Wednesday, October 26, 2011

MAANDAMANO Kupinga Serikali/DOWANS Jumamosi Hii!

Ndugu wananchi, wanaharakati, wanahabari na watu wote wenye Mapenzi mema na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Napenda kutumia nafasi hii kuwatangazia kuwa kutakuwa na Maandamano ya Kuelezea hisia, maoni na matakwa yetu SISI WANANCHI KUPINGA Kulipwa kwa Dowans. Maandamano hayo yatafanyika Siku ya JUMAMOSI HII, Tar 29 Oktoba 2011 kuanzia Saa 2:30 (Mbili na Nusu Asubuhi).


Maandamano hayo yataanzia UBUNGO mbele ya Jengo la TANESCO na kuishia Jangwani.


Malengo makuu ya Maandamano hayo ni:


1. Kupinga Serikali kuilipa kampuni tata ya DOWANS  - iliyorithi mkataba wa KAMPUNI HEWA YA RICHMOND kwa kutumia fedha za Umma/Walipa Kodi.


2. Kuitaka Serikali Kutekeleza Mapendekezo 23 ya Kamati ya Bunge kuhusiana na Richmond - ambayo ni pamoja na Kuwachukulia HATUA ZA KISHERIA wale wote waliohusika katika kuingia mkataba huu na kampuni hewa na kulisababishia taifa hasara kubwa.


3. Kuitaka serikali, IWAPO ITALAZIMIKA kulipa deni la Dowans, kuwafilishi mali WOTE waliohusika katika kufanikisha Mkataba wa Richmond na hatimaye Dowans - na pesa zitakazopatikana ndizo zitumike kuwalipa DOWANS...


... pamoja na mengine yahusianayo na hali ngumu ya kimaisha inayozidi kuharibika kila siku....



Vyama Mbalimbali vilialikwa kushiriki katika Maandalizi na Maandamano yenyewe - IKIWA NI PAMOJA NA CCM....


WANANCHI WOTE MNAKARIBISHWA KUSHIRIKI MAANDAMANO HAYO YA AMANI


Kwa Taarifa zaidi Soma TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI hapa Chini


Taarifa Hii Ilisomwa mbele ya Waandishi wa Habari na Mussa Billegeya, Marcosy Albany na Harold Sungusia kwenye Ofisi ya Legala and Human Rights Center (LHRC) – LEO Jumatano tar. 26 Oktoba 2011.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
MAANDAMANO YA KUPINGA SERIKALI KUILIPA DOWANS Sh. BILIONI 111
Novemba, 2010 Mahakama ya usuluhishi ya kimataifa ilitoa tuzo dhidi ya Tanesco kuilipa Dowans shillingi billion 94. Jambo hili liliibua hisia na hasira miongoni mwa wananchi kwa kulalamika na kupinga ulipaji huo wa fedha za umma kwa kampuni tata - kutokana na taarifa za kamati teule ya Bunge.

Baada ya tuzo hiyo watu binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mawakili wa Tanesco walipinga mahakama kuu  kusajili  tuzo hiyo. October 2011 Mahakama kuu ilitoa uamuzi wa kusajili tuzo hiyo na kuamuru Tanesco ilipe shillingi billion 94 na asilimia 7.5 ya gharama hizo. Hata hivyo kabla ya usajili wa tuzo hiyo, Dowans iliuza mitambo husika kwa kampuni ya Symbion Powers kinyume cha taratibu kwa kuwa kulikuwa na amri ya mahakama ya kuacha hali ya mitambo ibaki kama ilivyo. Cha kushangaza ni jinsi ambavyo Serikali ilikuwa mstari wa mbele katika kuingia mkataba wa uzalishaji wa umeme na Symbion Powers kwa gharama ya watanzania hali ikijua mitambo hiyo iko kwenye mgogoro uliopo mahakamani.

Kwa kuzingatia haya, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Asasi kadhaa za Kiraia na Wanaharakati wa Haki za binadamu tulitoa tamko tarehe 11 Oktoba 2011 kuitaka serikali kuchukua hatua ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa bila mafanikio.

Kwa kuwa serikali imeamua kudharau maoni yetu, na kwa kuwa kuna kila dalili kwa serikali kuilipa Dowans fedha za wananchi, sisi, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, serikali wakilishi za wanafunzi na raia wa kawaida wa Dar es salaam tunaitisha maandamano kwa uratibu wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu siku ya Jumamosi tarehe 29/10/2011. Kwa hapa Dar es salaam, maandamano yataanzia Ubungo, mbele ya zilipo ofisi za Makao makuu ya TANESCO hadi Viwanja vya Jangwani kuanzia saa 2:30 asubuhi.

Maandamano haya yanalenga kuitaka serikali kufanya yafuatayo:-
  1. Kutokuilipa kabisa Dowans kwa kutumia hela za walipa kodi wa Tanzania.
  2. Itoe maelezo ya kina kwanini ilipuuza ushauri wa kisheria wa kuvunja mkataba na Richmond toka awali kwani kwa mujibu wa washauri wa kimarekani Hunton & Williams LLP wakati Tanesco inaingia mkataba na Richmond Dev’t Co. Kampuni hiyo haikuwa imeshasajiliwa achilia mbali kuwa haikuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake chini ya mkataba huo.
  3. Itekeleze kwa dhati  maazimio 23 yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya mlolongo mzima unaopelekea mpaka sasa tutakiwe kulipa bilioni 111. Kwa kufanya hili Serikali pia ituthibitishie kuwa itaacha kabisa kukikosea heshima chombo ambacho ni kisemaji na wakilishi cha wananchi kupitia wabunge.
  4. Kama sheria za kimataifa zinatubana kulipa deni hili basi malipo haya yafanyike kwa kuuza mali za wale waliotusababishia kadhia hii na kwamba malipo ya kuilipa dowans yafanyike pale tu serikali itakuwa imeshawachukulia hatua kali wahusika wa kadhia hii. Umma ni lazima ujiridhishe kwa kuona hatua hizo zinachukuliwa.
  5. Kuchukuwa hatua ya kinidhamu kwa wale wote walioshiriki katika kuingiza serikali katika mkataba huu hata mawakili waliotoa ushauri huu.
  6. Serikali ipeleke Bungeni muswada wa utaratibu mzuri na sahihi wa kushirikisha wananchi na hata wabunge katika kuingia mikataba ya kimataifa na serikali ili kuepusha hali kama hii kutokea.

Kwa hiyo tunatoa wito kwa watanzania wote tuadhimishe kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutenda yafuatayo:-
  1. Tujitokeze  kwenye  maandamano ya amani na kupinga ufisadi na malipo ya kifisadi ya Dowans siku ya Jumamosi, tarehe 29 Oktoba 2011.
  2. Kuvaa nguo za maombolezo, nyeusi, kama ishara ya maombolezo tukikumbuka msimamo wake wa kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali  za taifa,
  3. Tuzitumie siku za ibada za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zote ndani ya muda huu, kumuomba Mungu atujalie Uzalendo na Ujasiri wa kuitetea nchi yetu, kama alivyofanya  Mwalimu Nyerere,
  4. Kuwasiliana na wanaharakati nchi nzima mahali walipo, ili kupanga na kuandaa mahali pa kukutania siku ya maandamano haya ya amani.

Mwisho, tunaomba walipa kodi (wananchi) wote ambao hawajapendezwa na mlolongo huu unaopelekea ulipaji wa deni hilo la Dowans na ufisadi mwingine wote kuwa na uthubutu na kujitokeza kwa wingi kusimamia kile ambacho wanaona ni haki na stahili  ya wananchi  wote na taifa letu kwa ujumla.

Taarifa Hii Ilisomwa mbele ya Waandishi wa Habari na Mussa Billegeya, Marcosy Albany na Harold Sungusia kwenye Ofisi ya Legala and Human Rights Center (LHRC) – LEO Jumatano tar. 26 Oktoba 2011.

No comments:

Post a Comment