kutengeneza wazo lako, ndoto yako, maono yako, kazi yako, biashara yako n.k. ukajiridhisha kwa kuwa na uelewa kuhusiana na “potential” ya kiini cha ndoto yako. Tambua kiini hicho ndicho kinakuruhusu kuishi kwa muda gani, kuishi kwenye mazingira gani na muhimu zaidi, unaweza kukua kwa kiasi gani. Kiini cha mchicha hata kikipewa huduma zote muhimu kwa mmea hakiwezi kuufikisha mchicha kwenye hatua ya mpapai – achilia mbali mbuyu! Lakini kwa upande mwingine, kiini cha mbuyu, hata pale mbuyu unapokuwa katika mazingira magumu kama ya porini na hata wakati mwingine kwenye maeneo makavu sawa na jangwa, yenye jua kali, yenye ukame, kiini kile hudumisha ndoto ya kuuwezesha siku moja kuja kuwa mkubwa sana katika nyika yote!
Je, wewe ni mmoja wa watu ambao wamekuwa wakijifariji kwamba hata mbuyu ulianza kama mchicha hivyo ukajiaminisha kuwa siku moja ndoto yako itakua na kuwa kama mbuyu? Kama ndivyo, jiulize swali hili moja la msingi: Je, kiini cha Ndoto yako ni kama cha mbuyu au ni kama cha mchicha! Kama kiini hicho ni kama cha mchicha, usipoteze muda kudhani siku moja unaweza kuwa kama mbuyu – USIPOTEZE MUDA kwa maana haitakaa iwezekane hata ukamilifu wa dahari! Lakini kama kiini hicho ni kama cha mbuyu, basi endelea na kujipa matumaini hayo, uyasimamie, usikubali kukatishwa tamaa wala kuyumbishwa, vumilia ukame na mafuriko, joto na baridi, siku moja utakuwa kama mbuyu!
Na hii ndiyo tafakari yangu kwako kwa leo!
Wasaalam
…mussa