Tuesday, October 11, 2011

"CCM Inaibomoa Tanzania" Beno Malisa

HOTUBA YA BENO MALISA ALIOITOA ARUSHA 


Ndg zangu Wana Arusha,

Awali ya yote ni washukuru kwa Kujitokeza kwa Wingi katika Mkutano huu.

Pia nitumie Mkutano huu kwa niaba ya Jumuiya ya Vijana ya CCM kuwashukuru wananchi wa IGUNGA kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi, ingawa Uchaguzi ulikuwa mgumu na changamoto zake lakini tumeshinda, Ushindi si mkubwa bali tumeshinda na sasa tuna fursa ya kutekeleza ahadi tulizotoa 2010/11 ili uchaguzi wa 2015 usiwe na changamoto tulizoziona Igunga.

Natumia Jukwa hili kwa washukuru wajumbe wa Baraza kuu UVCCM walioshiriki katika Uchaguzi wa IGUNGA, Ndg Martin Shigela, Ndg January Makamba, Ndg Hussein Bashe, Ndg Magembe (Mwenyekiti Mwanza) ndugu (M/kiti Kagera) nilifanya nao kazi usiku na Mchana kuleta ushindi huo. Pia namshukuru kwa dhati Katibu Mkuu wa UVCCM ndg Martin Shigela na Ndg Julius Peter katibu wa Mkoa wa Tabora,Pamoja na Ndg Kamoga Mkiti uvccm Mkoa wa Tabora kwa kazi waliofanya wote hawa waliiwakilisha Uvccm Vyema na leo Tumeshinda.

Ndugu zangu, sasa nikiombe Chama wakati wa kuendelea kusherehekea na kujadili Uchaguzi umekwisha; tuisimamie Serikali katika Utekelezaji wa ahadi tulizotoa kwa Watanzania ili uchaguzi mkuu ujao tusiwe na kazi kubwa.

Ndugu zangu, leo Taifa linakabiliwa na changamoto kubwa na changamoto inayotukabili ni pale ambapo viongozi wanatoa kauli RAHISI katika mambo mazito ya Taifa hili, nimesoma katika mitandao kuna kiongozi mkubwa wa Chama amesema ETI TANZANIA ni ya CCM. Jamani, Tanzania ni ya watanzania wote si ya CCM peke yake; tuache kauli hizi za kejeli na kifedhuli zitavuruga umoja wetu na Mshikamano tulionao ambao umejengwa kwa misingi imara ya kuheshimiana na kushirikiana.

Tusiwagawe watu kwa ITIKADI za Vyama sote tumepanda magari kuifikia Tanzania NJEMA; ama Ni sawa na Wakulima wanaolima shamba moja ambao kila Mmoja ameshika jembe lake analoliamini nia yetu sote ni kujenga nchi hii tusiwabeze ambao si Wana CCM.

Ndg wana Arusha sasa Niongee na Nyinyi uchaguzi umekwisha Tujenge Arusha yetu na Nitumie nafasi hii kuziomba Pande Zinazosigana kumaliza mgogoro ili Manispaa itulie watu wafanye kazi siku ya Mwisho tutawaumiza wananchi kwa tofauti zetu za vyama na kugombea Madaraka. Nimesikia kuna madiwani wamefukuzwa Chadema na kuna Viongozi ambao si wana chadema wanawakingia Vifua niwaombe tusiingilie mambo ya Vyama vyao na tusitumie nafasi tulizopewa na dhamana hizi kuingilia yasiyotuhusu niwatake vijana wa CCM kisheria kata hizo zitaenda katika uchaguzi jiandaeni kugombea.

Sisi kama Chama kinachoongoza, tujitahidi kuheshimu demokrasia na maamuzi ya vyama vingine tusipende kutumia Vyombo vya serikali kuwakomoa kwani siku ya mwisho wanaoumia ni wananchi na si Vyama vya siasa.

Nitumie nafasi hii kumuomba Mbunge wa Arusha Mjini kaka yangu Lema kuwa mstari wa Mbele katika kuleta Umoja na Mshikamano hapa Mjini na kumaliza tofauti za uCCMna uCHADEMA ili wakazi wa Arusha wapate maendeleo.

Ndugu zangu vijana wa CCM, mwakani ni mwaka wa Uchaguzi jitokezeni mgombee kwani zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa nchi hii ni sisi lazima tugombee tusiwe wapiga debe tuingie katika nafasi za maamuzi ili kujadili maslahi ya vijana kwani tusiposhiriki katika maamuzi hayo maslahi yetu kama vijana yataendelea kusahaulika na sisi kuwa nyuma kimaendeleo.

Niitake serikali yetu ya CCM kutambuwa kuwa muda wa kukaa likizo hakuna lazima kufikia matarajio ya watanzania; leo Sukari bei juu, leo mafuta bei juu, leo dola inakaribia 1,700, haya yote yanaathiri maisha ya watanzania lazima tusimamie uzalishaji wa ndani na masoko ya uhakika ili kupunguza ugumu wa maisha na kupunguza kupanda kwa bei za bidhaa leo tunaagiza sukari wakati hatuna uwezo wa kudhibiti shilingi tunatarajia nini? Tunatumia Polisi kuzuia wafanyabiashara kuvusha sukari tunasahau kuwa bei ndio kikwazo serikali itengeneze mfumo wa kuvipa Viwanda vya ndani ruzuku ili bei ishuke ya sukari viwandani wafanya biashara wapate faida nzuri. Ama serikali itafute mfumo utakaodhibiti upelekeji nje sukari kutaifisha kutatuletea matatizo. Hatuwezi kudhibiti tu bila kutafuta njia ya kupungiza makali kwa wafanya biashara, Mchele leo ni 1,500, sembe 1,000 serikali itafute majawabu na si majibu rahisi juu ya haya mambo.

Ndugu zangu, CCM inapitia wakati mgumu; badala ya kuisimamia serikali tunahangaikia kutafuta wachawi na kutuhumu watu! Tuache kabisa hili jambo halikisaidii chama wala Taifa letu kumekuwa na dhana na Fikra Potofu juu ya Ushindi wetu wa 2010; matokeo yale na tuliyoyaona Igunga ni funzo kuwa watu (na hasa Vijana wengi) wameanza kutokuwa na imani na CCM kwasababu tunashindwa kuwaonyesha kuwa tuna majibu ya matatizo yao tumebaki tunaimba historia na kumtaja Baba wa Taifa na kutumia nukuu zake bila kuwapa matumaini vijana kuwa Tanzania yao itakuwa njema watapata Elimu nzuri, Afya itakuwa ya uhakika, Uchumi utakuwa imara, Ajira zitapataikana, Fursa za kujiajiri zipo, Mikopo inapatikana tusipotoa matumaini haya na kuyafikia 2015 wapiga kura milioni sita (6) wapya watatukataa uelewa wa vijana wa Kitanzania sasa umekua mkubwa wanajua haki na wajibu wao tuache kufanyia siasa maisha ya Watanzania.

CCM tunalalamika wakati sisi wenyewe tunaibomoa nchi na chama chetu. Tazama sakata la DOWANS, waliosema wao watatusaidia kupinga kulipa DOWANS na ambao walitushauri na kutumia nafasi zao tusinunue mitambo ya Dowans nao sasa wanalalamika na kuanza Kutafuta wachawi wawajibike walitudanganya kama taifa leo tumeshindwa kesi MITAMBO ileile waliyosema haifai leo inatumika na kampuni ya Symbion wanatufanya watanzania mazuzu. Walisema heri tukae gizani wakati wao wanatumia majenereta na wanalipiwa na serikali huku wakinunua aspirini kwa mamilioni leo wanajifanya wazelendo! Nilitarajia wawajibike walidanganya TAIFA serikali ikavunja Mkataba. Wakasema MITAMBO haifai mibovu leo imenunuliwa na wamarekani na wanatuuzia umeme hawa watu wanafiki wametufikisha hapa. Niwaombe UVCCM na Vijana wa Vyama vyote tuungane hawa wawajibike.

Niwaombe UVCCM wenzangu, chama hiki ni chetu sote si mali ya mtu wala watu ni mali ya wanachama tusikubali kikundi kujipa utakatifu kuwa wao ndo wema na wana uchungu hawa tuwaogope kama Ukoma. 

Kuna watu wanatumia madaraka waliyopewa wazazi wao kuivuruga JUMUIYA, niwaonye wasirudie uhuni waliotaka kuufanya hapa jana na JUZI wasirudie tutawafukuza ktk jumuiya bila kujali wao ni watoto wa nani

CCM na UVCCM ni yetu sote haina mtu anaejiona yeye ni 'Boss' sisi wengine ni watwana, nampongeza katibu mkuu kumuondoa katibu wa mjini hapa Arusha lilitokea lisirudie tena, na hii tabia ya watu kujifanya wao wanatoa maelekezo eti haya maelekezo Msisite kuhoji nani katoa maelekezo kwa maslahi yapi msitishwe vijana wenzangu msiishi kwa kutarajia madaraka ya kupewa. Wapo wengine wanapita wanakusanya CV za vijana na kuwaahidi vyeo vya U DC! Msipotoshwe na wala msifungwe Fikra kwa sababu mmepewa ahadi ya kuteuliwa U DC. Tuna bahati mbaya wapo ambao mpaka leo wanaishi kwa kusubiri U DC wamegeuka 'NDIYO mzee' na watumwa FIKRA; tuukatae utumwa huu UVCCM, tusiwe 'ndiyo mzee'. 

Nawaagiza wenyeviti na makatibu wa mikoa na wilaya zote Tanzania wafatilie katika Halamshauri zao kujua Mipango ya maendeleo inayohusu vijana na kufatilia utekelezaji wake; wakiona hakuna utekelezaji watumie kamati za siasa za wilaya kuwabana wenyeviti wa Halmshauri. Nazitaka wilaya zote zifatilie zituletee taarifa juu hili jambo. Tusikubali kuwa NDIO mzee lazima tusimamie maslahi ya Vijana.

Nitumie hapa mwisho kuwaomba Vijana wenzengu tusigawanyike kwa maslahi ya Kisiasa na Vyama mambo yanayohusu Vijana. Tuungane na hapa Arusha msikubali tena kurudia yaliyotokea Mwezi Februari kugawanywa kwa maslahi ya vyama na kuumizana, uchaguzi umekwisha tujenge Arusha yetu.

Mwisho niwape POLE nyote mliotishwa katika kutekeleza majukumu ya Chama chetu; niwape Moyo Msiogope. Tuko Pamoja, UVCCM si mali ya mtu na wala asitokee ambaye anadhani ana mamlaka! Mimi ndio KAIMU MWENYEKITI WENU hakuna mwingine. Anayetuvuruga mnamfahamu, asitulazimishe tumvunjie heshima.



KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

1 comment:

  1. huyu watambakiza kweli??? sijui! Tunakumbuka nini kilimtokea Uncle Horace, sivyo?

    ReplyDelete