Friday, January 20, 2012

USALAMA: Tanzania Hatarini Zaidi Kuvamiwa!


Katika hotuba za bungeni za kila mwaka za Waziri wa Ulinza na zile za Waziri wa Mambo ya ndani huwa zimejaa maelezo mengi ambayo hulenga kuwapa uhakika wananchi kuwa nchi yao iko salama, mipaka yake inalindwa na wananchi waishi kwa amani na salama bila wasi wasi wowote. Maelezo hayo hayo huwa yanatolewa mara nyingi sana pia na Waziri wa Utalii katika kuwavutia watalii na kuwahakikishia kuwa Tanzania ni eneo salama.

HALI SIO SALAMA
Hata hivyo, uchunguzi wangu binafsi umenibainishia kuwa Tanzania kama taifa tuko katika hali ya hatari sana kuweza kuvamiwa na magaidi au makundi mengine ya kihalifu yasiyo na nia nzuri na nchi yetu. Ukweli ni kwamba Tanzania haiko salama kama wanasiasa na viongozi wetu wanavyodai, na wala sidhani kama wananchi tuna sababu ya kuwa na "starehe" kama ambayo viongozi wetu hutuamisha tuwe nayo.

NINA USHAHIDI

Taarifa za Chama Tawala CCM
Wakati wa Uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka jana, kulikuwa na Taarifa mbili Nyeti sana za Kiusalama hapa Nchini. ZOTE zilitolewa na Chama Tawala - CCM.

Ya Kwanza, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Wilson Mukama alieleza kuwa Chama chake kina Taarifa na Ushahidi kuwa CHADEMA imeingiza Kikosi cha Makomandoo / Magaidi 33 kutoka nje ya nchi na tayari walikuwa wako Igunga na CCM ilifahamu mgawanyo wao katika Kata za huko Igunga ulikuwa kama ifuatavyo: Itobo (4), Burede (5), Isakamaliwa (9) Bukene (9) pamoja na Chamacholo (6).
Katibu Mkuu wa CCM alithibitisha Uwepo wa MAKOMANDOO
Kutoka Pakistani, Libya na Israel
 Katibu Mkuu wa CCM ambaye kabla ya kushika nafasi hiyo alishawahi kushika nafasi nyingine nyeti na za juu hapa nchini alieleza kuwa makomandoo hao walipata mafunzo ya ukomandoo katika nchi za za Libya, Israel na Pakstani.

Ya Pili, Kwamba CHADEMA kilikuwa kimeingiza Majangiri wa kundi la Mungiki (kundi linaloongoza kwa mauaji ya kikatili nchini Kenya) wapatao 40 na kuwafikisha Igunga. 

Akithibitisha taarifa hizo za Chama Tawala CCM, Mbunge wa Nzega (CCM), Hamis Kigwangalla ambaye naye kwa wakati huo alikuwa huko Igunga kwenye kampeni alisema kwenye mtandao mmoja kuwa "kuna Mkenya mmoja tumemkimbiza huku Choma, na sasa tunamuwinda mpaka tumkamate labda hapo tutaelewana! Mkakati gani huu wa kutuletea Mungiki Igunga jamani? Na sisi tuko sawa, tutawakamata na kuwapeleka polisi wenyewe kwa mikono yetu!"
Hamis Kigwangall, Mbunge wa Nzega CCM alithibitisha Uwepo
wa Mungiki Kutoka Kenya huko Igunga
 Ebu fikiria, "madaidi"  yanapenya kwenye mipaka ya Nchi na kuingia hadi katikati ya nchi kama Igunga ndipo Chama tawala kinayabaini. Wakati huo huo, kamanda wa Polisi huko Nzega alipoulizwa alisema yeye hajui kama kuna magaidi hao wakati Jemedari Mkuu wa Majeshi na mwenyekiti wa CCM anafahamu!

Wakati mtu akitafakari hizo taarifa na kujaribu kuziona kuwa na za kisiasa, ni muhimu kuzingatia kuwa mwenyekiti wa Chama hizcho kilichotoa hizo Taarifa ndiye Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiye Mkuu wa Majeshi na Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama wa Taifa. Siamini kwamba Rais anaweza akatoa Taarifa za UONGO kuhusiana na hali ya usalama wa Taifa kupitia Chama chake.

Taarifa za POLISI (1)
Mwezi wa kwanza nilikuwa Jijini mbeya kwa mapumziko ya mwisho/mwanzo wa mwaka ambapo nilipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba kuna Maiti za Wahamiaji Haramu zimeokotwa mkoani Morogoro. Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro alithibitisha kuwa maiti hizo zilikuwa ni za Wasomali walioingia nchini Bila Vyombo vya Ulinzi na Usalama mipakani kutambua, hadi walikamatwa Morogoro!

Katika taarifa iliyonishtua zaidi, kamanda huyo alisema kwa mwezi mmoja tu, Polisi Morogoro walikuwa wamekamata wahamiaji haramu 200 (mia mbili) kutoka Somalia ambao walipita katika Mipaka ya Tanzania ambayo tunahakikishiwa inalindwa salama na hadi wakafika Morogoro. [Kumbuka mkoa wa Morogoro uko katikati ya nchi na hivyo haupakani na nchi yoyote ya jirani. Maana yake ni kwamba Wahamiaji hao hupitia katika mipaka yetu na kuingia hadi ndani ya nchi].

Katika mahojiano na BBC, kamanda huyo wa Mkoa alionekana wazi kuvilaumu vikosi vya ulinzi vilivyoko mipakani kwa kutokujali kazi zao na kuruhusu wahamiaji haramu kuingia.

N.B: Ni muhimu kufahamu na kuzingatia kuwa Somalia ni eneo lililojawa na Magaidi na Maharamia kuliko maeneo mengine ya Afrika kutokana na kutokuwapo kwa Serikali imara kwa zaidi ya miongo miwili sana.

Taarifa za POLISI (2)
Katika juma hili hili nilikuwa naangalia TBC1 walipoonesha kuwa Mkoani Mbeya, wamekamatwa wahamiaji Haramu kutoa Ethiopia wakiwa kwenye nyumba ya mkazi wa Mbeya. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya alipoulizwa alisema kwa Mwaka 2010, jumla ya wahamiaji haramu wa namna hiyo (wanaotoka Ethiopia na Somalia) waliokamatwa mkoani Mbeya walikuwa 710. Mwaka 2011 walikuwa 450 (Jumla = Zaidi ya 1100 kwa miaka miwili tu).

Ni muhimu kufahamu na kuzingatia kuwa Wahamiaji hao huingilia katika mikoa ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga na huweza kupenya hadi kufikia Mbeya (wanai-cross nchi) wakiwa katika safari zao za kuelekea Afrika ya Kusini.

ULINZI NA USALAMA UKO WAPI?
Maswali ambayo yanaacha hali ya kuogopesha na kutia hofu kwa kila mtanzania anayebaini udhaifu huu mkubwa katika mipaka yetu ni kwamba iwapo wahamiaji hao haramu - ambao mara nyingi huwa katika safari zao tu za kuekea Afrika ya Kusini wanaweza kuingia kwa urahisi na kusafiri masafa marefu ndani ya nchi, je, ni kwa kiasi mtu mwingine yeyote anaweza akafanya hivyo hivyo?
Majeshi yetu hufahamika na kusifiwa sana kwa Uwezo wao
wa Kuwapiga Wanafunzi na Wananchi katika Maandamano ya Amani,
Kulinda Mipaka ya Nchi Je?
Iwapo hao wahamiaji wasio na mafunzo ya kijeshi, kigaidi au kijasusi (wakisaidiwa na mawakala wao) wanaweza kujipenyeza na kui-cross nchi kwa maelfu-elfu yao, Je, Ni nani tuliye naye hapa Tanzania anayeweza kuwazuia Magaidi au Majasusi wanaoweza kupanga kujipenyeza na kuingia hapa nchini kwa nia Mbaya?

Iwapo Magaidi yaliyopewa Mafunzo Libya, Israel na Pakistani yanaweza kuingia hadi kufika Igunga wakati wa Uchaguzi mdogo wa jimbo Moja, je ni magaidi mangapi yanaweza kuingia Tanzania na kuwawinda wagombeaji kama yatakavy wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge na Madiwani wa Nchi nzima?
Jeshi letu lina uwezo wa kufanya mambo mengi sana....
Hata kuvunja Tofali kadhaa kwa Ngumi Moja
Je, ni kweli kwamba amani na utulivu tulionao kwa sasa ni matokeo ya ulinzi "thabiti" wa mipaka yetu (kama tunavyoshawishiwa kuamini na wanasiasa wetu) au ni kwa sababu tu hakuna waovu ambao wameshakusudia kuingia kigaidi katika nchi yetu na "kutuliza"?

Je, mipaka yetu imeandaliwa kwa ajili ya ukagusi wa kina wa vyombo vya usafiri ambavyo mara nyingi ndivyo hupenyeza watu "kinyemela" kama wale wanaopakiwa kwenye chemba za mafuta kwenye malori makubwaya mafuta?

Binafsi nina mashaka na wasiwasi na hali ya Ulinzi na Usalama wa taifa letu, siamini kuwa usalama tulio nao ni matokeo ya ulinzi bora - zaidi tu kwamba "tunaishi hivi kwa neema ya Mungu" - sijui. Tuache kutiana moyo kisiasa wakati taarifa za kila siku zinaashiria hatuko salama, tuyakabili masuala kama yalivyo, tuyafanyie kazi kabla hatujaja kuumizwa ndipo tuanze kutafuta mchawi....

N.B: Makala isichukuliwe kama tangazo la hali ya hatariau dharura kwa taifa - maana hali hiyo huweza kutangazwa na taasisi husika tu.

2 comments:

  1. Hizi ni propaganda za kisiasa usitutishe hapa.

    ReplyDelete
  2. Watu hujipenyeza na kuingia nchini bila Vyombo vyetu vya Usalama kujua? Taarifa zilizotumika zote ni za Jeshi la Polisi, Taarifa za Magaidi na Mungiki - ZOTE zilitolewa na CCM (Chama Kinachoongoza Serikali)!!! Hoja hapo ni Je, Iwapo wahamiaji haramu tu (ambao hawana mafunzo yoyote ya kijasusi wa kigaidi) wanaweza kujipenyeza kutoka Kaskazini ya Tanzania mpaka wakaonekana Kusini mwa Tanzania - wakiwa nyumbani kwa mtu, Je, Magaidi yenye Mafunzo ya Kigaidi na Kijasusi, yenye Siraha na Nia Mbaya yanaweza kuingia mpaka wapi??? Hapo Propaganda ni Ipi? Au hukuelewa kiini cha Makala?

    ReplyDelete