GADAFFI: Aliachukuliwa na Wengi kama MKOMBOZI - Alichukuliwa na Wengi kama MUUAJI! - Na Labda - ALIKUWA HAYO YOTE! |
Kanali Mouammar Gadaffi hatimaye ametutoka, siku chache tu baada ya ambayo yangekuwa maadhimisho ya miaka 42 ya Utawala wake. Gadaffi alifanikiwa kuwa mtu aliyegawanya fikra za watu wengi sana – hususan waafrika – kuhusu wema au ubaya wake.
Waafrika wengi wanapendelea kumuona shujaa kwa jinsi alivyowahi kuwa mstari wa mbele katika kupambana na wazungu kwa maneno na wakati mwingine kwa matendo kuliko viongozi wengi wa kiafrika walivyoweza kufanya. Baadhi walimuona na wanaendelea kumuona kuwa alikuwa ni mtu muovu sana, katili, dikteta… asiyefaa kuigwa kwa namna yoyote.
Kwa ufupi, kuna mambo mengi yamuhusuyo Gadaffi ambayo yaliwagawa waafrika kimtazamo na yataendelea kuwagawa kwa muda mrefu ujao. Tafakari yangu ya leo haitayachunguza maeneo hayo yote kwa undani wake, ila itajikita katika eneo moja tu – baadhi ya “makosa” aliyoyafanya Gadaffi – labda kwa kujua au kwa kutokujua – ya kisiasa, kijamii, kiuongozi au labda hata kiufundi – ambayo yalichangia katika kumuangusha.
Gadaffi, aliyeingia madarakani mwaka 1969 kwa mapinduzi ya kijeshi – baada ya kuongoza kikundi cha vijana wenzake wanajeshi kumpindua mfalme wa Libya wakati huo – anakumbukwa na kusifiwa na Waafrika wengi – HUSUSAN WANAOISHI KATIKA NCHI MASKINI kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na haya yafuatayo (Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Mtandaoni):-
- Umeme kwa Raia wote wa Libya – hakuna kulipia “bill” za umeme
- Hakuna Riba kwenye mikopo – mikopo yote ya benki hutolewa bila kutoza Riba
- Nyumba/makazi yalichukuliwa kuwa ni haki ya binadamu Libya
- Maharusi wapya walikuwa wanapewa Dola 50,000.00 (kama Milioni 80 za Kitanzania) kwa ajili ya kuanzia maisha
- Elimu na Afya ni huduma za Bure Libya
- Walibya waliotaka kuwa wakulima walikuwa wanapewa Mashamba, Nyumba na mitaji
- Walibya waliohitaji matibabu nje ya Libya walilipiwa gharama zote na Serikali
- Raia akinunua gari Serikali humpatia ruzuku ya 50% ya bei ya gari…. N.k. n.k.
Ni wazi kabisa kwamba huduma hizi ni nyingi mno, nzuri mno na kwa mtu yeyote – hususan katika nchi maskini – zinatosha sana kumfanya raia wan chi yoyote kutulia, kumpenda, kumheshimu na hata kuwa tayari kumlinda na kumtetea rais wake kwa gharama yoyote – Libya ilikuwa Kinyume kwa Gadaffi!!!
Gadaffi alikosea Wapi?
Baadhi ya mambo ambayo labda gadaffi hakuyajua au labda aliyapuuza, na ambayo yalichangia sana katika kumuangusha ndani ya muda mfupi, kama kiongozi, mtawala na mwanasiasa ni pamoja na haya yafuatayo:-
1. Siasa ni Watu SIO Vitu!
Kosa kubwa la kwanza ambalo Gadaffi alilifanya ilikuwa ni kudhani kuwa VITU vinaweza kufanikisha Siasa na Uongozi wake. Siasa huwa ni mchezo unaochezwa kwenye uwanja ambao ni Umma. Ukiweza kuupata Umma ukuunge mkono ni njia kubwa zaidi ya mafanikio kisiasa kuliko kuwa na mali na vitu vingi kiasi chochote.
Mali na Vitu vinaweza kukuhakikishia uhai wako kisiasa na katika uongozi kwa muda mfupi sana, lakini watu wakiwa nyuma yako, upande wako, utawala wako ni wa “milele”. Gadaffi alifanya kosa la kudhani akiwapa watu vitu basi watampenda na kumuona wa maana sana, au kwamba hawatakuwa na tamaa ya madaraka na nafasi zake kisiasa – KOSA!
2. Kuelewa Matakwa ya Watu na SIO Kupanga Matakwa ya Watu
Jambo la pili la msingi sana katika siasa, utawala au uongozi – ni muhimu sana kuelewa watu wanataka nini na sio kukaa na kukadiria na kuamua ni kitu KINAWAFAA wananchi! Kitu chochote utakachompatia mtu – hata kama ni kizuri namna gani, akiendelea kukipata kwa muda mrefu itafikia mahali atakiona cha kawaida na kisha ataanza kuwazia vile ambavyo hanavyo. Hakikisha kuwa matendo yako yote yanalenga kukidhi haja za watu na kujibu maswali yao.
Gadaffi, kwa kuelewa hali ngumu ya kimaisha inayowakabili waafrika na waarabu wengi katika nchi yao, alijua kuwa akiwapa vile vitu vinavyoliliwa na waafrika wengine katika nchi zao basi watampenda na kumuona wa maana sana – KOSA!
Utawala unaodumu na kufanikiwa SIO ule unamaliza matatizo ambayo viongozi wanadhani kuwa ndiyo yanawasumbua wananchi bali ule unaofanya yale wananchi wanayoyataka – hata kama hayamalizi shida na matatizo ya msingi. Kama kiongozi, hakikisha kwanza unashughulikia yale wanayoyataka wananchi, kisha waelimishe kuhusu hayo ambayo na wewe unadhani ni ya msingi. USI-IMPOSE WEMA WAKO JUU YA WATU – Wataukataa na kukukataa na wewe – kama Gadaffi!
3. Kutengeneza Marafiki ni Muhimu – Hata katika Uovu
Mafanikio ya kiuchumi aliyofanikiwa kuyaleta Gadaffi nchini kwake yyalimfanya alewe sifa na umaarufu aliokuwa anapewa na raia wake na watu wake wa karibu. Sifa hizi zilimvimbisha kichwa kiasi cha kutokuona kama alikuwa anahitaji kuwa na marafiki na mahusiano mazuri na jumuiya ya kimataifa.
Sifa zake zilimpelekea kuwatukana na kuwaona takataka viongozi wenzake wan chi za kiarabu na za Afrika – hali ilifikia hali mbaya zaidi siku alipofokeana na Mfalme wa Saudi Arabia kwenye mkutano wa Nchi za Kiarabu uliofanyika Sirte mwaka Jana 2010, siku chache kabla hajaenda kwenye Mkutano wa UN na kumtukana kila mtu aliyekuwapo – hatua hii ilikuwa mbaya.
Chuki na hasira walizokuwa nazo viongozi wengi duniani – ukianza na waarabu wenzake zilichangia sana katika kumng’oa madarakani. Azimio la kumpiga lilipitishwa bila kupingwa hata na taifa moja, huku nchi za kiarabu zikiwa za kwanza kuchangia siraha na ndege za kumpiga – achilia msaada wa wanajeshi na magari ya waasi!
Rais wa Syria, Assad, kwa mfano, ameshafanya maovu na mauaji mengi makubwa kwa raia kuliko aliyokuwa ameshayafanya Gadaffi wakati anaanza kushambuliwa na NATO, lakini Syria imepata uungaji mkono wa baadhi ya mataifa, yakiwemo ya kiarabu, Urusi na China kupinga TAMKO la Umoja wa Mataifa la Kulaani tu yale yanayofanyika – SIO AZIMIO LA KUMPIGA!
Kama Kiongozi, Ni Muhimu kuwa Mnyenyekevu, Hususan kwa Wananchi wako. Gadaffi alishindwa kwa kiasi kikubwa kuonesha huo Wasifu |
4. Kujihadhari na “Maskini Jeuri”
Gadaffi alidhani kwa kuwapatia fedha watu ambao hata hawafanyi kazi ilikuwa ni kigezo cha kuwafanya wanyamaze maisha yao yote – KOSA! Gadaffi alisahau kuwa huwa kuna watu “maskini jeuri”. Watu hawa huwa wako tayari kuukata msaada wako hata kama hawana chanzo kingine cha msaada iwapo tu wataona kuna dalili za kukosewa heshima kama watu.
Kosa alilolifanya Gadaffi ilikuwa ni kutaka kuwachukulia raia wote wa Libya kama watoto wake, na kwamba yeye na wake zake na watoto wake ndio wana mamlaka ya kuamua mustakabali wa raia wa nchi nzima – as if wote ni watoto na wajukuu zake!
Kitendo cha kuwaambia wanaumme hawana haja ya kutafuta ajira kwa sababu yeye atakuwa anawapa hela ya kula wao na wake zao na watoto wao na kuwalipia kodi za nyuma n.k. kwa “Maskini Jeuri” ni kitendo cha dharau kubwa – wakati alidhani ndo kitampa Siafa – KOSA!
Kwa Ufupi, Gadaffi hakufanya makosa makubwa ya kiuchumi ambayo yalipelekea kuangushwa kwake – tatizo lilikuwa ni kushindwa kuelewa na kuzingatia masuala ya kijamii na kisaikolojia ya wanadamu. Kushindwa kuelewa ni kitu kinachomfanya ajisikie vizuri linaweza kuwa ni kosa kubwa. Gadaffi alijitahidi kuwa “busy” kuhudumia mahitaji yao ya kiuchumi lakini hakuelewa kuwa mgogoro wa kisaikolojia uliokuwa unawatesa kwa miaka mingi ungekuja kuwa bomu kubwa kwake – NA SASA NI MAREHEMU!
Hitimisho langu
Japo bado kuna mjadala mkubwa kuhusu uongozi – iwapo viongozi huzaliwa viongozi au huweza kutengenezwa (kwa maana ya kufundishwa na kusoma) – ukweli unabaki kuwa hata kama mtu amezaliwa akiwa na sifa nyingi anazodhani ni za kiuongozi – bado kuna mambo mengi sana ambayo mtu huyo atatakiwa kuyasoma, kufundishwa na kuyaelewa kabla hajaweza kuwa kiongozi bora….
Binafsi naendelea na Programu Maalum ya “Uongozi Bora Wenye Kuleta Mabadiliko” inayoendeshwa na Shirika la Maendeleo na Sera la Afrika ya Kusini na mafundisho hufanyika nchini Mauritius. Mungu akipenda ufahamu na uzoefu huo nitauingiza miongoni mwa vijana wengine hapa Tanzania kinadharia na kivitendo.
Maoni yako
Maoni yako yanakaribishwa sana kuhusiana na mjadala wa “Legacy” ya Gadaffi Afrika. Waweza kuyaandika hapo chini kwa kuobnyeza Maoni au kupitia msbillegeya@hotmail.com
Gadaffi’s Leadership Philosophy: “Give the poor Libyans everything they need and then divide them, crush whoever revolts and rule forever”
No comments:
Post a Comment