Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete |
Kuna sakata kubwa lingine - kati ya mengi - yanayoendelea ndani ya Chama changu cha Mapinduzi CCM. Sakata lenyewe linahusiana na fununu za kuwepo kwa "kundi" linalotaka Kikwete avuliwe Uenyekiti wa Chama na aendelee tu na nafasi ya Urais. Leo, natoa maoni yangu kuhusiana na suala la Mtu kuwa Rais na Mwenyekiti wa Chama tawala kwa Wakati mmoja.
Tangu enzi za Mkapa (ndipo nilipoanza kufuatilia Siasa kwa jicho la kutafuta kuelewa na uchambuzi), Msimamo na ushauri wangu mara zote ulikuwa RAIS HAPASWI KUWA MWENYEKITI WA CHAMA TAWALA! Sababu nitakayoijadilia mimi hapa ni moja na ambayo kwa hoja yangu ndiyo ya msingi: Uwajibikaji
Wakati chama kinapokuwa kinajiandaa kuingia kwenye Uchaguzi wowote, huwa kinatengeneza Ilani. Ilani hii kwa kawaida ndiyo huja kuwa mwongozo wa Chama wa utekelezaji baada ya uchaguzi na chama kinapokuwa kimeshinda uchaguzi.
Kwa hali hiyo, Mgombea wa Urais/Rais hukabidhiwa dhamana na Chama kuongoza utekelezaji wa Ilani. Kwa maana hiyo, Rais atatakiwa kuwa anakuja kwenye Chama kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa Ilani, kuhojiwa, kurekebishwa, kuelekezwa, kukemewa, kurudiwa na hata kuadhibiwa iwapo kuna makosa au uzembe alioufanya au uliofanyika chini ya dhamana yake akiwa kama mwakilishi wa chama katika kutekeleza Ilani.
Kikwwte "akitumia" madaraka yake ya Urais |
Ni nani anayeitisha vikao kujadilia maendeleo ya utekelezaji wa Ilani? Ni Nani anayeandaa ajenda za Mikutano? Ni nani anayeandaa na kutoa taarifa ya Utekelezaji? Taarifa inawasilishwa kwa Nani? Nani anayeongoza mjadala wa Taarifa ya utekelezaji, ukosoaji, mapendekezo na makemeo kwa Rais pale alipokosea? La mwisho na kubwa zaidi: NI NANI ANAYEMUADHIBU RAIS PALE ANAPOKUWA HAJATEKELEZA ILANI YA CHAMA KAMA INAVYOTAKIWA????? n.k.
Ukiyatafakari haya maswali yote kwa mtazamo wa kiutawala bora na uwajibikaji, utaona kuwa milango ya kufanyika mambo hayo yote kwa kufuata misingi ya utawala bora na uwajibikaji katka taasisi IMEFUNGWA - kwa sababu Mtoa Taarifa Ndiye Mpokea Taarifa na ndiye anayesimamia mijadala ya kujadili taarifa yake - ukiachilia mbali kwamba ndiye anayeandaa ajenda!
Kikwete "akitumia" madaraka yake ya kichama |
Njia hii ya kumfanya Rais kuwa ndiye Mwenyekiti wa chama ilianza tangu wakati wa Nyerere na imekuwa ikifanyika hivi kwa miaka yote na katika nchi nyingi sana Afrika. Lengo lake kuu huwa ni kumpatia Rais madaraka juu ya Chama na Serikali kwa wakati mmoja na kwa namna hiyo kupunguza au kuondoa uwezekano wa chama kuweza kumgeuka na kumwajibisha kinyume cha vile atakavyo yeye.
Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa utaratibu huu umewekwa sio kwa ajili ya manufaa ya chama na taifa bali kwa maslahi ya Rais mwenyewe ili aweze kujihakikishia "usalama" wake awapo madarakani - kwa kukalia viti vyote viwili na kuwa na kauli kubwa katika nafasi zote hizo nyeti.
Upungufu wa Mfumo Huu
Utaratibu huu wa kumfanya Rais kuwa Mwenyekiti wa Chama haukuanzishwa kwa ajili ya kujenga na kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika Chama na serikali bali kwa ajili ya kumpatia nguvu Rais ya kusimamia Chama na Serikali kwa wakati mmoja. Hii inamuwezesha Rais kuweza ku-dictate maamuzi na matendo ya Serikali na ya Chama kwa wakati mmoja.
Utaratibu huu unaminya na kuziba mianya ya watu kuweza kuhoji na kuchukua hatua za uwajibishaji - hususan kwa upande wa Chama - kutokana na kutokuwa na nafasi "huru" ya kumchunguza, kumpima na kumhoji Rais juu ya Matendo yake katika kuitekeleza ilani, katiba na maamuzi ya Chama.
Matokeo ya "Uhodhi" huu
Matokeo yake huwa ni kwamba katika kila muda/awamu ya Utawala, sura na mwelekeo wa Chama huonekana kubadilika sana ku-akisi zaidi picha ya Mwenyekiti na Rais aliyepo madarakani zaidi kuliko sera, ilani na mwelekeo wa Chama kwa ujumla kama ulivyo kwenye "makaratasi". Sote ni Mashahidi kuwa CCM ya Nyerere, haikuwa ya Mkapa na haikuwa ya Kikwete (sijamtaja Mwinyi kwa makusudi).
CCM ya Nyerere kwa wale tunaoikumbuka vizuri, iliakisi zaidi falsafa, mitazamo na dira ya Nyerere kama Nyerere, vivyo kwa Mkapa na hatimaye kwa Kikwete. Mafanikio mengi na matatizo mengi yaliyokuwa yanatokea chini ya Nyerere, Mkapa na Kikwete (na namna yalivyo/yanavyo shughulikiwa) yanaakisi zaidi Uwezo, Utashi na mwelekeo wa Rais na Mwenyekiti kuliko Chama kama chama.
Ili kuficha mapungufu na udhaifu wa viongozi wahusika, watu wengi hupenda kuhusianisha tofauti za tawala hizo na kile ambacho hudai kuwa ni "changamoto tofauti" zilizowakabili viongozi husika.
Madhara ya Kugawanya Madaraka
Kuna nchi moja jirani - Malawi - ambako ilitokea Rais HAKUWA mwenyekiti wa Chama tawala. Katika mchakato wa kuwajibishana, kulitokea hali kubwa ya kutokuelewana baina ya Mwenyekiti wa Chama tawala na Rais kiasi cha kupelekea chama kugawanyika.
Mwisho, Rais alijiengua kwenye Chama tawala na akaanzisha Chama chake kingine na kuondoka na baadhi ya wafuasi kutoka Chama tawala. Katiba yao inawaruhusu kufanya hivyo na kuendelea kushikilia madaraka ya Urais! Kuna mifano mingi ya namna hii katika mataifa mengi.
Nini Kifanyike
Kwa hapa Tanzania, umekuwa ni ushauri wangu tangu zamani kwamba Rais ASIWE mwenyekiti wa Chama. Hii itasaidia uwepo wa mwenyekiti na uongozi tofauti katika chama kuweza kufuatiliana na kutaathimini kwa karibu utendaji wa Rais katika kutekeleza ilani ya Chama na kuweza kumshauri, kumuonya, kumkemea na hata kumuadhibu kisiasa ndani ya chama.
Hoja yangu hii inatiwa nguvu zaidi na jinsi ambavyo Rais wetu wa Sasa Kikwete J. M. ameonesha uwezo mdogo sana wa kukimudu chama tawala na Serikali kwa wakati mmoja. Changamoto nyingi sana zimeibuka chini ya utawala wake ndani ya chama na kitaifa kwa ujumla.
Changamoto hizi zilikuwa fursa kubwa sana kwake kuweza kutumia vizuri hizo kofia mbili ya kuthibitisha kwamba alistahili kuwa nazo zote - lakini kwa bahati mbaya ameonesha kushindwa kwa kiasi kikubwa sana.
Nashauri Kikwete aachie au anyang'anywe (kama hayuko tayari kuachia) Nafasi ya Uenyekiti wa Chama ili kutoa nafsi kwa mtu mwingine kukisimamia Chama katika shughuli zake za kila siku na yeye abaki na madaraka ya urais kwa ajili ya kutekeleza ilani na awe anatoa ripoti na kuwajibika kwa Chama kilicho chini ya mwenyekiti ambaye sie yeye - na utaratibu huu uendelee hivyo kwa wagombea na Marais wajao - bila kujali chama.
Naamini mgawanyo huu utasaidia kuongeza ubora wa utendaji na uwajibikaji - japo pia kunaweza kuwa na hatari za mgawanyiko kama ilivyotokea Malawi.
Wasaalam.... //msb
N.B: Maoni haya ni yangu binafsi, yaliyojengwa katika ufahamu wangu wa masuala ya siasa na utawala na hayahusiani na kundi au kambi zozote ndani ya chama changu cha mapinduzi.
Nadhani hapa tuwe makini, suala siyo "fulani", suala ni "structure and authority in realtion to our contemporary Africa, against the political will and the hidden agenda/motive behind the opinion in general". Msimamo wa wataalamu (ambao nauunga mkono) ni kuwa Africa kwa sasa siyo vyema sana kutenganisha authorities/powers kwa kiwango hicho, bado haijafikia hasa upeo wa utashi wa kisiasa wenye kuwezesha kuwa na separation kama hiyo without kuathiri amani. Kuna gap kubwa, hasa kwa hulka ya viongozi wa Africa kwa sasa, ambapo hata kuheshimiana tu ni suala gumu. Ni vyema powers zikabaki kwa one source kuliko kuzitapanya, athari zake ni mbaya sana. Tusiwe wepesi kudaka mambo tutakayoshindwa kuyahanlde. Tufanye utafiti mpana sana.
ReplyDelete