Maige: Majungu CCM yameniondoa uwaziri |
Monday, 28 May 2012 20:35, Shija Felician, Kahama |
Jana, Maige akiwa mjini Kahama katika mkutano wake na viongozi wa CCM wa Wilaya hiyo na Mkoa wa Shinyanga, baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili katika jimbo lake, alionya kwamba kwa hali hiyo, CCM kinaelekea kubaya. Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa, Hamis Mgeja, Maige alisema baadhi ya wanaCCM wamekuwa vinara wa kushabikia majungu aliyoyaita ya ‘kipumbavu’ badala ya kutembelea wananchi na kujua matatizo yao. Akaonya: “Majungu ya kipumbavu ya aina hiyo, yatasababisha chama kife.” Alisema kitendo cha baadhi ya wanachama wa CCM kushabikia kuondolewa kwake kwenye uwaziri, kinaonyesha jinsi gani ambavyo wameonyesha kuwa na uelewa mdogo wa kisiasa akisema walidhani wanamkomoa... “Kumbe wanajikomoa wenyewe.” Alihoji ni lini CCM kimefanya mkutano kwenye jimbo lake licha ya kuwa na nyenzo zote za usafiri ikiwemo magari na pikipiki lakini, Chadema wasiokuwa hata na baiskeli wameweza kupita jimbo zima wakifanya mikutano yao na kugawa bendera zao kama njugu. Alisema endapo majungu hayo yataendelea kitakufa na kuongeza kuwa wazee zaidi ya 300wa jimbo lake wamemfuata wakimtaka awaeleze anahama lini CCM ili wamfuate atakapokwenda. Hata hivyo, Maige alisema alitumia busara zaidi kuwatuliza na kuwapa pole kwa yaliyomfika ya kuzushiwa tuhuma kwenye wizara kwa lengo la kumchafua. Ailipua Kamati ya Maliasili Akizungumzia Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Maige alisema taarifa yake rasmi haiendani na ile iliyosomwa bungeni hali ambayo alidai ilikuwa na lengo la kumng’oa kwenye uwaziri. Maige alishangaa kuona Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Kahama, James Lembeli akimzushia kile alichokiita taarifa hiyo ambayo si kweli akisema madai yaliyokuwemo yalifanyiwa uchunguzi wa kina lakini, kwa kuwa ilikuwa imepangwa kwa lengo la kumng’oa ilitekelezwa. Alimtaka Lembeli warejee kwenye meza ya mazungumzo yenye kuwaletea maendeleo wananchi wa Kahama: “Baada ya kutekeleza lengo lake la kumng’oa kwenye uwaziri,” akisema kabla ya kupata wadhifa huo walikuwa marafiki na walitembea pamoja kwenye majimbo yote ya Kahama na Msalala kwenye mikutano yao. Lembeli: Maige apangue tuhuma Lembeli akizungumzia madai hayo ya Maige, alisema anachopaswa kufanya waziri huyo wa zamani ni kujibu tuhuma zilitolewa na kamati kuliko kuendeleza chuki binafsi zisizokuwa na msingi. Lembeli alisema kwamba haingii akilini kuona kwamba yeye mtu mmoja anaweza kutoa ripoti ya kamati ya watu 30 na kuweka mawazo yake binafsi. “Anachokifanya kunituhumu mimi ni chuki binafsi za kukosa uwaziri. Anachotakiwa ni kujibu hoja za kamati. Nilichokisoma pale ni ripoti ya kamati yote ya watu 30. Anachokifanya ni makosa,” alisema Lembeli. Katika ripoti yake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa ikiongozwa na Maige, ilituhumiwa kuhusika na upotevu wa Sh800 milioni za mazao ya misitu huku Kamati ya Maliasili na Utalii ikimtuhumu waziri huyo kwa kujimilikisha vitalu. |
No comments:
Post a Comment