Wednesday, December 28, 2011

USIWEKE Malengo Mwaka Mpya 2012!

Mojawapo ya mambo ambayo yamezoeleka na ambayo hufundishwa na kuelekezwa sana ni watu kuweka malengo kila mwaka mpya unapofika. Katika tafakari yangu ya leo, nakueleza ni kwa nini USIWEKE malengo yako na mipango yako katika wakati huu wa sikukuu za Mwaka Mpya! Makala hii inaangalia "miaka-mipya" yote, sio 2012 peke yake - hata hivyo.


Msimu huu ukoje!
Msimu wa sikukuu za Christmas na Mwaka mpya - kupita misimu mingine ya sherehe katika mwaka, hujawa na hisia nyingi sana. Hisia hizi nyingi huwa nzuri, mbaya na wakati mwingi huwa ni mchanganyiko. 


Hisia nzuri huwa ni za furaha kwa watu kumaliza mwaka, watu wengi huwa wako likizo, watu wengi ndipo hukutana na kujumuika na familia na jamaa zao ambao hawajonana kwa muda mrefu, ni msimu wa Ibaada nyingi na kuwa "karibu na Mungu", ni muda ambapo watu wengi huwa na pesa nyingi za kutumia - kutokana na malimbikizo ya mwaka mzima na Mikopo n.k. Kwa ufupi ni msimu ambapo hali ya kimaisha ya watu hubadilika sana - tangu kiuchumi, kijamii na hadi kihisia.


Wakati gani SIO wa Kuweka Mipango na Malengo
Kila mtu katika maisha yako unatakiwa kuwa na malengo na mipango ya kutekeleza hayo malengo yako. Watu wengi sana wamekuwa wakiweka malengo mengi wakati mwingine bila kuweka mipango ya kutekeleza malengo hayo. 


Wengine huweka malengo na mipango yake lakini wengi sana katika makundi haya mawili mwishoni huwa hawatekelezi hata mojawapo ya mambo hayo! (Jiulize wewe binafsi ni mambo mangapi ulishawahi kuyakusudia au kuyapanga lakini hukuyafanya katika muda wote uliokuwa unadhani utayafanya - Na wakati mwingine ULISAHAU hata kama ulishawahi kuwa na Malengo au Mipango).


Moja ya makosa makubwa ambayo watu huyafanya katika maisha yao wanapokuwa wanataka kuweka mipango na malengo huwa ni KUTOJUA WAKATI MUAFAKA wa kutengeneza Malengo na Mipango ya Kimaisha!


Kama ilivyo katika maeneo mengine ya kimaisha, mtu huwa hushauriwi hata mara moja kufanya maamuzi (yenye nafasi kubwa au muhimu maishani) katika wakati ambao hisia zako, fikra zako au hata afya yako haiko katika hali yake ya kawaida! Hii inamaanisha, kwa mfano, haishauriwi kufanya maamuzi ukiwa na hasira, ukiwa na furaha / hisia kubwa ya furaha (ambayo huwa sio hali yako ya kawaida kimaisha) n.k. 


Hii ni kwa sababu maamuzi mengi utakayoyafanya katika wakati huo yatakuwa yana-"reflect" zaidi hali yako ya wakati huo (hususan hisia) - ambayo SIO hali yako ya kawaida maishani!


Watu wengi ambao wamefanya maamuzi wakati wakiwa na hisia ambazo sio wanazoishi nazo katika maisha ya kaiwaida (kama hasira) wamejikuta wakiishia pabaya baada ya maamuzi yao NA WAO HUJUTA pale hasira zinapokuwa zimetulia. Maamuzi mengi yanayofanywa katika hasira huelekea katika kususa, kugombana / kutukana, kisasi n.k. Mwisho wake huwa ni kufukuzwa kazi, kufungwa jela, kuharibu mahusiano n.k.


Vivyo hivyo kwa watu ambao hufanya maamuzi wakiwa na furaha / hisia za furaha kupita ile wanayokuwa nayo katika maisha ya kawaida ya kila siku - hujikuta wakijutia maamuzi yao na wakati mwingine kubaini kuwa walikosea - BAADA ya kuingia hasara kutokana na maamuzi yao. 


Watu wengi katika hisia za furaha kupita kawaida hujikuta wakiahidi kutoa michango mikubwa kwa ajili ya sherehe au matukio mbalimbali, wakitoa ahadi ya kufanya mambo makubwa/mazuri kupita uwezo wao au utashi wao wa kawaida wanapokuwa hawana hisia hizo! Pale hisia zinapotulia wengi hubadilisha maamuzi yao au kukana kwaba sio wao walioahidi.... n.k.


Maamuzi yako Uyafanye Lini?
Wakati mzuri wa kufanya maamuzi ni pale unapokuwa umerudia hali yako ya kawaida ya kimaisha na kihisia. Subiria huu msimu wa sikukuu uishe, baada ya kuwa umesharudi katika hali yako ya kawaida, hisia za furaha na shamra-shamra zimeshatulia, hisia za hasira kutokana na madeni na makwazo mengine ya familia, ndugu na wapenzi zimeisha - ndipo ukae chini ufanye taathimini ya pale ulipo na ndipo uamue ni wapi unataka kwenda.


Usiruhusu hisia (nzuri au mbaya) za msimu huu wa sherehe na mapumziko ndizo zikaongoza maamuzi yako ya malengo na mipango, muda si mrefu utayaona maamuzi yako hayakuwa sahihi na hayahalisiki kwa hiyo utarudi  kwenye mfumo wako wa "maisha kama kawaida".


ZINGATIA: Muda unaoishi katikati ya Misimu ya Sherehe ni Mchache kuliko unaoishi katika maisha yako ya "kawaida". Usiweke Malengo na Mipango kana kwamba Maisha yako yote unaishi kwenye "sherehe".


Malengo yako Yaweje?
Muda wa kuweka malengo utakapofika - baada ya 'mavumbi" ya sherehe kutulia, baada ya kulipa karo za watoto na kulipa madeni uliyokopa ili kufanikisha sherehe na safari za mwisho wa mwaka, kaa chini uweke malengo na mipango ya kuyatekeleza malengo hayo. Malengo yako ni muhimu yakawa na sifa zifuatazo (pamoja na nyingine):


Moja; Yawe Yanahalisika! Moja ya mambo ambayo huwakwamisha watu wengi sana wanapotaka kutekeleza malengo waliyojiwekea huwa ni pale wanapobaini kuwa hayahalisiki katika hali yake halisi ya kimaisha! Hakikisha malengo yako yanazingatia hali halisi uliyo nayo kwa sasa na hali halisi ya fursa na uwezekano wa wewe kuweza kuyafanya hayo na kuyanikisha hayo unayoyapanga kwa muda unaoupanga.


Ukiweka mipango ya mambo ambayo hayahalisiki mwishoni utakuja kubaini kwamba yameshindikana na utakuwa "frustrated". Watu wengi wanapoona mipango yao imekwama na haitekelezeki huwa wana kata tamaa na kujifariji kwamba "kumbe maisha ni kubahatisha" na baada ya hapo huanza kuendesha maisha yao bila mipango wala malengo wakisubiri "bahati"! USIJI-"FRUSTRATE" MWENYEWE KWA KUWEKA MALENGO YASIYO HALISIKA!


Pili; Yawe na Kikomo cha Muda! Usiweke malengo ambayo yako "open-ended" kwenye suala la muda. Usiweke malengo ambayo unadhani utayafikia "muda wowote" ukiwa bado unaishi - HAPANA! Ni lazima malengo yako yawe na kikomo cha Muda. Hii inamaanisha kwamba unapaswa kujiwekea "ratiba" ya kuyatekeleza na kuyafikia malengo yako.


Kwa Mfano, sema ninataka kufanya jambo hili na hili ndani ya miaka mitatu ijayo, kisha uivunje-vunje hiyo miaka mitatu katika muda mfupi-mfupi kama wa miezi Sita-Sita ua mwaka Mmoja-Mmoja. Hii itakuwezesha kuyaona majukumu yako ni madogomadogo na yanayobebeka kwa urahisi (kwa miezi sita-sita kwa mfano), kuliko ukiyaangalia kwa ukubwa wake wa miaka mitatu! Pia hii itakusaidia kufuatilia maendeleo yako katika kutekeleza mipango yako ya kufikia malengo.


Tatu; Malengo yatokane na KUSUDI LA MAISHA yako! Hiki kigezo ni cha muhimu sana na kinapaswa kuwa cha kwanza kwa kipaumbele. Hata hivyo, kutokana na upana wa suala hili, hapa nitakupa maelezo machache yatakayokuwezesha kuelewa - japo kwa uchache.


Kwa ufupi ninachokimaanisha hapa ni kwamba KILA MTU UNAPASWA KUWA NA KUSUDI LA MAISHA YAKO! Kila mtu unapaswa kuwa unaelewa maisha yako kwa ujumla hapa duniani yapo kwa kusudi gani kubwa / la jumla ambalo ndilo unalitumikia na unalenga kuwa umelifikia mwishoni mwa maisha yako!


Watu wengi kwa kutokuwa na KUSUDI KUU la maisha huwa wanaweka malengo madogo-madogo na ya muda mfupi-mfupi kama mwaka mmoja-mmoja au miwili-miwili na wakati mwingine huwa wanayatekeleza na kuyafanikisha. 


Lakini kwa kuwa malengo yao yanakuwa hayaongozwi na "Picha" moja kubwa ya Kusudi la maisha yao kwa ujumla, hadi wanapozeheka wanakuwa hawana kitu chochote cha maana cha kujionesha wao wenyewe na watoto wao kwamba ndicho walichokifanya katika maisha yao. Watu hawa wanakuwa walifanikisha tu-mambo twingi tudogo-todogo na ambato hatu-link kwa hiyo tunakuwa hatuwezi kutoa picha kubwa ya mafanikio yao maishani!


HAKIKISHA: Kila lengo na tendo lako maishani linakusaidia na kukusogeza karibu zaidi na kulitimiza kusudi lako kuu la maisha. Usifanye mambo ambayo haya-link na hivyo mwishoni yanakuwa hayatoi picha yoyote kubwa ya mafanikio yako maishani!


Na Mwisho (kwa leo); Weka Malengo Yanayopimika. Hakikisha kuwa malengo utakayoyaweka yanaweza kupimika. Hii inamaanisha kuwa wewe mwenyewe au wengine watakaokuwa wanakusaidia kufuatilia mafanikio yako waweze kupima na kuona kwamba ni kweli kuna jambo limefanyika na limefanikiwa. Usiweke malengo ambayo hata yakifanikiwa hakuna tofauti inayopimika itakayoonekana katika maisha yako au eneo unalolifanyia kazi.


Mwandishi wa Makala Hii Ni Mwalimu ambaye hutoa Mafunzo na Semina kwa makundi mbalimbali kuhusiana na Namna ya Kuchagua, Kupanga na Kufanikisha Maisha Yako! Anapatikana kwa Namba 0659 219 046 au 0783 666 771.


Kama Makala hii umeipenda na Imekusaidia kwa Namna Yoyote, Mtumie na Rafiki yako Pia kwa Kubonyeza Alama ya Email hapa Chini.

No comments:

Post a Comment