Saturday, June 2, 2012

HOTUBA Ya Kikwete!


Ndugu Wananchi,

Kama ilivyo ada, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kumaliza mwezi Mei salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi, leo nitazungumzia mambo matatu.

Mkutano wa G-8
Jambo la kwanza, ni suala la usalama wa chakula na lishe. Duniani, inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 925 wanaokabiliwa na njaa na lishe duni. Kati ya hao Afrika ina watu milioni 239 ambao ni karibu theluthi moja ya watu wote wenye tatizo la njaa na lishe duni kote duniani.

Nchi za Afrika zenye tatizo la njaa kiasi cha kuhitaji msaada wa chakula kutoka nje ni 27. Kati ya hizo 11 zina matatizo makubwa zaidi. Tanzania siyo miongoni mwa nchi hizo, hata hivyo bado hatujafikia kiwango cha kujitosheleza kabisa. Hivi sasa tumefikia asilimia 95 na kila mwaka yapo maeneo nchini yanayopata msaada wa chakula kutoka Serikalini.

Mwaka 2009, katika mkutano wao wa L’Aquila, Italia, viongozi wa nchi nane tajiri kuliko zote duniani waliamua kuchukua hatua ya kuzisaidia nchi zinazoendelea duniani kukabiliana na tatizo la njaa na lishe duni. Katika mkutano ule waliahidi kutoa dola za Marekani bilioni 22 kwa ajili hiyo. Tanzania tunategemea kupata dola milioni 22.9.

Katika mkutano wa nchi hizo maarufu kwa jina la G-8 uliofanyika Camp David, Marekani tarehe 19 Mei, 2012, pamoja na mambo mengine walizungumzia suala la usalama wa chakula na lishe barani Afrika. Nia yao ni kuchangia katika juhudi zinazofanywa na mataifa ya Afrika zenye shabaha ya kutokomeza matatizo hayo. Tofauti na walivyofanya L’Aquila, safari hii waliamua kuchangia katika utekelezaji wa mipango na progamu za kuendeleza kilimo katika nchi za Afrika hasa zile zinazolenga
kujenga usalama wa chakula na lishe.

Aidha, waliamua kuwa wataanza na nchi tatu na kuendelea kuziongeza kila baada ya muda fulani, badala ya kuanza na nchi zote mara moja. Hoja yao kubwa ni kwamba, wanataka kukusanya nguvu zao kwa nchi hizo chache ili kufanya kazi ambayo itakuwa na matokeo yanayoonekana katika
kutokomeza njaa na kuboresha lishe. Hawakupenda kusambaza nguvu zao kwa nchi nyingi na kuishia kutokufanya kazi ya maana.


Ndugu wananchi;
Bahati nzuri katika programu na mipango ya nchi iliyokubaliwa kwa awamu ya kwanza ni Tanzania, Ethiopia na Ghana. Na, jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba mpango wetu wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania ulichukuliwa kuwa ni wa mfano. Maoni hayo ya nchi za G-8 ndiyo maoni ya WEF, Sekretariat ya NEPAD na Umoja wa Afrika, wote wameona kuwa mpango wetu unafaa kuenezwa barani Afrika kama mkakati sahihi wa kuendeleza kilimo, kujitosheleza kwa chakula na kupunguza umaskini.

Katika Bara la Afrika mkakati huo sasa unaitwa Grow Africa Partnership na tayari nchi saba zimeshajiunga nao. Nchi hizo ni Tanzania, Msumbiji, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Ghana na Burkina Faso. Katika mkutano wa Camp David, nchi za Marekani, Japani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Urusi zimeahidi kuchangia nchi yetu katika juhudi zetu za kuendeleza kilimo na hasa zile zenye lengo la kujitosheleza kwa chakula na kuboresha lishe nchini. Ukichanganya na ahadi iliyotolewa na Umoja wa Ulaya katika mkutano huo, kiasi cha dola za Marekani milioni 897 zimeahidiwa kutolewa kwa nchi yetu kati ya sasa na mwaka 2015.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2006 tulizindua Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo nchini maarufu kwa kifupi kama ASDP. Kwa kirefu kwa lugha ya Kiingereza ni the Agricultural Sector Development Programme. Programu hii ndiyo mwanzo wa safari yetu ya uhakika ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini
Tanzania. Jambo la kwanza lililofanyika katika utayarishaji wa Programu hii ni kutambua vikwazo vinavyozuia maendeleo ya kilimo nchini na kupendekeza hatua za kuchukua za kuondosha vikwazo hivyo.

Mwaka 2008, katika tathmini iliyofanywa kwa ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi kwa uamuzi wa Baraza la Biashara Tanzania, ilidhihirika kwamba sekta binafsi ambayo ni wadau muhimu, haijahusishwa vya kutosha katika mikakati, mipango na programu za kuendeleza kilimo nchini. Kwa
pamoja ilikubaliwa kuwa kasoro hiyo iondolewe ili wadau wote washirikishwe, yaani Serikali, wakulima wadogo, wakulima wakubwa na sekta binafsi. Vilevile, sote tulikubaliana kutoa kipaumbele cha juu kwa maendeleo ya kilimo. Kwa pamoja tuliafikiana kuwa mambo mengine
yanaweza kusubiri isipokuwa kilimo. Matokeo ya maelewano hayo ndiyo yaliyozaa mkakati na kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza”.

Ndugu Wananchi;
Tangu wakati huo, sekta binafsi nchini imekuwa inahusishwa na kushirikishwa kwa ka ribu katika utekelezajiwa ASDP na kuendeleza kilimo kwa jumla. Kwa upande mmoja sekta binafsi imekuwa inahusishwa katika upatikanaji wa zana na pembejeo za kisasa za kilimo kwa wakulima. Kwa ajili hiyo, wenzetu wa sekta binafsi wamekuwa wanategemewa kuleta na kuuza matrekta, mitambo na vifaa mbalimbali vya kilimo pamoja na mbegu, mbolea, dawa za kuua wadudu waharibifu wa
mazao na za kukinga na kutibu maradhi ya mimea na mifugo. Hali kadhalika, wamekuwa wanajihusisha na ununuzi na usindikaji wa mazao ya mkulima na kuongeza thamani. Tunataka tuachane na kuendelea kuuza nje mazao ya kilimo kama malighafi na kununua bidhaa zilizotengenezwa na mazao hayo.

Upande mwingine tuliwategemea wenzetu wa sekta binafsi washiriki kulima mashamba makubwa. Wasiache kazi ya kilimo kufanywa na wakulima wadogo peke yao ambao uwezo wao si mkubwa wa kukabili matatizo ya kuongeza tija. Nafurahi kwamba wito wangu huo waliupokea vizuri na
baadhi yao wameshaanza kufanya hivyo.

Ndugu Wananchi;
Swali kubwa walilouliza ndugu zetu hao siku ile ya tarehe 2 – 3 Juni, 2009 pale Kunduchi Beach Hotel ni kuhusu upatikanaji wa ardhi. Niliwaeleza kuwa upo utaratibu mzuri wa kuwapatia wakulima wakubwa ardhi ya kilimo na ufugaji. Utaratibu wenyewe ni kwamba kila wilaya imetakiwa kutenga ardhi kwa ajili ya wakulima wakubwa. Hilo likishafanyika, taarifa hutolewa kwa Kituo cha Uwekezaji na kuingizwa katika kitu kinachoitwa Benki ya Ardhi. Mwekezaji anapojitokeza,
kulingana na aina ya kilimo anachotaka kujihusisha nacho, hugawiwa ardhi hiyo. Ardhi hiyo ni ile ambayo siyo inayotumiwa na wakulima wadogo. Katu hawanyang’anywi ardhi wakulima wadogo ili kuwapa wakulima wakubwa. Hiyo siyo sera wala madhumuni na malengo ya ASDP au Kilimo
Kwanza. Nalifafanua hili kuondoa hofu iliyokuwepo na upotoshaji uliokuwa unafanywa makusudi wa kuhusisha wakulima wakubwa na uporaji wa ardhi. Siyo makusudio yake hata kidogo.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2010 tukapanua wigo wa ushiriki wa sekta binafsi kwa kuihusisha sekta binafsi ya kutoka nje ya nchi. Mwaka huo pia, tukaamua kuipa sekta binafsi lengo maalum la kutekeleza nalo ni kushiriki katika kilimo cha kuhakikisha kuwa nchi yetu inajitosheleza kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje, kwa majirani zetu na kwingineko. Shabaha yetu hasa ilikuwa ni kujitosheleza kwa vyakula vikuu vya mahindi, mchele na sukari.

Aidha, tuliamua pia kuwa, kwa kuanzia tuelekeze nguvu zetu kwenye mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa na Morogoro kwa vile mikoa hiyo ndiyo ghala la chakula la nchi yetu. Kwa vile mikoa hiyo ipo ukanda wa kusini ndio maana ikaja kuitwa Southern Agriculture Growth Corridor of
Tanzania au SAGCOT. Tumeamua tukusanye nguvu za Serikali, wakulima, sekta binafsi na washirika wetu wa maendeleo kuwekeza katika kuendeleza kilimo katika mikoa hiyo.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mpango wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa SAGCOT una shabaha kuu mbili: Kwanza kabisa mpango unalenga kuboresha kilimo cha wakulima wadogo ili kitoke kuwa duni na cha kujikimu na kuwa cha kisasa na kibiashara. Chini ya mpango huu wakulima wadogo watasaidiwa
na kuwezeshwa kupata na kutumia zana na pembejeo za kisasa za kilimo. Pia watawezeshwa kupata mikopo kwa ajili ya kilimo na masoko ya uhakika na yenye bei nzuri kwa mazao yao. Vile vile, huduma muhimu zitaimarishwa. Hapa tunazungumzia maafisa ugani na miundombinu ya
umwagiliaji, barabara, umeme, maji safi na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Pili, kwa pale inapowezekana kwa maana ya upatikanaji wa ardhi na aina ya mazao, kuihusisha sekta binafsi katika kilimo. Tayari utekelezaji wa mpango wa SAGCOT umeanza. Kamati ya Utendaji imeshaundwa na Sekretariati yake imeshateuliwa. Aidha, Mfuko wa Kuchochea Uwekezaji
umeshaanzishwa na unaendelea kuchangiwa fedha.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa malengo ya SAGCOT kwa kilimo cha mpunga na kuongeza uzalishaji wa sukari yameanza kutekelezwa. Matayarisho yanaendelea kwa kilimo cha mahindi na mazao mengine.

Mpango huu utakapofanikiwa utakuwa na manufaa makubwa. Nchi yetu itajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada kubwa ya kuuza nje. Inakadiriwa kuwa mapato yatokanayo na kilimo katika ukanda huu yatafikia dola bilioni 1.2 kwa mwaka, watu 420,000 watapata ajira na watu 2,000,000 wataondokana na umaskini uliokithiri.

Uwekezaji wake ni mkubwa na kwamba kiasi cha dola bilioni 3.4 kinahitajika kwa kipindi cha miaka 20. Kwa ushirikiano uliopo baina ya Serikali, sekta binafsi na wabia wetu wa maendeleo wakiwemo wa nchi za G-8, hayo yote yanawezekana.

Ndugu Wananchi;
Tukijitosheleza kwa chakula na kwa maana pana ya chakula chenye lishe bora tutakuwa tumefanikiwa kupata ufumbuzi wa tatizo kubwa la ukosefu wa lishe bora miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Wanaoathirika sana na tatizo hili ni kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Ukosefu wa lishe bora huchangia asilimia 20 ya vifo vya kinamama wajawazito nchini na theluthi moja ya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano. Aidha, asilimia 42 ya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano wamedumaa na asilimia 16 wana uzito mdogo kulingana na umri wao na asilimia 59 wana upungufu wa damu. Kwa kina mama wajawazito asilimia 41 wana matatizo ya upungufu wa damu. Hali hii sio nzuri hata kidogo lazima tuibadili na tunaweza kufanya hivyo. Tunao mkakati wa kitaifa wa kuboresha lishe ambao kwa sehemu kubwa utanufaika sana na kufanikiwa kwa mkakati wa kujitosheleza kwa chakula.

Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
Ndugu Wananchi;
Jana tarehe 31 Mei, 2012 nilishiriki katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mkutano wa 38 wa Mfuko wa Maendeleo wa Afrika. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Benki hii tangu ianzishwe mwaka 1964 kwa nchi yetu kuwa mwenyeji wa mikutano hii inayofanyika kila mwaka. Ni heshima kubwa sana kwa nchi yetu, nami kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, nimemshukuru sana Rais wa Benki hiyo, Dkt. Donald Kaberuka kwa ihsani kubwa aliyoifanyia nchi yetu.

Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu ni jambo lenye manufaa mengi kwetu. Kwanza husaidia kuitangaza nchi yetu Barani Afrika na kwingineko duniani. Pili, ni fursa nzuri ya kuzungumza na viongozi wa Benki kuhusu mipango na miradi yetu ya maendeleo tunayohitaji msaada kutoka Benki hiyo.

Na, tatu, ni fursa nzuri ya watu wetu kufanya biashara. Mkutano huu umeshirikisha watu 2,500 ambao wametoka nje ya Tanzania na wanajitegemea kwa kila kitu. Wenye hoteli, migahawa, vyombo vya usafiri, huduma ya simu, internet na nyinginezo watakuwa wamefanya biashara nzuri katika wiki nzima kabla ya tarehe 28 Mei mkutano ulipoanza hadi 2 Juni, mkutano utakapofungwa. Ni kutokana na manufaa kama haya, ndio maana huwa tunahangaika kuvutia mikutano mikubwa kuja
kufanyikia hapa nchini.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao. Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu. Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la
kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya
Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni tena niwashukuru wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa mchango mkubwa waliotoa na wanaoendelea kutoa kuchangia maendeleo ya nchi yetu. Kwa miaka mingi Benki hii imekuwa inatupatia mikopo na misaada muhimu kwa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini pamoja na zile za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara, reli, umeme n.k.

Kwa msaada wa Benki hii tunajenga barabara ya Namanga – Arusha, Minjingu – Singida, Namtumbo – Tunduru, Iringa – Dodoma, Mayamaya – Babati, na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala. Miaka ya nyuma pia walituwezesha kujenga barabara ya Mutukula – Muhutwe. Aidha, hivi sasa wanagharamia upembuzi yakinifu na usanifu wa reli mpya tunayotaka kuijenga kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi.

Matukio ya Uvunjifu wa Amani Zanzibar
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni matukio ya wiki iliyopita huko kwenye Jiji la Zanzibar katika mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja. Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la
Uamsho. Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za siasa.

Siku za nyuma, ndugu zetu hawa walikuwa wakitumia muda mwingi kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki. Lakini, mara tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa. Isitoshe wamekuwa wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka Tanzania Bara na wale wafuasi wa dini ya Kikristo.

Baya zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawilizilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa. Kwa kweli vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki. Naungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake aliyoitoa jana katika mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaaniuhalifu huo.

Ndugu Wananchi;
Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano. Haiwezekani mtu anayepinga Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja maduka ya watu na kupora mali zao. Ukristo haukuingizwa Zanzibar na
Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar. Kanisa kuu la Anglikan Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande wa Zanzibar na Bara.

Katika hotuba yake ya jana, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed Shein,pamoja na kueleza kwa ufasaha ukweli huu, pia alisisitiza suala la haki na uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au imani yake. Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au kulazimishwa na mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu wa Uamsho ya kuchoma moto makanisa siyo sawa hata kidogo. Na, wanapoyafanya kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki. Labda wenzetu wana lao jambo.

Ndugu Wananchi;
Jambo lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia hizi dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kama tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na inajiandaa kupita
kote nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya waitakayo. Kama mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo ndiyo fursa ya kufanya hivyo. Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote, vurugu za nini?

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Mimi sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa amani kwa jambo ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta mifarakano katika jamii na yanayosababisha uvunjifu wa amani na
yanaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania isivyostahili.

Ndugu zangu,
Haipendezi wala haifurahishi kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya raia wake. Lakini, kama hapana budi, Serikali lazima ifanye na haitasita kufanya hivyo. Narudia kuwasihi viongozi na wafuasi waJumuiya ya Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao. Wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo na Waislamu. Watanzania ni ndugu na wamekuwa wanaishi pamoja kwa upendo na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila,
dini na maeneo watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya? Aidha nawaomba wenye maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na uendeshaji wake watumie fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao. Huhitaji kufanya ghasia kutoa maoni yako!

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia fursa hii pia kuwapa pole wale wote walioathirika na vurugu zilizotokea. Nawaomba wawe wastahamilivu, hiyo ndiyo mitihani ya maisha. Serikali zetu mbili zitafanya kila lililo kwenye mamlaka yake kuwahakikishia wananchi wote usalama wa maisha yao na wa mali
zao.

Nawapongeza vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema. Nawaomba waendelee kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na watu wake wasipate nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu. Naamini tukidumisha utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana na kuzungumza pale tunapotofautiana hakuna litakaloharibika. Haya shime tufanye hayo.


Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

2 comments:

  1. Hotuba ina ukomavu wa kisiasa na kiutawala hasa kwenye suala la Muungano na UAMSHO!!! Rais ameonyesha nia ya dhati ya kutaka amani ya taifa sula hapa ni kuichukua hii kama changamoto yetu maana waliochoma makanisa ni raia na waliochomewa ni raia. Busara ya hali ya juu na hekima vishike mkondo wake. Namsapoti Rais kwa hili

    ReplyDelete
  2. Hongera sana jm kikwete kwa kaz nzuri uliyoifanya kwenye kipindi cha uongozi wako

    ReplyDelete