Thursday, November 10, 2011

Tanzania Inahitaji MAPINDUZI pia!

Mapinduzi ya Libya, kwa Mfano, yalibadilisha
Serikali na Bendera, SIYO Mapinduzi tunayoyahitaji sisi kwa sasa
Kumekuwa na wimbi kubwa la mapinduzi na mabadiliko ya tawala na serikali mbalimbali duniani, yaliyoanzia Afrika, Mwezi Disemba mwaka jana!


Kiini cha Mapinduzi katika nchi hizi ni wananchi kuchoka tawala za Muda mrefu, zisizotaka wala kuleta mabadiliko, zinazowadhalilisha raia wake huku Viongozi wake kujinufaisha binfasi. Tunisia, Misri, Libya, Ugiriki, Italia..... zinazofuatia Yemen na Syria (Bahrain imesaidiwa na Saud kuwazima wananchi Kijeshi)....


Ukweli ni kwamba, pamoja na ukimya na utulivu, amani na upendo uliopo Tanzania, nchi hii inahitaji Mapinduzi - TENA HARAKA SANA!


Mapinduzi Tunayoyahitaji Sisi
Tofauti ni kwamba Mapinduzi tunayoyahitaji Tanzania, KWA KUANZIA, sio ya Serikali wala Chama Tawala - Ni MAPINDUZI YA KIFIKRA na KIMTAZAMO!


Kiini cha Matatizo yetu
Kiini cha matatizo makubwa yanayolikabili hili taifa kiko kwenye Fikra na Mtazamo wa Watanzania kuhusu taifa na utaifa wao. Kiini cha Matatizo yetu kama taifa SIO SERIKALI, ni wananchi!. Tanzania bado ina wananchi wengi sana ambao hawajitambui kama Raia na kwa jinsi hiyo hawatimizi wajibu wao kama raia wa Taifa!


Raia wa nchi wasiojitambua na wasiowajibika kama raia makini kwenye nchi yao KAMWE hawawezi kulisaida taifa lao kuendelea - hata wakipata Viongozi wazuri namna gani! Viongozi, ambao na wao ni wanadamu kama waongozwa, huhitaji kuzungukwa na kundi kubwa la wananchi wanaojitambua ambao muda wowote wako tayari kusimamia wajibu na kuutimiza - ikiwa ni pamoja na wajibu wa kuwawajibisha viongozi wao wasiowajibika!


Raia wawanaowalinda na kuwatetea viongozi wasiowajibika kwa sababu za kikabila, Kidini au vyama vyao vya siasa HAWAFAI na HAWAWEZI kulisaida Taifa kuendelea. Tanzania ya leo imejawa na watu ambao wako tayari kufumbia uovu wowote - NA HATA KUUTETEA - iwapo tu umefanywa na mtu wa Chama chao cha Siasa, mtu wa Kabila lao au hata Dini yao!


Watanzania tunajitaji kuanza jitihada za haraka na za kimakusudi za kufanya mapinduzi ya kimtazamo na kifikra kutoka katika mtazamo mgando ambao wengi wetu tunao kwa sasa na kuelekea katika mtazamo chanya wa kimaendeleo, wa kimageuzi na endelevu ambao utalisaidia hili taifa kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.


Hatuna budi kuanza kujenga mtazamo wa kujiona kuwa na sisi tunaweza kuwa Taifa tajiri, taifa lenye Maisha bora kwa kila mtu, taifa lenye huduma bora za kijamii - na haya yote PASIPO KUTEGEMEA MISAADA YA WAZUNGU!


Mtazamo wetu wa sasa wa kujiona sisi ni maskini, sisi hatuwezi, SISI TUNAHITAJI KUSAIDIWA NA WAZUNGU, sisi hatujui n.k. n.k. hautalisaidia wala kuliendeleza hili taifa. Tunahitaji kufanya mapinduzi ya jinsi tunavyojiona kama watu binafsi na jinsi tunavyoliona taifa letu!


Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, pamoja na mambo mengine, imependekeza kuwe na jitihada za kimakusudi za kujenga uelewa na kubadilisha mtazamo wa Watanzania. Hili lilikuwa ni jambo la muhimu sana, japo utekelezaji wake bado hauoneshi kuwa na utashi wa kuleta mabadiliko. Kwa hali ilivyo sasa, hatuhitaji tu Uelewa TUNAHITAJI MAPINDUZI!


Yakishafanyika mapinduzi ya kimtazamo na kifikra miongoni mwa Watanzania, sasa yanaweza kufuatiwa na mapinduzi ya kiutawala - kutoa tawala ambazo zinaweza kuwa zinang'ang'ania fikra pooza na ukale kuweka tawala zenye kuangalia, kuona na kulipeleka taifa mbele.


Pasipo mapinduzi ya kiufahamu, mtazamo na kifikra miongoni mwa Watanzania, mapinduzi ya Kiserikali au Kiutawala hayatasaidia sana kuiendeleza hii nchi. Mabadiliko ya watu ni ya muhimu sana katika kuiendeleza nchi kuliko mabadiliko ya kiuongozi na kiserikali tu....

No comments:

Post a Comment