Miaka 34 ya Utawala Mfulizo Tanzania |
Mimi na Siasa za Tanzania
Nimekuwa nikifuatilia kwa miaka 22 hadi sasa siasa za hapa Tanzania kwa karibu sana. Nimeshudia Tanzania ikitawaliwa na chama kimoja ambacho kilikuwa kinasimamisha wagombea wawili kwenye uchaguzi wa wabunge, hatimaye kukaja vyama vingi vya upinzani – vikavuma ghafla halafu vikapotea ghafla – na mambo mengine mengi.
Kuibuka Upya kwa Upinzani
Tangu mwaka 2005 mabadiliko yakaanza kuonekana wazi kwenye kambi ya Upinzani – hususan matumizi ya helkopta kwenye kampeni kwa upande wa CHADEMA. Matokeo ya Urais yalionesha wazi kuwa Helkopta ile ilikuwa Maarufu kuliko Mbowe kwenye zile kampeni - hilo likapita, ila “impact” yake ilibaki.
Utendaji wa Slaa
Utendaji na umahiri wa Slaa bungeni (2005 - 2010) ulimfanya akawa maarufu sana kuliko hata CHADEMA yenyewe, na hivyo akaibeba CHADEMA vizuri kwenye uchaguzi wa mwaka 2010! CCM ikaendelea kuonekana ikilemewa na wimbi la mabadiliko linalosukumwa na hamu ya wananchi kuachana na “kawaida” na kutaka kuona mambo yakifanyika kwa namna ya tofauti.
Utendaji wa Slaa Ndani na Nje ya Bunge Ulimpa umaarufu na Kuwa Kivutio kwa wananchi Wengi Kumsikiliza |
Toauti kuu za CCM na CHADEMA
Mambo mawili makuu yameitofautisha CCM na CHADEMA katika miaka Sita Iliyopita:
- Wakati CHADEMA kimejikita katika Uchambuzi wa masuala mbalimbali ya Kitaifa; kutoa mitazamo mbadala; Kushawishi fikra, mtazamo na itikadi ya Watanzania; Kufichua maovu kwa ujasiri na kuwalenga Vijana; kwa upande Mwingine,
- CCM kimebaki kuwa ni Chama kilichoonekana kutokuwa na jipya kwa wananchi zaidi ya kujisifu chenyewe na kujificha kwenye kivuli cha Historia yake – huku kikikwepa kwa bayana jukumu la kuzikabili changamoto za leo! Mbaya zaidi, CCM kinaendele kuonekana na chama cha Wazee, cha “Kizee” na kwamba hata vijana wake wengi wanaenenda kwenye vivuli vya wazee wao!
Hata rafiki zangu ambao kwa umri ni vijana na wako CCM, wengi wao wakitoa comment kuhusu masuala ya siasa unaona wazi kabisa wana fikra chakaavu, fikra “nzee”, fikra ambazo zingeweza kufaa kabisa siasa za mwaka 84 lakini sio za 2012, I mean 2012!
Wakati CHADEMA wanazungumzia masuala yanayowakabili wananchi LEO – DOWANS, Umeme, Maji, Afya, Elimu na Mikopo, Uwajibikaji, Safari LUKUKI za Kikwete Ughaibuni n.k., hotuba nyingi za CCM hulenga kuwakumbusha Watanzania kuwa CCM ndicho chama alichokuwamo Nyerere, kuwakumbuksha Watanzania nukuu NZURI za Nyerere kuhusiana na CCM (maana Nyerere alishawahi kuongea hata kauli mbaya kuhusu CCM pia), kuwakumbusha “amani” na utulivu ambayo KINADAI kimeileta chenyewe n.k.
CCM Ina Wasomi Wengi
CCM ni chama ambacho kina-“wasomi” wengi sana pia – ikiwa ni pamoja na wale waliosoma Sayansi ya Siasa katika vyuo vikuu. Lakini pamoja na kuonekana kujawa na Madokta na Maprofesa (wa kusomea na wa mitishamba) – ukiachilia mbali wale wenye shahada za kwanza na za uzamili – bado hotuba na “meseji” zinazotolewa na Chama au Wanachama waandamizi zinaonekana kwa asilimia kubwa sana kujikita kwenye Ushabiki na kusifia historia!
CCM Haijibu Hoja na Maswali ya Wananchi!
Hotuba nyingi za viongozi wa CCM, na kauli za wananchama wengi wa CCM – hususana wale unaoweza kudhania kuwa ni “wasomi”, badala ya kulenga katika kutoa majibu ya maswali magumu ambayo wananchi wanajiuliza kila siku kutokana na kuzidi ugumu na kuharibika kwa maisha – kauli zao zimekuwa zikilenga zaidi katika kuisifu CCM, kusifu historia yake ya kushinda chaguzi mbalimbali, kujisifu kwamba kilianzishwa na Nyerere, kujisifu kwamba kina Ilani nzuri, kujisifu kwamba “kimeleta” amani na utulivu Tanzania, kujisifu kwamba kimeenea nchi nzima n.k.
Masimulizi haya yote ya CCM ukiyaunganisha hayatoi jibu hata moja kuhusiana na lini Tanzania itakuwa na Umeme wa Uhakika, Sifa hizi za CCM hazimsaidii mkazi wa Tabata kuelewa ni lini maji yataanza kutoka kwenye mabomba waliyofungiwa na Wachina na sasa yanatoa buibui badala ya maji. Historia ya CCM haimsaidi kijana wa Sekondari kuwa na uhakika wa Kupata mkopo wakti aingiapo Chuo Kikuu!
Majibu haya hayaelezi ni lini ufisadi, rushwa, wizi na matumizi mabaya ya mali ya umma yatakomeshwa na serikali hapa Tanzania. Sifa hizi za CCM hazimsaidii Mtanzania kuelewa ni lini serikali itachukua hatua madhubuti za kudhibiti mfumko wa bei na kushuka kwa thamani ya hela yetu! KWA BAHATI MBAYA SANA, HAYA YANAFANYWA NA “WASOMI”.
CCM Mitandaoni / Facebook
Katika hatua nyingine, kuna mitandao mingi ya kijamii kwenye intaneti, maarufu zaidi ukiwa ni Facebook. Kwenye hii mitandao kuna makundi mengi ambayo kwa ujumla wake hulenga kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa – siasa zikiongoza mijadala.
Hapo Juu Ni baadhi tu ya Magroup ya Facebook ambapo Mijadala Mingi ya Kisiasa Hufanyika |
Miaka kadhaa sasa nimefuatilia na kufanya taathimini ya mitazamo, hoja na misimamo ya wanachama na “mashabiki” wa hivyo, kwa kiasi kikubwa sana nimebaini kuwa Wanachama na mashabiki wa CCM wanajikita zaidi katika kusifia Chama, kujiaminisha kwamba hakiwezi kushindwa, Kuwatukana wapinzani, kujisifia idadi ya mashina na wanachama wenye kadi n.k.
CCM Ina Maprofesa Hadi wa Mitishamba! Pichani ni "Profesa" Maji Marefu |
Wasomi Wanakiangusha Chama
Wasomi wa CCM katika mitandao mingi – kama ilivyo ndani ya Chama na Serikali pia – sioni wakisimama na kutoa mitazamo,ushauri na misimamo madhubuti ambayo ungetarajia kuipata kutoka kwa wasomi wenye dira ya taifa! Wasomi wameshindwa kukisaidia chama kuchukua hatua madhubuti na hata maamuzi magumu pale yanapohitajika kufanywa na watu waeledi! Ushabiki, Uoga na Unafiki unabaki kuwa kiini cha mahusiano yao ndani ya Chama.
Salaam za 2010 Kwa Chama
Matokeo ya mwaka jana ya Uchaguzi ambayo yalishuhudia KIKWETE AKIPATA KURA KIDOGO KULIKO IDADI YA WANA-CCM WENYE KADI ni ushahidi kuwa Watanzania wa leo hawataki Ushabiki na “misifa” ya mtu kujipatia mwenyewe. Watanzania wa leo hawataki historia za miaka ya 70 ambazo haziwawekei sukari kwenye chai, Watanzania wa leo wanataka majibu ya matatizo na shida zao ambazo zinazongezeka kila kukicha na si vinginevyo.
Wasomi Chukueni Hatua
Wasomi wamekuwa wakilaumiwa sana hapa Tanzania kwa kutoa mchango mdogo kwenye maendeleo ya taifa ukilinganisha na ilivyotarajiwa, lakini nadhani mchango wao kwenye Chama ni duni na butu zaidi. WASOMI ISAIDIENI CCM IACHE U-MBUMBU, kwa namna hiyo mtakuwa mmeishaida Tanzania. Msipofanya hivyo CCM ni hakika itakufa, na mtakimbilia vyama vingine na kujidai ni “wana-mapinduzi”.
Wasaalam…. //mussa
Hii blogu bado ipo? Wasomi tuliotajwa nadhani tunakisaidia chama vizuri na matokeo sasa yanaonekana.
ReplyDelete