Thursday, May 31, 2012

"NAPE Ni GAMBA Linalotakiwa Kuvuliwa!" - MAIGE


Akizindua matawi mawili ya wakereketwa wajasiriamali wa CCM katika Kijiji cha Isaka, Kahama, Shinyanga, Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala alimtaka Nape kuacha tabia yake ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja au nyingine zinaelekea kukidhoofisha chama.

Alimtaka kupima utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo ya Itikadi na Uenezi na kujiuliza ni wanachama wangapi wameingia ndani ya chama hicho.

Alisema sasa hivi kuna wimbi kubwa la wanachama wa chama hicho kuhama na kukimbilia upinzani na kusema ni wajibu wa Nape kupima na kuona kuwa kazi ya itikadi na uenezi haiwezi na kwani hajui wajibu wake akisema ni mtu wa kumhurumia.

Maige alisema mbali ya kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama CCM pia hapaswi kuvumiliwa kutokana na kauli yake kwamba hata kama wanachama watahama wote na akabaki yeye (Nape) peke yake, haitakufa. Alisema kauli hiyo haikijengi chama, bali kuchochea makundi ambayo yanaweza kukibomoa.

Alisema akiwa mwana CCM anaona kwamba sasa hivi Nape amekuwa hafanyi kazi ya uenezi na kukirejeshea haiba na mvuto ambao umepotea kwa wananchi na kwamba, kazi anayoifanya sasa ni kukuza makundi na kusema ovyo.

Aliendelea kumshambulia Nape kwa maneno akisema amejenga jeuri, kiburi, dharau na ulevi wa madaraka huku akidai kwamba kitendo cha CCM kupoteza wanachama zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja mkoani Arusha na sehemu nyingine wanachama 3,000 ni ishara ya hatari lakini, Nape amekuwa akiwaita wanaohama kwamba ni mzigo.

“Huyu Nape ni lazima atupishe. amekifanya chama kama mali yake, yeye ndiye mwenye jukumu la kueneza sera za chama na kutafuta wanachama wapya, lakini ndiyo kwanza anasema waachwe waondoke, Chadema wanatamba kila siku yeye hajali, huyu nasema ni gamba ni bora atupishe,” alisema.

Baada ya mashambulizi hayo, Maige alijitetea kwamba maneno yake dhidi ya Nape yasitafsiriwe kama ni kuulilia uwaziri: “Ni uchungu nilionao kwa chama changu kuona kila siku zinavyokwenda ndivyo tunavyopoteza idadi kubwa ya wanachama, tuliyemkabidhi jukumu la uenezi anasema hajali, sasa huyu si atupishe mapema kabla mambo hayajaharibika?”

“Nikuombe Mwenyekiti wa CCM Mkoa mzee wangu, Mgeja (Hamis), nafikiri ninyi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec ya CCM) mnapaswa kuchukua hatua haraka juu ya Nape... huyu sasa ni tatizo. Chama kitawafia hivihivi mkiona, avuliwe gamba maana tukisubiri ajivue atatuchelewesha, CCM ni wanachama si Nape.”

Wakati Maige akitoa maneno hayo, Mgeja alikuwa ameinamisha kichwa chake chini huku mikono ikiwa kichwani, lakini wana CCM na wananchi wengine walikuwa wakishangilia.

Aidha, Maige aliwalaumu viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya na kata ambao wamekuwa na tabia ya kutowatembelea wananchi katika maeneo yao kusikiliza kero zao wakisubiri mpaka viongozi wa kitaifa ndipo na wao wajitokeze.

“Jamani inakuwaje kiongozi mwenezi wa CCM kata ama wilaya anakaa kimya kabisa hakuna kazi yoyote anayoifanya! Viongozi wa aina hii wasipewe nafasi kabisa katika uchaguzi ujao. Tupate safu ya viongozi wenye kukifia chama chetu.”

“Maana kama watu wanakuja na Operesheni Sangara hakuna anayesimama kujibu, Operesheni Vua Gamba Vaa Gwanda hakuna aliyewajibu wala CCM haijatafuta operesheni yoyote ile kukabiliana nao, sasa wameanza Operesheni Movement For Change (M4C), sisi na Nape wetu kimya tunawaangalia tu wanazoa wanachama. Tuwe makini chagueni viongozi wenye uchungu na chama,” alisema Maige.

Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo za Maige, Nape alisema: “Nasubiri taarifa rasmi ya chama na nikiyakuta hayo nitajibu. CCM ina taratibu zake katika utendaji wake wa kazi. Katika taratibu hizo, ziara zote za viongozi wetu zinaandikiwa taarifa ambayo lazima zipite kwangu. Hayo unayosema yakinifikia, nitayajibu lakini siwezi kuzungumza bila hakika kwamba amesema.”

Bonyeza Hapa Ilikusoma Makala Inayozungumzia Utendaji wa Nape katika Nafasi aliyonayo Na Jinsi ambavyo unaweza kukiponza Chama cha Mapinduzi

Taarifa hii ni sehemu ya Taarifa ya Gazeti la Mwananchi, May 31 2012!

Wednesday, May 30, 2012

UDINI: TAMKO la WAISLAMU Dhidi ya WAKRISTO!

 Utangulizi
Oktoba 31, 2010 Tanzania ilifanya uchaguzi mkuu ambapo wananchi walipata fursa ya kumchagua Rais, wabunge pamoja na madiwani. Katika uchaguzi huo, Watanzania kwa ujumla wao walikichagua Chama cha Mapinduzi, CCM, kuongoza tena nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Hata hivyo, wakati wananchi wakiamini kwamba wanaongozwa na watu waliowapigia kura, matukio yanayoendelea hivi sasa yanaashiria serikali kutelekeza majukumu yake na kuwaacha maaskofu wakielekeza nchi wanakotaka.

Itakumbukwa kwamba awali kabla ya uchaguzi mkuu maaskofu walikuwa wametoa Ilani yao ya uchaguzi bila kueleza kipi chama chao kitakachosimamia na kutekeleza Ilani hiyo. Baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala, CCM, walishabikia Ilani hiyo na kuwatetea maaskofu. Kwa hakika taarifa za vyombo vya habari zilifahamisha kwamba baadhi ya watendaji waandamizi ndani ya serikali walishiriki katika kuandaa Ilani hiyo.

Ilipofika wakati wa kampeni hadi kuingia siku ya kupiga kura, ilikuwa imedhihiri kipi kilikuwa chama cha maaskofu ambacho walitarajia kitekeleze Ilani yao. Haikuwa tena jambo la siri kwani walisimama wazi wazi kuwaelekeza waumini wao wampigie nani kura. Na katika juhudi zao za kutaka wafuasi wao wawaelewe vizuri, maaskofu walithubutu hata kuweka kando mafundisho ya Biblia yao juu ya masuala ya uzinzi wakawahimiza waumini kumpigia kura mtu wanayemtaka bila kujali kwamba anakabiliwa na kashfa ya kupora mke wa mtu. Waliwaambia wasihangaike na maisha binafsi ya ndoa ya mgombea.
 
Hata hivyo, matokeo ya kura yalitoa majibu kwamba Watanzania walikuwa wameikataa Ilani ya Maaskofu.

Waislamu tumelazimika kukutana na kutoa tamko hili kwa sababu matukio yanayotokea hivi sasa yanaonesha kuwa wale ambao Watanzania walikataa kuwapa uongozi na Ilani yao iliyoandaliwa na maaskofu, ndio sasa wanaielekeza nchi pa kwenda huku viongozi wa CCM na serikali wakijitahidi kadiri ya uwezo wao kunyenyekea kwa maaskofu hao.

Tumeona na tumemsikia Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda akihangaika kuwapigia magoti na kuwaomba radhi maaskofu kule Sumbawanga. Tumesikia jinsi viongozi wanaojaribu kuwaambia maaskofu kwamba kama wanataka kuingia katika siasa wavue majoho na vyeo vyao vya kikanisa kama Padiri mwenzao waliyekuwa wakimpigania kuingia Ikulu, wanavyokemewa na kutakiwa wawaombe radhi maaskofu hao.
 

Lililo baya zaidi maaskofu walioshindwa kuwashawishi wananchi waipokee na kukubali Ilani yao, wamekuja na kampeni za kuchochea uasi kwa serikali iliyopo madarakani. Lakini pamoja na hali hiyo, viongozi wa CCM na serikali wamebaki wanagwaya. Hakuna aliyeweza kupata ujasiri wa kukemea hali hii. Kinyume chake Waziri Mkuu na Mzee John Samwel Malecela wanahangaika huku na kule wakiwapigia magoti maaskofu hao na kuwakemea wanaothubutu kuwakosoa.

Hali kama hii ni hatari kwa usalama na utulivu wa nchi. Ni hali ya kuchochea udini na kuweka ombwe la uongozi wa kisiasa ambao utazua balaa. Waislamu hatuwezi kukubali hali hii. Kwa hiyo, ama CCM na serikali vitekeleze wajibu wao wa kuongoza au kama wanaona hawawezi, basi waseme rasmi ili Maaskofu na wengine wenye Ilani zao za uchaguzi waingie tena ulingoni kuomba ridhaa ya Watanzania kuongoza nchi kuliko kuishi katika hiki kiini macho ambapo maaskofu na mawakala wao ndani ya serikali wameachwa waikokote nchi wanakotaka.
 

Kiini cha Hali hii ya Kisiasa
Hali hii ya kisiasa tunayoishuhudia leo nchini mwetu ni matunda ya mbegu liliyopandwa na kupaliliwa kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita. Wakoloni walikuwa na kanuni yao waliyoiita divide et impero yaani wagawe ili uwatawale. Huko Rwanda wakoloni waliwagawa wananchi kwa misingi ya kikabila. Watusi ambao ni watawala wapewe elimu ya juu na wanfundishwe kwa Kifaransa, na Wahutu ambao ni watawaliwa wapewe elimu duni na wafundishwe kwa Kiswahili. Ubaguzi huo wa kuwagawa raia wa nchi moja ulipandikiza sumu iliyokuja kusababisha Wanyarwanda kuuana.

Hapa kwetu wakoloni walitugawa kwa misingi ya dini. Kabla ya uhuru wa Tanganyika, wakoloni kwa kushirikiana na makanisa waliwaona Waislamu kama ni mahasimu wao kidini na kisiasa. Na kwa sababu hiyo serikali za kikoloni zikaweka mikakati maalum ya kuwakandamiza Waislamu katika maeneo matatu: kwanza kuwawekea vikwazo katika kutangaza dini yao ili wasiongezeke; pili kuwabana katika elimu na ili kuhakikisha kuwa Waislamu wanabanwa jukumu la kuwaelimisha Waafrika likawekwa mikononi mwa makanisa na kazi ya serikali ni kuzigharimia tu shule hizo. Lengo likiwa ni kuwabatiza Waislamu wachache watakaoruhusiwa kusoma, na tatu kuwabana katika ajira serikalini kwa sababu makanisa yote yalisisitiza kuwa kuwaajiri Waislamu serikalini ni kusaidia kuenea kwa Uislamu..
 

Kwa kuwa ubaguzi huo haukuwa na kificho chochote, Waislamu wengi walijitokeza kupambana na ukoloni kwa matarajio kuwa serikali huru itaondosha chuki na uadui huo dhidi ya Waislamu. Lakini msiba mkuu wa taifa hili ni kwamba kinyume chake, baada ya uhuru msimamo ukawa ni ule ule wa kuwaona Waislamu kuwa ni maadui wa kupigwa vita na mikakati ya kuwabana Waislamu katika maeneo yale matatu ikaimarishwa zaidi wakati wa utawala wa Nyerere. Kuanzia 1957 mkakati uliopangwa na Kanisa Katoliki ukawa ni kuhakikisha kuwa nafasi zote muhimu za uongozi na serikali zinashikwa na wao. [Taz. Confidential Diary – Tanganyika, March-April 1957, uk. 3-4 Maryknoll Central Archives, New York ]. 

Na ni mkakati huu ndio ambao Mwalimu Nyerere aliokuwa akimuhakikishia Askofu Rweyemamu mwaka 1970 kuwa anatumia mamlaka yake kama Rais na kama kiongozi wa TANU kuhakikisha kuwa anatoa upendeleo maalum kwa Wakristo ili wasimamie sera za Chama. Na kwamba amemteua padiri katika nafasi nyeti ya Chama si kwa sababu anajua siasa bali kwa sababu ni Mkristo safi. Lakini Nyerere huyo huyo akisimama hadharani alijidai kukemea udini. Na kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuliimarisha kanisa na kuwadhoofisha Waislamu, leo Kanisa lake limo katika mchakato wa kumtangaza Nyerere kuwa ni Mtakatifu!
 
Sivalon anaarifu katika kitabu chake kuwa mara baada ya uhuru Kanisa katoliki liliwahamasisha Wakristo wote na hasa watendaji wa serikali juu ya hatari ya Ukomunisti na Uislamu na walikusanya nguvu zao zote katika kukabiliana na maadui hao.

Matokeo ya Hujuma Hizo
Matokeo ya hujuma hizo za kichinichini ni kwamba katika sura ya nje na katika propaganda za kisiasa Tanzania ni nchi moja yenye mshikamano na umoja na kisiwa cha amani. Lakini uhalisia wa mambo ni kuwa Tanzania ni nchi yenye jamii kubwa mbili. Jamii ya Wakristo wanaopewa msaada, upendeleo, ulinzi na heshima, na jamii ya Waislamu ambao wanachukiwa, kudharauliwa na kudhoofishwa na serikali kabla na baada ya Uhuru.



Maazimio ya Waislamu
Kwa kuzingatia muktadha wa hali ya kisiasa ilipofikia hivi sasa, Waislamu tumefikia maamuzi yafuatayo:

(1) Maadam Mfumo Kristo umeimarika kiasi cha kuweza kuitisha serikali na viongozi wake na wakatishika, na maadam Mfumo huo Kristo una nguvu za kuweza hata kuvitisha na kuvikemea vyombo vya dola na vikasalimu amri, Waislamu tutake tusitake, kama alivyohadharisha Mh. Membe, ukweli unabaki kuwa hautapita muda mrefu, dhulma hii ya udini italisambaratisha Taifa letu, kama udini ulivyoisambaratisha Ivory Coast ambayo katika miaka ya 1960 na 1970 ilikuwa mfano wa kuigwa.

Hivyo basi wajibu wetu wa mwanzo ni kuufikisha ujumbe huu kwa Waislamu wote nchini, na kuwataka wazingatie kuwa kwa kuwa wanabaguliwa na kudhalilishwa katika nchi hii kwa sababu ya Uislamu wao, basi ni wajibu wao na wao kushikamana kama Waislamu.
 

(2) Kwa kuwa kila wanchosema Maaskofu ndicho kinachofuatwa na serikali, na kwa kuwa Maaskofu wamekwishatamka hadharani na kwa sauti kali kuwa katika nchi yetu hakuna kabisa udini na atakayesema kuna udini basi ni yeye ndiye anayetaka kuleta udini, na kauli hiyo kudakwa na mawakala wa Maaskofu katika serikali, ni dhahiri kuwa dhulma za udini zinazoendelea kuwakandamiza Waislamu miaka 50 baada ya Uhuru hazitaondoshwa na Katiba mpya. Hivyo wajibu wetu mwingine ni kupigania ukombozi wa Waislamu ili washiriki katika kuandaa katiba mpya wakiwa ni raia huru na sawa na wenzao. Waislamu popote tulipo tunao wajibu wa kuorodhesha dhulma zote za udini tunazofanyiwa na kupigania ziondolewe kwanza na kulipwa fidia.

(3) Kwa kuwa tangu ukoloni hadi leo Waislamu wanahesabiwa na serikali na Maaskofu kuwa ni maadui wa kupigwa vita na wasiostahiki haki sawa na wengine, na kwa kuwa Waislamu wameazimia kutokukubali tena kudhulumiwa na kuonewa kwa namna yoyote ile iwayo, ni wazi kuwa hakuwezi kuwa na katiba itakayoweza kulinda haki za madhalimu na wadhulumiwa kwa wakati mmoja. Ingawa kwa propaganda za kisiasa Tanzania ni nchi moja, lakini kiuhalisia ni nchi yenye jamii mbili zenye hadhi na haki tofauti kabisa. 


Umefika sasa wakati wa kugawana nchi ili Waislamu wanaochukiwa na kunyimwa fursa sawa na Wakristo waishi katika maeneo yenye Waislamu wengi na Wakristo waishi katika maeneo yenye Wakristo wengi. 

Mwalimu Nyerere alipigania kwa nguvu zake zote Nigeria igawanywe ili Wakatoliki ambao walikuwa wanadhulumiwa Nigeria wajitenge na waruhusiwe kuishi katika nchi ya Biafra. Na katika kijitabu alichokiandika 1966 Nyerere alisema madai ya kuhifadhi umoja wa kitaifa wa Nigeria hayana maana yoyote pale ambapo baadhi ya raia wa taifa hilo wanadhulumiwa. Ushahidi wa dhulma za Waislamu upo wazi. Kugawana nchi kutawawezesha Waislamu kuwa na Mahakama ya Kadhi na kujiunga na OIC bila ya kuwakera Maaskofu. Ni wajibu wetu kulifikisha hili kwa Waislamu wenzetu nchi nzima ili lijadiliwe zaidi kabla halijafikishwa rasmi

(4) Kwa kuwa hakuwezi kuwa na amani ya kweli bila ya haki, na kwa kuwa amani ya Tanzania inashikiliwa na Waislamu walioruhusu dhulma hiyo, Waislamu tunayo dhima kubwa kwa kustawi kwa Mfumo Kristo ambao sasa hapana shaka yoyote unalisambaratisha Taifa. Lakini kama alivyosema Nyerere, anayedhulumiwa ni mtu anayeteseka. Asipopambana na huyo dhalimu, yeye ataendelea kuteseka wakati dhalimu anastarehe kwa amani. Akiamua kupambana, wote yeye na dhalimu watateseka.  


Baada ya miaka 50 ya kuachia kundi moja la jamii likistarehe na hali Waislamu wanateseka, umefika wakati sasa wa kugawana machungu ya udini tuliyoyabeba peke yetu kwa miaka hamsini.

NYERERE na SERIKALI 2: Natofautiana Naye katika Hili!

Nyerere: Hakika Namheshim Sana
 Nimesoma sehemu hii hapa Chini ya hotuba ya Nyerere kuhusu kuanzishwa kwa Serikali Mbili katika Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania. Inawezekana ni kweli kwamba maelezo aliyokuwa anayatoa ya ukweli ndani yake, lakini ni ukweli pia kwamba yana Ombwe kubwa sana linaloacha maswali mengi ya msingi bila kujibiwa. 

Kwa Ufupi, namaanisha maelezo ya Nyerere kuhusu suala la Serikali Mbili - Ni Majibu Mepesi kwa Maswali Mazito! Inawezekana Nyerere hakuwa na majibu mazuri zaidi ya haya kwa wakati huo, au pia inawezekana kwa sababu alikuwa amezungukwa na watu ambao - aidha hawakuwa na UWEZO wa kuhoji au kurekebisha maamuzi yake binafsi - au HAWAKUWA NA UHURU wa kufanya hivyo. Hivyo matokeo yake ikawa kwamba kila atakalolisema yeye linafutiwa na makof mengi na vigeregere huku mkutano mzima ukiitikia kwa Sauti - ZIDUMU FIKRA ZA MWENYEKITI!

Maswala yangu ya Msingi

Kwanza: Nani aliamua Kuziunganisha Nchi hizi Mbili Zilizo Huru? 

Nyerere na Karume Wakisaini Hati ya Muungano
Kwa maelezo ya Nyerere, Tanganyika na Zanzibar "ZILIAMUA" kuungana! Sijui Nyerere aliposema "ziliamua" alikuwa anamaanisha nini? Kwamba ni Watu wa Wenye Nchi (wananchi) hizi mbili ndio waliamua au Ni VIONGOZI wa Nchi hizi Ndio waliamua?

Kama ni Viongozi Ndio waliamua - Basi Huu ulikuwa MSINGI MBOVU SANA wa kujengea Muunganoa wa Mataifa mawili YALIYO HURU! Muungano wa Nchi ni suala pana sana ambalo haliwezi kuachwa na kufanywa na Viongozi wachache wa KISIASA ambao wanatekeleza Ilani za Vyama vya Kisiasa - katika mataifa ambayo SI KILA RAIA ni mwanachama au hata kama ni "Mwanachama wa Kulazimishwa" - Basi SI Muumini wa vyama hivyo! 

Ndio maana LEO, ni muhimu sana suala la Muungano likarudishwa kwa wananchi wao ndio walijadili na kulitolea uamuzi. Kama Serikali ina wasiwasi kwamba wananchi hawatafanya maamuzi ambayo yenyewe inayaona ndiyoo "sahihi" basi ianze kwanza kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maamuzi gani yanaweza kuwa ni sahihi, lakini mwisho wa siku wnanchi ndio waamue wenyewe kipi ni sahihi!

PILI: Kumezwa kwa Zanzibar!

Karume
Nadhani kati ya hoja nyepesi MNO zilizo katika maelezo ya Nyerere ni suala la "Kumezwa" kwa Zanzibar kwa kisingizio cha Uchache wa Watu! Kwa kawaida, Nchi huendeshwa na MIFUMO, Mifumo ambayo kwa kawaida hutengenezwa kulingana na mahitaji ya Jamii/Taifa husika. Ni hoja nyepesi mno kusema ETI Zanzibar inaweza kumezwa kwa sababu ya Uchache wa Watu!

Nini kingefanyika?
Jambo lililotakiwa ilikuwa ni kuwekwa kwa mifumo mizuri ambayo ingehakikisha uwakilishi mzuri wa pande zote mbili katika ufanyaji wa maamuzi na katika uchangiaji wa gharama za huo Muungano! Taifa likiingia kwenye mahusiano au muungano na taifa lingine haliwezi kumezwa kutokana na Idai ya watu wake - litamezwa na mifumo isiyo mizuri ambayo hailipi nafasi ya kuonekana na kusikika katika hayo mahusiano!

TATU: Gharama za Kuendesha Muungano

Jambo la tatu ambalo halikuwa la Msingi kuliweka kama sababu ya Kuvunja Serikali ya Tanganyika na kuunda ya Muungano tu, lilikuwa ni suala la gharama. Kwa wakati huo (baada ya kuanzishwa kwa Muungano), hoja hii ilionesha mapungufu makubwa wakati wa uanzishaji wa muungano wenyewe. Kauli hii inamaanisha Mambo haya hayakufikiriwa wala kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa Muungano:


  1. Faida za Muungano: Katika hali ya kawaida, mtu hauwezi kuingia katika mahusiano pasipo kufanya mahesabu ya faida utakayoipata katika mahusiano hayo na iwapo faida hiyo inatosha kugharimikia Uendeshaji wa  Mahusiano hayo!
  2. Gharama za Kuendesha Mifumo itakayoundwa Chini ya Muungano: Suala la Nyerer kusema kwamba kuendesha Serikali ya Tanganyika ingekuwa gharama kubwa linaonesha ni kwa kiasi gani taathimini haikufanyika KABLA YA KUUNGANISHA NCHI kuona ni kwa kiasi gani Mifumo itakayozaliwa na Muungano (ikiwa ni pamoja na Serikali ya Muungano) itaweza kugharimikiwa. Hatua ya kuiua Serikali ya Tanganyika na kulivunja Bunge lake ilikuja kama Zimamoto ambayo ilitokana na kutokufanyika kwa taathimini ya kutosha kuuhusu Muungano husika kabla haujaundwa!
  3. Maelezo ya Nyerere yanaonesha kwamba haukufanyika Uchunguzi wa kina gharama za uendeshaji wa mifumo itakayoundwa chini ya Muungano - Huu ni upungufu mkubwa mno ambao unaleta matatizo hadi sasa kuhusu gharama za kuendesha muungano na Nani anufaike vipi na mapato yatokanayo na Muungano!
NNE: Hofu

Tayari Zanzibar Kuna Vurugu za Kuupinga Muungano!
Labla katika hoja zote zilizotumika kufanya maamuzi kuhusu nini kifanyike katika muungano, hakuna hoja isiyofaa kama ya "Hofu". Nyerere alisema ETI maamuzi ya kutengenza muundo uliopo wa Muungano YALITOKANA NA HOFU ya kumezwa kwa Zanzibar! Kama kuna jambo baya ambayo mtu anaweza akalifanya maisha yake basi ni kufanya maamuzi kutokana na hofu inayokuzunguka!

Kwa mara nyingine tena, HOFU hii ilitokana kwa kiasi kikubwa sana na Kutokuwashirikisha Wananchi katika Kufanya maamuzi - hivyo walioyafanya WALIOGOPA iwapo maamuzi yatakuwa mzigo wa gharama kwa wananchi - wananchi wanaweza kuinuka na kuyapinga! 

Na kwa upande mwingine, Hofu hii ilitokana na kutokufanyika kwa taathimini ya kina kuhusu gharama, faida na mahitaji mengine ya kuuendesha Muungano. Taathimini hiyo ingefanyika mapema, hakika tusingehitaji kufanya maamuzi kwa "Hofu" ya kitu Chochote!

Kweda Mbele....

Kimsingi, binafsi napenda uwepo wa Muungano, na ningependa uendelee. Tatizo kubwa lilipo ni kwamba Muungano wetu huu wa sasa Umejengwa kwenye MSINGI MBOVU ambao hauwezi kuuhakikishia huu Muungano UENDELEVU wake!

Najua kubomoa ni rahisi kuliko Kujenga, ndio maana wengi hupenda kukimbilia wazo la kuuvunja Muungano kuliko kutumia akili na nguvu zao kufikiria namna ya kuuboresha! 

Maoni ya Wananchi zamu hii LAZIMA yatumike Kuamua Hatma ya Muungano
Binafsi nalishauri taifa - kwa uongozi wa Serikali kubadilisha mawazo yake ya Sasa ya Hofu na Wasiwasi kuhusu maamuzi ya Wananchi. Serikaoli yetu - Iwapo inao uwezo wa kufanya hivyo - Inatakiwa ijipange zivuri na kuliwasilisha hili suala RASMI kwa wananchi kwa ajili ya kulijadilia na kulifanyia maamuzi.

Kitendo cha Serikali kulikwepesha suala hili lisiwemo kwenye Mjadala wa Katiba Mpya haimaanishi kwamba ndo inajihakikishia kwamba Muungano utadumu. Hali ikiendelea hivi kuna siku wananchi watagoma kuendelea kufanya jambo lingine lolote mpaka Suala la Muungano likizungumzwa na kufanyiwa maamuzi. Ikifikia huko, Ni hakika Nafasi hata ile ndogo iliyopo sasa ya Kuulinda na kuudumisha Muungano itakuwa imeshapotea, na HAKIKA, MUUNGANO UTAVUNJWA!




HOTUBA YA NYERERE AKIFAFANUA KUUNDWA SERIKALI 2 NA SIO 3 TANZANIA


Nchi mbili zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya katiba ni miwili;

Muungano wa serikali moja, au shirikisho la serikali tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake,na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka Fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.

Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, basi zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo Fulani Fulani. Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Zilikuwa ni nchi tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa nchi tatu zilizoungana kuwa Nchi moja yenye muundo wa shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, serikali ya shirikisho, na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.

Tanganyika na zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa ina watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000).

Muungano wa serikali moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya! Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa serikali Moja na Shirikisho la serikali tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha  serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha serikali ya shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha serikali ya shirikisho.

 Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha serikali yake ya watu 12,000,000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha serikali ya shirikisho la watu 12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni wazanzibari) na wala ya serikali ya shirikisho isingekuwa ndogo, hata bila gharama za mambo yasiyo ya shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.

Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali  ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na serikali moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha serikali mbili zenye uzito unaolingana.

Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo utakaotufaa zaidi.

IDD SIMBA Aburutwa Mahakamani!

Idd Simba















 
Tausi Ally na James Magai MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Usafiri  Dar es Salaam (Uda) Ltd, Iddi Simba, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka manane, likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh2.4 bilioni.Mbali na Simba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, washtakiwa wengine ni Meneja Mkuu wa Uda, Victor Milanzi na Mkurugenzi wake Salim Mwaking’inda ambaye pia aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Sinza (CCM).

Baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Benny Lincoln kumaliza kuwasomea mashtaka yanayowakabili, aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na wanaomba kesi ipangiwe tarehe ya kutajwa kabla ya kupangiwa  tarehe ya maelezo ya awali. Wakili Said El- Maamry anayemtetea Simba na mwenzake, Alex Mgongolwa waliiomba Mahakama impatie dhamana mteja wao hoja ambayo haikuwa na pingamizi kutoka kwa Lincoln ambaye alisema mashtaka yanayowakabili washtakiwa yanadhaminika.

Ili kujidhamini, Hakimu Mfawidhi, Ilvin Mgeta aliwataka washtakiwa kutoa hati ya nyumba na kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika, kila mmoja wao asaini bondi ya Sh500 milioni.

Baada ya kutolewa kwa masharti hayo, Simba aliwasilisha hati ya nyumba yenye thamani ya Sh8 bilioni na kuridhia wenzake waitumie kupata dhamana.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hati hiyo ya nyumba ni ya kiwanda cha Kays Hygiene Products Ltd, kilichoko Mikocheni eneo la Viwanda, Plot namba 23, kinachomilikiwa na Simba na mkewe Khadija.

Simba ni Mwenyekiti wa Taasisi ya mikopo kwa Wajasiriamali ya Pride (T) Ltd na Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam. Akisoma hati ya mashtaka jana Lincoln alidai kuwa  Septemba 2, 2009 Dar es Salaam, Simba na Milanzi  walikula njama ya kuchepusha fedha kinyume na Kifungu cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 11 ya 2007.

Lincoln alidai kuwa Simba na Milanzi walighushi barua  wakionyesha kuwapo kwa kiwango zaidi cha fedha kwenye akaunti zote za benki za Uda wakati wakijua kuwa si kweli. Aliongeza kuwa siku hiyo hiyo, Simba na Milanzi kwa pamoja, walichepusha Sh320 milioni wakijifanya ni malipo ya awali ya mauzo ya hisa katika shirika hilo fedha ambazo walijipatia kutokana na nyadhifa zao.

Aidha, kati ya Septemba 3, 2009 na Machi 31, 2010, Simba na Milanzi wanadaiwa kujipatia Sh320 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Robert Simon Kisena wakijifanya ni sehemu ya malipo ya hisa za Uda. Lincoln alidai kuwa washtakiwa Simba na Mwaking’inda kati ya Septemba 2009 na Februari 2011, wakati wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya nafasi zao waliharibu hisa  milioni 7,880,330 zisizotumika za Uda ambalo ni shirika linalomilikiwa kati ya Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zinazokadiriwa  kuwa na thamani ya Sh1,142,643,935  bila kufuata taratibu za zabuni kitendo ambacho ni uvunjwaji wa masharti ya Kanuni ya 63 (1) ya Ununuzi ya umma.

Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa  kati ya Septemba 9 na Februari 11, 2011 wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kugawanya hisa 7,880,330  zisizotumika za UDA kitendo ambacho ni uvunjwaji wa masharti ya vifungu vya ushirikiano katika kampuni  na Kifungu cha 74 cha Sheria ya Makampuni Sura ya 212 iliyorekebishwa mwaka 2002.

Mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru, alidai kuwa Februari 11, 2011 washtakiwa hao walishindwa kuchukua tahadhari zinazostahili, walimuuzia Simon hisa milioni 7,880,303 zisizotumika za Uda kwa bei ya Sh1,142,643,935  bila kufuata utaratibu wa zabuni ambao ungeweza kutoa nafasi kwa mnunuzi kutoa ofa ya bei inayolingana na thamani ya hisa hizo, jambo ambalo liliisababishia Uda hasara ya Sh2,378,858,878.80.

Tuesday, May 29, 2012

Zanzibar: KANISA Lininge LACHOMWA MOTO!


BAADA ya Kanisa la Assemblies of God kuchomwa moto katika vurugu zilizoanza mwishoni mwa wiki iliyopita, jana Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae nalo limechomwa moto.

Akizungumzia hali hiyo jana, kiongozi wa Kanisa hilo, Ambaros Mkenda, alidai kwamba Kanisa hilo lilichomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha uharibifu mkubwa.

Alidai Kanisa hilo lilichomwa moto jana saa 8.30 mchana na watu wanaohisiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, waliokuwa wakitoka katika Mahakama ya Mwanakwerekwe kusikiliza kesi ya wenzao waliokamatwa juzi.

Mkenda alidai kuwa watu hao waliwazidi nguvu walinzi wawili wa Kanisa hilo na kuvunja lango kuu la kuingilia ndani ya Kanisa na kuchoma moto na waliharibu madirisha na vifaa kadhaa vyenye thamani ya Sh milioni 20.

“Tunasikitika sana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika Kanisa letu ambalo lilikuwa tegemeo kubwa kwa wafuasi wapatao 2,000 wa eneo la Parokia ya Mpendae na jirani,” alisema Mkenda.

Mkenda alidai kuanzia juzi, viongozi wa makanisa mbalimbali waliwasilisha maombi yao Polisi kuhusu kupewa ulinzi katika nyumba za ibada, baada ya kupokea vitisho. Hata hivyo, Mkenda alidai ombi lao hilo halikutekelezwa na Polisi na uharibifu mkubwa ukatokea katika Kanisa la Assemblies of God la Kariakoo.

Wafuasi na waumini wa Kanisa hilo walikusanyika nje ya jengo hilo, huku vijana wakishikwa na hasira wakitaka kwenda kulipiza kisasi katika maeneo ya jirani wakidai wanawatambua vijana waliofanya vitendo hivyo.

Mmoja wa waumini wa Kanisa hilo ambaye ni mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Susan Kunambi alilazimika kuwatuliza wafuasi vijana wa Kanisa hilo waliopandwa na jazba wakitaka kulipa kisasi.

“Hakuna sababu ya kupandisha jazba na kutaka kufanya vitendo ambavyo vitasababisha hasara na uharibifu ... Kanisa siku zote linahimiza amani na upendo na si chuki,” alisema Kunambi.

Polisi walifika haraka katika eneo la tukio na kurusha mabomu ya machozi ili kutawanya makundi ya vijana waliojikusanya na wengine kurusha mawe.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alithibitisha kuchomwa moto Kanisa hilo na kusema ulinzi umeimarishwa katika baadhi ya maeneo ya nyumba za ibada yakiwamo makanisa. Baadhi ya mitaa ya Jang’ombe na Mwanakwerekwe njia zimewekwa mawe na vikundi vya vijana waliochoma mipira ya gari na kusababisha moshi mkubwa.

Vikundi marufuku Wakati huo huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepiga marufuku maandamano, mihadhara ya kidini na mikusanyiko isiyo na kibali.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema hayo wakati akitoa taarifa rasmi ya SMZ baada ya vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Uamsho baada ya kukamatwa kwa viongozi wao wa kidini.

Aboud alisema Serikali haitakubali kuona kikundi cha watu wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kuvuruga utulivu wa nchi kwa kisingizio cha kudai mabadiliko ya Katiba na imani ya dini.

“Wapo watu wanataka kuona tunarudi nyuma katika kipindi cha fujo na vurugu za kisiasa...wakati huo umepita,” alisema Aboud. Kutokana na hatua hiyo ya Serikali, mihadhara na maandamano kuanzia sasa italazimika kupata kibali kutoka taasisi husika ikiwamo Polisi. Alitaka wazazi wakataze watoto wao kujishughulisha na ushawishi wa kufanya vitendo vitakavyohatarisha amani na utulivu wa nchi.

Utulivu wajirudia mjini Jana hali ya utulivu ilirejea kisiwani hapa ikiwamo Mji Mkongwe na sehemu za mitaa ya Ng’ambo, huku wananchi wakifanya shughuli zao za maendeleo na biashara bila matatizo.

Maduka na huduma za usafiri viliendelea kama kawaida huku wafanyakazi wa Manispaa wakifanya usafi ikiwa ni pamoja na kuondoa matairi ya magari yaliyochomwa barabarani katika vurugu za juzi.



“Tunasafisha barabara zilizoharibiwa na waandamanaji kwa kuchoma moto mipira ya magari,” alisema Ali Juma mfanyakazi wa Manispaa ya Mji wa Unguja. Kamishna Mussa alisema Polisi waliendelea kuweka doria katika maeneo mbalimbali ya mji kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ.

“Tutaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ikiwamo nyumba za ibada ili kuhakikisha hakuna vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema Mussa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alionya kuwa suala la amani na ulinzi wa raia na mali zao halina mjadala na kuvihadharisha vikundi vinavyohatarisha amani, kwamba vitapambana na mkono wa Dola.

Dk Nchimbi aliyekuja hapa ili kukutana na viongozi wa vikundi vya dini na mihadhara na Polisi, alisema athari ya kuvunja amani na utulivu ni kubwa na wananchi wa Zanzibar wanafahamu vizuri mazingira yalivyokuwa miaka ya nyuma.

Alitaka viongozi wa dini wajifunze sheria za nchi na kuzifuata na kuwataka wasihusishe Uislamu na vurugu na fujo kiasi cha kuhatarisha amani ya nchi.

Pia alitaka wananchi walioharibiwa mali zao kwenye vurugu na fujo kutoa taarifa Polisi kwa hatua zaidi.

Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, alisema Polisi itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya nchi.

Watu 30 wakiwamo wafuasi wa Uamsho walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe kujibu mashitaka yakiwamo ya kuandamana kinyume cha sheria na ukorofi wa kuwashambulia polisi kwa mawe.

Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka katika makundi matatu tofauti; kundi la kwanza likiwa la viongozi wawili wa jumuiya hiyo; Mussa Juma Issa (57) na Mbarouk Said Khalfan (45). Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mohamed Ali Sheni ya kujikusanya kinyume cha sheria na kufanya maandamano ambayo yalianzia Uwanja wa Lumumba kupitia Msikiti wa Kwabiziredi na kumalizia uwanjani hapo.

Watuhumiwa hao walikana mashitaka na kupewa dhamana ya masharti ya Sh 300,000 kila mmoja kwa kiasi hicho hicho; walitimiza masharti na wako nje kwa dhamana hadi Juni 11 kesi yao itakapotajwa. Kundi la pili la watuhumiwa wengine sita walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Janet Sekihola ambayo ni ya uzembe, ukorofi na kushambulia polisi waliokuwa doria.

Watuhumiwa hao ni Abdulrahman Simai Khatib, Hashim Juma Issa, Martar Said Ramadhan, Mbwana Hamad Juma, Masoud Hamad Mohamed na Mohamed Juma Salum.

Kesi ya watuhumiwa hao iliahirishwa hadi Juni 11 itapotajwa huku baadhi yao wakitafuta wadhamini na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja kwa Sh 500,000.

Maimamu wawakana Jumuiya ya Maimamu na Mihadhara ya Jumaza, imesema waliofanya fujo na vurugu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi si wafuasi wao.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Muhidin Zubeir Muhidin ambayo pamoja na jumuiya hiyo ndizo taasisi zinazojishughulisha na mihadhara ya dini ya Kiislamu ambayo hutoa elimu kuhusu marekebisho ya Katiba.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Shehe Zubeir alisema jumuiya hiyo haijatuma watu kufanya fujo, kwa sababu katika dini hiyo ni makosa mtu kuharibu mali ya mwenzake. “Tunataka Waislamu wote na wafuasi wa Jumaza na Uamsho kuacha fujo na kurudi nyumbani kusubiri hatma ya viongozi wao,” alisema Shehe Zubeir.

Serikali ya Marekani imesema matukio yaliyotokea kwa siku mbili Zanzibar yanaweza kuchafua taswira nzuri iliyowekwa na visiwa hivyo, katika uchaguzi mkuu uliosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutokana na ghasia zilizotokea visiwani humo na kusababisha Kanisa na gari la kiongozi wa Kanisa kuchomwa moto.

“Kudumisha mazingira ya amani visiwani Zanzibar ambayo yanaruhusu utalii na maendeleo kuna maslahi kwa Wazanzibari wote na hata wageni waingiao visiwani humo,” alisema Balozi Lenhardt katika taarifa yake iliyotolewa jana Dar es Salaam.

Alisema ni muhimu kwa kila mtu kujizuia na kulinda maisha na mali za watu wasio na hatia na aliunga mkono waliozitaka pande zinazozozana kushirikiana kuleta amani na utulivu katika visiwa hivyo.

“Tunatambua umuhimu wa mjadala wa kisiasa unaoendelea lakini tunavitaka vyama vyote kuendelea kuufanya kwa njia ya amani na kidemokrasia zaidi,” alisema Balozi huyo.

Aliongeza kuwa anakubaliana na anaunga mkono hatua za haraka zilizochukuliwa na viongozi waandamizi wa kisiasa waliojitokeza kushughulikia masuala yaliyosababisha matukio hayo ya kusikitisha.

Selasini (CHADEMA): Mazishi ya Mama Yake Kesho!


Naendelea kuwashukuru Makamanda na Ndugu zangu wote mnaoniombea mimi na familia yangu kuweza kuvuka katika kipindi hiki kigumu tunachokipitia kwa majonzi na maumivu makubwa!... AHSANTENI SANA!...

Kesho tutafanya maziko ya Marehemu Mama yangu ambapo itatanguliwa na ibada ya mazishi kwenye Kanisa Katoliki Mkuu kuanzia saa sita mchana na baadaye kuzikwa nyumbani Kata ya Makiidi...

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA.. Jina la Bwana lihimidiwe!..
R.I.P my Mom!.

Joseph Selasini
Mb. Rombo (CHADEMA)

Monday, May 28, 2012

Muungano: TUUZUNGUMZE au TUUVUNJE!


Ni hivi majuzi tu mwezi uliopita Muungano wetu umetimiza miaka 48, kama kawaida tulifanya Sherehe. Lakini ukweli ni kwamba kwa Sasa Muungano wetu unahitaji kuadhimishwa kwa kitu kingine zaidi ya Maonesho kwenye viwanja vya mipira, magwaride ya majeshi na hotuba zilizojaa nukuu za Nyerere na za Karume.
Kuzaliwa kwa Muungano
Muungano wetu umedumu kwa miaka yote hii katika mazingira ya usiri na ulinzi mkuwa mkubwa wa "mada" hiyo. Lakini ukweli ni kwamba, zama hizo zimepita.

Maswali kuhusu Muungano

Sheikh Karume
Muungano huu ni wa nchi mbili ambazo kabla ya kuungana zilikuwa huru. Katika mazingira ambayo hayafahamiki vizuri kwa Watu wa Nchi hizi mbili mpaka sasa - hususan vijana - nchi hizi ziliungana na kuunda Nchi Moja iliyokuja kuitwa Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania. Maswali mengi yaliyobaki tangu kuundwa kwa Muungano huu hadi leo ni pamoja na:
  1. Majadiliano baina ya Nchi hizi mbili ili ziungane yalifanyika wakati gani na kwa muda gani?
  2. Ni wajumbe wapi na wapi walioziwakilisha nchi hizi mbili katika majadiliano hayo?
  3. Ni yapi yaliyokuwa makubaliano ya mwisho baina ya pande hizi mbili?
  4. Makubaliano ya majadiliano ya pande hizo mbili yalijadiliwa na Wananchi wa Nchi husika (moja kwa moja au kupitia mabunge yao) na kuridhia kuunganishwa kwa Nchi zao?
  5. Nakala ya Mkataba/Makubaliano baina ya nchi hizi mbili yalifikishwa kwa wananchi na kusambazwa kwa uwazi ili waelewe misingi ya kuunganishwa kwa nchi zao?
  6. Nani anayenufaika Zaidi na Nani anayepoteza Zaidi kwenye huu Muungano?
Maswali haya yote - pamoja na mengine mengi - inawezekana katika nchi hii kuna watu wana majibu yake, lakini ukweli unabakia kuwa walio na hayo majibu ni wachache (kama wapo kweli). Kwa misingi hiyo Muungano tangu zama hizo mpaka leo umebakia ni kama kitendawili ambacho wananchi wengi hawawezi kukitegua. Na wengine wamefikia hatua ya kuamini kuwa Siri ya Muungano alikuwa nayo Nyerere na Karume (ambao walikuwa marais wa Tanganyika na Zanzibar kwa wakati huo) na sio Watanzania wote!

Mwisho wa Zama Umefika

Wanasiasa na viongozi wa Serikali kwa ujumla walijitihidi sana kwa miaka kuutunza, kuudumisha na kuulinda Muungano kwa njia mbali - kubwa ikiwa ni kutoruhusu ujadiliwe - na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini ni wazi kwamba Zama hizo za "Giza" kuuhusu Muungano zinapita kwa kasi - kama sio kwamba zimeshapita kabisa mpaka sasa!
Zanzibar: Wanawake Barabarani kutaka Muungano Upigiwe Kura!
Zama za kuulinda na Kuudumisha Muungano kwa kutumia mbinu ya kuuficha usijadiliwe waziwazi zimefikia mwisho wake sasa.

Mapinduzi ya Uarabuni Yamewaamsha Watanzania!

Watanzani wa leo - hususan baada ya kushuhudia "Mapinduzi ya Umma" katika nchi kadhaa za Kaskazini mwa Afrika na Uarabuni - leo hii wengi wao nao wanaamini kwamba jambo lolote linawezekana kwa nguvu za Umma, hata hapa Tanzania - NA INAWEZEKANA WAKO SAHIHI! Na huu ni ukweli usiopingika kwamba Hakuna Nguvu Duniani hapa inayoweza kuishinda Nguvu ya Umma - hata Serikali na Majeshi haziwezi kuzima nguvu ya Umma - Umma uliojiunga na Kusimama pamoja!


Mubaraka: nguvu ya Umma ilimng'oa


Ukiwa unaongoza watu kama hao, ni wazi kwamba unapaswa kuwa makini sana na mambo ambayo wao wanayataka au kuyaona ni ya kipaumbele na kuyapatia nafasi stahiki - badala ya kudhani unaweza kuwanyamazisha kwa "kujifanya" unashughulikia mambo mengine ambayo kwako ndiyo ya muhimu zaidi - UTAKUWA UNAJIDANGANYA!

Maswali yanayobaki

Utaratibu huu wa sasa wa "kuulinda na kuudumisha" Muungano unaweza kudumu iwapo tu Nchi ingeendelea kutawaliwa na CCM kwa Asilimia 100 siku zote (kutokana na sababu zinazojulikana). Lakini hilo kwa sasa hilo halipo tena! CCM Inazidi kupoteza majimbo na Ushawishi miongoni mwa raia kwa kasi kubwa kila kunapokucha. Vyama vyenye Upinzani vilivyojawa na hamu ya kuhoji kila Sera ya CCM ndivyo vinazidi kupata mvuto na kusikilizwa zaidi Nchini!

Sera za CHADEMA zinamaswali mengi kuhusu Muungano!
MOJA: Kwa Mfano, Iwapo CHADEMA Itachukua dola mwaka 2015 na ikaamua kuigawa nchi katika Majimbo kama sera yake inavyoelekeza kwa sasa, ZANZIBAR Itakuwa katika jimbo Lipi? Je, Itabakia ba hadhi yake ya Sasa ambayo hata hivyo haijulikani Vizuri - au kutakuwa na Badiliko?

PILI: Iwapo Jumuiya ya Afrika Mshariki Itaanzisha Shirikisho la Kisiasa (kuwa na rais Mmoja wa AM), Zanzibar itakuwa mgeni wa Nani chini ya huo Mfumo? (maana muundo wa Muungano wa Sasa hauko wazi katika hilo pia)!... na mengine mengi!


Dalili kutoka Zanzibar

Zanzibar Leo! - Tatizo ni Muungano!
Mambo yanayoendelea kwa sasa visiwani Zanzibar - kwa hakika ni ishara kubwa sana kwamba zama za kuulinda na kuudumisha Muungano kwa mbinu ya Ukimya imepitwa na wakati. Vurugu zinazoendelea kwa sasa huko Zanzibar - hususan zinapoanza kuhusisha hisia za Ubaguzi dhidi ya "wabara", ni wazi kwamba Siku sio nyingi zitaweza kuigia bara, na kundi la kwanza kutafutwa wanaweza kuwa Makamu wa Rais na Mawaziri kutoka Zanzibar - kabla ya kuingia mitaani na kuwageukia wapenmba waliojazana kwenye miji ya Tanganyika!


Katiba Mpya SIO Jibu!

Wakati vuguvugu la kudai katiba mpya lilipoanza kushika kasi mwishoni mwa mwaka juzi (wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu) na hatimaye Serikali ikazidiwa nguvu na Upinzani na kukubali Madai ya CHADEMA ya kuundwa kwa katiba mpya (ikumbukwe CCM haikuwa na Mpango wa Kuunda Katiba Mpya Tanzania wakati wa Awamu ya Pili ya Kikwete Madarakani), binafsi nilidhani kwamba hii ndiyo ingekuwa fursa muhimu sana kwa Serikali "kujivua lawama" za usiri na tatizo la Muungano kwa kuruhusu wananchi waujadili Muungano huu wakati wanajadili katiba mpya na kuutolea majibu! HAIKU WA HIVYO!

Uundaji wa Sheria ya Katiba Mpya bado ulighubikwa na "WOGA" ule ule wa miaka neda rudi, na hatimaye Suala la Muungano kuondolewa kwenye masuala yatakayojadiliwa! Ukweli ni kwamba hili NI KOSA, na kuna "mtu" atalilipia hili kosa!

Nini Kifanyike?

Ushauri wangu kwa Rais Kikwete na Serikali kwa ujumla ni kutambua na kufanya yafuatayo:
  1. Kwanza, ni muhimu kwa Kikwete na Serikali yetu ya leo kutambua kwamba Watanzania wa leo sio wa miaka ile ya Uhuru - au enzi za Nyerere! Watanzania wa leo sio watu unaoweza kuwaridhisha kwa "maneno mepesi" huku ukikwepa kujibu maswali yao Magumu?  Watanzania wengi wanataka waelezwe - kabla hawajashawishiwa kuendelea nao au kuuvunja - ni nani anayenufaika zaidi na huu Muungano na Nani anayepunjwa zaidi kwenye huu Muungano. Hili ni swali gumu ambalo linahitaji majibu magumu, zaidi ya zile hotuba ambazo tumezoea kuzisikia za kuuremba na kuupamba Muungano pasipo takwimu na Vielelezo!
  2. Serikali itafute njia nzuri ya kulileta Suala la Muungano katika mjadala wa Wazi wa Kitaifa. Kama nilivyosema hapo juu - Fursa kubwa ya kufanya hivyo ilikuwa ni Mjadala wa Katiba. Ninaposema "njia nzuri" ninamaanisha kwamba iwapo Serikali tayari ina mtazamo wake ambao isingependa ubadilishwe - hata na "wenye nchi" wenyewe (wananchi), basi ijipange kuuleta huu mjadala kwa namna ambayo itawavuta Watanzania wengi kuunga mkono matakwa ya Serikali ya kuudumisha!
Kinyume cha Hapo, kuendelea kuuficha-ficha na kuutetea Muungano kwenye Hotuba pasipo kujibu maswali ya Msingi ya Wananchi, kutazidi kuongeza idadi ya watu wanaotaka kujua kiini hasa cha "Usiri"huo, na hapo ndipo tatizo litakuwa kubwa zaidi hata ya hapa lilipo leo!


Watanzania kwa Sasa wanahitaji Majibu magumu Zaidi
 Kuendelea kukwepa kuujadili Muungano SIO kuulinda wala kuudumisha kama ambavyo wanasiasa wetu wengi wanaweza kuwa wanajidanganya kwa sasa. Kitendo hicho ni kuzidi kuongeza watu wanaouhoji na wale wanaotaka majibu mazidi. Kwa kadri idadi ya watu wanaouhoji na kuutilia mashaka Muungano itakavyoongezeka ndivyo Uwezekano wa Kuwapa Majibu Sahihi na kuwaridhisha utakavyozidi kuwa mgumu - NA HUO NDIO UTAKUWA MWISHO WA MUUNGANO!

The Union: It's Now or Never!

"UGAIDI" Zanzibar: Tamko la Waislam!

 THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION

P. O. BOX: 1266
Tel: +255-777-419473 / 434145-
FAX +255-024-2250022
E-Mail: jumiki@hotmail.com
MKUNAZINI ZANZIBAR

Tarehe 27MAY2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika Uislamu.

Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila
kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na  likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala zisiharibiwe.

Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali, mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na  yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi  zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na  utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil ya kulinda haki za wengine.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu kwa watu wote.

WABILLLAH TAWFIQ