MAAMUZI YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA CUF TAIFA JUU YA WANACHAMA 14 WALIOKIUKA MIIKO YA UONGOZI NA UANACHAMA NDANI YA CHAMA CHA WANANCHI CUF.
Baraza kuu la uongozi la taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF - CHAMA CHA WANANCHI) limemaliza kikao chake cha siku moja katika hoteli ya MAZSONS mjini Zanzibar limepokea tuhuma zinzowakabili viongozi na wanachama 14 wa chama kutoka kamati ya utendaji ya taifa.
Hadi saa 9 jana jioni lilisikiliza tuhuma za watano kati ya watuhumiwa ambao ni,
1.HAMAD RASHID MOHAMED(MBUNGE WA WAWI NA MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA)
2.DOYO HASSAN DOYO (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - TANGA),
3.SHOKA KHAMIS JUMA (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - PEMBA),
4.JUMA SAID SANANI (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - UNGUJA),
5.YASINI MROTWA (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - MBEYA).
Baraza kuu liliwasomea tuhuma zao watano hawa na kuwapa nafasi ya kujitetea kwa sababu wao ni viongozi wa baraza kuu(viongozi wa kitaifa wa chama) kwa mujibu wa kifungu cha 10 (5) cha katiba ya chama.
Baada ya kutafakari kwa kina maelezo ya tuhuma zao na utetezi walioutoa, baraza kuu la uongozi la taifa limeridhika kwamba wanne kati yao wamefanya vitendo vinavyowapotezea sifa za kuendelea kuwa wanachama. Hivyo basi, baraza kuu la uongozi la taifa limeamua kuwafukuza uanachama wa CUF viongozi hao wanne ambao ni HAMAD RASHID MOHAMED, DOYO HASSAN DOYO, SHOKA HAMIS JUMA na JUMA SAIDI SANANI. Uamuzi wa baraza kuu la uongozi la taifa kuwafukuza umefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 63 (1) (j), kifungu cha 64 (4), 64 (5), 64 (6) vya katiba ya chama.
Hamad Rashid, AMEFUKUZWA Uanachama CUF! |
Katika kufikia maamuzi hayo, baraza kuu la uongozi la taifa pia lilizingatia matakwa ya kifungu cha 62 (4), 62 (5), na 59 (8) (d) vya katiba ya chama ambavyo vinataka uamuzi wa kuwafukuza uanachama viongozi wa kitaifa wa Chama uwe ume umeungwa mkono na zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa baraza kuu kutoka tanzania bara na zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa baraza kuu wanaotoka zanzibar.
Uamuzi wa kuwafukuza uanachama viongozi hao wanne umeungwa mkono na wajumbe 23 kati ya 25 wa tanzania bara na wajumbe wote 22 wa zanzibar.
Wajumbe 2 wa tanzania bara hawakukubaliana na uamuzihuo.
Kwa upande wa Yasin Mrotwa, Baraza kuu la uongozi la taifa liliamua kumpa karipio kali kwa mujibu wa kifungu cha 64 (5), (b) huku mwenendo wake ukiendelea kuchunguzwa kati ya kikao hiki na kikao kijacho cha baraza kuu la uongozi la taifa.
Baada ya kutoa maamuzi juu ya wanachama hao 5 ambao ni viongozi wa kitaifa. Baraza kuu la Uongozi Taifa liliendelea na kikao na kuwahoji watuhumiwa wengine waliobakia. Baada ya mahojiano, baraza kuu lilitoa maamuzi juu yao kama ifuatavyo:
•Waliovuliwa uongozi ni:
1.DONI WAZIRI – ALIYEKUWA MWENYEKITI WA WILAYA YA ILALA,
2.MASAGA MASAGA – ALIYEKUWA KATIBU WA WILAYA YA ILALA,
3.MOHAMED ALBADAWI – ALIYEKUWA MWENYEKITI WA WILAYA YA ILALA,
4.HAJI NANJASE – ALIYEKUWA MWENYEKITI WA WILAYA YA NACHINGWEA.
•Waliopewa karipio kali kwa mujibu wa kifungu cha 64 (5), (b) huku mienendo yao ikiendelea kuchunguzwa kati ya kikao hiki na kikao kijacho cha baraza kuu la uongozi la taifa ni;
5.KIRUNGI AMIR KIRUNGI – MWANACHAMA,
6.TAMIM OMAR TAMIMU –MWENYEKITI WA CUF MTAA WA MKUNDUGE- KATA YA TANDALE, KINONDONI.
7.AYUBU MUSA KIMANGALE – MWANACHAMA
•Ambao hawakukutwa na hatia yoyote na kwamba waliingizwa katika kadhia hii kimakosa NA KWAMBA BARAZA KUU LIMEWAPA POLE KWA USUMBUFU WALIOUPATA KUTOKA NA KUHUSISHWA NA NJAMA ZA KUKIDHOOFISHA CHAMA ni;
8.YUSUPH MBUNGIRO – MKUU WA KITENGO CHA OGANAIZESHENI NA UCHAGUZI WILAYA YA TEMEKE.
9.AHMED ISSA - MWANACHAMA.
Baraza kuu la uongozi Taifa linamtaka mwanachama yeyote aliyefukuzwa au kuonywa au kuvuliwa uongozi, iwapo hajaridhika na maamuzi ya baraza atumie fursa ya kikatiba kukata rufaa mkutano mkuu wa taifa na sio vinginevyo.
Kukiuka katiba ya chama ambayo imeundwa na ndiyo inawaunganisha wana CUF wote ni makosa makubwa na hayatavumilika.
Baraza kuu linawataka watanzania wote kuendelea kuiunga mkono CUF kama chama pekee kinachofuata maadili na hakisiti kuchukua hatua pale ambapo taratibu ziunavunjwa na litaendelea na msimamo huo hata pale ambapo CUF itakabidhiwa kazi ya kuwaongoza watanzania.
''HAKI SAWA KWA WOTE''
Imetolewa na;
JULIUS MTATIRO
NAIBU KATIBU MKUU (TANZANIA BARA),
05 JANUARI 2012
No comments:
Post a Comment