Wednesday, December 28, 2011

"Tanzania is IRRELEVANT" - Barak!


Marekani rafiki "mkubwa" wa Tanzania na Israeli
Tukio
Alipokuwa akihojiwa na Mtangazaji Ayala Hasson wa Kituo cha redio cha Israeli, waziri wa Ulinzi wa Israeli Ehud Barak alitoa maelezo ambayo kimsingi yalimaanisha Tanzania ni "Irelevant" kwa Israel. “Germany, France and England are not Tanzania, Mauritania or Tripolitania [jimbo mojawapo nchini Libya],”.... alieleza Ehud na kuongezea “These are very important, very relevant countries and we don’t have an interest in increasing tensions with them or making them bitter enemies.”


Reaction ya Tanzania
"Balozi wa heshima" wa Tanzania nchini Israel, Kasbian Nuriel Chirich alimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli kulaani kauli hiyo ya Barak na kumualika kiongozi huyo kuitembelea Tanzania. Katika barua hiyo, "balozi" huyo pia alilaani kitendo cha Waziri Barak kuishusha hadhi Tanzania na kuilinganisha na nchi ambayo, kimsingi haipo hapa duniani (Tripolitania) ambalo ni jimbo tu nchini Libya!


Ehud Barak, Waziri wa Ulinzi wa Israel
aliyesema  Tanzania ni "Irrelevant" kwa Israel
Ukweli wa Hali halisi!
Watu wengi wamejitokeza hapa Tanzania kulaani hiyo kauli ya Barak na kumtaka aifute na kuomba msamaha. Labda wako sahihi, lakini mimi napinga! Na sababu kubwa ya mimi kupinga NI UZALENDO WANGU!


Maneno ya Barak ni ya kweli kwa kiasi kikubwa sana - "Tanzania is Irrelevant to Israel" na hata kwa mataifa mengi sana pia duniani! Mimi ninaamini kuna mataifa mengi mno duniani - hata wale wanaotupatia misaada ambao nao wanaiona Tanzania iko irrelevant kwao! Tofauti tu ni kwamba hao wengine ni wanafiki wakubwa hivyo wanapokuwa na viongozi wetu hujitahidi kuwaonesha kwamba wanawathamini kama watu na kama viongozi wa "taifa" fulani - ambalo ni irrelevant kwao - though!


Unapokuwa na taifa lenye rasilimali na utajiri mkubwa sana kama Tanzania lakini viongozi wake wanazurura duniani kote kuomba-omba misaada na wala hawana sauti katika masuala ya msingi ya kidunia - na hata yale ya nchi zao wenyewe - hizo nchi ni irrelevant kwa taifa kama Israel!


Mataifa mengi ambayo yana nguvu na ushawishi mkubwa hapa duniani - ikiwa ni pamoja na kwa Israel - ni yale ambayo, kwa kutumia rasilimali na utajiri wao wa asili na wa kutafuta, yameweza kuwa na nguvu na sauti kubwa duniani kiasi cha kuweza kuheshimiwa na Israel. Mataifa kama hayo aliyoyataja Ehud na mengine kama Urusi, Iran n.k. yemtumia vizuri utajiri wao na rasilimali zao kujiweka kwenye ramani ya "relevance" duniani kiasi kwamba Israeli inaelewa haina namna zaidi ya kuwa na mahusiano mazuri na nchi hizo.


Ehud anafahamu kabisa kuwa na urafiki au mahusiano mazuri na nchi kama Tanzania ni kujivutia omba-omba asiye na faida karibu yako. Niambie iwapo mahusiano kati ya Tanzania na Israeli yataimarika, ni nini zaidi Tanzania itakachokitafuta katika mahusiano ZAIDI YA KUOMBA-OMBA MISAADA kila iitwapo leo???


Huu ni ukweli ambao naamini hata Marekani wanaufahamu, ila uzuri tu ni kwamba wao ni WANAFIKI SANA kuliko Israel, hivyo wanaweza ku-pretend kutuheshimu wakati behind the curtain wanatuona kuwa tuko "irrelevant" kama Israeli tu wanavyotuona.


Ukweli ni kwamba kwa hali ya sasa ya Tanzania, hususan kwa uongozi na sera tulizo nazo na tunazotumia, TANZANIA IS IRRELEVANT kwa namna nyingi sana kwenye ramani ya dunia!


Masuala makubwa yanayoikabili Israeli kwa sasa ni pamoja na Nyuklia za Iran, Mapinduzi nchi za Kiarabu, Migogoro ya ndani ya Kiuchumi, Suluhu na Wapalestina n.k. Katika haya masuala yote, Tanzania haina nafasi yoyote relevant ya kuifaa Israel, hivyo tusimlaumu Ehud kwa lolote - yuko sahihi kabisa.


Hili linapaswa tu kuwa changamoto kwetu kama taifa, ni kwa muda gani tutaendelea kufanya mambo ya kulidhraulisha na kulitukanisha taifa letu kama kuwa na viongozi maomba-omba wanaozunguka dunia nzima kuomba misaada huku wamegawa utajiri wa taifa na rasilimali zake "bure' kwa wazungu?


Tunayo kazi ya kuifanya Tanzania Relevant! I SUPPORT ISRAEL!

USIWEKE Malengo Mwaka Mpya 2012!

Mojawapo ya mambo ambayo yamezoeleka na ambayo hufundishwa na kuelekezwa sana ni watu kuweka malengo kila mwaka mpya unapofika. Katika tafakari yangu ya leo, nakueleza ni kwa nini USIWEKE malengo yako na mipango yako katika wakati huu wa sikukuu za Mwaka Mpya! Makala hii inaangalia "miaka-mipya" yote, sio 2012 peke yake - hata hivyo.


Msimu huu ukoje!
Msimu wa sikukuu za Christmas na Mwaka mpya - kupita misimu mingine ya sherehe katika mwaka, hujawa na hisia nyingi sana. Hisia hizi nyingi huwa nzuri, mbaya na wakati mwingi huwa ni mchanganyiko. 


Hisia nzuri huwa ni za furaha kwa watu kumaliza mwaka, watu wengi huwa wako likizo, watu wengi ndipo hukutana na kujumuika na familia na jamaa zao ambao hawajonana kwa muda mrefu, ni msimu wa Ibaada nyingi na kuwa "karibu na Mungu", ni muda ambapo watu wengi huwa na pesa nyingi za kutumia - kutokana na malimbikizo ya mwaka mzima na Mikopo n.k. Kwa ufupi ni msimu ambapo hali ya kimaisha ya watu hubadilika sana - tangu kiuchumi, kijamii na hadi kihisia.


Wakati gani SIO wa Kuweka Mipango na Malengo
Kila mtu katika maisha yako unatakiwa kuwa na malengo na mipango ya kutekeleza hayo malengo yako. Watu wengi sana wamekuwa wakiweka malengo mengi wakati mwingine bila kuweka mipango ya kutekeleza malengo hayo. 


Wengine huweka malengo na mipango yake lakini wengi sana katika makundi haya mawili mwishoni huwa hawatekelezi hata mojawapo ya mambo hayo! (Jiulize wewe binafsi ni mambo mangapi ulishawahi kuyakusudia au kuyapanga lakini hukuyafanya katika muda wote uliokuwa unadhani utayafanya - Na wakati mwingine ULISAHAU hata kama ulishawahi kuwa na Malengo au Mipango).


Moja ya makosa makubwa ambayo watu huyafanya katika maisha yao wanapokuwa wanataka kuweka mipango na malengo huwa ni KUTOJUA WAKATI MUAFAKA wa kutengeneza Malengo na Mipango ya Kimaisha!


Kama ilivyo katika maeneo mengine ya kimaisha, mtu huwa hushauriwi hata mara moja kufanya maamuzi (yenye nafasi kubwa au muhimu maishani) katika wakati ambao hisia zako, fikra zako au hata afya yako haiko katika hali yake ya kawaida! Hii inamaanisha, kwa mfano, haishauriwi kufanya maamuzi ukiwa na hasira, ukiwa na furaha / hisia kubwa ya furaha (ambayo huwa sio hali yako ya kawaida kimaisha) n.k. 


Hii ni kwa sababu maamuzi mengi utakayoyafanya katika wakati huo yatakuwa yana-"reflect" zaidi hali yako ya wakati huo (hususan hisia) - ambayo SIO hali yako ya kawaida maishani!


Watu wengi ambao wamefanya maamuzi wakati wakiwa na hisia ambazo sio wanazoishi nazo katika maisha ya kaiwaida (kama hasira) wamejikuta wakiishia pabaya baada ya maamuzi yao NA WAO HUJUTA pale hasira zinapokuwa zimetulia. Maamuzi mengi yanayofanywa katika hasira huelekea katika kususa, kugombana / kutukana, kisasi n.k. Mwisho wake huwa ni kufukuzwa kazi, kufungwa jela, kuharibu mahusiano n.k.


Vivyo hivyo kwa watu ambao hufanya maamuzi wakiwa na furaha / hisia za furaha kupita ile wanayokuwa nayo katika maisha ya kawaida ya kila siku - hujikuta wakijutia maamuzi yao na wakati mwingine kubaini kuwa walikosea - BAADA ya kuingia hasara kutokana na maamuzi yao. 


Watu wengi katika hisia za furaha kupita kawaida hujikuta wakiahidi kutoa michango mikubwa kwa ajili ya sherehe au matukio mbalimbali, wakitoa ahadi ya kufanya mambo makubwa/mazuri kupita uwezo wao au utashi wao wa kawaida wanapokuwa hawana hisia hizo! Pale hisia zinapotulia wengi hubadilisha maamuzi yao au kukana kwaba sio wao walioahidi.... n.k.


Maamuzi yako Uyafanye Lini?
Wakati mzuri wa kufanya maamuzi ni pale unapokuwa umerudia hali yako ya kawaida ya kimaisha na kihisia. Subiria huu msimu wa sikukuu uishe, baada ya kuwa umesharudi katika hali yako ya kawaida, hisia za furaha na shamra-shamra zimeshatulia, hisia za hasira kutokana na madeni na makwazo mengine ya familia, ndugu na wapenzi zimeisha - ndipo ukae chini ufanye taathimini ya pale ulipo na ndipo uamue ni wapi unataka kwenda.


Usiruhusu hisia (nzuri au mbaya) za msimu huu wa sherehe na mapumziko ndizo zikaongoza maamuzi yako ya malengo na mipango, muda si mrefu utayaona maamuzi yako hayakuwa sahihi na hayahalisiki kwa hiyo utarudi  kwenye mfumo wako wa "maisha kama kawaida".


ZINGATIA: Muda unaoishi katikati ya Misimu ya Sherehe ni Mchache kuliko unaoishi katika maisha yako ya "kawaida". Usiweke Malengo na Mipango kana kwamba Maisha yako yote unaishi kwenye "sherehe".


Malengo yako Yaweje?
Muda wa kuweka malengo utakapofika - baada ya 'mavumbi" ya sherehe kutulia, baada ya kulipa karo za watoto na kulipa madeni uliyokopa ili kufanikisha sherehe na safari za mwisho wa mwaka, kaa chini uweke malengo na mipango ya kuyatekeleza malengo hayo. Malengo yako ni muhimu yakawa na sifa zifuatazo (pamoja na nyingine):


Moja; Yawe Yanahalisika! Moja ya mambo ambayo huwakwamisha watu wengi sana wanapotaka kutekeleza malengo waliyojiwekea huwa ni pale wanapobaini kuwa hayahalisiki katika hali yake halisi ya kimaisha! Hakikisha malengo yako yanazingatia hali halisi uliyo nayo kwa sasa na hali halisi ya fursa na uwezekano wa wewe kuweza kuyafanya hayo na kuyanikisha hayo unayoyapanga kwa muda unaoupanga.


Ukiweka mipango ya mambo ambayo hayahalisiki mwishoni utakuja kubaini kwamba yameshindikana na utakuwa "frustrated". Watu wengi wanapoona mipango yao imekwama na haitekelezeki huwa wana kata tamaa na kujifariji kwamba "kumbe maisha ni kubahatisha" na baada ya hapo huanza kuendesha maisha yao bila mipango wala malengo wakisubiri "bahati"! USIJI-"FRUSTRATE" MWENYEWE KWA KUWEKA MALENGO YASIYO HALISIKA!


Pili; Yawe na Kikomo cha Muda! Usiweke malengo ambayo yako "open-ended" kwenye suala la muda. Usiweke malengo ambayo unadhani utayafikia "muda wowote" ukiwa bado unaishi - HAPANA! Ni lazima malengo yako yawe na kikomo cha Muda. Hii inamaanisha kwamba unapaswa kujiwekea "ratiba" ya kuyatekeleza na kuyafikia malengo yako.


Kwa Mfano, sema ninataka kufanya jambo hili na hili ndani ya miaka mitatu ijayo, kisha uivunje-vunje hiyo miaka mitatu katika muda mfupi-mfupi kama wa miezi Sita-Sita ua mwaka Mmoja-Mmoja. Hii itakuwezesha kuyaona majukumu yako ni madogomadogo na yanayobebeka kwa urahisi (kwa miezi sita-sita kwa mfano), kuliko ukiyaangalia kwa ukubwa wake wa miaka mitatu! Pia hii itakusaidia kufuatilia maendeleo yako katika kutekeleza mipango yako ya kufikia malengo.


Tatu; Malengo yatokane na KUSUDI LA MAISHA yako! Hiki kigezo ni cha muhimu sana na kinapaswa kuwa cha kwanza kwa kipaumbele. Hata hivyo, kutokana na upana wa suala hili, hapa nitakupa maelezo machache yatakayokuwezesha kuelewa - japo kwa uchache.


Kwa ufupi ninachokimaanisha hapa ni kwamba KILA MTU UNAPASWA KUWA NA KUSUDI LA MAISHA YAKO! Kila mtu unapaswa kuwa unaelewa maisha yako kwa ujumla hapa duniani yapo kwa kusudi gani kubwa / la jumla ambalo ndilo unalitumikia na unalenga kuwa umelifikia mwishoni mwa maisha yako!


Watu wengi kwa kutokuwa na KUSUDI KUU la maisha huwa wanaweka malengo madogo-madogo na ya muda mfupi-mfupi kama mwaka mmoja-mmoja au miwili-miwili na wakati mwingine huwa wanayatekeleza na kuyafanikisha. 


Lakini kwa kuwa malengo yao yanakuwa hayaongozwi na "Picha" moja kubwa ya Kusudi la maisha yao kwa ujumla, hadi wanapozeheka wanakuwa hawana kitu chochote cha maana cha kujionesha wao wenyewe na watoto wao kwamba ndicho walichokifanya katika maisha yao. Watu hawa wanakuwa walifanikisha tu-mambo twingi tudogo-todogo na ambato hatu-link kwa hiyo tunakuwa hatuwezi kutoa picha kubwa ya mafanikio yao maishani!


HAKIKISHA: Kila lengo na tendo lako maishani linakusaidia na kukusogeza karibu zaidi na kulitimiza kusudi lako kuu la maisha. Usifanye mambo ambayo haya-link na hivyo mwishoni yanakuwa hayatoi picha yoyote kubwa ya mafanikio yako maishani!


Na Mwisho (kwa leo); Weka Malengo Yanayopimika. Hakikisha kuwa malengo utakayoyaweka yanaweza kupimika. Hii inamaanisha kuwa wewe mwenyewe au wengine watakaokuwa wanakusaidia kufuatilia mafanikio yako waweze kupima na kuona kwamba ni kweli kuna jambo limefanyika na limefanikiwa. Usiweke malengo ambayo hata yakifanikiwa hakuna tofauti inayopimika itakayoonekana katika maisha yako au eneo unalolifanyia kazi.


Mwandishi wa Makala Hii Ni Mwalimu ambaye hutoa Mafunzo na Semina kwa makundi mbalimbali kuhusiana na Namna ya Kuchagua, Kupanga na Kufanikisha Maisha Yako! Anapatikana kwa Namba 0659 219 046 au 0783 666 771.


Kama Makala hii umeipenda na Imekusaidia kwa Namna Yoyote, Mtumie na Rafiki yako Pia kwa Kubonyeza Alama ya Email hapa Chini.

Friday, December 23, 2011

MAAFA: Tamko la CHADEMA




CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SALAAM ZA RAMBIRAMBI NA POLE KWA WANAFAMILIA NA WANANCHI KUHUSIANA NA
JANGA LA MAFURIKO YALIYOKUMBA JIJI LA DAR ES SALAAM, MBEYA NA DODOMA .

Usiku wa kuamkia tarehe 20.12.2011 Maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, Mbeya na Dodoma yamekumbwa na maafa makubwa ya mafuriko ambayo yamesababishwa na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha mfululizo katika maeneo hayo.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kutoa pole za dhati kwa wanafamilia na wananchi wote ambao wamekumbwa na janga hili kubwa , kwani limesababisha maafa makubwa sana ya vifo, kupoteza mali na miundombinu mbalimbali kuharibiwa vibaya kwenye maeneo husika.
Tunapenda kuwahakikishia wananchi hawa kuwa tutakuwa nao pamoja katika kipindi hiki kigumu katika maisha yao kutokana na madhara waliyopata yaliyosababishwa na maafa haya.

Kutokana na janga hili limetukumbusha jambo moja kuwa kama Taifa hatujajiandaa kikamilifu kuweza kukabiliana na majanga kama haya pindi yanapotokea na hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeonyesha dhahiri kuwa havijaandaliwa kimfumo na kinyenzo katika kuweza kukabiliana na majanga kama haya na huu ni udhaifu mkubwa sana kwa taifa lenye miaka 50 baada ya uhuru wake .

Mathalani mpaka sasa hatujaona jitihada zozote ambazo zimechukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa katika kuonyesha juhudi za kukabiliana na janga hili kubwa kwa taifa letu,hii inaonyesha wazi kuwa kitengo hiki hakijaandaliwa kuweza kukabiliana na maafa kama ambavyo majukumu yake  anavyopaswa kuwa . Na hii ni hatari kwani kama chombo cha kukabiliana na maafa hakiwezi kufanya hivyo kwa wakati ni kuendelea kuwaacha wananchi waendelee kupata madhara makubwa zaidi. Na
haswa ikizingatiwa kuwa idara ya hali ya hewa ilishatahadharisha kuhusiana na mvua hizi.

CHADEMA tunapenda kuikumbusha serikali kuhusiana na ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo ilieleza wazi kuhusiana na kukosekana kwa mifumo thabiti ya kujulisha umma kuhusiana na majanga mbalimbali katika miji yetu (Early Warning Systems) kama ambavyo ipo katika nchi nyingi , mfumo huu ni muhimu sana katika kuweza kuufanya umma uwe na elimu ya jinsi ya kuweza kujikinga na majanga haya kwa lengo la kupunguza madhara yasiwe makubwa kama ambavyo taifa hivi sasa linashuhudia.

CHADEMA inapendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa haraka na serikali ili kuweza kukabiliana na majanga/maafa mbalimbali hapa nchini yanapojitokeza;

I) Kuandaa mfumo wa awali wa kutahadharisha umma juu ya ujio wa majanga (Early Warning Systems) kwa kutumia vyombo na nyenzo mbalimbali ili kuepusha madhara makubwa kwa watu na mali zao.

II) Kutunga sheria mpya ya ujenzi na kuweka viwango vya ujenzi viwe vyenye hadhi ya kimataifa na haswa ujenzi wa kuta mbalimbali na majengo marefu na kuhakikisha kuwa ujenzi holela haujitokezi kwenye miji na majiji yetu hapa nchini.

III) Kuhakikisha kuwa kwenye miji yote mikubwa mtandao wa mabomba ya maji ya dharura unawekwa ili kuweza kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.

IV) Serikali ijiandae mara moja kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile kuhara ,kipindupindu na mengineyo ambayo yatajitokeza kutokana na mafuriko haya kuharibu miundombinu ya kusambaza maji,
makazi ya watu n.k.

V) Kitengo cha maafa kiwe na vifaa wakati wote , na haswa vifaa kwa ajili ya uokoaji na wawe na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuweza kutumia vifaa hivyo kuweza kujiokoa na sio kuacha hali iwe kama ambavyo imejionyesha Dar Es Salaam jana baada ya baadhi ya majaketi okozi kufikishwa kwa wahanga na kushindwa kuyatumia kikamilifu.

VI) Serikali itoe elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko haya ili kuepusha wananchi wengi kukumbwa na magonjwa hayo pindi yakijitokeza.

Mwisho tunapenda kuendelea kutoa pole kwa wanafamilia wote na wananchi kwa ujumla kutokana na madhara makubwa waliyoyapata , Mungu awajaze nguvu katika kipindi hiki kigumu. Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu CHADEMA .

……………….

DR. Willbroad P. Slaa.

Katibu Mkuu –CHADEMA.