Monday, October 10, 2011

IGUNGA: Kitaalam CHADEMA Ilishinda!

Katika mojawapo ya makala zangu zilizotangulia nilijaribu kuelezea ni kwa namna Wasomi ndani ya CCM hawakisaidii Chama kwa Namna inavyotakiwa na kutarajiwa. Nilielezea ni kwa namna gani wasomi waliomo ndani ya CCM nao wametekwa na kuingizwa kwenye mfumo wa Siasa Uchwara, Majitaka na ushabiki wa Kisiasa badala ya kuwa Viongozi wa Kisiasa. 
Matokeo ya Idadi: CCM Ilishinda!

Matokeo yake ni kwamba maneno na matendo mengi ya CCM kwa leo huonekana kama yameamuliwa kwenye vikao ni mikutano ya mashabiki na sio wasomi, weledi na watu wenye uelewa wa kile wananchokifanya. Ushabiki huu unapopitiliza hupoteza nafasi ya usomi na ueledi. Leo Natafakari "kitaalam" matokeo ya Uchaguzi wa Igunga.

Matokeo ya Igunga yalipotangazwa, ilikuwa ni shangwe na Nderemo kwa wana CCM – nadhani wote! Hii ikiwa ni pamoja na viongozi, wasomi na mashabiki wote wa chama. Wachache ndani ya CCM tulikaa na kutaathimini maana ya huu ushindi kwetu kama chama. Ninapozungumzia taathimini ya kitaalamu, namaanisha sio kuangalia matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi – bali matokeo hayo yamepatikanaje, tuliowashinda walipata nini, na iwapo mbegu yetu inaota na itazaa matunda baadaye au ya wapinzani ndiyo ina uwezekano wa kuzaa matunda baadaye?

Wana CCM wengi tulishangilia sana ushindi huu, na wengine tukaenda mbali kukebehi “alama” ambayo CHADEMA wameiweka Igunga. Wachache sana miongoni mwetu waliangalia kwa karibu maana ya matokeo haya na wachache wakaipongeza CHADEMA “kwa kujitahidi”.

Kitaalam, katika uchambuzi huwa tunazingatia mambo mengi sana ili kuelewa “mshindi” wa kweli kwenye uchaguzi. 

Kwanza, tunapima fursa: Ni nani alikuwa na fursa nyingi kuliko mwingine? E.g. CCM lile jimbo lilikuwa ni la kwetu tokeapo, kwa hiyo tulikuwa tunatetea ubingwa. Tofauti na CHADEMA ambao hawajawahi kushinda Ubunge Igunga – hata mara moja.

Pili, CCM tulishagombea mara nyingi kwenye hilo jimbo, tofauti na CHADEMA ambao hawajawahi kusimamisha mgombea kwenye hilo jimbo hata mara moja! Hii inamaanisha kwamba wananchi walishasikia na kupima hoja na ilani zetu za CCM mara nyingi wakati walikuwa hawajawahi kusikia wala kupima sera za CHADEMA katika nafasi ya Ubunge – HATA MARA MOJA!
CHADEMA 'wameivamia" Igunga kwa Mara ya Kwanza na Kupata 44%
ya Kura, CCM Imekaa miaka 34 ikapata 46%. Awamu Ijayo Hali inaweza ikawaje??

Tatu, Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye “Rais” wa wilaya, japo wananchi wengi hudhani kwamba ni mtumishi wa umma tu na kwamba anatumikia wananchi wote “bila ubaguzi wala upendeleo”, kivitendo NI LAZIMA awe mjumbe wa kamati ya Siasa ya Wilaya – kwa hiyo anakisaidia Chama – akiwa katika nafasi ya Umma – CHADEMA HAWANA DC WAO!

 Hii ni pamoja na vyombo vingine “vya umma” ambavyo hata hivyo hufanya kazi chini ya serikali ya CCM na kwa kutekeleza ilani ya CCM kama Polisi, Msimamizi wa Uchaguzi Jimboni n.k. n.k.!

Nne, Chama cha Mapinduzi kimekaa madarakani Igunga na Tanzania kwa ujumla tangu siku kilipozaliwa – miaka 35 hivi iliyopita. Ninamaanisha CCM imekuwa na nafasi ya kutumia fedha za Chama na Za Serikali kwa ajili ya Kueneza Propaganda za Chama, Kujitangaza na kutekeleza Ilani yake hapa Nchini – na Igunga – kwa zaidi ya miaka 34 mfululizo. Hii inamaanisha kuwa serikali ya CCM imekuwa na nafasi ya kuwafanyia mambo yote mazuri ambayo wanayahitaji wana Igunga kwa Miaka 34 MFULULIZO. 

Muda huu, iwapo chama kimeutumia izuri, unatosha sana chama kutokupiga kampeni na kutoa ahadi yoyote mpya – maana wananchi tayari wanakuwa na picha halisi ya chama, utendaji na utekelezaji wa ilani zake. Na katika hali ya kawaida, ni rahisi hata wananchi wenyewe wakasema hawataki kusikia ilani wala ahadi za mtu mwingine yeyote maana wametosheka na huyo waliye naye!

Tano, CCM tuliingia kwenye Uchaguzi huu tayari tukiwa na kura 35,000 tulizozipata miezi michache tu iliyopita – hata mwaka haujaisha! CHADEMA wameingia wakiwa na Kura Ziro/Sifuri/0/NIL!

Kwa upande wa CHADEMA, hakikuwa na hata mojawapo ya Sifa na Fursa hizo zilizotajwa na ambazo hazikutajwa hapo juu! CHADEMA, kwa namna hiyo, kilitegemea zaidi mbinu nyingine mbadala, kubwa ikiwa ni kutumia rekodi yake fupi ya utendaji na umahiri wake bungeni, ilani yake mpya kwa wana Igunga na hamasa tu ya kutaka kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo – hata kule ambako chama hakina mizizi wala historia ya muda.

Matokeo ya Kwenye Karatasi!
Matokeo ya kwenye karatasi yalipotoka – CCM 46% Chadema 44%!.... Swali unaloweza kujiuliza kwa haraka kabisa – NI NANI ALIYESHINDA KATI YA HAO WAWILI…? Ukirudi kwenye utangulizi wangu ambao unashauri tuwe tunayaangalia mambo kwa umakini – unaweza kuwa na jibu tofauti kabisa na ambalo atakuwa nalo “shabiki” akiyaangalia matokeo hayo!

Ukichukua orodha ya fursa ambazo CCM iliingia nazo kwenye Uchaguzi, ukalinganisha na Fursa za CHADEMA utabaini kuwa hadi kipenga cha kampeni kinapulizwa – matokeo yalikuwa ni CCM – 100% CHADEMA 0%

CCM tuliingia kwenye Uchaguzi huu tayari tukiwa na kura 35,000 tulizozipata miezi michache tu iliyopita – hata mwaka haujaisha! CHADEMA wameingia wakiwa na Kura Ziro/Sifuri/0/NIL! 

Siku Chache tu za Kampeni ziliporomosha Historia ya miaka 34 ya CCM Igunga kutoka 100% dhidi ya CHADEMA hadi 46% - 2% ZAIDI YA CHADEMA iliyopata 44%! – NI NANI MSHINDI HAPO!

Nasisitiza Utaalam na Ueledi
Ni kweli kwamba watanzania wote tunahitaji maendeleo – bila kujali vyama vyetu, dini zetu au makabila yetu. Lakini wito wangu siku zote huwa ni kuwakumbusha na kuwataka watanzania kutambua na kukubali kwamba maendeleo ya taifa hili, kama ilivyo kwa mataifa mengine, hayatakuja kutokana na USHABIKI wa vyama – bali matumizi ya utaalamu katika kuchambua, kutaathimini mambo na kuweka mipango na kuitekeleza KITAALAMU!

Ushabiki hautaisaidia hii nchi WALA VYAMA VYETU. Naamini watanzania wote tukiweka mbele utaalamu na ueledi katika msuala yote tunayoyapanga na kuyafanya – ndani ya chama na serikali – tutaweza kuvisaidia sana vyama vyetu na taifa letu kupita tunavyofanya wengi wetu kwa sasa – KUPIGA PROPAGANDA ZA USHABIKI…!

Wasaalam…… //mussa

5 comments:

  1. Kaka nakupongeza kwa mtizamo chanya wenye weledi na takwimu sahihi waache waendelee kulala usiwaamshe maana wao wanajua watatawala milele kama mungu na wananchi wa Tanzania wa leo ni sawa na wale wa miaka 50 kabla ya uhuru, waache tu kesho yao inakuja sasa.

    ReplyDelete
  2. Kaka nimekupata kamili this Tanzania thinkers will think on this thanks for this we' are behind your sceneKaka nimekupata kamili this Tanzania thinkers will think on this thanks for this we' are behind your scene

    ReplyDelete
  3. kwa namna moja au nyingine kuna kitu nime-gain thank you brother

    ReplyDelete