Tuesday, September 13, 2011

MAAFA: RUSHWA ya Rambirambi!

Ndugu wananchi wenzangu, nawapa pole tena kwa msiba na majanga yanayoendelea kujitokeza katika nchi yetu!
Meli iliyotengenezwa mwaka 1967 yenye uwezo wa Kubeba watu 600 ilizama
ikiwa na watu zaidi ya 1,000 ndani! KWA TANZANIA kubaini kwamba
hapa kuna makosa au Uzembe inahitaji tume.
Juzi wakati ajali ya Zanzibar ikitokea, kuna ajali nyingine ya namna kama hiyo hiyo iliyotokea Uchina. Kule China walikufa watu 12 wakati Zanzibar haijajulikana ni wangapi - wengine wanasema ni 250, wengine mia 300 wengine 600!
Katika hali ya kawaida, vyombo vya uokoaji kama hiki kilipaswa kutumiwa
na watu wachache zaidi, kusingekuwa na uzembe wa kuzidisha abiria kwenye Meli.


Mara baada tu ya ajali ile ya China, Serikali ya China ILIWAFUKUZA KAZI MAAFISA WATATU wa nafasi tofauti tofauti hata kabla ya uchunguzi haujaanza! Nilipofuatilia kwa nini walifukuzwa nikapata kufahamu kwamba ilibainika kuwa Chanzo cha Ajali ni kuzidishwa kwa Abiria na Mizigo katika ule Mtumbwi. 


Kuzidishwa kwa Abiria na Mizigo kwenye Mtumbi, kwa Wachina, halikuhitaji kuafanya uchunguzi ili kujua kwamba kuna uzembe umefanyika, na haihitaji uchunguzi kuelewa ni nani aliyezidisha Abiria! WAKAFUKUZWA KAZI MARA MOJA!!!


Hapa Tanzania, kumekuwa na mifululizo ya majanga na maafa ambayo mengi kati ya hayo yameonesha wazi kuwa kuna makosa au uzembe ambao umekuwa ukifanywa na watu/watendaji. Reaction ya Watanzania - kwa maana ya serikali mara nyingi huwa ni kutanguliza "Salaam za Rambirambi", Pole Nyingi, Pesa za Kugharimikia Mazishi, Fedha za Rambirambi, Kutembelea Wafiwa, Viongozi Kuhudhuria Mazishi n.k.


Kwa upande wa uwajibikaji hatima huwa ni ahadi ya kuundwa kwa Tume za Uchunguzi ambazo mara nyingi hata taarifa zake huwa ni Siri!!! Hausikii watu wakiwajibishwa achilia mbali wazembe kujiwajibisha wenyewe kwa kuachia ngazi!


MGOMO WA MAOMBOLEZO
Zamu hii mimi Binafsi nimeamua kwamba SIOMBOLEZI TENA - NATAKA HATUA ZICHUKULIWE! Hakuna sababu ya kuendelea kuisifu Serikali na kuiunga mkono katika ugawaji wa fedha kwa ajili ya Rambirambi na Mazishi ya Ndugu zetu wakati hakuna mtu anayehitaji rambirambi - WATU TUNATAKA UHAI WETU!


RUSHWA YA RAMBIRAMBI
Utaratibu wa Utoaji wa Rambirambi kutoka serikalini unatia mashaka zaidi. Wwakati watu wakiwa na majonzi, kuwapelekea pesa na viongozi kuwatembelea ni jambo jema, lakini linaweza kuwa na madhara makubwa mbeleni - na limeshakuwa hivyo.
Kuwahi kwa viongozi katika matukio kama haya huwa ni kwa muhimu, lakini
inakuwa tatizo sana pale kunapotumika kama "Rushwa" ya kuwapoza
 wananchi wasidai uwajibikaji kutoka kwa Viongozi hao.
Yanapotokea majanga, mara zote wananchi wameshakuwa na mtazamo wa kusubiria rambirambi za Serikali. Wakati ni jambo jema kuwafariji watu wanapokuwa wamepatikana na maafa, kitendo hiki hakipaswi kabisa kuchukuliwa kama njia ya kuwanyamazisha wananchi wasihoji na kutaka uwajibikaji kutoka Serikalini.


Mifano ya MV Bukoba, Mabomu, Spice Islanders.. n.k.
Maafa makubwa yaliyotokana na Ajali ya MV Bukoba, Mabomu ya Mbagala na Gongo la Mboto na hii ya juzi ya Zanzibar zinazidi kuamsha ari yangu ya kutaka kuelewa Suala la UWAJIBIKAJI linasimama wapi? Nadhani ni wakati muafaka wananchi tuamue kuanza kudai na kuweka uwajibikaji kwanza kwenye majanga yanayoambatana na Uzembe na Mazoea ya Kutokuwajibishwa!
Milipuko wa mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala Dar es Salaam ilisababisha
maafa na hasara ya mali, Serikali ilitoa pesa nyingi kwa ajili ya Rambirambi, Mazishi,
kugharimikia Makazi n.k. Lakini Uwajibishwaji kwa Wazembe haujaonekana kwa wananchi!


Ni wakati Watanzania Tuanze kuongea Uwajibikaji badala ya Kuendelea Kujifariji na Rambirambi. Sikatai Rambirambi, lakini naerejea kusema, isitumike kama Rushwa ya Kuwanyamazisha Wafiwa na Wanachi kwa ujumla wasidai Uwajibkaji ndani ya Watendaji.


..wasaalam

1 comment:

  1. this is true 200%. inaboa tena inatia hasira na kasirani. nina dukuduku. UWAJIBIKAJI umefutwa kwenye kamusi ya viongozi wetu, and by the way tukiushikia bango haponi mtu kwani wote ni wale wale.

    ReplyDelete