Salaam ndugu zangu Waafrika. Mimi ni rais wa nchi mojawapo maskini barani Afrika – Jamuhuri ya Muungano wa Gambia, huko Afrika Magharibi. Kwa sasa nipo hapa Davos, Uswiss kuhudhuria mkutano wa mwaka – ambao kimsingi ni wa Nchi na Makampuni tajiri duniani. Nchi yangu ni maskini na inaishi kwa kutegemea misaada kwa zaidi ya 40% ya mahitaji yake kila mwaka – hivyo naamini wengi wenu mnashangaa nimefuata nini huku.
Ukweli ni kwamba Davos ni pazuri jama – tuache utani. Kuna hoteli kali sijawahi ona, pamoja na kuwa na baridi kali na barafu imefunika mji, lakini uzuri sisi viongozi tunapita kwenye barabara ambazo zimesafishwa, magari yetu yana heater na muda wote tunakaa mahali penye joto – barafu tunaiangalia kwenye TV tu kama nyie mlioko huko kwenye joto.
Hakuna foleni kama huko mliko nyie, na hapa sina cha msafara wala nini, sitanguliwi na ving’ora wala Polisi maana hata Rais wa hapa hajui kama nimekuja. Niliomba viza ya mtalii maana ningeomba viza kama Rais wangenikatia kwa sababu siko kwenye ratiba yoyote wala sijaalikwa. NInatumia kigari fulani cha kukodi walichonikodia CIA wa nchini kwangu, hamuwezi amini hiki ki gali nakilipia dola 5,000 kwa siku kukikodi - ila kizuri kusema ukweli.
Kwa sababu natokea nchi maskini, kimsingi sihitajiki wala sihitajiwi na mtu yeyote mimi kuwepo hapa – infact kuna hata baadhi ya viongozi waliopo hapa hawajui kama mimi na marais wenzagu wa Afrika tumekuja pia – mmoja nilimsikia jana akijishangaa tumekuja kufanya nini? Mzungu haelewi kinachotuketa sisi.
Ratiba yangu
Kwa sasa ninapo watumia hizi salaam nimekaa kwenye restaurant moja hapa karibu na mlango wa kutokea kwenye ukumbi wa mkutano walimo kina Obama. Nimemaliza kunywa chai na mapochopocho mengine. Niko na marafiki zangu marais wengine kutoka Afrika. Tunakaa hapa mlangoni ili kusubiri wanaohusika na huu mkutano wakimaliza tuwaombe kupiga nao picha.
Idadi ya Marais kutoka Afrika tulioko hapa ni wengi kuliko wale tunaohudhuriaga mkutano wa Umoja wa Afrika. Mi nashauri mkutano wa AU tuwe tunaufanyia huku huku Davos, tutapata washiriki wengi zaidi kuliko kuufanyia Uganda.
Picha hizi kama mnavyojua huwa zinatusaidia sana kuuzia sura huko Afrika tunapozisambaza kwenye mitandao Kama Facebook. Na hata kwenye kampeni huwa zinatusaidia kuonesha kwamba na sisi tunafahamiana na viongozi maarufu.
Kuuza Sura CNN
Jambo lingine la muhimu ambalo mimi binafsi na wenzangu wa Afrika huwa linatuvutia sana kuzamia mikutano kama hii (tunazamia kwa sababu sisi ambao kwetu Afrika tunaitwa viongozi huwa hatualikwi kwa maana wanaogopa tutakuja kuwaomba-omba misaada) huwa ni kupata nafasi ya kuonekana kwenye vyombo vikubwa vya habari kama CNN, Al-jazeera, BBC, CCTV, RT, Sky News, Fox News n.k.
Kwa kawaida vyombo hivi huwa haviwezi kuja hata nchini kwangu kunihoji nikiwa Ikulu, japo nilishawaalika mara nyingi, nikawaahidi kuwapa vyumba vya kulala pale pale ikulu na kuwalipa Allowance kama ya mimi Rais lakini walisema sina jambo la maana la kuwaambia – jama huwa wananidharau sana.
Lakini nikiwepo hapa, huwa wanaweza kunionesha – hata kama ni kwa bahati mbaya – nikiwa nasalimia na mtu kama Bill Gates, Obama, Sarcozy, M-Kameron n.k. Kuna wakati pia mida kama hii tunapokunywa chai kwa sababu waandishi hawa wanakuwa hawana kazi – wakisubiri mkutano uishe ili wapewe tamko la mkutano – huwa wanaweza kutuhoji kimtindo wakati wanapoteza-poteza muda kusubiri habari zenyewe.
Mwaka juzi nakumbuka niliwahi kuhojiwa hivi-hivi kwa bahati mbaya huko Ufaransa nikachapia kwamba sijui kwa nini Nchi yangu ni maskini. Ilikuwa soo kishenzi huko nyumbani Gambia, lakini niliporudi nikasambaza picha zangu nilizopiga na Bill Gates, Sarcozy na 50 Cent zikasaidia kupoteza soo nzima.
Nikawaambia pia 50 Cent amesema atakuja kuwekeza Gambia wananchi wakufurahi kishenzi na ile soo ikaisha. 50 Cent kumbe hata namba yangu ya simu hakui-save, nilimpigia siku nyingine akapokea Secretary wake, alipomuuliza kama anamjua rais wa Gambia akakana kujua hata kama hiyo nchi ipo duniani!
Nasikia jirani zangu Senegal wameondolewa kwenye michuano ya Afrika, huku mechi za Afrika wala hawajui kama zipo – hivyo hazioneshwi.
Gambia nasikia madktari nao wameamua kugoma. Jana shemeji yangu alinipigia simu kaniambia madaktari wamegoma na wagonjwa wanazidi kufa. Mke wake alikuwa ana upele nimeagiza Wizara ya Afya impele India akachekiwe afya yake. Kusema kweli mimi siwaelewi hao Madaktari, na ninaamini lengo lao tu niahirishe safari yangu na mishe mishe zangu Ulaya ili kuja kuwasikiliza.
Kwa taarifa yenu madaktari SIRUDI hadi nimalize ratiba zangu, nikitoka hapa natembelea nchi nyingine za Ulaya kwa ajili ya “kuimarisha mahusiano” halafu ndo narudi Bongo. Nawaahidi nikifika kabla hamjamaliza mgomo wenu nitaunda tume kuchunguza chanzo cha mgomo wenu na itanipa maepndekezo ya nini cha kufanya….
Ninamengi ya kuwaelezea ila naona mwandishi wa CNN anakuja kuelekea nilipokaa nadhani anataka kunifanyia intavyuu, ngoja nikae mkao wa kuhojiwa, nitaendelea kesho…. Ila kwa ufupi huku maisha matamu, Allowance inatumika vilivyo, ila kwa jinsi maisha yalivyo ghali, nadhani inabidi ofisi iniandalia Bonus ili kujazia pesa zangu nilizotumia….
NITARUDI kwetu Gambia mwezi ujao, Niombeeni Rais niendelee kuwa na Afya huku Ughaibuni!
Mussa, napenda kazi uanayoifanya una maono....keep on moving on...waTZ tunakupenda.
ReplyDeleteKaribu, Mary. Asante! Mussa
Delete