Monday, August 1, 2011

KIKWETE NA UMEME: Majibu Finyu au Mawazo Finyu?

Hivi karibuni kulitokea tukio moja la aibu sana kwa Rais wetu na taifa letu kwa ujumla, japo kama kawaida yetu watanzania, huwa ni wepesi sana wa kusahau masuala ya msingi, na hilo nalo tayari ‘sio habari’ tena. Ni kitendo cha KIKWETE kuamua kuendelea na ziara Afrika ya Kusini, wakati hali ya taifa ikiwa ni mbaya.
"tatizo ni pale mtu anapoti msisitizo pasipohitaji kuongelewa kabisa na kuweka matani kwenye masuala nyeti"

Bajeti ya Wizara ya Nishati (moja ya mihimili muhimu ya uchumi na maendeleo ya taifa) imekataliwa na Bunge ambalo majority ya wabunge wake ni wale ‘anaowaongoza’ yeye kwenye chama chake! Zaidi ya hapo, fedha za umma zinatumiwa kuwahonga wabunge ili wapitishe bajeti mbovu. Mtuhumiwa ananaswa, mfukuzaji ambaye ni Rais, anasema suala hilo liachwe hadi atakaporudi (badala ya kurudi saa hiyo hiyo)!!!!!!!!!!!!!!!!!

Kibaya zaidi ni kwamba, wakati hayo yanatokea Tanzania, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alikuwa huko huko Afrika ya Kusini kwenye ziara ya kiofisi. Aliposikia kulikuwa na tatizo linahosisha uchunguzi wa bunge nchini kwake, aliacha mara moja ziara yake na kupanda British Airways kurudi nchini kwake kushughulikia matatizo kwa karibu zaidi (kiongozi wa taifa tajiri kama Uingereza hana ndege binafsi ya kazi kama RAIS WETU)!!!!!

Akiwa huko, nasikia Kikwete alihojiwa na mtangtazaji wa BBC kuhusiana na matatizo ya umeme hapa nchini. Baadhi ya majibu aliyoyatoa (japo sio mara ya kwanza kwake kuonesha huo mtazamo), ndiyo yalinifanya nijiulize kwa mara nyingine; Je, Majibu yake ndiyo finyu kuhusiana na Upana na Unyeti wa tatizo hili; AU MTAZAMO WAKE NDIYO FINYU KUHUSIANA NA TATIZO HILI???

Baadhi ya Majibu ambayo rais wan chi (katika karne ya leo) aliyodiriki kuyatoa redioni ni kama haya:
i.                     Tatizo la umeme kimsingi ni suala la ukame tu.”… 
ii.                   Kwanza, serikali haina uwezo wa kufanya mvua inyeshe, unajua unajua hivyo, Kwa sababu (kicheko) ingekuwa na uwezo wa kufanya mvua inyeshe mabwawa yale yangejaa.”…
iii.                  Sasa ni hivi, unajua hii mitambo ya umeme si mitambo unaenda kununua kama unavyonunua jaketi lako hili. Ni kwamba ukitaka mitambo ya umeme, lazima uweke order wakutengenezee”…
iv.                 Sasa kama kuna mtu ana maarifa ya haraka zaidi nasema mtu atoe maarifa hayo na sisi kama yapo tutayafanyia kazi.”…
Haya ni sehemu ya majibu aliyokuwa akiyatoa RAIS WA NCHI YETU!!!!! Majibu haya yaliongezea maswali kumuhusu rais wetu, uwezo wake au uwezo wa serikali kuweza kushighulikia changamoto zinazolikabili taifa na raia wake – bila kujali itikadi za vyama vyao!

Majibu yake yanaacha maswali mengi sana kama:
i.                     Ina maana Rais wetu anaamini matatizo yetu ya Umeme yatamalizwa na Mvua za Uhakika mabwawani??
ii.                   Ina maana Rais wetu anaona kwamba Mitambo ya Umeme inapaswa kuagizwa pale mgao unapoanza, ndio maana wananchi inabidi wasubirie muda mrefu (kumbuka mgao umeanza miezi michache tu baada ya yeye kuingia madarakani 2005)!!!!
iii.                  Ina maana hadi sasa hivi KIKWETE na serikali yake hawana Options zote zinazowezekana ambazo wanaweza kuchagua kati yake ili waitumie kumaliza hili tatizo (hivyo amekaa Ikulu akisubiri apelekewe options azifanyie kazi)??? N.k n.k.

Majibu haya yananirudisha nyuma na kunikumbusha wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita wakati Kikwete alipoulizwa iwapo alikuwa na picha ya serikali ambayo angependa kuiacha mwaka 2015 baada ya uraia wake akasema HANA PICHA! Sasa, nadhani hata watanzania ambao walikuwa hawaelewi anamaanisha nini, sasa wanaelewa wazi na kweli kwamba KIONGOZI HUYU HANA PICHA!

Kwa ufupi, mimi binafsi naona jambo linalolisumbua taifa letu sana kwa miaka kadhaa sasa, ni ukosefu wa Uongozi hapa Nchini. Kuna ombwe (vacuum) kubwa katika nafasi nyeti za uongozi na maendeleo ya taifa, na ni wazi kuwa taifa hili halitaweza kuendelea hadi nafasi hizi muhimu zilizo wazi zitakapojazwa!!!



Ni wazi kuwa mtazamo finyu kama huu kwenye masuala mapana na mazito kama haya hauwezi kulisaidia taifa hata siku moja. Japo maendeleo huwa yanahitaji subira, lakini huwa ni muhimu sana kuelewa una-‘subiri’ nini! Kusubiri mtazamo finyu kama huu kumaliza matatizo ya taifa ni kama ndoto ya abunuasi!

Kama makala hii inavunja katiba au sheria yoyote ya nchi, natanguliza kuiomba msamaha nchi yangu
picha na au michoro iliyotumika ni mali ya wenye hakimiliki zake, pale inapohusika

YAFUATAYO NI MAHOJIANO YA KIKWETE NA OMAR MUTSA HUKO AFRIKA YA KUSINI

Majibu niliyoyapaka Rangi ndo “Nimeyapenda” ZAIDI



BBC: Suala la Umeme Mheshimiwa Rais Kikwete ungependa kulizungumzia nini?

Rais Kikwete:
 Tatizo la umeme kimsingi ni suala la ukame tu. Kwa sababu mabwawa yetu ya kuzalisha umeme yanayotoa umeme karibu MW600 sasa hivi yanatoa umeme kidogo sana. Maji pungufu ndio maana kuna tatizo hilo.

BBC:Mheshimiwa, hili suala si la leo wala si la jana limekuwepo kwa muda mrefu, kwanini serikali haina njia mbadala ya kuweza kutatua suala hili? Tanzania ina raslimali nyingi mheshimiwa Kikwete!

Rais Kikwete:
 Kwanza, serikali haina uwezo wa kufanya mvua inyeshe, unajua unajua hivyo, Kwa sababu (kicheko) ingekuwa na uwezo wa kufanya mvua inyeshe mabwawa yale yangejaa. Ni kweli kuwa Tanzania inazo raslimali za kutosha na katika kipindi hiki - toka wakati ule - sisi tulipoingia tumekuta suala la Ukame na mwaka 2007 tukapata matatizo ya kwanza. 

Baada ya pale tukafanya uamuzi kwamba sasa tuanze kuwekeza katika vyanzo vingine; tuongeze uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vingine. Tuongeze uzalishaji wa umeme kutoka vya vya kutumia gesi asilia twende kwenye makaa ya mawe. Kutoka vyanzo vya gesi asilia tayari tuna mtambo pale Ubungo, na toka mwaka 2009 mpaka sasa tumeshaongeza MW145, itakapofika Disemba tutakuwa tumeongeza MW160 nyingine. Tutakuwa tumeongeza MW300 siyo kidogo.

BBC:
 Mhe. Kikwete Mmoja katika wabunge Bw. John Mnyika ambaye ni Mbunge wa upinzani ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati amekuwa akilalamika na kwamba amewahi kusema kwamba hili tatizo ni tatizo linalowahusu Watanzania wote na amesema mje pamoja na kuona vipi mtakavyotatua tatizo hili. Na sasa hivi Bungeni wamesimamisha mswada, wa kutoa bajeti ya nishati ya Tanzania. Wewe unachukulia vipi matamshi kama haya kutoka kwa Wabunge?

Rais Kikwete:
 Mimi nasema hivi yeye si Mbunge atoe maarifa yake tu; anayo maarifa gani na anapendekeza kitu gani. Kwa sababu toka Uhuru mabwawa tuliyotengeneza ni Kidatu MW200, Mtera MW80, Kihansi MW 165 mimi nilipokuwa Waziri wa Nishati, pale Pangani tumeongeza.
Sasa ufikirie kwamba toka Uhuru tumeweza kuzalisha umeme wa MW600, lakini toka 2009 mpaka Disemba mwaka huu tutakuwa tumeongeza MW300! Ni jitihada kubwa. Mimi nasema kwamba usipozitambua hizo ni kwamba wewe mwenyewe siyo mkweli.
 

Sasa ni hivi, unajua hii mitambo ya umeme si mitambo unaenda kununua kama unavyonunua jaketi lako hili. Ni kwamba ukitaka mitambo ya umeme, lazima uweke order wakutengenezee. Huu mtambo unaofika mwaka huu Disemba order tuliweka mwezi wa Juni mwaka jana. Inachukua muda huo kutengeneza. Sasa ingekuwa mnaenda kutafuta mitumba, mitumba ya mitambo tu ya kununua iko mingi kweli. Tukasema hatuwezi kufanya hivyo. 

Mimi nasema hivi, kitu kikubwa ni kuwa na subira. Tumefanya jitihada kubwa. Ni lazima watu watambue kuwa tumefanya jitihada kubwa katika miaka hii toka 2009 mpaka sasa hivi 2011 Disemba tutakuwa tumeongeza MW300 kulinganisha na MW600 ambazo tumeziongeza katika miaka yote hii. Nasema ni lazima watu watambue hivi.Sasa kama kuna mtu ana maarifa ya haraka zaidi nasema mtu atoe maarifa hayo na sisi kama yapo tutayafanyia kazi.

BBC:
 Kuna njia kama umeme wa jua, umeme wa kutokea ardhini wa mvuke, kwanini serikali haitafuti njia mbadala kuzalisha umeme kwa njia hizo?

Rais Kikwete:
 Nasema hivi, hata umeme wa jua lazima ujenge, umeme wa mvuke lazima ujenge, si kitu cha mwezi mmoja. Nasema huo ndio ukweli wenyewe nawakati mwingine na nyinyi mjifunze hayo mambo ya kitaalamu kulikoni kuuliza tu hivi hivi. Unajua ungekuwa na wewe unauliza kwa hoja - “unajua kwamba hiki kitu hiki ingekuwa umeme wa jua miezi miwili tu upo” - tungeweza kufanya hivyo.

Sisi sasa hivi kwa mfano tunajiandaa kuzalisha umeme wa kutumia Upepo, pale Singida. Tuna mwaka wa tatu sasa tuna mipango na Wakorea wa Kusini, umeme haujakuwepo. Kwa hiyo nasema hayo ni maelezo rahisi.
 Wanasema “mbona jua lipo?” katengeneze umeme wa jua kama jua lipo! (kicheko). 

BBC:
 Watanzania wamekuwa wakisema (mwisho kabisa) kwamba Tanesco ingebinafsishwa ili waweze kupata makampuni kufanya kazi hiyo ya umeme?

Rais Kikwete:
 Aah! Kwani ukitaifisha kesho ndio utapata mitambo kesho? Nasema hivi ni vizuri kuelewa tu - kwanza tatizo la msingi - ni maji kukauka kwenye mabwawa. Maji yasingekauka kwenye mabwawa tatizo hili halipo. Maji yamekauka kwenye mabwawa kwa sababu ya ukame. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia ukame usiwepo. Sasa hiki ndicho kiini cha tatizo. Sasa nasema sisi jitihada ambayo tumeifanya ni kupunguza sasa kutegemea umeme unaotakana na nguvu ya maji. 

Toka mwaka 2009 tumewekeza adi Disemba 2011 tutakuwa tumeongeza MW 310, yenyewe hiyo ni hitihada kubwa, ni vizuri ukaitambua jitihada hiyo. Kulikoni kusema kitu tu nasema hatakam huna majawabu rahisi utuambie tu.
 

MWISHO.

6 comments:

  1. Hatuna Rais hapa.

    ReplyDelete
  2. Hatuna Viongozi!!!!

    ReplyDelete
  3. Waziri wa Nishati na Madini AJIUZULU HARAKA SANA! Na huyo Mr Jairo AJIUZULU HARAKA! Kwanini wangojee mpaka Raise aje? WAJIUZULU! Tuache kuendesha nchi Kiushkaji!

    ReplyDelete
  4. Wasi wasi wangu ni kuhusu nani Bora zaidi ya mwenzake katika ya Waziri wa Nishati na Aliyemteua????

    ReplyDelete