Friday, October 7, 2011

CCM Kukataliwa Mijini!

Kama nilivyoahidi katika makala yangu iliyotangulia - unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa http://msbillegeya.blogspot.com/2011/10/ccm-na-ushindi-wa-vijijini.html, katika tafakari yangu ya leo naangalia kukataliwa kwa CCM mijini kuna maana gani.
Mikutano ya CCM Maeneo ya Mjini imepoteza mvuto sana,
na wakati mwingine huhudhuriwa zaidi na watoto.
Katika miji ya Tanzania, kama ilivyo mijini mingine mingi duniani, ndiko kuna idadi kubwa ya watu ambao ni muhimu na tegemeo sana kwa taifa. Shule na Vyuo vya Elimu ya Juu, Wataalam, Wanazuoni, Wanauchumi, Wachambuzi na Washauri, Vyombo vya Habari, Wafanyabiashara, Wageni wa Kidiplomasia, Weledi n.k. n.k. n.k

Kwa upande wa pili vijiji vya Tanzania ndiko kunakaa jamii kubwa ya watu wasiojua kusoma wala kuandika, watu wasio wahi kuona hata gazeti moja maishani mwao, watu ambao hawajawahi kusikia matangazo ya kituo chochote cha radio cha kitaifa, watu ambao wengine HAWAJUI HATA KAMA KUNA KIFAA KINAITWA TV achilia mbali kuwa na simu ya mkononi – na kwa leo tusitaje Intanet.

Chama cha Mapinduzi katika chaguzi mbili mfululizo kimeonesha kusaidiwa na kutegemea sana ushindi unaotokana na kura za maeneo ya vijijini. Hii imetokana kwa kiasi kikubwa sana na CCM kupoteza umaarufu na kukubalika  kwake miongoni mwa jamii ya watu ufahamu, maarifa, hekima elimu na ushawishi.

CCM imepoteza kukubalika na umaarufu wake kwa kiasi kikubwa sana kutokana na kushindwa kujibu maswali na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi – miaka 34 baada ya kuzaliwa kwake.
Ukubalifu wa CHADEMA mijini ni tishio la wazi kwa CCM!

Mbaya zaidi, jamii hii ya watu walioko mijini wanavyo vyanzo vingi sana vya habari na taarifa ambavyo kwa kiasi kikubwa vinawasaidia kuelewa kuewa matatizo waliyonayo katika maisha yao ya kila siku yanaweza  kutatulika – tena mengine kwa muda mfupi kabisa – japo CCM na serikali “zake” hakioneshi dalili ya kuwa na uwezo – wakati mwingine hata nia – ya kutatua matatizo na kuboresha maisha ya wananchi.

Uwepo wa vyombo vingi vya habari na vyanzo vingi vya habari kumewawezesha wananchi wengi wa mijini kubaini kwamba matatizo yanayowakabili yanatatulika. Wengi wanashuhudia kila siku kwenye televisheni, intaneti na magazeti kuwa jamii na mataifa mengi Serikali zao zimekwisha kutatua matatizo mengi ya wananchi ambayo na Tanzania yapo lakini kwa upande wa CCM na Tanzania maelezo yake mengi yamekuwa ni ya kuonesha ugumu na changamoto ya kufanya kazi na wakati mwingi kukwepa kuzungumzia masuala ya msingi ambayo wananchi wanataka kupataiwa majibu yake.
Wana vijiji huupenda sana "unyenyekevu" wa CCM
Pasipo kutumia maelezo mengi wala kuzunguka sana – maneno na matendo mengi ya Serikali ya CCM – HUSUSAN CHINI YA KIKWETE – yanaweza kuelezewa kuwa si kitu kingine zaidi ya  UBABAISHAJI! Ni ubabaishaji huu ambao umewafanya watu wengi wa mijini kukikataa Chama cha Mapinduzi ambacho walijitahidi na kujilazimisha kukiamini, kukitetea na kukisifu kwa miaka mingi – HADI WALIPOCHOKA KWA KUTOONA MATOKEO YA “SUPPORT” YAO KWA CHAMA!

Wakazi wengi wa mijini, na ambao wengine miongoni mwao wamekuwa wakupata nafasi ya kutembelea nchi nyingine duniani, wamechoka kuona nchi nyingine zilizowahi kuwa sawa na Tanzania kimaendeleo zikipiga hatua kubwa za kimaendeleo wakati Tanzania tukiendelea kupeana ahadi na msisitizo ukiwekwa kwenye kukisifu chama kwa “kuleta” amani na utulivu – japo umaskini na shida pia zimezidi kuongezeka chini ya Utawala wa chama hiki hiki!

Maandishi Ukutani

Katika dunia ya leo – kisiasa – kukataliwa na wasomi, watu weledi, wataalamu, wafanyabiashara na wanaharakati, ni “maandishi ukutani”! Unachohitaji ni kutafuta “nabii” wa kukusomea na kukutafsiria maana ya maandishi hayo ukutani. CCM inahitajika kutafuta nabii wa kukisaidia kusoma na kutafasiri maandishi haya ukutani.

Niko Tayari Kuisaidia CCM

Nikiwa Mtanzania, Mwanasiasa kwa Taaluma na kwa Utendaji, niko tayari kukisaidia Chama cha Mapinduzi – kufanya jambo moja tu – KUKISOMEA NA KUKITAFSIRIA MAANDISHI YA UKUTANI! Hata hivyo ni muhimu kuelewa kuwa kusomewa na kutafsriwa haitoshi kukisaidia Chama. Kunahitajika kuwe na Mfalme na Wasaidizi wake ambao watakuwa na uwezo na utayari wa kufanya maamuzi na vitendo sahihi ili kurekebisha hali!

CCM ya Kikwete Haisadiki, hata hivyo

Kwa bahati mbaya CCM KWA SASA HAINA KIONGOZI WA UONGOZI UNAOWEZA KUISAIDIA kukabili haya mapinduzi ambayo tayari yalishaanza na yatakikumba chama na kukiondoa kutoka madarakani hivi karibuni… 

CCM inayoongozwa na Kikwete imejawa na inaongozwa na kikund au vikundi vya mashabiki NA SIO VIONGOZI! Kikwete amejizungushia na amezungukwa na MASHABIKI wake badala ya WASAIDIZI wake! Namaanisha wazi kuwa ANGUKO LA CCM KUTOKA MADARAKANI TANZANIA HALIKO MBALI.

Wasaalam…… //mussa

No comments:

Post a Comment