Monday, November 14, 2011

UDHAIFU WA CHADEMA


Katika makala yangu hii natafakari udhaifu wa Vyama vya Upinzani hapa Tanzania na changamoto zinazovikabili ili kuweza kufikia ndoto zao za kushika hatamu ya kuliongoza hili taifa. 

Hata hivyo, kutokana na kuibuka kwa CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani hapa Tanzania kinachoonesha upinzani mkubwa kwa Chama cha Mapinzduzi, mifano mingi na tafakari italenga katika kuelezea udhaifu na changamoto zinazoikabili CHADEMA, ambazo kwa namna nyingi hata hivyo zinavikabili vyama vingine ya Upinzani pia.
Pamoja na Kasi Kubwa ya CHADEMA katika "kuwashika" Watanzania,
bado Chama hiki kinakabiliwa na Changamoto  Nyingi

1.       “Uchanga”
Changamoto mojawapo kubwa ambayo inavikabili vyama vingi vya upinzani kwa hapa Tanzania ni “uchanga” wa vyama hivi katika siasa za Tanzania. Ninapozungumzia uchanga hapa simaanishi uelewa mdogo wa kisiasa ndani ya vyama hivi, bali uchanga wa vyama vyenyewe kimifumo na uongozi ndani ya vyama hivi.

Vyama hivi vingi vilianzishwa au vinaendeshwa na watu ambao hawakuwahi kupata uzoefu wa kiuendeshaji na utendaji katika mifumo ya kitaasisi kubwa, hususani ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, vyama vingi vinaongozwa kwa nadharia ya “learning by doing” (kujifunza kwa kutenda).

Hii inamaanisha kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kukosea, lakini kunapokuwa hakuna aliye bora zaidi ya huyo katika mfumo wa uongozi wa chama husika kunakuwa hakuna jambo la kufanya zaidi ya “kurekebishana” hivyo hivyo na kuendelea mbele.

Muda unavyozidi kwenda hata hivyo, vyama kadhaa vya upinzani vineonekana kuzdi kuishind hii changamoto ya “uchanga” wa kitaasisi na kuanza kujiimarisha.

2.       Kukosa “mizizi”
Changamoto nyingine kubwa ambayo inavikabili vyama vya upinzani Tanzania ni ukosefu wa “mizizi” ya kisiasa katika maeneo mbalimbali ya taifa – hususan vijijini. Kukosa wanachama wengi  - na zaidi oganaizesheni ya kiuongozi – katika maeneo ya “chini” inamaanisha vyama vingi vinabakia na nguvu katika maeneo machache ya nchi, hususan mijini.

Kwa jamii ya kitanzania ambapo takribani 70% ya watu wanaishi vijijini, kukosa mfumo wa kiutawala wa chama unaoanzia vijijini ni upungufu mkubwa mno ambao unaweza kumaanisha vyama hivi itabidi viendelee kusubiri miaka mingi zaidi kuweza kushinda chaguzi za kitaifa na kushika hatamu ya kuongoza taifa.

Vyama vya upinzani Tanzania vikiweza kupenya na kuingia vijijini na kukita mizizi yao kuanzia huko, hakuna ubishi kwamba mwisho wa Chama cha Mapinduzi utakuwa umekaribia sana – kama sio kwamba utakuwa umeshafika kabisa.
CHADEMA kimefanikiwa sana kuwa na Nguvu Mijini,
Nguvu hii ikiingia vijijini, CCM inaweza ikaanza rasmi
Kuwa Chama cha Upinzani Tanzania

Hii ni kwa sababu Vyama vya Upinzani, hususan CHADEMA vimeonekana kukubalika sana katika maeneo karibu yote ambako vimefika – mifano mizuri ni namna ambavyo vimeweza kushinda viti vya upinzani katika maeneo ya mijini ambako vimefika na kukubalika. 

Siku vikipenya na kuingia kwenye kambi kuu ya CCM ambayo imebakia kwa sasa – vijijini – CCM imekwisha!

3.       Ujinga wa Kisiasa
Watanzania wengi sana, kwa sababu zinazofahamika na zisizo fahamika, ni wajinga wa siasa. Ujinga ni hali ya kutokujua – SIO kwa maana ya kuwatusi. Ujinga huu unatokana na kutokuelewa hasa maana na sababu ya kuwepo kwa siasa katika jamii na taifa kwa ujumla. Lakini tatizo kubwa zaidi ni ujinga wa Siasa za Vyama vingi.

Watanzania wengi, hususan walio vijijini, walizaliwa na kulelewa katika mfumo wa Chama kimoja – Chama cha Mapinduzi. Sambamba na mfumo huo, pia wananchi walizoea mfumo ule wa “Chama na Serikali” ambapo utendaji wa chama na serikali ulikuwa hautofautishwi, hivyo wananchi wengi walielewa “Chama ndio Serikali”.

Watanzania wengi kwa "Ujinga", wako tayari kufa na
vyama vyao vya Siasa - hata kama hawaelewi ni kwa nini?!

Kwa hiyo tangu vyama vya upinzani vilipoanza kushiriki kwenye chaguzi mwaka 1995, wananchi wengi walikataa kuvichagua kwa kuhofia kuwa CCM ikiondoka madarakani Tanzania hakutakuwa na serikali – kwa sababu walijua CCM ndio Serikali! 

Mijadala mingi wakati wa kampeni za Uchaguzi mwaka 1995 ilitawaliwa na maswali ya hofu kama: NCCR watatoa wapi Polisi wao, watatoa Wapi Walimu wao, Watatoa wapi Wakurugenzi wao wa Halmashauri?. Hivyo wengi wakaogopa kuvichagua kwa kuwa walijua watendaji karibu wote waliokuwepo serikalini ni wa CCM hivyo wataondoka na CCM!

Zaidi ya hapo, imani waliyokuwa nayo kwa baba wa taifa wa Taifa Mw. Nyerere ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba wengi wao hadi leo hawadhani kwamba kuna Chama kingine tofauti na “Chama cha Nyerere” kinaweza kuongoza hii nchi vizuri – bila kujali kama hicho “cha Nyerere” chenyewe kwa sasa kinaongoza kama Nyerere alivyokuwa akiongoza au la.

4.       “Ulimbukeni”
Changamoto nyingine kubwa ambayo inavikabili vyama vya upinzani hapa Nchini – Hususan CHADEMA – ni ulimbukeni wa wananchama wao. Ni wazi kwamba chama kama CHADEMA kimepata umaarufu zaidi miaka kama 7 iliyopita. 

Hii, pamoja na mambo mengine ilichangiwa na Umahiri wa Wabunge wake wachache bungeni walioonesha Ujasiri na Uchapa kazi wa hali ya juu kiasi cha kuwafanya watanzania wengi kuamini kwamba hiki ndicho chama walichokuwa wanakitaka.

Matumizi ya Helkopta kwenye Uchaguzi wa mwaka 2005, pamoja na kebehi za CCM na vyama vingine vya upinzani, yalisaidia sana kui-promote CHADEMA maskioni mwa wananchi.

Umaarufu uliwafanya wananchi wengi kukimbilia kujiunga CHADEMA – ikiwa ni pamoja na wale waliohama CCM. Wengi miongoni mwao ni watu ambao hawakuwa na historia wala uelewa wa masuala ya Siasa, achilia mbali uongozi.

Wingi wa wafuasi kutoka maeneo tofauti ulimaanisha kulikuwa na uhitaji wa viongozi wengi zaidi wa mashina, kata, wilaya na mikoa. Wengi waliopewa nafasi hizi hawakuwa na uelewa wala uzoefu wa uongozi – zaidi kwamba WALIKUWA WAKISUKUMWA NA MHEMUKO NA HAMU KUBWA YA KUTAKA KUONA MABADILIKO TANZANIA – maarufu kama “Tanzania bila CCM”.
Hamu ya Mabadiliko imewasukuma watu wengi kutaka
 nafasi za Uongozi - hata zile ambazo ni bayana hawaziweki

Kusimamia na ku-handle kundi kubwa namna hii ya Wanachama ni changamoto kubwa sana. Mara nyingi sana nimekuwa nikiona mwanya mkubwa wa CHADEMA kuweza kupasuka na kusambaratika kirahisi sana kukitokea tatizo lolote – ikilinganishwa na vyama vingine vya siasa – CCM na vya Upinzani!

Mgogor wa Madiwani wa Arusha ni mfano mwingine mzuri wa namna ambavyo CHADEMA bado inakabiliwa na tishio la kuweza kuvunjia au kusambaratika katika baadhi ya maeneo kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wanachama wake.

Changamoto, vikwazo na matishio kwa vyama vya Upinzani Tanzania ziko nyingi sana, nitaendelea na tafakari hii katika sehemu ya pili yamaka hii, lakini nikiendelea kujiuliza: Pamoja na kuwa na Udhaifu na Mapungufu mengi kiasi hiki, kwa nini Watanzania wengi wanazidi kuendelea kuviamini hivi vyama na kukipa kisogo Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho kilitakiwa kushika hatamu zaidi....
Changamoto nyingine kwa CHADEMA ambayo
sijaiongelea Leo ni "NDOA" ya CCM na CUF!... tutaendelea

....itaendelea

Thursday, November 10, 2011

Tanzania Inahitaji MAPINDUZI pia!

Mapinduzi ya Libya, kwa Mfano, yalibadilisha
Serikali na Bendera, SIYO Mapinduzi tunayoyahitaji sisi kwa sasa
Kumekuwa na wimbi kubwa la mapinduzi na mabadiliko ya tawala na serikali mbalimbali duniani, yaliyoanzia Afrika, Mwezi Disemba mwaka jana!


Kiini cha Mapinduzi katika nchi hizi ni wananchi kuchoka tawala za Muda mrefu, zisizotaka wala kuleta mabadiliko, zinazowadhalilisha raia wake huku Viongozi wake kujinufaisha binfasi. Tunisia, Misri, Libya, Ugiriki, Italia..... zinazofuatia Yemen na Syria (Bahrain imesaidiwa na Saud kuwazima wananchi Kijeshi)....


Ukweli ni kwamba, pamoja na ukimya na utulivu, amani na upendo uliopo Tanzania, nchi hii inahitaji Mapinduzi - TENA HARAKA SANA!


Mapinduzi Tunayoyahitaji Sisi
Tofauti ni kwamba Mapinduzi tunayoyahitaji Tanzania, KWA KUANZIA, sio ya Serikali wala Chama Tawala - Ni MAPINDUZI YA KIFIKRA na KIMTAZAMO!


Kiini cha Matatizo yetu
Kiini cha matatizo makubwa yanayolikabili hili taifa kiko kwenye Fikra na Mtazamo wa Watanzania kuhusu taifa na utaifa wao. Kiini cha Matatizo yetu kama taifa SIO SERIKALI, ni wananchi!. Tanzania bado ina wananchi wengi sana ambao hawajitambui kama Raia na kwa jinsi hiyo hawatimizi wajibu wao kama raia wa Taifa!


Raia wa nchi wasiojitambua na wasiowajibika kama raia makini kwenye nchi yao KAMWE hawawezi kulisaida taifa lao kuendelea - hata wakipata Viongozi wazuri namna gani! Viongozi, ambao na wao ni wanadamu kama waongozwa, huhitaji kuzungukwa na kundi kubwa la wananchi wanaojitambua ambao muda wowote wako tayari kusimamia wajibu na kuutimiza - ikiwa ni pamoja na wajibu wa kuwawajibisha viongozi wao wasiowajibika!


Raia wawanaowalinda na kuwatetea viongozi wasiowajibika kwa sababu za kikabila, Kidini au vyama vyao vya siasa HAWAFAI na HAWAWEZI kulisaida Taifa kuendelea. Tanzania ya leo imejawa na watu ambao wako tayari kufumbia uovu wowote - NA HATA KUUTETEA - iwapo tu umefanywa na mtu wa Chama chao cha Siasa, mtu wa Kabila lao au hata Dini yao!


Watanzania tunajitaji kuanza jitihada za haraka na za kimakusudi za kufanya mapinduzi ya kimtazamo na kifikra kutoka katika mtazamo mgando ambao wengi wetu tunao kwa sasa na kuelekea katika mtazamo chanya wa kimaendeleo, wa kimageuzi na endelevu ambao utalisaidia hili taifa kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.


Hatuna budi kuanza kujenga mtazamo wa kujiona kuwa na sisi tunaweza kuwa Taifa tajiri, taifa lenye Maisha bora kwa kila mtu, taifa lenye huduma bora za kijamii - na haya yote PASIPO KUTEGEMEA MISAADA YA WAZUNGU!


Mtazamo wetu wa sasa wa kujiona sisi ni maskini, sisi hatuwezi, SISI TUNAHITAJI KUSAIDIWA NA WAZUNGU, sisi hatujui n.k. n.k. hautalisaidia wala kuliendeleza hili taifa. Tunahitaji kufanya mapinduzi ya jinsi tunavyojiona kama watu binafsi na jinsi tunavyoliona taifa letu!


Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, pamoja na mambo mengine, imependekeza kuwe na jitihada za kimakusudi za kujenga uelewa na kubadilisha mtazamo wa Watanzania. Hili lilikuwa ni jambo la muhimu sana, japo utekelezaji wake bado hauoneshi kuwa na utashi wa kuleta mabadiliko. Kwa hali ilivyo sasa, hatuhitaji tu Uelewa TUNAHITAJI MAPINDUZI!


Yakishafanyika mapinduzi ya kimtazamo na kifikra miongoni mwa Watanzania, sasa yanaweza kufuatiwa na mapinduzi ya kiutawala - kutoa tawala ambazo zinaweza kuwa zinang'ang'ania fikra pooza na ukale kuweka tawala zenye kuangalia, kuona na kulipeleka taifa mbele.


Pasipo mapinduzi ya kiufahamu, mtazamo na kifikra miongoni mwa Watanzania, mapinduzi ya Kiserikali au Kiutawala hayatasaidia sana kuiendeleza hii nchi. Mabadiliko ya watu ni ya muhimu sana katika kuiendeleza nchi kuliko mabadiliko ya kiuongozi na kiserikali tu....

Wednesday, November 9, 2011

USHOGA: Poleni Mliomsifu KIKWETE!

Siku Moja tu Baada ya Serikali ya Tanzania
Kutoa Tamko "Kali" Dhidi ya Serikali ya Uingereza,
Mwana-Mfalme wa Uingereza Anapewa
Mapokezi ya Heshima Kabisa na RAIS WETU!!

Jana katika tafakari yangu kuhusiana na Sakata la Tanzania kutakiwa kuruhusu Ushoga ili iendelee kupokea misaada kutoka Uingereza, nilielezea kwa ufupi ni kwa kiasi Gani Sera KUOMBA-OMBA MISAADA za Rais wetu KIKWETE zimachangia kulifikisha taifa kwenye hali hii.

Siku chache baada ya kauli ya David Cameron, Waziri Mkuu wa Uingereza, kutishia kusitisha misaada, Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje Membe iliirukia hiyo fursa na kutaka kuitumia kutunisha misuli kwa Wazungu. 

Kauli ya Membe ilijawa na kauli zenye kuonesha Ujasiri, Msimamo, Kutokuyumbishwa, Uhuru wa Taifa na mbwembwe nyingi ambazo mtu yeyote anatarajia kuzikuta kwenye hotuba ya Kiongozi wa Nchi wa Maskini anayetaka kuonekana kwa wanachi wake kuwa ni Maskini Jeuri!

Namfaham KIKWETE wa DOWANS...!
Tarehe 5/februari/2011 kwenye maadhimisho ya miaka 34 ya CCM, Kikwete wakati akihutubia alitoa kauli ambazo kwangu HAZIKUFAA kutoka kwa kiongozi wa taifa. Kwa ufupi, alitoa kauli ya kukana kata-kata kuwajua wamiliki wa DOWANS! 
Akihutubia Wana-CCM Dodoma, KIKWETE alikana kuwajua DoWANS,
siku Chache baadaye ALIMKARIBISHA IKULU MMILIKI WA DOWANS
 MPYA (Symbion Power)!!!

Kauli hii, kwa wananchi wengi ambao hawamjui Kikwete ninayemjua mimi, walishangilia na kuichukulia kama kauli inayomaanisha Kikwete hahusiki kwa namna yoyote na DOWANS (japo hata kwa Uzembe tu)!

Miezi michache baadaye, nikiwa safarini kuelekea Iringa, nilinunua Gazeti moja na kukuta Picha kubwa ya rais Kikwete akiwa IKULU amekaa anazungumza na kucheka na Mmiliki wa Kampuni ya Symbion Power (AMBAYO NDIYO ILINUNUA MITAMBO NA MKATABA WA DOWANS)!!!!!!!!!!!!

Serikali Yaipinga Uingereza!
Baada ya tamko la Serikali kupinga "vikali" kauli ya waziri Mkuu wa Uingereza, Viongozi wa Dini mbalimbali walimimina Salaam nyingi za pongezi kwa Serikali kwenye makongamano yao ya Sherehe na Ibaada! 

Taarifa za Vyombo vya habari siku ya Idd, kwa mfano, zilifunikwa na Pongezi za Masheikh kwa Serikali kwa kupinga Ushoga! Maaskofu na Mapdre hawakuwa nyuma katika "mbwembwe" hizo pia za "kuipongeza" serikali - HAWAIJUI Serikali yetu, labda!

Mfalme wa "Ushoga" Atinga Ikulu!
Kama ilivyotokea kwa DOWANS na hatimaye Symbion Power, Siku moja tu Baada ya Wananchi kuimiminia Serikali Pongezi nyingi kwa kauli yake dhidi ya Ushoga, SIKUAMINI MACHO YANGU KUMUONA KIKWETE YUKO PRINCE CHARLES WA UINGEREZA, IKULU, DAR ES SALAAM!!!!!!!!!!!!!!!!!
Muda Mfupi baada ya Serikali "Kuikoromea" Uingereza,
Ni tabasamu na Vicheko IKULU, KIKWETE na
Mwana-Mfalme wa Uingereza!!!!!!!!!!!!!!!
Kitendo hakikunishangaza sana kwa jinsi ambavyo tayari namfaham Kikwete, lakini nilijua ni sawa na kofi la usoni kwa walimimina pongezi nyingi kwa Serikali siku moja kabla. Nilipouliza nikaambiwa tena SIO kwamba Prince Charles aliomba kuja Tanzania, BALI ALIALIKWA NA KIKWETE!!!!!!!!!!!!!!!

Iwapo ni kweli kauli ya Membe ilikuwa ina mashiko na nguvu kama ilivyodhaniwa wakati anaitoa kwa waandishi wa habari, basi ilikuwa ni dhahiri kwamba Tanzania ilikuwa imefikia katika hatua nzuri ya kuwaonesha Waingereza kwamba "haipelekeshwi" na masharti yao.

Kwangu mimi, safari hii ya Mwana Mfalme Charles hapa Tanzania ingekuwa ni fursa nzuri ya Serikali kuonesha kwamba imekasirishwa na kauli ya Cameron kivitendo. Hakuna kitendo ambacho kingeonesha kuwa Serikali imekasirishwa na hiyo kauli kama KUMZUIA Prince Charles ASIJE Tanzania hadi hapo baadaye.
kama kawaida, Mzungu akija kwa WATU MASKINI KAMA SISI
Lazima atoe msaada - japo wa  Vitabu - Hata kama Msaada
una thamani ndogo KULIKO CHAKULA TULICHOMLISHA SISI!!!
Mambo ya msingi ambayo serikali yetu ambayo ingeyafanya, iwapo ilikuwa serious na zile kauli za Membe, ni pamoja na kutaka Maelezo Rasmi ya kimaandishi kutoka kwa Serikali ya Uingereza kuhusiana na hiyo kauli au kuikanusha, na hata kuahirisha Ziara za Viongozi wa Uingereza hapa Tanzania hadi suala husika litakapokuwa limetolewa ufafanuzi na kueleweka vizuri kwa pande zote....!

IKAWA KINYUME....
BADALA YAKE Vicheko, hoi hoi, Nderemo na vifijo vilitawala Ikulu wakati Mwana Mfalme wa Uingereza alipotinga Ikulu ya Tanzania na kupokelewa na KIKWETE kwa tabasamu, furaha na amani yote ya moyo!!!

Kawaida, Hotuba fupi ikasomwa, sina uhakika ni nini kilikuwemo kwenye hotuba hii, lakini mara nyingi huwa zinakuwa na maelezo ya kueleza "shida" tulizo nazo na kuzitumia "KUOMBA MISAADA"...
Hotuba hizi mara nyingi hutumiwa kuelezea Shida
zetu katika nchi "maskini" kama Tanzania na kutumiwa Kuombea Misaada!
Poleni ambao hamuzifahamu Serikali za Afrika!
Nawapa pole wale wote ambao labda - kwa kujua au pasipo kujua - walikimbilia kuipongeza Serikali kwa kauli yake kuhusiana na Ushoga majuzi, kwa sababu hawakujua kuwa Serikali ya Tanzania ni sawa na serikali nyingi za Afrika - Inaongozwa na Watu ambao wanategemea sana MISAADA na wakati huo huo WANAPENDA SANA Kusifiwa na wananchi wao kuwa "Mashujaa" wa kupinga "Ukoloni Mambo leo" - japo kwa kauli tu....

Tanzania bila Misaada inawezekana, Japo sioni kama tuna viongozi Tanzania wanaoliona, kuliamini na kuliweka hilo kwenye vitendo......

Sherehe Za UHURU Miaka 50 Zitagharim Shilingi Ngapi?



Nilipoipokea hii post hapa Chini kwenye Email yangu, iliamsha hamu yangu ya kufahamu haya maandalizi ya Sherehe za Uhuru yataligharimu taifa kiasi gani Cha fedha??


Kwa bahati mbaya sana nina experience mbaya ya Matumizi ya fedha za Umma kwenye sherehe au matukio mbalimbali. taarifa zinaonesha kuwa MABILIONI KWA MABILIONI hutumika kwa kuandalia Sherehe mbalimbali ambapo watu wengi hulipwa Posho pamoja na manunuzi yenye gharama kubwa.


Ninaomba kama kuna Mtu ana taarifa japo za mfano kutoka Wilayani, Mikoani au hata kwenye Wizara / Taifa kuhusiana na Bajeti mbali mbali ambazo zimetengwa kwa ajili ya "Sherehe" hizi. Tayari naona matumizi makubwa ya fedha kwenye "Vipindi Maalum" vya Televisheni taasisi zikijisifu kwa jinsi zilivyo "thubutu, weza na kusonga mbele"....


Mwenye taarifa na takwimu tafadhari!

"Wapendwa wana AZAKI napenda kueleza dukuduku langu juu ya nilichosikia na kushuhudia katika maadhimisho ya sherehe ya miaka 50 ya Uhuru wa TZ.Kwa kweli kinacho fanyika ni ULAJI MTUPU.Habari nilizo zipata ni kwamba viongozi walio alikwa kwenye sherehe hizi hapa kwetu Iringa ni LUKUKI.


Kila Wilaya imeleta  wakuu wa idara ambao kwa kawaida ni idara 12 mara wilaya zetu saba unapata 84,Wakuu wa Wilaya 7,Wakurugenzi 7,Hawa nikutoka wilayani.Bado wale wa Idara za Mkoani,Wanajeshi,Usalama wa Taifa,TakukuruWenyeviti wa Halmashauri toka Halmashauri 7,wenyeviti na makatibu wa CCM wa wilaya 7.Jumlisha madereva,na kama unavyo jua wa TZ kila BOSI anataka kuja na gari lake,Ndiyo, atajulikanaje?


Hawa wote kwa jiji tarajiwa la Iringa wana lipwa posho ya   tsh 80,000/=achana na MATUPUTUPU kama sio Maluplupu mengine.Ni sherehe ya siku karibu tano hivi.Ukipiga hesabu za darasa la tatu,ni mamilioni.Wakubwa hawa wana kula na kunywa kuadhimisha miaka 50 ya kushindwa kuwaondoa maadui wale ambao aliwaacha mkoloni miaka hamsini,UJINGA,UMASIKINI NA MARADHI.


Wakubwa wanajipongeza kwa hayo.Hakika ni aibu sana,katika hospitali zetu hakuna dawa,shuleni hakuna madawati walavitabu,Hivi kweli tuna sababu ya kujisifia?



 Oneni mambo haya wana AZAKI.Nyuma yake msafara wa mwenge nao unakula mapesa ya walala hoi.Mungu ibariki Tanzania,tubariki wanyonge wote,ili siku moja tuwapate viongozi wenye uchungu na wananchi wao na watetea haki.
 
Nawatakia kazi njema."
 
Severin mtitu
mkurugenzi-ADG.
Box 1002.
Iringa.

Tuesday, November 8, 2011

USHOGA: KIKWETE Umechangia Kutufikisha Hapa!

Kikwete akiwa na Waziri Mkuu
Mstaafu wa Uingereza ofisini kwake London.


Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alitoa kauli moja ambayo sijui kama yeye mwenyewe alikuwa ameifikiria madhara yake kwa watu anaozungumza nao au la! Kwa Ufupi, alieleza kuwa Uingereza itaanza kuzuia misaada kwa nchi zinazopinga / zisizoruhusu uhuru wa Mashoga na Ushoga!


Hakujua Watu VIONGOZI (wa kiafrika) aliokuwa akizungumza nao ni Viongozi ambao wanaishi kwa kutegemea Misaada mingi kwa upande mmoja na kwa upande wa Pili wanaopenda kusifiwa na wananchi wao kila inapotokea fursa ya kuonesha kuwa wao ni mashujaa na majasiri - Cameron ALIKOSEA!


Kauli hiyo ilipokelewa "vibaya" na watu wengi Afrika, ikiwa ni pamoja na Watanzania! Serikali yetu haikupoteza muda kuirukia hiyo Fursa kwa ajili ya kujionesha kwa wananchi wake kuwa "haiburuzwi" kwa misaada, na ikatoa tamko kupinga kauli ya Cameron na ya kuonesha kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kukosa misaada ya Uingereza iwapo itakuwa na sharti la Ushoga (japo tulimpokea Mfalme wa Ushoga (Uingereza) kwenye Ikulu yetu jana kwa Mbwembwe na Sherehe kubwa)!!!!!!!!!!!
Kikwete hujisifia sana kukutana na watu maarufu,
 kupiga nao picha na Kuwaomba Misaada!


Usahaulifu wa Watanzania
Watanzania, pamoja na mambo mengine huwa wana sifa moja kubwa ya kusahau kwa haraka sana mambo na matukio muhimu yanayotokea kwenye jamii yao hata yale ambayo yanagusa sana maisha yao, na huwa wepesi wa kurukia mada / hoja mpya ambazo nazo huisha na kupotea haraka kwenye kumbukumbu na ufahamu wao.
Kikwete akipigwa-pigwa bega na Bush
baada ya kuahidiwa Msaada na Marekani!


Kikwete na Misaada
Sijui kama hapa Tanzania kuna Rais aliyewahi kufurahia kuomba-omba misaada, kufurahia kupewa misaada na kujivunia waziwazi na hadharani kupewa misaada na Wazungu KAMA KIKWETE! Nakumbuka Mkapa alikuwa mstari wa mbele katika kulipa madeni ili nchi ipewe misaada lakini sijui kama alifikia "rekodi" iliyowekwa na Kikwete.


Kwenye Kampeni za mwaka jana za Urais, Kikwete akihojiwa ITV, alitumia muda mwingi kujisifu kwa jinsi ambavyo amefanikiwa kuzunguka karibu dunia nzima - na mara zote watu walipokuwa wakipinga safari nyingi za Nje alikuwa AKIZIHALALISHA kwa KIWANGO CHA MISAADA alichokuwa anapewa / kuahidiwa na Wazungu!
Kikwete mara nyingi sana huonekana kwenye
Mikutano ya Kimataifa na wazungu, ambapo
hutumia nafasi hizo kuomba misaada
Kilicho NISIKITISHA SANA, KUNIUMIZA NA KUNISHANGAZA ni pale Kikwete - pasipo kuonesha anaelewa anachokisema - alipojisifu kwa jinsi alivyofikia hatua ya KUOMBA MISAADA KWA WATU BINAFSI (WAZUNGU) ili hao watu waje kuisaidia Nchi!!!!!!!!!!!!


Madhara ya Misaada!
Mimi ni mmoja wa Watanzania ambao wamekuwa msitari wa mbele kwa miaka mingi kupinga utegemezi wa misaada kwa taifa tajiri na lenye rasilimali nyingi kama Tanzania.


Siku moja nilimuuliza Mkurugenzi wa Benki ya Dunia iwapo misaada wanayotupatia inatusaidia na iwapo itatuwezesha kujitegemea alisema hiyo ni ndoto na tutaendelea kutegemea misaada kwa miaka mingi ija. Sehemu ya Taarifa hiyo inapatikana hapa: http://www.ippmedia.com/frontend/functions/print_article.php?l=13683
Sijui kama kuna rais yeyote mashuhuri ambaye Kikwete
hajawahi kukutana naye - na kuitumia hiyo nafasi KUOMBA MISAADA.
Hapa akiwa na Rais wa Ufaransa, Sarkozy
Sio tu kwa sababu misaada hudhalilisha "utu" wa taifa na watu wake, bali pia kwa sababu huwa ni mlango wa wale wanaotoa msaada kupenyesha ajenda zao katika taifa linalopokea misaada. Ukweli ni kwamba misaada ni zana ya kuzibana, kuzidhibiti na kuzinyanyasa nchi maskini kuliko inavyotumika kama chombo cha kuleta maendeleo.


Hii inajidhihirisha wazi kutokana na Masharti ambayo huambatanishwa na misaada katika nchi zote - ambapo masharti hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. 


Kwa mfano, wakati Nchi kama Marekani na Uingereza zinapotoa misaada kwa Tanzania na nchi nyingine za kiafrika husisitiza "Haki za Binadamu", "Demokrasia" n.k., Nchi hizo hizo zinapotoa misaada Pakistan, Afghanistan n.k. huwa haziweki mashari ya Demokrasia na Haki za Binadamu!!! Hii ni kwa sababu malengo yao huko yako tofauti na malengo yao kwa Tanzania na Afrika!


Uhusika wa Kikwete
Tabia ya Rais wetu kuwa mstari wa mbele katika kuzunguka duniani kuomba-omba misaada na kujisifu kwa jinsi anavyopewa misaada ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa leo tunaona kauli ya Cmaeron kuwa tishio.
Kikwete akisaini Mkataba wa "Msaada" kutoka Marekani


Kikwete angekuwa ametumia muda mwingi wa utawala wake kusimamia ukusanyaji, utumiaji na uendelezaji wa rasilimali za taifa hapa ndani ya nchi leo watanzania wasingeona kuwa kauli ya Cameron inalihusu taifa Letu!


Kilichotushitua wengi, na tukakimbilia kuisifu serikali kwa kauli yake ni mtazamo, akili na fikra zatu ambazo wote tumeaminishwa kuwa Misaada ni kitu muhimu na cha lazima sana kwetu, hivyo jambo lolote likisemwa kuhusiana na misaada lazima lituguse sana - JAPO HAIKUPASWA KUWA HIVYO!!!


Kitendo cha Kiongozi wa Nchi yetu kutokuweka msisitizo katika kuwawezesha Wananchi na Serikali yao kumiliki na kuendesha nyenzo kuu za Uchumi wa Taifa kama Sekta za Madini na Utalii na badala yake kukimbilia kuwaita Wazungu waje kuwekeza, kimeliacha taifa "UCHI" kwa kiasi kikubwa sana mbele ya Wazungu na Wageni wengine.
Kikwete huzunguka na Kukutana na watu wengi Maarufu
ambao huwakaribisha Nchini kama "Wawekezaji"...


Tabia ya kuwa na kiongozi anayezunguka dunia nzima kuomba misaada na kisha kuja kujisifu kwa raia zake pale anapopewa misaada ndicho mlango mkuu kwa taifa kuweza kuingizwa au kujiingizwa katika masharti magumu na mabaya ambayo wakati mwingine yanalidhalilisha Taifa na Raia wake!



Mapendekezo yangu
Wakati taasisi za Kidini, vyama vya siasa na wananchi tukiendelea kumimina sifa zetu kwa "Membe" kwa kauli yake ya kupinga Sharti la Ushoga, ni lazima tuangalie na kubaini kuwa  mlango huo wa Masharti ya Ushoga Umetokana na nini.


Mlango huu tumeufungua wenyewe kama taifa, tukiongozwa na "viongozi" wetu wa sasa na waliopita. Tumeufungua kwa kuamua kama taifa kuacha kuwajibika kwa namna ipasavyo katika kujipanga kitaifa kutumia na kunufaika na rasilimali zetu wenyewe, badala yake tumeamua kwa makusudi kama taifa KUWAONA WAZUNGU KAMA MIUNGU ambayo haiepukiki ili tuweze kuendelea kama taifa.


Kasumba ya kupenda na kusifia MISAADA YA WAZUNGU imetufanya tufikie mahali tuone kama vile hatuwezi kuishi bila kufanya ziara za Ulaya, Hatuwezi kutumia na kunufaika na rasilimali zetu bila kuwauliza na kusaidiwa na Wazungu n.k.


Hili la Ushoga ni moja, tukiendelea na tabia hii ya kuwa na SERIKALI LEGELEGE katika kushughulikia maendeleo ya kitaifa, muda si mwingi tutapewa masharti magumu zaidi ya Ushoga, na kwa UPUMBAVU WETU tutalazimika kuyakubali Ili tuendelee kupokea misaada!


Tuchukue Hatua
Moja ya mambo ya msingi ambayo tunapaswa kuyafanya kama taifa, ni kurudi kwenye msingi alioanza kutujengea baba wa taifa wa Kujitegemea kama taifa. Hii kasumba ya kuwaabudu wazungu na kujiona kama vile sisi hatuwezi kitu pasipo Wazungu ndiyo imetufikisha hapa na Itatufikisha pabaya zaidi!
......


Kama taifa, tunapaswa kujipanga na kutafuta njia zinazoweza kulisaidia taifa na raia wake kutumia na kunufaika na rasilimali zao badala ya kuendelea kujisifia LUNDO LA WAZUNGU ambao huwa tunawapamba kwa majina ya wabia na wawekezaji - wakati wengi wao ni wanyonyaji tu!


Hitimisho langu kwa Leo
Mimi naamini hata kwa misaada ambayo tumeshapewa, tunaendelea kupewa na tunaendelea kuipokea, TAYARI TUMESHAKUBALI MASHARTI MENGI KULIKO USHOGA, na tunajisifia kwenye hotuba zetu na kampeni zetu za Uchaguzi!!!


Kasumba hii ya kuwa na Viongozi VIPOFU NA MASKINI WA FIKRA, wasioamini kwamba Tanzania na watanzania wanaweza kuendelea pasipo misaada ya Wazungu imeshatuponza sana na itaendelea kutuponza sana.


Kauli za Kupinga masharti ya Ushoga kwenye Misaada
hazitatusaidia iwapo hatutachukua hatua za
Kuachana na Utegemezi wa Misaada na Badala yake
Kujisifia kutembelewa / kukutana na Marais Maarufu Duniani!
Tusipobadilika kama taifa, kauli kali za kujifanya tuna uhuru hazitalisaidia hili taifa iwapo tutaedelea kuwa na viongozi wasio amini kuwa Tanzania inaweza kuendelea kwa jitihada zake pasipo misaada ya Wazungu!!!