Monday, November 14, 2011

UDHAIFU WA CHADEMA


Katika makala yangu hii natafakari udhaifu wa Vyama vya Upinzani hapa Tanzania na changamoto zinazovikabili ili kuweza kufikia ndoto zao za kushika hatamu ya kuliongoza hili taifa. 

Hata hivyo, kutokana na kuibuka kwa CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani hapa Tanzania kinachoonesha upinzani mkubwa kwa Chama cha Mapinzduzi, mifano mingi na tafakari italenga katika kuelezea udhaifu na changamoto zinazoikabili CHADEMA, ambazo kwa namna nyingi hata hivyo zinavikabili vyama vingine ya Upinzani pia.
Pamoja na Kasi Kubwa ya CHADEMA katika "kuwashika" Watanzania,
bado Chama hiki kinakabiliwa na Changamoto  Nyingi

1.       “Uchanga”
Changamoto mojawapo kubwa ambayo inavikabili vyama vingi vya upinzani kwa hapa Tanzania ni “uchanga” wa vyama hivi katika siasa za Tanzania. Ninapozungumzia uchanga hapa simaanishi uelewa mdogo wa kisiasa ndani ya vyama hivi, bali uchanga wa vyama vyenyewe kimifumo na uongozi ndani ya vyama hivi.

Vyama hivi vingi vilianzishwa au vinaendeshwa na watu ambao hawakuwahi kupata uzoefu wa kiuendeshaji na utendaji katika mifumo ya kitaasisi kubwa, hususani ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, vyama vingi vinaongozwa kwa nadharia ya “learning by doing” (kujifunza kwa kutenda).

Hii inamaanisha kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kukosea, lakini kunapokuwa hakuna aliye bora zaidi ya huyo katika mfumo wa uongozi wa chama husika kunakuwa hakuna jambo la kufanya zaidi ya “kurekebishana” hivyo hivyo na kuendelea mbele.

Muda unavyozidi kwenda hata hivyo, vyama kadhaa vya upinzani vineonekana kuzdi kuishind hii changamoto ya “uchanga” wa kitaasisi na kuanza kujiimarisha.

2.       Kukosa “mizizi”
Changamoto nyingine kubwa ambayo inavikabili vyama vya upinzani Tanzania ni ukosefu wa “mizizi” ya kisiasa katika maeneo mbalimbali ya taifa – hususan vijijini. Kukosa wanachama wengi  - na zaidi oganaizesheni ya kiuongozi – katika maeneo ya “chini” inamaanisha vyama vingi vinabakia na nguvu katika maeneo machache ya nchi, hususan mijini.

Kwa jamii ya kitanzania ambapo takribani 70% ya watu wanaishi vijijini, kukosa mfumo wa kiutawala wa chama unaoanzia vijijini ni upungufu mkubwa mno ambao unaweza kumaanisha vyama hivi itabidi viendelee kusubiri miaka mingi zaidi kuweza kushinda chaguzi za kitaifa na kushika hatamu ya kuongoza taifa.

Vyama vya upinzani Tanzania vikiweza kupenya na kuingia vijijini na kukita mizizi yao kuanzia huko, hakuna ubishi kwamba mwisho wa Chama cha Mapinduzi utakuwa umekaribia sana – kama sio kwamba utakuwa umeshafika kabisa.
CHADEMA kimefanikiwa sana kuwa na Nguvu Mijini,
Nguvu hii ikiingia vijijini, CCM inaweza ikaanza rasmi
Kuwa Chama cha Upinzani Tanzania

Hii ni kwa sababu Vyama vya Upinzani, hususan CHADEMA vimeonekana kukubalika sana katika maeneo karibu yote ambako vimefika – mifano mizuri ni namna ambavyo vimeweza kushinda viti vya upinzani katika maeneo ya mijini ambako vimefika na kukubalika. 

Siku vikipenya na kuingia kwenye kambi kuu ya CCM ambayo imebakia kwa sasa – vijijini – CCM imekwisha!

3.       Ujinga wa Kisiasa
Watanzania wengi sana, kwa sababu zinazofahamika na zisizo fahamika, ni wajinga wa siasa. Ujinga ni hali ya kutokujua – SIO kwa maana ya kuwatusi. Ujinga huu unatokana na kutokuelewa hasa maana na sababu ya kuwepo kwa siasa katika jamii na taifa kwa ujumla. Lakini tatizo kubwa zaidi ni ujinga wa Siasa za Vyama vingi.

Watanzania wengi, hususan walio vijijini, walizaliwa na kulelewa katika mfumo wa Chama kimoja – Chama cha Mapinduzi. Sambamba na mfumo huo, pia wananchi walizoea mfumo ule wa “Chama na Serikali” ambapo utendaji wa chama na serikali ulikuwa hautofautishwi, hivyo wananchi wengi walielewa “Chama ndio Serikali”.

Watanzania wengi kwa "Ujinga", wako tayari kufa na
vyama vyao vya Siasa - hata kama hawaelewi ni kwa nini?!

Kwa hiyo tangu vyama vya upinzani vilipoanza kushiriki kwenye chaguzi mwaka 1995, wananchi wengi walikataa kuvichagua kwa kuhofia kuwa CCM ikiondoka madarakani Tanzania hakutakuwa na serikali – kwa sababu walijua CCM ndio Serikali! 

Mijadala mingi wakati wa kampeni za Uchaguzi mwaka 1995 ilitawaliwa na maswali ya hofu kama: NCCR watatoa wapi Polisi wao, watatoa Wapi Walimu wao, Watatoa wapi Wakurugenzi wao wa Halmashauri?. Hivyo wengi wakaogopa kuvichagua kwa kuwa walijua watendaji karibu wote waliokuwepo serikalini ni wa CCM hivyo wataondoka na CCM!

Zaidi ya hapo, imani waliyokuwa nayo kwa baba wa taifa wa Taifa Mw. Nyerere ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba wengi wao hadi leo hawadhani kwamba kuna Chama kingine tofauti na “Chama cha Nyerere” kinaweza kuongoza hii nchi vizuri – bila kujali kama hicho “cha Nyerere” chenyewe kwa sasa kinaongoza kama Nyerere alivyokuwa akiongoza au la.

4.       “Ulimbukeni”
Changamoto nyingine kubwa ambayo inavikabili vyama vya upinzani hapa Nchini – Hususan CHADEMA – ni ulimbukeni wa wananchama wao. Ni wazi kwamba chama kama CHADEMA kimepata umaarufu zaidi miaka kama 7 iliyopita. 

Hii, pamoja na mambo mengine ilichangiwa na Umahiri wa Wabunge wake wachache bungeni walioonesha Ujasiri na Uchapa kazi wa hali ya juu kiasi cha kuwafanya watanzania wengi kuamini kwamba hiki ndicho chama walichokuwa wanakitaka.

Matumizi ya Helkopta kwenye Uchaguzi wa mwaka 2005, pamoja na kebehi za CCM na vyama vingine vya upinzani, yalisaidia sana kui-promote CHADEMA maskioni mwa wananchi.

Umaarufu uliwafanya wananchi wengi kukimbilia kujiunga CHADEMA – ikiwa ni pamoja na wale waliohama CCM. Wengi miongoni mwao ni watu ambao hawakuwa na historia wala uelewa wa masuala ya Siasa, achilia mbali uongozi.

Wingi wa wafuasi kutoka maeneo tofauti ulimaanisha kulikuwa na uhitaji wa viongozi wengi zaidi wa mashina, kata, wilaya na mikoa. Wengi waliopewa nafasi hizi hawakuwa na uelewa wala uzoefu wa uongozi – zaidi kwamba WALIKUWA WAKISUKUMWA NA MHEMUKO NA HAMU KUBWA YA KUTAKA KUONA MABADILIKO TANZANIA – maarufu kama “Tanzania bila CCM”.
Hamu ya Mabadiliko imewasukuma watu wengi kutaka
 nafasi za Uongozi - hata zile ambazo ni bayana hawaziweki

Kusimamia na ku-handle kundi kubwa namna hii ya Wanachama ni changamoto kubwa sana. Mara nyingi sana nimekuwa nikiona mwanya mkubwa wa CHADEMA kuweza kupasuka na kusambaratika kirahisi sana kukitokea tatizo lolote – ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa – CCM na vya Upinzani!

Mgogor wa Madiwani wa Arusha ni mfano mwingine mzuri wa namna ambavyo CHADEMA bado inakabiliwa na tishio la kuweza kuvunjia au kusambaratika katika baadhi ya maeneo kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wanachama wake.

Changamoto, vikwazo na matishio kwa vyama vya Upinzani Tanzania ziko nyingi sana, nitaendelea na tafakari hii katika sehemu ya pili yamaka hii, lakini nikiendelea kujiuliza: Pamoja na kuwa na Udhaifu na Mapungufu mengi kiasi hiki, kwa nini Watanzania wengi wanazidi kuendelea kuviamini hivi vyama na kukipa kisogo Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho kilitakiwa kushika hatamu zaidi....
Changamoto nyingine kwa CHADEMA ambayo
sijaiongelea Leo ni "NDOA" ya CCM na CUF!... tutaendelea

....itaendelea

No comments:

Post a Comment