Labda hata 'wenzetu' wanamuona ni Mwanafunzi Zaidi |
(Discalimer: Uandishi wa Makala Hii haukulenga kwa namna yoyote kuvunja sheria au katiba ya Nchi au chombo kingine chochote halali nchini. Kama mojawapo ya hayo limetokea, sio kwa makusudi, na linaombewa msamaha tangu mwanzo).
Wakati nilipoenda field nikiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, nilipokelewa na Bw. Andrew Mushi katika Shirika la TANGO (Tanzania Association of NGOs) (kwa sasa ni mwanabidii pia). Ukweli ni kwamba siku za mwanzo za kuwepo kwangu zilikuwa ngumu kidogo, kutokana na ukweli kwamba nilikuwa sijawahi kuwa na uzoefu wowote wa kufanya kazi katika ofisi.
Moja ya changamoto ambazo nilikabiliana nazo ilikuwa ni kutokuelewa kitu chochote ambacho nilitakiwa kukifanya au kile ambacho kila mtu ofisini alitarajia nikifanye katika nafasi niliyokuwa nayo. Kutokujua huko kulinifanya nitumie muda mwingi kujisomea vitabu, taarifa na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kujiongezea ufahamu – hata wakati nilipokuwa natakiwa katika kutekeleza majukumu yangu kwa vitendo, nilijikuta nikitumia muda mwingi kusoma!
Hali hii iliendelea hadi siku Ndg. Mushi alipoiniambia: “We umekuja hapa Kusoma au Kufanya Kazi? Kama bado hujajua cha kufanya rudi shule ukasome, ukishajua unachotakiwa kukifanya ndipo uje ufanye kazi!” Maneno yale yalikuwa mazito sana kwangu, na sijayasahau na sitayasahau katika muda wote nifanyapo kazi!
Hivi karibuni, katika kufuatilia matangazo ya TBC1, nilikutana na kipindi cha “Makala yangu”. Katika makala ile, mtangazaji alikuwa akielezea taarifa mbalimbali kuhusiana na safari ya Rais Jakaya Kikwete kwenye nchi moja ya visiwani, hapa hapa Afrika. Moja ya mambo niliyoya-note yaliyokuwa yakijitokeza mara nyingi katika majibu aliyokuwa akiyatoa Kikwete kwenye mahojiano aliyoyafanya, alikuwa akisisitiza muda wote kwamba amejifunza mambo mengi, na atawatuma wataalam wa kitanzania kwenda kujifunza zaidi huko!
Nimejifunza… Nimejifunza… nimejifunza… Yalikuwa ni maneno yaliyokuwa yanajirudia mara nyingi sana, yakiambatana na msisitizo wa kutumwa kwa wataalam wa kitanzania kwenda “kujifunza”… Nikayakumbuka tena maneno ya ndugu Mushi wa TANGO, “kama bado unataka kujifunza Rudi Shule, ukishaelewa cha kufanya, Njoo Ufanye kazi”.
Nikajiuliza, hivi kwa taifa lililobado nyuma sana kimaendeleo kama Tanzania, linahitaji kuwa na Rais “anayejifunza” au anyefanya kazi? Je, taifa kama hili linahitaji kuwa na wataalamu wanazunguka duniani “kujifunza” au ni kuwa na wataalam wanaofanya kazi?
Hapa akiwa anaendelea "kujifunza" kwa kusoma kitabu, huku kushoto kwake Waziri wa Nishati Ngeleja akiwa ANACHAPA LEPE LA USINGIZI! |
Hoja yangu inatokana na ukweli kwamba Tanzania ni mojawapo ya mataifa duniani ambayo yanasifiwa kwa kuwa na sera, sheria na mipango mingi mizuri sana – ikilinganishwa na mataifa mengi sana ya kiafrika na hata duniani kwa ujumla miongoni mwa nchi maskini na zinazoendela. Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika masuala mengi ya kisera na mipango hata na kuyapita baadhi ya mataifa yaliyoendelea kuliko Tanzania. Mipango kama Dira ya 2025, MKUKUTA, MKURABITA, Programu za Maboresho za Kisekta kama ASDP, LSRP, WSDP, ESDP n.k. ni moja ya mipango bora kabisa kuwahi kupatikana katika mataifa maskini.
Pamoja na mipango hiyo mizuri na sera, bado taifa letu ni moja ya mataifa yenye raia maskini kabisa duniani! Changamoto kubwa ambayo, pamoja na mambo mengine, imechangia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha huu umaskini hapa nchini, ni taifa kutokuwa na watu wanaoweza kusimamia utekelezaji wa sera na mipango na kuhakikisha kuwa matokeo na shabaha zote za malengo na mipango hiyo vinafikiwa.
Taifa kama hili, katika hali hii tuliyonayo, linahitaji kwa kiasi kikubwa sana kuwa na watu wenye uwezo wa kiufundi na kiutaalam wa kuweza kuliongoza taifa katika utekelezaji wa mipango na sera iliyopo. SIO WATU WANAOSHIKA MADARAKA ILI WAJIFUNZE! Uzuri wa sera, mipango na programu za taifa hautakuwa na manufaa yoyote kwa taifa na raia wake ikiwa haitatekelezwa. Mipango yetu mizuri haitatekelezwa na WANAFUNZI bali WATENDAJI!
Swali la msingi la kujiuliza kwa hapa Tanzania ni Je, taifa hili linaowataalam wanaoweza kuliongoza taifa kwenye kutekeleza mipango iliyopo, au wataalam tulionao bado ni wale wanaohitaji kukaa na kusoma vitabu maofisini au kwa kufanya ziara za kujifunza? Je, wataalam walio kwenye nafasi mbali mbali za utendaji hapa nchini, kama Rais, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi n.k. ni watu wenye uwezo wa kutenda kile wanachotakiwa kukitenda au ni watu ambao hawana hata uwezo wa kufanya hayo madogo yanayotakiwa kulitoa taifa “maskini” kama Tanzania hapa lilipo na kulipeleka hatua nyingine?
Makusudi ya tafakari yangu hii ya leo SIO kueleza kwamba mtu akishakuwa na nafasi ya uongozi/utendaji hatakiwi kuhitaji kujifunza, HAPANA. Ninachopenda kieleweke hapa ni kwamba kila mtu anayepewa nafasi fulani ya uongozi/utendaji anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya kazi za msingi katika nafsi hiyo.
Hutomlaumu kwa kutozunguka duniani na kukutana na watu tofauti (wengine sijui hata kama wana TIJA kwa taifa letu)! |
Kwa mfano, mtu anapoajiriwa kuwa mhasibu, hatutarajii kwamba baada ya kusaini mkataba, mhasibu huyu aombe kwenda kozi ya book-keeping au basic accounting! Hatutarajii kwamba mtu akiajiriwa kuwa CEO wa kampuni ya ndege, baada ya kusaini mkataba wa kazi aanze kuzunguka duniani kufanya “study-tour” ya namna ya kuendesha kampuni ya ndege!
Tunatarajia kwamba mtu anapopewa nafasi kama hiyo, hususan ya juu ya utendaji, mtu awe tayari na uelewa wa kitu gani anapaswa kukifanya katika nafasi hiyo. Tunatarajia kuwa hadi mtu anapopewa nafasi ya juu ya uongozi (kama ya kisiasa) au utendaji tayari, awe na dira na uelewa wa kile anachotakiwa au kutarajiwa kukifanya.
Ziara za “kujifunza” zinatarajiwa zianze baada ya mtu kutekeleza yale masuala ya msingi aliyopaswa kuyatimiza katika nafasi yake. Ziara za kujifunza hazipaswi kuwa suala la kuanza nalo kazini, au kufanywa kama sehemu ya kazi alizoajiriwa kuzifanya mtu. Mtu asifanye ziara “za kujifunza” kama sehemu ya ajira yake, bali liwe ni suala litakalojitokeza mara moja au mbili na hiyo iwe ni baada ya taathimini ya muda mrefu ya kubaini uhitaji wa hizo “ziara”.
Miaka SITA ya Kikwete kuwepo Madarakani bado taifa linakabiliwa na changamoto nyingi sana. Katika changamoto hizi, nyingi ni ndogondogo, ila zinapokuwa nyingi mno, zinafika mahali zinaonekana kuwa kubwa sana. Ufisadi, matumizi mabaya ya mali ya umma, kutokuwajibika kwa watumishi wa umma na serikali kwa umma, kutokuwajibika kwenye matumizi ya fedha na mali za umma, huduma mbovu za umma, Mgao wa Umeme tangu aingie madarakani hadi leo, njaa katika baadhi ya sehemu za nchi wakati vyakula vikiharibika sehemu nyingine n.k. Kero hizi zimeendelea kudumu hapa nchini na zimetoka katika hatua mbaya (bad) kuwa mbaya zaidi (worse) kila siku, kila mwezi na kila mwaka.
Lakini, tangu mwanzoni kabisa mwa utawala wa Kikwete, ZIARA zimekuwa nyingi utadhani ni sehemu ya majukumu yake ya kila siku. Sina uhakika ni kwa kiasi gani hizo ziara zina tija au zinalenga kwa vitendo kumaliza hizi kero za watanzania. Ni kwa kiasi gani ziara hizi zinaongeza matumizi bora ya fedha za umma, ni kwa kiasi gani ziara hizi zimesaidia kupunguza au kudhibiti ufisadi, kumaliza mgao wa umeme n.k.? Je ziara za Kikwete “kujifunza“ zimepunguza ufisadi nchini? Zimemaliza mgao wa umeme? Zimemaliza ufujaji wa mali ya umma kwenye wizara, Idara na Serikali za Mitaa? Zimeongeza uwajibikaji serikalini? n.k. Kuna wengine watadai kwamba safari hizo zimeongeza misaada (kama ambavyo Kikwete mwenyewe hudai), lakini TAIFA HILI HALIHITAJI MISAADA!
Zaidi ya hapo, iwapo kuna huo ulazima wa hizo ziara, basi nadhani kuna haja ya taifa kujiridhisha kwamba ni kweli RAIS WETU HAJUI JAMBO HILI NA HILI NA HIVYO TUMTUME AKAJIFUNZE MALAWI, BURUNDI AU KWINGINEKO. Ni muhimu tukajiridhisha kama taifa kwamba Rais wetu hajui abcd na taifa letu tunahitaji abcd, hivyo tukubaliane kumtuma akajifunze! Isije ikawa anasema kwenda kujifunza, aidha mambo ambayo taifa haliyahitaji au kumbe ni mambo ambayo tayari alikuwa anayafahamu! Au labda, TAIFA TUELEWE KWAMBA TUNA RAIS AMBAYE HAELEWI MAJUKUMU YAKE ALIYOOMBA NA KUAHIDI KUYAFANYA HIVYO TUMLIPIE ADA AU GHARAMA YA KWENDA KUJIFUNZA au TUAMUE VINGINEVYO!
Sijui kama kweli ndio maneno aliyokuwa anayatamka, lakini pozi linaonesha alikuwa haelewi vizuri kinachosemwa! |
Ukweli unabaki kuwa ‘mafunzo kazini’ ni sehemu ya muhimu katika kuboresha uwezo wa mtu kutekeleza majukumu yake. Lakini mafunzo kazini hayapaswi kuwa ndiyo kazi kuu ya mfanyakazi! Inapaswa kufanyika pale tu taathimini inapoonesha kuwa na haja ya hayo mafunzo, na pia kuwe na makubaliano ya uelewa gani ambao mtendaji anahitaji kuupata kwa kwenda kujifunza kwa wengine. Kwa kuwa safari za nje ya nchi huwa zinaambatana na posho nyingi na zilizonona, isijekuwa safari hizo ni njia zak ujipatia posho nyingi halali kwa kisingizio cha kwenda kujifunza!
Mwisho: Hutomlaum kwa kutokucheka hata pale alipotakiwa kuwa serious! |
Na hii ndiyo tafakari yangu ya leo!
Wasaalam, mwana wenyu
…mussa
No comments:
Post a Comment