Monday, October 31, 2011

LEMA (Mb) Aenda Jela, Aacha barua kwa Watanzania!

Godbless Lema akiwahutubia Wananchi


WARAKA WA GODBLESS LEMA KWA WANA WAARUSHA NA WATANZANIA WAPENDA MABADILIKO KOKOTE KULE WALIPO ULIMWENGUNI

JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.

Wapendwa wapiga kura wangu na Watanzania wenzangu.

Sina wakati mgumu kuchukua maamuzi haya yanayotokea leo. Upendo huu nilio nao kwa watu wa Arusha na nchi yangu ni sababu ya msingi ya maamuzi haya. Nimetishwa mara nyingi, rafiki zangu wametishwa, jamii ya watu duni imeendelea kuishi kwa mashaka na matisho kwa muda mrefu.

Katika mazingira haya, nikawaza sana kuwa anatakiwa kutokea mtu mmoja jasiri atakayeweza kuona thamani ya watu wengine. Huyo mtu anaweza kuwa wewe lakini kwa wakati huu siwezi kumsubiri tena na nimechagua kuwa mimi nikiamini kuwa utanikuta nikiendelea na safari ya ukombozi. 

Tupo wengi sana tunaotaka mabadiliko, haki na ukweli. Hata hivyo hofu, woga na mashaka yamepoteza thamani yetu yote ya maana ya kuishi.

Waliofungwa kwa kuonewa na kuteswa, waliokosa chakula na kulala nje, waliokwenda hospitali na kukosa madawa, waliokosa ajira na kipato mpaka kujikuta wametoroka familia zao, waliopoteza matumaini ya maisha, waliopora utajiri wa nchi yetu kwa manufaa yao binafsi, walionunua haki na sheria dhidi ya wajane na wanyonge na kuwapora vipato vyao vidogo na mashamba yao, USIULIZE SABABU NINI!

Nimetafakari sana na nikatambua kuwa sababu ni mimi pale nilipokuwa kimya wakati wajane na wanyonge wanaonewa.

NIliposikia wengine wanaandamana kupinga uovu, uonevu, wizi, ufisadi na ukandamizaji wa haki nikasema ni hao na wala sio mimi, kumbe nilipaswa kuwa mbele katika harakati hizi.

Nilipoona wenzangu hawawezi kupata matibabu nikasema mimi sio mgonjwa, nilipopata taarifa za rafiki zangu kufungwa kwa makosa yasiyo yao, nilipoona watoto wa mitaani wanaomba chakula, nilipoona wazee wamepoteza matumaini ya kuishi katika uzee wao, nilipoona vijana hawana ajira, nilipoona mabinti wasichana wadogo wameamua kufanya biashara ya ukahaba, NIKATAFAKARI,TENA NIKATAFAKARI, dhahabu zetu, almasi yetu, Milima na mabonde yetu, Tanzaninte yetu, samaki wetu, Uranium yetu, makaa ya mawe yetu, utalii wetu, ardhi na kilimo chetu na zaidi utu na mahusiano yetu.

Na sasa siwezi kukaa kimya tena. NI afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu. Na katika msingi huu hofu na mashaka vimekosa thamani kwangu, sitamwogopa mtu yoyote, mwenye silaha yoyote, mwenye cheo chochote na wala sitaogopa jela yoyote katika kupigania haki, utu wa kweli katika jamii yangu. 

Wanafikiri wataendelea kutuogopesha kwa sababu wana jela na silaha, wanafikiri tutaendelea kuabudu uoga, wanafikiri wataendela kutunyanyasabila sababu ya msingi LAKINI SISI TUNAJUA TUTASHINDA KWA SABABU HAKI TUNAYOIPIGANIA NI MAKUSUDI YA MWENYEZI MUNGU.

Leo nitakwenda jela kwa hiari yangu binafsi kwa siku kadhaa na si kwa NIA YA KUJITAFUTIA UTUKUFU WANGU bali ,” JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.

Kila mara nilipotishiwa nikagundua wanaonitishia, wananitishia kwa jela na mauti. Na mimi nikagundua na nikatambua ni afadhali kuishi miaka hamsini jela huku sababu ikiwa ni kupinga uonevu na ukandamizaji kuliko maisha ya woga na anasa yasiyo na kusudi katika kutetea utu na heshima ya mwanadamu mwenzangu.

Wale mlionitishia kunipeleka jela sasa nimetangulia kwa hiari yangu na wale mliobaki msiogope jela endeleeni kupigania ukombozi utakaoleta usawa katika nchi yenu. 

Watakaotubeza na kututukana wasameheni kwani wanahitaji ukombozi wa fikra, watakaotupongeza na kutuonea huruma wafundisheni ujasiri na waambieni mapambano bado yanaendelea tunahitaji umoja wao. Nitarudi mapema. MSIOGOPE, MSIOGOPE, MSIOGOPE , MUNGU YUPO UPANDE WETU.

Mhe Godbless Lema (MB) – Arusha Mjini 31 Oktoba 2011.

Taarifa BINAFSI YA ZITTO KABWE Kuhusiana na Afya yake INDIA!

Zitto Zuberi Kabwe

Ndugu zangu,

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha muda huu kuwa na nguvu za kukaa katika kiti na kuweza kuandika haya machache kwenu. Nawashukuru sana Wanamabadiliko kwa salaam zenu nyingi za pole mara mliposikia ninaumwa na kulazwa hospitalini. Najua hamkuwa na taarifa kamili za kuumwa kwangu na kwa kweli suala la kuumwa ni suala la mtu binafsi (hata kwa mtu mwenye dhamana ya kiuongozi wa umma japo umma nao una haki ya kujua kinachomsibu kiongozi husika).

Mwanzo
Nilianza kupatwa na maumivu ya kichwa usiku wa siku ya Ijumaa tarehe 20 jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kutoka Jimboni tayari kwa kazi za Kamati za Bunge ambapo Kamati yangu ilikuwa imekwishaanza kazi wiki hiyo kwa kupitia mahesabu na utendaji wa Mamlaka za Maji nchini.

Kama kawaida yangu niliona maumivu hayo makali kama ni sehemu tu ya uchovu wa ziara za Jimboni na safari za mara kwa mara nilizofanya kuinigilia ziara za Jimboni ikiwemo kuhudhuria Mdahalo wa Umeme na Mkutano wa Uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika. 

Hivyo nililala na nilipoamka kichwa kilikuwa kimepona na hivyo nikahudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma katika Ofisi ya Bunge mpaka saa saba mchana.

Siku ya Jumapili saa kumi na moja jioni nikiwa katika Hoteli ya Southernsun nilipatwa na homa kali ghafla. Nilikatisha mkutano niliokuwa nao na kuamua kurejea nyumbani, lakini nilishindwa kuendesha gari na hivyo kumwomba Dereva wa Mhe. Mhonga anifuate ili anisadie kunifikisha nyumbani.

Nilipofika nyumbani kwangu Tabata, homa ilizidi kupanda na hivyo kuamua kwenda Hospitali mara moja. Nikapelekwa Agakhan Hospital na nikapata huduma.

Nilipochukuliwa vipimo ilionekana sina malaria wala homa ya matumbo na pia hawakuweza kuona sababu ya homa ile namna ile (maana ilifikia degree 40).

Walituliza homa, nikapewa Panadol na baadaye nikaruhusiwa kurudi nyumbani mnamo saa tano usiku. Nilipoamka siku ya Jumatatu nikaenda kazini kuongoza Kikao cha Kamati ya Bunge ambapo tulikuwa tunashughulikia Hesabu za Bodi ya Utalii na Benki ya Posta Tanzania.

Nilipita Agakhan kupata majibu ya ziada na kuambiwa nipo sawa ila nipumzike nisifanye kazi kwa siku kadhaa na nitakuwa sawa.

Hali kubadilika
Siku ya Jumanne niliamka nikiwa salama, kichwa kikiuma kwa mbali lakini sio vya kutisha. Nikawajulisha wajumbe wenzangu wa kamati kuwa sitakwenda kazini na wao waendelee na kazi. Hata hivyo ilipofika saa sita kamili nilianza kutetemeka mwili mzima na homa kuwa kali sana huku kichwa kikiniuma sana sana sana!

Dada zangu wakamwita Driver na kunikimbiza Hospitali ya Agakhan. Wakarejea vipimo vilevile na matokeo yakawa yaleyale. Joto lilifika degree 39.8 Hivyo wakanipa dawa za kupoza homa na maumivu ya kichwa kwa drips na sindano kadhaa.

Siku ya pili hospitalini nikafanya vipimo zaidi ikiwemo ultra sound na vyote kuonekana sina tatizo lolote. Niliendelea kuwepo Hospitali na kwa kweli hali ilikuwa inatia moyo sana kwani nilipata nguvu na hata kuweza kuzungumza, homa ilikuwa imepungua sana.

Pamoja na kwamba Mganga Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Waziri wa Masuala ya Bunge na Daktari wangu binafsi kuwataka waangalie upya vipimo vya malaria, madaktari wa Agakhan waliwahakikishia viongozi hawa na Daktari wangu kwamba hawajaona Malaria na hivyo wanaendelea na uchunguzi wa ‘a trigger’ ya homa kali niliyokuwa napata.

Hali kuwa Mbaya
Usiku wa siku ya Jumatano Hali ilikuwa mbaya sana. Joto lilipanda tena kufikia 40 na kichwa kuuma zaidi. Nilikuwa kama ninatwangwa kwenye kinu kwa kweli. Nilikuwa natetemeka sana. Ilikuwa taharuki kubwa sana katika chumba nilicholazwa.

Wageni waliokuwa wamekuja kunijulia hali wakati hali inabadilika ilikuwa ni pamoja na Ndugu Murtaza Mangungu na Mohamad Chombo ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya POAC, walishauri mara moja nihamishwe Hospitali kupelekwa Muhimbili.

Muda si mrefu kupita Waziri Lukuvi na Katibu wa Bunge walifika, wakaafiki na nikahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwa hali niliyokuwa nayo nikalazwa katika Chumba wanachokiita Mini-ICU. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mama Blandina Nyoni alikuwepo Hospitalini tayari.

Usiku huo huo nilifanyiwa vipimo upya. Full Blood picture pamoja na BS. Vile vile kufuatia malalamiko kuhusu maumivu ya kichwa ikaamuliwa kuwa nifanyiwe CT Scan usiku ule. Ikaonekana nina wadudu wa Malaria 150 na mara moja nikaanza matibabu. Namshukuru sana Daktari kijana Dkt. Juma Mfinanga kwa umahiri mkubwa aliouonyesha tangu nilipofika pale Mini ICU.

Asubuhi ya siku ya pili nikapata majibu ya tatizo la maumivu ya kichwa. Nimekuwa nasumbuliwa na kichwa kwa miaka zaidi ya Kumi sasa na katika kipindi hicho mara nne nilipoteza fahamu na kuanguka (Mara ya kwanza mwaka 2000 nikiwa Jijini Mwanza nikielekea kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum, Mara Pili Mjini Dodoma katika mkutano kama huo mwaka 2001 lakini ilikuwa usiku, Mara ya tatu Nikiwa chumbani, Hall II mara baada ya kutoka *Prep, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2002 na mara ya Nne Bungeni siku ya kupitisha Muswada wa Madini 2010 kufuatia wiki nzima ya Kamati na Mjadala wa Bunge (Ndugu Katulanda anakumbuka siku hii kwani yeye ndiye niliyemkamata njiani kunikimbiza Zahanati ya Bunge).

Tatizo lililogundulika ni SINUSITIS, ambayo tayari imekuwa sugu. Daktari Bingwa wa magonjwa haya Dkt. Kimaryo akanieleza kwa kirefu juu ya tatizo hili na kuniambia suluhisho ni ‘surgery’ na pale Hospitali ya Taifa hawafanyi hiyo operesheni. Akashauri niletwe India ambapo kuna Daktari mpasuaji wa ugonjwa huu. Nikakubali.

Baada ya kuwa Malaria imedhibitiwa kwa kufikia nusu ya ‘dozi’ nilopewa na wadudu kuonekana kutokomea, Ofisi ya Bunge ikaandaa safari. Nimefika India. Nimebakiza sindano mbili ili kumaliza ‘dozi’ hiyo na tayari nimefanyiwa taratibu zote kwa ajili ya ‘surgery’ hiyo.

Sijafa
Uvumi ulienezwa nimekufa. Kwa kupitia kwenu ndugu zangu Wanamabadiliko, napenda Watanzania wenzangu wajue mimi ni mzima wa Afya. Nimepata maradhi kama Binadamu mwingine yeyote anavyoweza kupata na namshukuru Mungu kwamba ninapata matibabu mazuri kabisa.

Shukran
Nawashukuru sana Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili chini ya Prof, Mwafongo kwa juhudi kubwa walioonyesha katika kunihudumia. Naishukuru Ofisi ya Bunge kwa Kutimiza wajibu wao kwangu kama Mbunge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwa kuonyesha upendo wa hali ya juu na watumishi wote wa Wizara ya Afya, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Slaa kwa ufuatiliaji wa karibu wa Afya ya Naibu wake, Wabunge wajumbe wa Kamati ya POAC, Dkt. Alex Kitumo, ndugu, jamaa na marafiki zangu wote.
Nawapa pole wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa uvumilivu mkubwa hasa kufuatia uvumi mbalimbali ulioenezwa, pia Watanzania wengine kwa uzito huo huo.

Nitawajulisha kwa lolote Mungu akipenda. Ninaendelea na matibabu na hali yangu ni nzuri

Ndugu yenu

Zitto
source: https://zittokabwe.wordpress.com/2011/10/31/statement-hali-yangu-ya-afya/

GADAFFI: MAKOSA na UJINGA Uliomponza!!

GADAFFI: Aliachukuliwa na Wengi kama MKOMBOZI -
Alichukuliwa na Wengi kama MUUAJI! -
Na Labda - ALIKUWA HAYO YOTE!
Kanali Mouammar Gadaffi hatimaye ametutoka, siku chache tu baada ya ambayo yangekuwa maadhimisho ya miaka 42 ya Utawala wake. Gadaffi alifanikiwa kuwa mtu aliyegawanya fikra za watu wengi sana – hususan waafrika – kuhusu wema au ubaya wake.

Waafrika wengi wanapendelea kumuona shujaa kwa jinsi alivyowahi kuwa mstari wa mbele katika kupambana na wazungu kwa maneno na wakati mwingine kwa matendo kuliko viongozi wengi wa kiafrika walivyoweza kufanya. Baadhi walimuona na wanaendelea kumuona kuwa alikuwa ni mtu muovu sana, katili, dikteta… asiyefaa kuigwa kwa namna yoyote.

Kwa ufupi, kuna mambo mengi yamuhusuyo Gadaffi ambayo yaliwagawa waafrika kimtazamo na yataendelea kuwagawa kwa muda mrefu ujao. Tafakari yangu ya leo haitayachunguza maeneo hayo yote kwa undani wake, ila itajikita katika eneo moja tu – baadhi ya “makosa” aliyoyafanya Gadaffi – labda kwa kujua au kwa kutokujua – ya kisiasa, kijamii, kiuongozi au labda hata kiufundi – ambayo yalichangia katika kumuangusha.

Gadaffi, aliyeingia madarakani mwaka 1969 kwa mapinduzi ya kijeshi – baada ya kuongoza kikundi cha vijana wenzake wanajeshi kumpindua mfalme wa Libya wakati huo – anakumbukwa na kusifiwa na Waafrika wengi – HUSUSAN WANAOISHI KATIKA NCHI MASKINI kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na haya yafuatayo (Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Mtandaoni):-

-          Umeme kwa Raia wote wa Libya – hakuna kulipia “bill” za umeme
-          Hakuna Riba kwenye mikopo – mikopo yote ya benki hutolewa bila kutoza Riba
-          Nyumba/makazi yalichukuliwa kuwa ni haki ya binadamu Libya
-          Maharusi wapya walikuwa wanapewa Dola 50,000.00 (kama Milioni 80 za Kitanzania) kwa ajili ya kuanzia maisha
-          Elimu na Afya ni huduma za Bure Libya
-          Walibya waliotaka kuwa wakulima walikuwa wanapewa Mashamba, Nyumba na mitaji
-          Walibya waliohitaji matibabu nje ya Libya walilipiwa gharama zote na Serikali
-          Raia akinunua gari Serikali humpatia ruzuku ya 50% ya bei ya gari…. N.k. n.k.

Ni wazi kabisa kwamba huduma hizi ni nyingi mno, nzuri mno na kwa mtu yeyote – hususan katika nchi maskini – zinatosha sana kumfanya raia wan chi yoyote kutulia, kumpenda, kumheshimu na hata kuwa tayari kumlinda na kumtetea rais wake kwa gharama yoyote – Libya ilikuwa Kinyume kwa Gadaffi!!!
Gadaffi alikosea Wapi?

Baadhi ya mambo ambayo labda gadaffi hakuyajua au labda aliyapuuza, na ambayo yalichangia sana katika kumuangusha ndani ya muda mfupi, kama kiongozi, mtawala na mwanasiasa ni pamoja na haya yafuatayo:-

1.      Siasa ni Watu SIO Vitu!
Kosa kubwa la kwanza ambalo Gadaffi alilifanya ilikuwa ni kudhani kuwa VITU vinaweza kufanikisha Siasa na Uongozi wake. Siasa huwa ni mchezo unaochezwa kwenye uwanja ambao ni Umma. Ukiweza kuupata Umma ukuunge mkono ni njia kubwa zaidi ya mafanikio kisiasa kuliko kuwa na mali na vitu vingi kiasi chochote.

Mali na Vitu vinaweza kukuhakikishia uhai wako kisiasa na katika uongozi kwa muda mfupi sana, lakini watu wakiwa nyuma yako, upande wako, utawala wako ni wa “milele”. Gadaffi alifanya kosa la kudhani akiwapa watu vitu basi watampenda na kumuona wa maana sana, au kwamba hawatakuwa na tamaa ya madaraka na nafasi zake kisiasa – KOSA!

2.       Kuelewa Matakwa ya Watu na SIO Kupanga Matakwa ya Watu
Jambo la pili la msingi sana katika siasa, utawala au uongozi – ni muhimu sana kuelewa watu wanataka nini na sio kukaa na kukadiria na kuamua ni kitu KINAWAFAA wananchi! Kitu chochote utakachompatia mtu – hata kama ni kizuri namna gani, akiendelea kukipata kwa muda mrefu itafikia mahali atakiona cha kawaida na kisha ataanza kuwazia vile ambavyo hanavyo. Hakikisha kuwa matendo yako yote yanalenga kukidhi haja za watu na kujibu maswali yao.

Gadaffi, kwa kuelewa hali ngumu ya kimaisha inayowakabili waafrika na waarabu wengi katika nchi yao, alijua kuwa akiwapa vile vitu vinavyoliliwa na waafrika wengine katika nchi zao basi watampenda na kumuona wa maana sana – KOSA!

Utawala unaodumu na kufanikiwa SIO ule unamaliza matatizo ambayo viongozi wanadhani kuwa ndiyo yanawasumbua wananchi bali ule unaofanya yale wananchi wanayoyataka – hata kama hayamalizi shida na matatizo ya msingi. Kama kiongozi, hakikisha kwanza unashughulikia yale wanayoyataka wananchi, kisha waelimishe kuhusu hayo ambayo na wewe unadhani ni ya msingi. USI-IMPOSE WEMA WAKO JUU YA WATU – Wataukataa na kukukataa na wewe – kama Gadaffi!

3.   Kutengeneza Marafiki ni Muhimu – Hata katika Uovu 
Mafanikio ya kiuchumi aliyofanikiwa kuyaleta Gadaffi nchini kwake yyalimfanya alewe sifa na umaarufu aliokuwa anapewa na raia wake na watu wake wa karibu. Sifa hizi zilimvimbisha kichwa kiasi cha kutokuona kama alikuwa anahitaji kuwa na marafiki na mahusiano mazuri na jumuiya ya kimataifa.

Sifa zake zilimpelekea kuwatukana na kuwaona takataka viongozi wenzake wan chi za kiarabu na za Afrika – hali ilifikia hali mbaya zaidi siku alipofokeana na Mfalme wa Saudi Arabia kwenye mkutano wa Nchi za Kiarabu uliofanyika Sirte mwaka Jana 2010, siku chache kabla hajaenda kwenye Mkutano wa UN na kumtukana kila mtu aliyekuwapo – hatua hii ilikuwa mbaya.

Chuki na hasira walizokuwa nazo viongozi wengi duniani – ukianza na waarabu wenzake zilichangia sana katika kumng’oa madarakani. Azimio la kumpiga lilipitishwa bila kupingwa hata na taifa moja, huku nchi za kiarabu zikiwa za kwanza kuchangia siraha na ndege za kumpiga – achilia msaada wa wanajeshi na magari ya waasi!

Rais wa Syria, Assad, kwa mfano, ameshafanya maovu na mauaji mengi makubwa kwa raia kuliko aliyokuwa ameshayafanya Gadaffi wakati anaanza kushambuliwa na NATO, lakini Syria imepata uungaji mkono wa baadhi ya mataifa, yakiwemo ya kiarabu, Urusi na China kupinga TAMKO la Umoja wa Mataifa la Kulaani tu yale yanayofanyika – SIO AZIMIO LA KUMPIGA!
Kama Kiongozi, Ni Muhimu kuwa Mnyenyekevu,
Hususan kwa Wananchi wako.  Gadaffi alishindwa
kwa kiasi kikubwa kuonesha huo Wasifu
4.      Kujihadhari na “Maskini Jeuri”
Gadaffi alidhani kwa kuwapatia fedha watu ambao hata hawafanyi kazi ilikuwa ni kigezo cha kuwafanya wanyamaze maisha yao yote – KOSA! Gadaffi alisahau kuwa huwa kuna watu “maskini jeuri”. Watu hawa huwa wako tayari kuukata msaada wako hata kama hawana chanzo kingine cha msaada iwapo tu wataona kuna dalili za kukosewa heshima kama watu.

Kosa alilolifanya Gadaffi ilikuwa ni kutaka kuwachukulia raia wote wa Libya kama watoto wake, na kwamba yeye na wake zake na watoto wake ndio wana mamlaka ya kuamua mustakabali wa raia wa nchi nzima – as if wote ni watoto na wajukuu zake!

Kitendo cha kuwaambia wanaumme hawana haja ya kutafuta ajira kwa sababu yeye atakuwa anawapa hela ya kula wao na wake zao na watoto wao na kuwalipia kodi za nyuma n.k. kwa “Maskini Jeuri” ni kitendo cha dharau kubwa – wakati alidhani ndo kitampa Siafa – KOSA!

Kwa Ufupi, Gadaffi hakufanya makosa makubwa ya kiuchumi ambayo yalipelekea kuangushwa kwake – tatizo lilikuwa ni kushindwa kuelewa na kuzingatia masuala ya kijamii na kisaikolojia ya wanadamu. Kushindwa kuelewa ni kitu kinachomfanya ajisikie vizuri linaweza kuwa ni kosa kubwa. Gadaffi alijitahidi kuwa “busy” kuhudumia mahitaji yao ya kiuchumi lakini hakuelewa kuwa mgogoro wa kisaikolojia uliokuwa unawatesa kwa miaka mingi ungekuja kuwa bomu kubwa kwake – NA SASA NI MAREHEMU!

Hitimisho langu
Japo bado kuna mjadala mkubwa kuhusu uongozi – iwapo viongozi huzaliwa viongozi au huweza kutengenezwa (kwa maana ya kufundishwa na kusoma) – ukweli unabaki kuwa hata kama mtu amezaliwa akiwa na sifa nyingi anazodhani ni za kiuongozi – bado kuna mambo mengi sana ambayo mtu huyo atatakiwa kuyasoma, kufundishwa na kuyaelewa kabla hajaweza kuwa kiongozi bora….

Binafsi naendelea na Programu Maalum ya “Uongozi Bora Wenye Kuleta Mabadiliko” inayoendeshwa na Shirika la Maendeleo na Sera la Afrika ya Kusini na mafundisho hufanyika nchini Mauritius. Mungu akipenda ufahamu na uzoefu huo nitauingiza miongoni mwa vijana wengine hapa Tanzania kinadharia na kivitendo.

Maoni yako
Maoni yako yanakaribishwa sana kuhusiana na mjadala wa “Legacy” ya Gadaffi Afrika. Waweza kuyaandika hapo chini kwa kuobnyeza Maoni au kupitia msbillegeya@hotmail.com

Gadaffi’s Leadership Philosophy: “Give the poor Libyans everything they need and then divide them, crush whoever revolts and rule forever”

Sunday, October 30, 2011

POLISI Inatumiwa Kisiasa - Lema (Mb)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.


Nawasalimu nyote.

Nimewaita kutoa taarifa juu ya kilichotokea juzi tarehe 28/10 /2011 baada ya kuhairishwa shauri la kesi ya uchaguzi iliyoko mahakamani dhidi yangu .

Tarehe 27/10/2011 kesi hii ilihahirishwa na Judge A . Mujuluzi kwani usikilizaji wake usingewezekana kwa kuangalia idadi ya watu walivyokuwa wamejaa pale mahakamani ,maagizo yalitoka kwamba shauri litakalofuata mahakama iwe imetayarisha vipaza sauti kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Lakini kwa bahati mbaya jambo hilo halikuwezekana kabisa kwa sababu ambazo baadaye Mh. Judge alizitolea ufafanuzi mzuri na mawakil wa pande zote wakakubaliana kuendelea na shauri hilo bila vipaza sauti lakini kwa ahadi kuwa mpango huo unatekelezwa haraka na wakati mwingine wa kesi itakapokuja mahakami utaratibu huo utakuwa umekamilika.

Jambo la kushangaza siku hiyo wakati nafika mahakamani nilikuta polisi wengi sana na wamevaa nguo zinazoashiria tayari wako kwa mapambano na watu wakizuiwa kabisa kuingia mahakamani kuanzia geti kubwa na polisi walikuwa wanajaribu kuhoji kila mtu kuwa anakwenda kusikiliza shauri gani na kama mtu angejibu ni shauri la kesi ya uchaguzi basi halikuwa haruhusiwi kuingia mahakamani kuanzia geti la mwanzo wa mahakama.

Nilikata dhambi hii na uonevu huu kwa wapiga kura wangu nilimfuata OCD Bwana Zuberi Mwombeji kuongea naye juu ya jambo hili la kuzuia watu* na alikataa kabisa na kusema* “ hao watu wanaenda wapi kwani kesi inawahusu ? na yeyote atakaye vuka* hawa polisi hapa hatakuwa chambo na kuniambia kuwa hata watu wakija maelfu na maelfu mahakamani* lazima kesi hii initie kidole “ ( Zuberi) , tulibishana huku* nikijaribu kutetea utu wangu na mamlaka yangu kama Mbunge* , ikawa zogo mahakamani muda *mrefu bila mafanikio *mpaka nilipomuomba wakili wangu aingilie kati kisheria ndipo watu waliporuhusiwa kwenda kusikiliza kesi .

Baadaye baada ya kesi* nilikuta wananchi waliokuwa nje ya chumba cha mahakama *wakiwa na hasira huku wakilalamika na kwani kwa mara nyingine tena OCD Zuberi alikuwa amewaita tena wananchi PANYA na akiamuru polisi wa ngazi ya chini* kwa kusema “sogezeni hao *PANYA nyuma”

Lugha hii ni mbaya* haikubaliki hata kidogo, niliongea na wanachi na na kukemea lugha hii kwa hasira *baadaye nilielekea ofisini kwangu kwa miguu huku nikisindikizwa na polisi na watu wengi waliokuwa mahakamani *na baadhi *ya watu niliomba tukutane nao ofisini kwangu wengi wakiwa ni viongozi wa matawi na vijana naotarajia kuwa mashaidi katika kesi ya uchaguzi *, niliongea nao ofisini kwangu nikawaaga* nikaondoka* na wachache niliwaacha ofisini kwangu na Katibu wangu na baadhi ya wageni wengine, baada ya muda nilipigiwa simu kuwa polisi wameingia ofisini kwangu na kukamata watu wote , nilimpigia simu Kaimu RPC kumueleza suala hili na* yeye alisema ni bora nifike ofisini kwake tuongee jambo hili , nilipofika nilimueleza jinsi OCD anavyoendelea kufanya kazi kibabe, kwa shuruti za siasa na bila busara na kuhumiza watu bila sababu , alinisikiliza kwa muda usiopungua saa nzima na baadae nikifikiri nimeeleweka* ghafla niliwekwa chini ya ulizi na kuambiwa nitoe maelezo na kushitakiwa kwa kosa la kuongea watu nje kabisa ya viwanja* vya Mahakamani na ofisini kwangu .

Ninafahamu mipango yote ya siri na wazi iliyokusudiwa kwangu na wafuasi wangu , ndio maana sishangai kwamba vyama vingine vinaweza kufanya mikutano na maandamano bila kibali na kuchungwa na polisi na yeye OCD* na polisi walipohojiwa na waandishi wa habari juu ya jambo hilo UVCCM kufanya mkutano na maandamano bila kibali,, Polisi walisema wanataarifa na wametoa onyo kwa viongozi waliohusika.

Lakini mimi *Mbunge nimekatazwa hata kutembea kwa miguu kutoka mahakamani na ni *lazima nipande gari hata kama nataka kutembea kwa miguu na hata kuongea na Wananchi mahakamani na ofisi kwangu ni kufanya mkutano bila kibali ? Jambo hili limenisikitisha sana lakini moyo wangu huko imara kwani naamini kila matatizo yanayotokana na kupigani haki au usawa* matatizo hayo mara nyingi huwa ni mpango wa Mungu juu ya kusudi Fulani.

Kesi *ya uchaguzi bado inaendelea, nilichaguliwa kwa kupata kura zaidi ya elfu 56. Wakija takribani asilimia kumi tu ya walionichagua ni watu zaidi ya 5,600. Watu hawa wakija kusikiliza kesi na baada ya kesi* wakaamua kuondoka kwa kuelekea mjini na sehemu mbali mbali* , je kundi hili la watu wataondokaje mahakamani ili msongamano huu usiitwe maandamano ? Hatuhitaji nguvu kubwa ya jeshi la polisi kutawanya watu wanaotoka mahakamani tunahitaji ulinzi wao na busara zao ili watu wasambae kwa amani *“ kwani kusudi la mkusanyiko huu hautokani na nia mbaya bali ni kesi ya uchaguzi ambayo hauwezi kushanga kwanini kuna watu wengi mahakamani.

Matukio mengi ya uhalifu Tanzania huwa yatokei kukiwepo na msongamano *wa watu tu bali yanatokea tu pale penye dhamira ya uovu bila hata msongamano , mara nyingi tunasikia taarifa za mabenki kuibiwa , watu kuvamiwa katika nyumba zao usiku na kuchomwa visu na kuporwa mali zao mambo haya huwa yanafanyika tena msongamano wa watu ukiwa usingizini, sio kweli kuwa kila msongamano wa watu ni maandamano au ishara ya vita na uovu ndio maana sokoni na sehemu za ibada huwa hakuna polisi wanaolinda kuepusha msongamano kwani kusudi la msongamano huo unajulikana maudhui yake. Haitoshi kutembea kwa miguu idadi kubwa ya watu kuita maandamano. *Maandamo yanatafsiri pana sana.

Hakuna shaka ni siasa ambayo iko wazi juu ya kilichotokea* tahere 28/10/2011* kwani sio mara ya kwanza kutoka mahakamani kwa miguu na kuja ofisi kwangu *kwani tarehe 21/10/2011 tulitoka mahakamani kuelekea Ngarenaro kwa miguu tena kupitia* njia ya polisi , mbona siku hiyo kutembea huko hakuitwa maandamano ? ama kwa vile OCD hakuwepo ? *.

Ninatoa wito kwa serikali na viongozi wa jeshi la polisi sio afya hata kidogo mwakilishi wa wananchi *kama mimi kuwa na uhusiano mbaya na Jeshi la polisi *kwa sababu ya mtu mmoja.

Ndugu wananchi na wanahabari Wakati Fulani huko Nyuma *OCD *alituma kwa katibu wetu wa Mkoa Meseji kuwa mimi Mbunge nimeandaa mpango wa kumteka mtoto wa OCD *na kumuua , Mimi pamoja na Mkiti wetu wa Taifa Mh Mbowe *tulienda kumuona RPC* na viongozi wengine kujadili na RPC alihaidi na kuona umuhimu wa kukaa pamoja na kujaribu kutafuta uhusiano mwema na suluhu jambo ambalo halikuwezekana mpaka leo kwa sababu pengine za msingi.

Sasa najiuliza nikiwa nimevamiwa usiku au nahitaji polisi kwa msaada wowote ule , je nitakuwa na ujasiri gani wakumuita OCD kwa msaada , kwangu mimi hofu niliyonayo dhidi yake kama kiongozi wa polisi ni kubwa kuliko kukutana na majambazi usiku* , hata hivyo” LETS GO, LETS GOD”

*Lakini kutafakari kwangu historia mara kwa mara* inatia moyo kwamba hakuna harakati ambazo hazikuitwa ukorofi ,uvunjaji wa sheria , uhaini, na ukiukwaji wa taratibu , niweke wazi *kwamba nitapinga ukandamizaji wowote ule mbele ya yoyote Yule mwenye silaha yoyote ile na mwenye magereza yenye mateso makali* kuliko jehanamu bila woga , na sheria yeyote inayokiuka misingi ya *

Kwa kweli nimejiandaa hata kupokea mauti* japo najua Mungu anapenda niishi muda mrefu ili kutimiza kusudi lake ,* sitarudi nyuma *katika harakati hizi* za kupinga uonevu , dhuluma na ukandamizaji wa haki za binadamu nasubiri kwa hamu sana kuona mikakati yote iliyopangwa kinyume nami na wafuasi wote wanaopinga uonevu. Hata hivyo Nimeiandaa* familia yangu *kuwa tiyari wakati wowote kwa jambo lolote na kwa taarifa yoyote dhidi ya ukweli tunaoupigania.

Ndugu wanahabari **kila mara huwa nawaambia wananchi kuwa dhambi mbaya kuliko zote Duniani ni UOGA. Lazima watambue kuwa *wengine watateswa ,wengine watauwawa lakini wengine watafurahia haki na uhuru kamili tunaoupigania* hata kama hatutakuwepo kwa sababu tu wengine walipitia mateso mbali mbali. Mimi natambua kuwa faida ya kuishi* sio kuishi vizuri tu wewe na familia yako bali ni wewe kuwa sehemu ya mabadilikio ya watu wanaokuzunguka , katika kupigani UTU , HAKI ,* ustawi mzuri wa Jamii. Na kila mtu anayemuogopa Mwenyezi* Mungu ataishi kufanya hivyo kama* Mahatma Gadhi alivyopata kusema* “The best way to find yourself is to loose yourself in the service of others”*

Godbless Jonathan Lema (MB)

30/10/2011

Friday, October 28, 2011

DOWANS: Kamanda KOVA Anasikitisha na Anashangaza!

Kamanda Wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam
Jana jioni nikiwa katika Shughuli zangu za Kijamii nilipokea Simu kutoka kwa Mhariri wa Gzeti moja la Kila siku la Kiingereza akiniuliza nilikuwa na Mtazamo gani kuhusiana na Kauli ya Kova Kusitisha maandamano ya Kupinga kulipwa kwa DOWANS siku ya Jumamosi, nilipigwa na butwaa lakini nikamwambia tu Ampigie Simu Mwanasheria Wetu atampa maelezo kamili.


SIASA ZA DOWANS
Wakati akisoma Hukumu iliyoagiza TANESCO wailipe DOWANS, Jaji Mushi wa Mahakama Kuu alisema "Nafahamu fika kuwa kesi hii ya Dowans ina sayansi nyingi sana za kisiasa".


Ni jambo lililo wazi na linalofahamika kwamba kuna  nguvu kubwa ya kisiasa inayolizunguka suala la DOWANS, hivyo ni muhimu kuangalia na kuzingatia uwezekano wa kuwepo kwa "Siasa" katika maamuzi yoyote yanayofanywa kuhusiana na Suala hili.


"Visingizio" Vya Kova
Leo niliposoma kwenye Magazeti Kova alinukuliwa akitoa sababu kubwa ya kuzuia Maandamano hayo kuwa ni "Tishio la Mashambulizi ya Al-Shabaab".


Tuichambue Hiyo sababu
1. Kamanda Kova alipoulizwa kuhusu Mikusanyiko mingine ambayo na yenyewe inaweza ikashambuliwa na Al-Shabaab alisema ETI Al-Shabaab Wanapendelea Sehemu ambazo Zina Wanaharakati. Sipendi Kusema HUU NI UONGO lakini sidhani kama Kova mwenyewe ana uthibitisho wa kauli hii. Nitaichambua hapa Chini.


2. Pili, Alipoulizwa kuhusu Mechi ya Simba na Yanga ambayo na yenyewe itachezwa siku hiyo hiyo ambapo Yeye amekataza maandamano kwa sababu za Kiusalama akasema "Kutakuwa na Ulinzi Mkali". Suala la kujiuliza hapa, POLISI ishindwe kuhakikisha Usalama kwa waandamanaji 1,000 (Elfu Moja) POLISI hiyo hiyo ihakikishe Usalama wa watu 60,000 (Elfu Sitini) Uwanja wa Taifa?
Uwanja Wa Taifa Unachukua watu 60,000 mara 20 ya
Waandamani ambao Kova Alisema Hawataweza
kuwahakikishia Usalama!
Na zaidi ya hapo, POLISI Iko tayari kuwalinda na kuwahakikishia usalama Mashabiki wa Mechi ya Mpira wa Miguu LAKINI Polisi hao hao hawawezi kuwahakikishia usalama wananchi wanaoandamana kutimiza haki yao ya kikatiba NA KUTETEA MASLAHI YA TAIFA....


Madai ya Kova  ETI Al-Shabaab Wanapendelea Walipo Wanaharakati


Matukio ya hivi karibuni ambayo yalipelekea uwepo wa wasiwasi wa Mashambulizi ya Al-Shabaab hapa Nchini ni mashambulio ya Al-Shabaab yaliyofanywa huko Kenya. Mashambulio hayo yalikuwa kama Ifiatavyo:


Shambulio la Kwanza: Bomu la kutupwa kwa mkono lilirushwa kwenye kituo cha Matatu (Daladala) na kujeruhi watu kama 10 hivi


Shambulio la Pili: Bomu lilitupwa kwenye Night Club moja Nairobi na kuua Mtu Mmoja na Kujeruhi wengine kadhaa.


Shambulio la Tatu: Al-Shabaab walishambulia kwa maguruneti gari lililokuwa na Mitihani ya Shule na kumuua Afisa Elimu na mtu mwingine.


Kabla ya Hapo:
Kwanza, Alshabaab walimteka Nyara mwanamke mmoja Mtalii pwani ya Kenya na kumuua mumewe kwa kumpiga Risasi


Pili: Waliteka wafanyakazi wa Shirika la Medicins Sans Frontier (madaktari wasio na Mipaka) huko Kasikazini mwa Kenya na Kutokomea nao Somalia (Tukio hili lilifuatiwa na jeshi la Kenya Kuingia Somalia na Kuanza Vita Rasmi na Al-Shabaab)!!


MAPENGO Hotuba ya Kova!
Katika matukio hayo yote, hatuoni eneo hata moja ambapo Al-Shabaab wanawalenga wanaharakati...!!!!! Maelezo ya Kova yametokana na MSINGI UPI????? Wanaharakati wapi waliowahi kushambuliwa na Al-Shabaab??? 


Na zaidi ya hayo, KWANI ALSHABAAB WANAFUNGAMANO NA DOWANS hadi wawakasirikie Wanaoipinga DOWANS????


Tafakari yangu hadi hapo ilinirudisha nyuma kwenye Maneno ya Jaji Mushi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam: "Nafahamu fika kuwa kesi hii ya Dowans ina sayansi nyingi sana za kisiasa"....


Hoja za Kova nimezitafakari na kweli, kwa kiasi kikubwa sana ZINAPWAYA. Ni nyepesi mno kuweza kutolewa kama kisingizio cha kuzuia Maandamano ya Kudai haki na kutetea Raia wa Tanzania na mali zao!


Kama hoja na Sababu ni hizo tu, basi Kova amenisikitisha sana, maana sikutarajia kama Mtu mwenye nafasi ya juu kama yake kutoa hoja nyepesi kiasi hicho kupinga jambo zito kiasi hicho --- Lakini, Iwapo kuna sababu za kisiasa ambazo hakuzitaja - basi namuelewa!


Nina Imani siku moja Tanzania tunayoitaka Itapatikana, lakini kuna dalili za Wazi kwamba Bado Safari ni Ndefu na Ina mashimo na Miiba Mingi...


Wasaalam, ...//msb

Wednesday, October 26, 2011

MAANDAMANO Kupinga Serikali/DOWANS Jumamosi Hii!

Ndugu wananchi, wanaharakati, wanahabari na watu wote wenye Mapenzi mema na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Napenda kutumia nafasi hii kuwatangazia kuwa kutakuwa na Maandamano ya Kuelezea hisia, maoni na matakwa yetu SISI WANANCHI KUPINGA Kulipwa kwa Dowans. Maandamano hayo yatafanyika Siku ya JUMAMOSI HII, Tar 29 Oktoba 2011 kuanzia Saa 2:30 (Mbili na Nusu Asubuhi).


Maandamano hayo yataanzia UBUNGO mbele ya Jengo la TANESCO na kuishia Jangwani.


Malengo makuu ya Maandamano hayo ni:


1. Kupinga Serikali kuilipa kampuni tata ya DOWANS  - iliyorithi mkataba wa KAMPUNI HEWA YA RICHMOND kwa kutumia fedha za Umma/Walipa Kodi.


2. Kuitaka Serikali Kutekeleza Mapendekezo 23 ya Kamati ya Bunge kuhusiana na Richmond - ambayo ni pamoja na Kuwachukulia HATUA ZA KISHERIA wale wote waliohusika katika kuingia mkataba huu na kampuni hewa na kulisababishia taifa hasara kubwa.


3. Kuitaka serikali, IWAPO ITALAZIMIKA kulipa deni la Dowans, kuwafilishi mali WOTE waliohusika katika kufanikisha Mkataba wa Richmond na hatimaye Dowans - na pesa zitakazopatikana ndizo zitumike kuwalipa DOWANS...


... pamoja na mengine yahusianayo na hali ngumu ya kimaisha inayozidi kuharibika kila siku....



Vyama Mbalimbali vilialikwa kushiriki katika Maandalizi na Maandamano yenyewe - IKIWA NI PAMOJA NA CCM....


WANANCHI WOTE MNAKARIBISHWA KUSHIRIKI MAANDAMANO HAYO YA AMANI


Kwa Taarifa zaidi Soma TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI hapa Chini


Taarifa Hii Ilisomwa mbele ya Waandishi wa Habari na Mussa Billegeya, Marcosy Albany na Harold Sungusia kwenye Ofisi ya Legala and Human Rights Center (LHRC) – LEO Jumatano tar. 26 Oktoba 2011.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
MAANDAMANO YA KUPINGA SERIKALI KUILIPA DOWANS Sh. BILIONI 111
Novemba, 2010 Mahakama ya usuluhishi ya kimataifa ilitoa tuzo dhidi ya Tanesco kuilipa Dowans shillingi billion 94. Jambo hili liliibua hisia na hasira miongoni mwa wananchi kwa kulalamika na kupinga ulipaji huo wa fedha za umma kwa kampuni tata - kutokana na taarifa za kamati teule ya Bunge.

Baada ya tuzo hiyo watu binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mawakili wa Tanesco walipinga mahakama kuu  kusajili  tuzo hiyo. October 2011 Mahakama kuu ilitoa uamuzi wa kusajili tuzo hiyo na kuamuru Tanesco ilipe shillingi billion 94 na asilimia 7.5 ya gharama hizo. Hata hivyo kabla ya usajili wa tuzo hiyo, Dowans iliuza mitambo husika kwa kampuni ya Symbion Powers kinyume cha taratibu kwa kuwa kulikuwa na amri ya mahakama ya kuacha hali ya mitambo ibaki kama ilivyo. Cha kushangaza ni jinsi ambavyo Serikali ilikuwa mstari wa mbele katika kuingia mkataba wa uzalishaji wa umeme na Symbion Powers kwa gharama ya watanzania hali ikijua mitambo hiyo iko kwenye mgogoro uliopo mahakamani.

Kwa kuzingatia haya, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Asasi kadhaa za Kiraia na Wanaharakati wa Haki za binadamu tulitoa tamko tarehe 11 Oktoba 2011 kuitaka serikali kuchukua hatua ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa bila mafanikio.

Kwa kuwa serikali imeamua kudharau maoni yetu, na kwa kuwa kuna kila dalili kwa serikali kuilipa Dowans fedha za wananchi, sisi, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, serikali wakilishi za wanafunzi na raia wa kawaida wa Dar es salaam tunaitisha maandamano kwa uratibu wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu siku ya Jumamosi tarehe 29/10/2011. Kwa hapa Dar es salaam, maandamano yataanzia Ubungo, mbele ya zilipo ofisi za Makao makuu ya TANESCO hadi Viwanja vya Jangwani kuanzia saa 2:30 asubuhi.

Maandamano haya yanalenga kuitaka serikali kufanya yafuatayo:-
  1. Kutokuilipa kabisa Dowans kwa kutumia hela za walipa kodi wa Tanzania.
  2. Itoe maelezo ya kina kwanini ilipuuza ushauri wa kisheria wa kuvunja mkataba na Richmond toka awali kwani kwa mujibu wa washauri wa kimarekani Hunton & Williams LLP wakati Tanesco inaingia mkataba na Richmond Dev’t Co. Kampuni hiyo haikuwa imeshasajiliwa achilia mbali kuwa haikuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake chini ya mkataba huo.
  3. Itekeleze kwa dhati  maazimio 23 yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya mlolongo mzima unaopelekea mpaka sasa tutakiwe kulipa bilioni 111. Kwa kufanya hili Serikali pia ituthibitishie kuwa itaacha kabisa kukikosea heshima chombo ambacho ni kisemaji na wakilishi cha wananchi kupitia wabunge.
  4. Kama sheria za kimataifa zinatubana kulipa deni hili basi malipo haya yafanyike kwa kuuza mali za wale waliotusababishia kadhia hii na kwamba malipo ya kuilipa dowans yafanyike pale tu serikali itakuwa imeshawachukulia hatua kali wahusika wa kadhia hii. Umma ni lazima ujiridhishe kwa kuona hatua hizo zinachukuliwa.
  5. Kuchukuwa hatua ya kinidhamu kwa wale wote walioshiriki katika kuingiza serikali katika mkataba huu hata mawakili waliotoa ushauri huu.
  6. Serikali ipeleke Bungeni muswada wa utaratibu mzuri na sahihi wa kushirikisha wananchi na hata wabunge katika kuingia mikataba ya kimataifa na serikali ili kuepusha hali kama hii kutokea.

Kwa hiyo tunatoa wito kwa watanzania wote tuadhimishe kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutenda yafuatayo:-
  1. Tujitokeze  kwenye  maandamano ya amani na kupinga ufisadi na malipo ya kifisadi ya Dowans siku ya Jumamosi, tarehe 29 Oktoba 2011.
  2. Kuvaa nguo za maombolezo, nyeusi, kama ishara ya maombolezo tukikumbuka msimamo wake wa kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali  za taifa,
  3. Tuzitumie siku za ibada za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zote ndani ya muda huu, kumuomba Mungu atujalie Uzalendo na Ujasiri wa kuitetea nchi yetu, kama alivyofanya  Mwalimu Nyerere,
  4. Kuwasiliana na wanaharakati nchi nzima mahali walipo, ili kupanga na kuandaa mahali pa kukutania siku ya maandamano haya ya amani.

Mwisho, tunaomba walipa kodi (wananchi) wote ambao hawajapendezwa na mlolongo huu unaopelekea ulipaji wa deni hilo la Dowans na ufisadi mwingine wote kuwa na uthubutu na kujitokeza kwa wingi kusimamia kile ambacho wanaona ni haki na stahili  ya wananchi  wote na taifa letu kwa ujumla.

Taarifa Hii Ilisomwa mbele ya Waandishi wa Habari na Mussa Billegeya, Marcosy Albany na Harold Sungusia kwenye Ofisi ya Legala and Human Rights Center (LHRC) – LEO Jumatano tar. 26 Oktoba 2011.

Tuesday, October 25, 2011

PICHA ZA GADDAFI: Uhai na Kifo Chake!

Picha Zote ni kwa hisani ya Mashirika ya Habari ya Kimataifa na Mtandao wa Intaneti.
Col. Muammar Al Qaddafi


Hapa akiwa Addis Ababa akikumbatiwa na Mmojawapo wa Marais wa Afrika

Mwishoni mwa Miaka ya '00 "aligeuka na kutubu" na kuamua kuwa "mtoto mzuri" machoni pa Wazungu

Hadi Alikuwa na Album ya Picha za Condoleeza Rice tu Ikulu...!!!!

Vuguvugu la Nchi za Kiarabu lilipoingia Libya, Taifa liligawanyika - WACHACHE wakimuunga Mkono WENGI wakimpinga


Kwa Sababu Vita kama hizi huwa sio za Siraha tu, bali na Vita ya "publicity", hadi Lugha za Kigeni zilitumika katika kuifahamisha Dunia kwamba Gadaffi ana wanaomuunga mkono 



  


Vita ilipochanganya kwa miezi kadhaa na mashambulizi ya NATO KUZIDI, mwezi wa Ogasti ilivumishwa kwamba Gadaffi ameuawa kwenye shambulio la NATO, na Picha hii feki ilisambazwa kwenye mtandao kwamba ni ya maiti yake. 

Ukweli ni kwamba picha hii SIO YA GADAFFI, ni ya kijana mmoja aliyeuawa na Wamarekani siku waliposhambulia nyumbani kwa Osama na kumuua, huko Pakistan.
Picha Ilibadilishwa Hivi
Hatimaye, mwezi Oktoba, Alhamis tarehe 20, Qaddafi akiwa ni walinzi wake walishambuliwa na ndege za NATO ambazo ziliwaua walinzi wake na yeye akafanikiwa kuponyoka na kujificha kwenye hii "karavati" kabla hajakamatwa na Askari wa NTC akiwa hai (na majeraha kidogo sana)
 Muda mfupi baadaye, taarifa na picha zilionesha kwamba amekufa - katika mazingira ya kutatanisha. Inasadikiwa kuwa aliuawa na walewale waliomkamata - jambo ambalo ni kinyume cha sheria za kivita. Hata hivyo, uwezekano wa yeye kuuliwa mara moja ulikuwa ni mkubwa sana kwa sababu alikamatwa na Vikosi vilivyotokea mjini Misrata. Misrata ni moja ya miji iliyowahi kushuhudia mauaji makubwa kabisa ya raia na wakazi chini ya Utawala wa Miaka 42 ya Qaddafi, na hususan, baada ya vuguvugu la mapinduzi kuanza. Hivyo ni wazi kuwa "alianguka" mikononi mwa mahasimu wake wakubwa. 

Maiti yake ilisafirishwa kutoka Sirte alikokamatwa na kuuliwa hadi Mjini Misrata, vilikotokea vikosi vilivyo mkamata. Huko Misrata, maiti iliwekwa kwenye Kontena la Barafu la Kutunzia Nyama ili kusaida isiharibike na likaachwa wazi kwa ajili ya maonesho ya watu kupiga picha na kushangilia....

Baadaye ilibainika kuwa kontena hilo lilikuwa halifanyi kazi ipasavyo (labda kutokana na kuachwa wazi) na hadi leo Asubuhi, Jumanne tarehe 25, mwili wa Qaddafi na mwanawe aliyeuawa siku hiyo hiyo Martassem ilikuwa imeharibika na inatoa harufu kali sana. Serikali iliamuru azikwe lakini mvutano ulikuwa ni mahali pa kuzikwa.



 Kanali Mouammar All Qaddafi, Shujaa kwa Baadhi na Muovu kwa Wengine - Utawala wake wa Miaka 42 na ndoto zake zote kuihusu Libya na Afrika Zimepotea ndani ya Miezi SITA tu!

"Innalillah wa yna Lillayih Rajiun"