Sunday, October 2, 2011

"UBIA" wa CCM NA BAKWATA Utawaumiza Waislam!

Pichani: Katibu Mkuu wa CCM Mukama alipomtembelea
Mufti Bin Simba ofisini kwake hivi karibuni.
Siasa Zetu!


Siasa za Tanzania kwa wakati fulani huonekana kuingiliwa na migawanyiko ya kidini. Wakati mwingine mtazamo kama huu huwa umejengwa kwenye hisia tu za watu lakini kuna wakati huwa kunakuwa na mambo yanayoambatana na siasa ambayo kwa namna nyingi huonesha muunganiko wa vitu hivi viwili.


Siasa na Dini
Wakati ni ukweli kwamba vyama vya siasa huhitaji kwa kiasi kikubwa kuungwa mkono na makundi ya kidini na madhehebu mbalimbali, kwa upande mwingine uhitaji wa dini kuungwa mkono na vyama vya siasa unaweza kuwa ni mdogo sana - kama upo.


Kwa maana hiyo kunabaki swali moja kubwa - Pale kunapokuwa na muunganiko, ushirikiano au ubia kati ya Chama cha Kisiasa na Dini au Madhehebu fulani - ni nani huwa anasimama kwenye upande wa Dini? Jibu la rahisi ni kwamba kwa upande wa Dini, watu binafsi wenye maslahi ya kisiasa ndio husimama na kutumia majina na migongo ya dini zao kujenga mahusiano na vyama vya siasa!


Uchaguzi wa Mwaka jana
Mufti akimkaribisha Mwenyekiti wa CCM na rais wa Tanzania
kwenye mojawapo ya matukio ya Kidini hivi Karibuni
Kampeni na matokeo ya uchaguzi mwaka jana yalionesha wazi kuwa mahusiano ya muda mrefu ya CUF na Uislamu/waislamu yalikuwa yanafifia na badala yake CCM ilikuwa inaelekea kuchukua nafasi ya CUF katika hayo mahusiano.


Sakata la DC Igunga


Hivi karibuni huko Igunga wakati wa Kampeni za Uchaguzi kujaza pengo la Rostam Aziz, kulitokea Sakata la Mkuu wa Wilaya "kudhalilishwa" na "makomando" wa CHADEMA. Sakata hili lilibadilika sura haraka sana kutoka kuwa sakata la Kisheria na Kisiasa na kuwa sakata la Kidini na Kiimani!


Muda mfupi tu baada ya hapo, kauli za BAKWATA na viongozi wengine wa kiislamu zilionekana kujikita zaidi kwenye Siasa - hususan kuipinga CHADEMA na kuitetea CCM. Msisitizo ulitolewa kwenye kupinga kitendo chenyewe ambacho kilidaiwa kufanyiwa "Mwanamke Mwislamu" ambaye kimsingi hakufanyiwa kama "Mwanamke Mwislamu" bali kama "Mkuu wa Wilaya" aliyekuwa kwenye shughuli za kisiasa!


Magazeti mengi, hususan lile la UHURU la CCM yalichapisha kauli nyingi zilizotolewa na BAKWATA na Masheikh wa Kiislam wakiishambulia CHADEMA, muhimu WAKIWATAKA WAISLAMU WASIICHAGUE CHADEMA. Wakati haya yakiendelea, msisitizo haukuwa kwenye tukio lenyewe au kuhusiana na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kidini na kiimani - Adhabu waliyoipendekeza Viongozi waislamu NI YA KISIASA - WAISLAMU KUICHUKIA CHADEMA!!!


DC Fatma Kimario SIO MWISLAMU!


Taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti moja la kila wiki siku chache baadaye zilibainisha kwamba KUMBE MWANAMKE MWENYEWE (mrs. Kimario) SIO MWISLAMU....!!!


Taarifa ya gazeti hilo ilibainisha kwamba wanamke huyo, Fatma Kimario ameolewa na Mr. Kimario ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam na kwamba Mumewe na watoto wake pia ni Wakristo! Swali la Msingi linakuja BAKWATA ILIINGIAJE KATIKA SUALA HILI????

Tafakari yangu


Tafakari yangu ya Leo inalenga kuangalia uwezekano wa madhara haya ya kulazimisha maslahi binafsi ya kisiasa yafanikishwe kwa mgongo wa dini. Fikra yangu ni kutahadharisha - aidha Waislam au BAKWATA au jamii ya kiislamu kw ujumla - kuwa makini na kujenga mahusiano au "uadui" na vyama vya kisiasa. 


Hii ni kutokana na ukweli kuwa katika siasa, hususan siasa za Tanzania, vitu kama Uongo, Utapeli, U-"Opportunist", Unafiki, Uchakachuaji, Majungu, Kuchafuana, Ufisadi, Wizi wa mali ya Umma... n.k. n.k. ni vitu vya kawaida kabisa kutokea. Hali itaanza kuwaje pale waumini, hususan wasio na mapenzi na siasa au vyama vya siasa watakapoanza kushuhudia dini au taasisi zao za kidini zikihusishwa na maovu haya ambayo hufanyika kwa jina la siasa?


Kutokana na utamaduni wa nchi kutokuunganisha imani za kisiasa na imani za kidini, mwenendo huu unaojionesha wazi katika siasa zetu ni wa hatari. Watanzania wengi wamejenga na wana imani kubwa sana kwa viongozi wao wa dini na dini zao kwa ujumla. Jaribio lolote la kutaka kuoanisha vyama na dini au taasisi za kidini ni la hatari sana kwa taifa na wananchi kwa ujumla.


Hatari Nyingine


Hatari yake kubwa nyingine ni kwamba watanzania wataacha kuangalia siasa kwa mtazamo wa sera, ilani, utendaji, na uwezo wa kiuongozi, na kuanza kuvichagua kwa kufuata fungamano lake na dini fulani fulani! 


Zaidi ya hayo, upepo wa kisiasa hubadilika, na chama kinachotawala au kuwa na nguvu leo, sio lazima kwamba kitakuwa na nguvu na ushawishi muda mfupi ujao. Katika hatua mbaya zaidi, chama cha Siasa huweza kufa au kufutwa kisheria na hivyo kisiwepo kabisa! Waislamu au Watanzania wengine wataanza na wataendelea kwa muda gani kuhama-hama na dini kufuata vyama vya siasa?


Kwa taasisi za kidini au kiimani, ambazo msingi wake ni katika kuamini uwepo wa Mungu na hatimaye kwenda katika Ufalme wake milele na milele, sidhani kama ni busara kuziunganisha na taasisi za kisiasa. Sio tu kwamba ni jambo la hatari kwa jamii - bali pia HALINA BUSARA kabisa katika Imani!


Hapo juu nimeelezea kuwa mara nyingi unapoona "ndoa" kati ya Chama cha Siasa na Dini, kwa Kawaida kwa Upande wa Dini huwa sio dini yenyewe BALI NI WATU BINAFSI NDANI YA DINI ambao huwa na maslahi binafsi ya kisiasa ambayo hupenda kuyawasilisha kwa mgongo wa Dini zao.


Usafi / Uchafu wa CCM


CCM ambayo imekuwa madarakani wakati Wizi wa EPA unafanyika Benki kuu, Wizi Unafanyika Ujenzi wa BoT, Mauaji ya Watanzania waliokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi mwaka 2001, Ununuaji wa Rada kwa njama za Wizi na Utapeli wa pesa za Umma, LEO IWE KIPENZI CHA WAISLAMU/BAKWATA! Naona hatari ya kuanza kuharibu Imani na Dini na kuzifanya ni makundi ya wanasiasa Wahalifu na Wanyang'anyi wanaojificha nyuma ya imani waliyopewa na wananchi kwa jina la dini....


Maumivu kwa Waislamu


"Ndoa" hii iwapo ni ya kweli na ikiendelea ni bayana kwamba itawaumiza Waislam wengi ambao inawezekana, ni waaminifu na wanaipenda dini yao lakini hawana upenzi wa siasa achilia mbali vyama. Wengine wanaweza kuwa ni wale wanaoupenda uislamu na siasa lakini hawana ushabiki wa vyama vya siasa au basi wanachokipenda sio kile kinachoshabikiwa na viongozi wao wa kidini.


Lakini mbaya zaidi ni pale ambapo dini yao au taasisi zao za kidini zitakapoanza kuhusishwa na maovu yanayofanywa na vyama vya siasa katika siasa zake! Haya yatakuwa ni maumivu kwa waislamu wengi ambao wasingependa dini 'yao' kuchanganywa na siasa, hususan "siasa za maji taka"...


nitarudi na taathimini ya CHADEMA na Ukristo......


wasaalm.... //mussa

1 comment:

  1. Ujinga wetu ndo hasa chanzo cha huu upuzi wa kutumiwa na viongozi walafi

    ReplyDelete