Monday, August 19, 2013

ZITTO: Tume ya KATIBA Ilipotoshwa


Zitto Kabwe ametahadharisha kuwa mtu aliyeishauri Tume ya Katiba kudhani kuwa Chanzo kikuu cha mapato yake kinaweza kuwa ni Ushuru wa Bidhaa yawezeka HAJUI, au ALIIDANGANYA Tume. Maneno haya yanamaanisha kwa upande mwingine kuwa iwapo tume haikushauriwa na mtu kuhusiana na hilo - basi ni aidha HAIJUI ilichokisema au Inajidanganya yenyewe!

Nimesoma maneno haya za Zitto Kabwe kwenye post yaka kwenye Facebook, nikaona yana mashiko na yanatakiwa kutafakariwa kwa kina. Tahadhari yake hii kuhusu  mapato ambayo yanadhaniwa ndiyo yanaweza kutumika kuendeshea serikali ya Muungano yamekuja siku chache baada ya gezeti la Mwananchi kumnukuu Mmoja wa Wajumbe wa Tume hiyo - Humprey Polepole akiwaambia wananchi huko Wilayani Nanyumbu kwamba Hakuna gharama kubwa na kwamba chanzo cha mapato tayari kimekwisha kuainishwa!

Chanzo kikubwa ambacho ndicho kinatakiwa kutoa mapato ya kuiendeshea Serikali ya Muungano ni Ushuru wa Bidhaa - ambao kwa mujibu wa Zitto, mapato yatokanayo na chanzo hicho kwa mwaka 2012/13 ni Shilingi Trilion 1.5 pekee - Mapato ambayo hayatoshi hata kuendesha Wizara Moja tu ya Muungano ambayo ni ya Ulinzi na Usalama!!!

Soma Taarifa ya Gazeti la Mwananchi likimnukuu Humprey Polepole kwa kubonyeza hapa.

Post ya Zitto:

"Rasimu ya Katiba ibara ya 215 inasema vyanzo vya mapato ya Muungano, kikubwa, ni ushuru wa bidhaa. Wajumbe wa Tume wanasema walifanya hesabu sawa sawa na fedha hizo zitatosha kuendesha Muungano. Lazima aliyewafanyia hayo mahesabu ama aliwapotosha au hajui. 

Mwaka 2012/13 Ushuru wa bidhaa (ndani na nje) uliingiza mapato ya tshs 1.5 trilioni tu. Fedha hii inatosha kuendesha Wizara ya Ulinzi peke yake! Haitoshi hata kuhudumia Deni la Taifa (ambalo mkopaji ni Jamhuri ya Muungano). Huu muungano utaendeshwaje? 

Rasimu inapaswa kufanyiwa kazi sana. Nahisi Tume ilikuwa na haraka na haikutafakari kwa kina baadhi ya masuala. Mambo ya Muungano inabidi yaangaliwe upya kabisa ili kuboresha mfumo wa Serikali 3 unaopendekezwa ikiwemo kuzuia Washirika wa Muungano kuunda vikosi vyao vya kijeshi, Ulinzi na usalama. Suala la biashara ya kimataifa na hata suala la usimamizi wa maliasili (regulatory function)."

Binafsi naamini kuna mambo mengi kuhusiana na Muungano na Muundo wa Serikali tatu ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa kina zaidi - japo tunataka kuharakisha ili kuepusha mjadala wa kina kwa sababu tunadhani ETI ni suala "sensitive" sana!

No comments:

Post a Comment