Thursday, October 6, 2011

CCM Na Ushindi wa Vijijini!

Kama ilivyokuwa mwaka jana mwanzoni mwa Novemba, kitimtim cha Uchaguzi kimetulia, zamu hii ilikuwa ni Igunga! Jambo lingine muhimu sana katika kusoma na kuelewa mwenendo wa upepo wa kisiasa, ambalo lilijitokeza sana kwenye Uchaguzi wa mwaka jana limejitokeza tena – Ushindi wa CCM umetegemea kwa kiasi kikubwa sana “Kura za Vijijini!”.

Tuvichambue Vijiji

Katika nchi karibu zote duniani (ukiacha nchi chache zilizoendelea), vijiji au wanavijiji huwa na hueleweka kuwa ni wenye sifa kuu zifuatazo:

  •           Wasiosoma (sana)
  •           Wasio na Ufahamu wa mambo mengi yanayoendelea katika dunia ya sasa (current/contemporary issues)
  •           Wenye upeo mdogo wa kifikra na kiufahamu
  •           Maskini
  •           Walio nyuma kisayansi na kiteknolojia
  •           Wasio na Ufahamu mkubwa wa masuala ya kitaifa (achilia mbali kimataifa)
  •          Wagumu na wazito wa kupokea mabadiliko
  •          Wanaodharauliwa au kutengewa na jamii nyingine (hususan za mijini)
  •           Wanaojidharau wenyewe
  •           Wasio na elimu ya Uraia – haki na wajibu wao

Sifa hizi nyingi – labda sio zote – pia zinafanana na wanavijiji wa Tanzania.
Mazingira wanayosomea Watoto wa Vijijini ambao baadaye huja kuwa
Wapiga kura Huathiri Sana Uwezo wao wa kuelewa na kupambanua
bado hata wakiwa watu wazima

Wanavijiji vya Tanzania

Wana vijiji wengi wa Tanzania wanakaa katika vijiji ambavyo vilianzishwa na baba wa taifa vikijulikana kama vijiji vya ujamaa. Kutokana na sababu mbalimbali, watanzania wengi wanaokaa vijijini bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya wawe ni watu wenye elimu ndogo zaidi (ikilinganishwa na wale wa mijini), ni watu wasiopata taarifa nyingi za kila siku na mabadiliko ya taifa na dunia kwa ujumla kutokana na kutokuwa na vyanzo vingi vya habari kama Radio, Televisheni, Magazeti na Intaneti kama wa mjini.

Wananchi wengi wa vijijini Tanzania pia wanakabiliwa na changamoto ya kuwa na ufahamu mdogo sana wa uraia – haki na wajibu wao. Hii inachangiwa sana na mfumo wa elimu ambao hauweki msisitizo kwenye elimu ya uraia. 
Wanafunzi wa Mijini Wana mazingira mazuri zaidi ya kusomea ambayo
 huwasaidia kuwa na mtazamo mzuri zaidi, upeo na ufahamu wa kuwasaidia
kupamabanua mambo kuliko wa vijijini

Hii inamaanisha kuwa elimu ya uraia imebaki kwa kiasi kikubwa sana kuwa ni jukumu la wananchi wenyewe na liko mikononi mwa wananchi wenyewe kuelimishana wao kwa wao. 

Wingi, ukaribu na elimu walizonazo wakazi wa mjini vinawasaidia sana wakazi wa mijini kuamshana na kuelimishana wao kwao pasipo kuhitaji jitihada zozote za serikali – hali haiku hivi vijijini.

Ukosefu huu wa taarifa na maarifa unamaanisha watanzania wengi walioko vijijini wako nyuma kielimu, kiufahamu, kimaarifa na uwezo wak upambanua mambo. Ukosefu wa taarifa na maarifa haya muhimu ya kila siku unamaanisha kifikra na kimtazamo katika mambo mengi wananchi hawa wa vijijini wako nyuma sana pia.

Kuwa nyuma kitaarifa, kifikra na kimtazamo inamaanisha kuwa wananchi hawa wanaweza kudanganywa na kuhadaiwa kiurahisi, wanaweza kutishwa au kurubuniwa kiurahisi na kwa ujumla wao wenyewe wanaokuwa hawana uwepesi wa kupokea mabadiliko yoyote katika jamii na maisha yao.
Kwa wananchi Maskini, wenye elimu na uelewa mdogo wa siasa, uraia
na maendeleo, WALI MCHUZI unatosha sana kuwafanya wakampatia Mgombea Kura.

Wana Vijiji wengi wa Tanzania wanajua tuliko toka – Mkoloni, TANU, Ujamaa na hatimaye CCM ya Nyerere na Mwinyi kidogo. Wanachi wengi wa Vijijini hawajui tulipo sasa, mahali CCM ilipotufikisha, achilia mbali tunakoenda!

Siku wananchi hawa wakifanikiwa tu kufahamu TUKO WAPI kwa sasa na wakaelewa "realistically" TULIPASWA KUWA WAPI, hatima ya CCM itakuwa imefika!

Mifano halisi

Kuna wanavijiji wengi hadi leo hapa Tanzania ambao wanaamini Rais wa Tanzania ni Nyerere. Kwao, uchaguzi ukija, inatosha sana kuwaambia wachague chama cha Nyerere wakakichagua bila kuhitaji kusikiliza sera, kampeni, ahadi wala taarifa zozote za utekelezaji wa ilani zilizotangulia.

Ikitokea mpinzani akaenda “kuwadanganya” kwamba Nyerere amekufa, inatosha sana kuwaambia kuwa Nyerere amemweka “mtoto wake” agombee kwenye nafasi yake na wao wakamchagua “mtoto wa Nyerere”.

Mkoani Kagera, hususan wilaya ya Ngara, mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa Vyama vingi, wananchi wengi vijijini waliambiwa kuwa wakichagua “rais wa upinzani” atauawa na Jeshi ambalo ni la Chama cha Mapinduzi na kisha vita na mauaji ya wenyewe kwa wenyewe itaanza! 

Taarifa hii ilikuwa inatosha sana kuwafanya wananchi waichague CCM na kuvikimbia vyama vya Upinzani kama ukoma. Sababu ilikuwa ni moja kuu: kumbukumbu ya mauaji ya kikatili yaliyofanyika Burundi baada ya Mgombea wa Upinzani, Melchior Ndadaye, kushinda uchaguzi na kuuawa na jeshi la serikali ilikuwa bado mbichi sana katika macho, fikra na mioyo yao!

Taarifa za uvumi na uongo wa namna hii umekuwa ukitumika katika maeneo mengi sana hapa nchini – mara nyingi kwa ajili ya kukisaidia chama changu cha Mapinduzi - CCM! Kwa wote wanaotokea vijijini, tukipewa nafasi ya kutoa maoni, shuhuda nyingi sana za matukio ya namna hii yataelezwa hapa mtandaoni.

CCM Kukataliwa Mijini

Chaguzi za mwaka jana na mwaka huu zimezidi kuonesha kuwa Chama cha Mapinduzi kinazidi kukataliwa kila kukicha katika maeneo ya mijini hapa Tanzania. Kwa hali ya miji ya Tanzania, inamaanisha CCM inazidi kukataliwa na raia makini, wasomi, wasomi watarajiwa, wataalamu, weledi, wanazuoni, wachambuzi, wanaharakati, wafanyabiashara n.k.

Cha ajabu ni kwamba makundi haya ndiyo muhimu sana katika kuliendesha taifa lolote duniani! Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa na miji mingine mingi, CCM imeonekana kutokubaliwa kabisa – kwingi imeshindwa na hata pale iliposhinda ilikuwa ni jasho jingi – na “labda” hata kwa “mikakati mingine”!
Wananchi wa Mijini kwa kiasi kikubwa sana huelewa na  kuunga
mkono Sera na harakati za CHADEMA kuliko CCM. Pichani ni
Wananchi wa Igunga "Wakienda Sawa" na Mwenyekiti wa CHADEMA,
Mbowe, F.A

Katika uchaguzi mdogo wa Igunga, wanachama na mashabiki wengi wa CHADEMA walianza kushangilia ushindi mapema baada ya matokeo ya vituo vya mjini kutoka – walisahau kwamba ushindi wa CCM hutoka vijijini! Yalipotoka ya Vijijini – kilichofuata sote tunafahamu!

Mwanzo wa Mwisho wa CCM?

Victor Yanukovic, Rais wa Ukraine alipinduliwa na wananchi mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya kushinda uchaguzi kwa kupata kura nyingi za vijijini lakini wananchi katika miji yote wakagoma na kuandamana kutoka aondoke kwa tuhuma za wizi wa kura. 

Wananchi wa vijijini hawakumsaidia Yanukovic maana walikuwa hawajui hata kinachoendelea – zaidi ya yote kwamba hawakuwa na sauti ya kuwawezesha kusikilizwa. Victor Yanukovic alipinduliwa na kuondoka, Victor Yushenko aliingia Ikulu nak uongoza Nchi.

Tukiacha ushabiki na maelezo ya kujifariji, kitendo cha chama kukataliwa mijini ambako ndiko watu wana uelewa na ufahamu zaidi na badala kutegemea ushindi unaotoka kwa watu wasio na uelewa na upeo wa maamuzi wanayoyafanya ni wazi kuwa mwisho wa chama unakuwa umekaribia – TENA UMEKARIBIA SANA.
Mikutano ya CCM ambayo kwa miaka mingi ilikuwa inavutia
sana Wananchi, Siku Hizi Imeanza KUVUTIA ZAIDI WATOTO,
kama inavyoonekana hapo pichani. Mchambuzi mmoja alisema
watoto hawa hufuata muziki, kama wanacyofuata helkopta
kwenye mikutano ya CHADEMA!

CCM tuendelee kujifariji tu kwa sasa, lakini ukweli ni kwamba mwisho wa chama chetu umekaribia mno – KAMA SIO KWAMBA UMESHAFIKA. Hatua madhubuti sana zinahitajika ili kurudisha imani ya wananchi, wasomi na wenye uelewa watuunge mkono kama chama kuliko kuendelea kujisifia na kujifariji kwa kura za vijijini. 

KWA BAHATI MBAYA SANA – KWA SASA CHAMA CHA MAPINDUZI HAKINA KIONGOZI NA UONGOZI UNAOWEZA KUKISAIDIA KUIKABILI HII CHANGAMOTO – maandishi tayari yako ukutani!

CCM tukumbuke na tuukubali ukweli huu kuwa: “NI KHERI KUKEMEWA NA KUKOSOLEWA NA WENYE HEKIMA KULIKO KUSIFIWA NA KUTUKUZWA NA WAJINGA NA WAPUMBAVU!”…. kufurahia sifa unazopewa na wajinga ni ujinga uliopitiliza!
Mkala yangu ijayo naangazia tafsiri halisi ya CCM kukataliwa mjini…
Wananchi wengi wa Vijijini Huvutiwa sana "Unyenyekevu"
 unaooneshwa na Viongozi wa CCM wakati wa Kampeni pasipo kuelewa
kuwa haihusiani na Maendeleo. Pichani ni Kiongozi wa CCM
ikiwaomba kura WATOTO vijijini Igunga
(nadhani alikuwa amesahau kuwa WATOTO HUWA HAWAPIGI KURA)!

Sidhani kama kuna Chama hapa Tanzania kinachonufaika na Ujinga wa Watanzania kama CCM!

Wasalaam…. //mussa

No comments:

Post a Comment