Kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifuatilia Utendaji wa viongozi kadha wa kadha wa vyama vya siasa katika nafasi zao mbalimbali hapa nchini. Leo, nimeona nitafakari na kujiuliza kwa sauti maswali kadhaa kuhusiana na katibu mwenezi wa CCM - Kijana Nape Nauye!
Kuteuliwa kwake
Kijana huyu, baada ya kuhusishwa na tuhuma za kuwa mmoja wa waanzilishi wa CCJ na baadaye kutaka kujiunga na CHADEMA kabla ya kupewa ukuu wa Wilaya na hatimaye ukatibu uenezi wa CCM, aliibuka na kuwa mmoja ya watu "maarufu" na walioonekana kuwa na nguvu za kisiasa ambazo zinahitajika sana ndani ya Chama kama CCM. Kupewa kwake nafasi hii hakukutokana TU na haja ya kufanyika kwa mabadiliko katika Uongozi wa juu wa Chama hicho, bali haja kubwa zaidi ya CCM kuonesha kuwa na yenyewe inatambua na kuthamini uwezo na mchango wa vijana katika siasa zake - kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa - hususan CHADEMA na NCCR Mageuzi!
Kauli Zake Kisiasa
Kauli zake Nyingi haziendani na Nafasi yake Kichama na Kitaifa |
Kwa bahati mbaya sana, matarajio yangu na ya watu wengi kwa huyu kijana yalianza kuingiwa na mashaka tangu katika hatua za awali kabisa za kuanza kwake kutekeleza majukumu katika nafasi aliyopewa. Baada ya kuanza kumsikiliza mambo anayoyazungumza na namna anavyoyazungumza nilianza kuhisi CCM inaweza kuwa imefanya makosa kumuamini kijana huyu kwa nafasi nyeti kiasi hicho ndani ya chama.
Siku 90 za Gamba
Mwanzoni kabisa mwa kazi yake, atakumbukwa kwa kuibuka na UONGO kwamba mkutano wa CCM Dodoma uliazimia kuwavua "gamba" baadhi ya wanachama wake ambao walikuwa wanatuhumiwa kuwa mafisadi hapa nchini, iwapo wanachama hao hawatajiondo wenyewe ndani ya Chama hicho ndani ya Siku 90. Baadaye ilikuja kubainika kuwa kijana huyu alikuwa anadanganya baada ya katibu Mkuu wa Chama hicho Mukama kukanusha mbele ya waandishi wa habari kuwa suala la siku 90 halikuwemo katika maazimio ya mkutano huo - na baadaye mwaka huu kusema kuwa chama hicho hakitamfukuza mwanachama yeyote katika mpango huo wa kujivua gamba.
Matumizi Mabaya ya Madaraka
Pamoja na hayo, Nimekuwa nikishangaa namna ambavyo Nape amekuwa akitumia majukwaa ya mikutano ya hadhara ya Chama "kuwasimanga" baadhi ya wanachama wa chama hicho kwa tuhuma mbalimbali husususan za Ufisadi - mambo ambayo kimsingi yalitakiwa kujadiliwa kwenye mikutano ya ndani ya chama na kufanyiwa maamuzi huko.
"Nape Anaigeuza CCM kama Mali yake" - Makamba! |
Wakati fulani pia niliwahi kusikia Lowassa alilalamika kwenye mkutano mmojawapo wa CCM akihoji ni kwa nini baadhi ya viongozi wa chama wanatumia rasilimali na mikutano ya hadhara ya Chama kumchafulia jina kwa tuhuma ambazo zilipaswa kujadiliwa kwenye vikao!
Nilienda kujiuliza iwapo Nape alikuwa amekomaa kisiasa kiasi cha kumtosha kushikilia Nafasi hiyo nyeti kwa Chama cha Mapinduzi, hususan katika wakati huu mgumu sana kisiasa kwa chama - kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake ya miaka 35!
Kutumia Majukwaa kuongelea mambo yaliyopaswa kuwa kwenye Vikao! |
Baadhi ya kauli za Nape! |
Kwenye Mitandao ya Kijamii - hususan Facebook - ambapo kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifuatilia "post" zake, ndizo zilizonifanya zaidi kufikia hatua ya kuandika hii makala. Kiukweli ni kwamba Facebook ni mahali pa wazi ambapo kila mtu ana uhuru wa kuandika chochote anachoona kinafaa bila kujali wengine watachukuliaje - hususan iwapo hajamtukana mtu au taasisi fulani. LAKINI, kama ilivyo sehemu nyingine yoyote, maneno anayoyasema mtu athari yake huwa haitegemei TU ni nini alichokisema - BALI NI NANI ALIYESEMA!
Ukweli ni kwamba Post nyingi za Nape zimekuwa zikionesha aidha UCHANGA wa hali ya juu kisiasa au UJINGA wa hali ya juu Kisiasa! Maandishi yake mengi huonesha zaidi dhamira ya kuwafurahisha "mashabiki" ambao wako tayari kushabikia kauli yoyote inayotoka kwa kiongozi wao, pasipo kujali Ubora wa kauli hiyo, zaidi kwa kuzingatia nafasi aliyo nayo mtoa kauli.
Kauli ya Kiongozi wa Kitaifa kwa Umma! |
Ushauri wangu kwa Nape
Kwanza kabisa, ni muhimu kwa nape kufahamu tofauti ya kauli za kuongea na za kuandika. Kuna kauli ambazo mtu yeyote anaweza akaziongea, hususan anapokuwa na marafiki zake wa karibu - ambazo hata kama ni mbaya zitaishia hapo hapo, kwa hao hao, na hazitakuwa na athari na kwa jamii pana kwa ujumla.
Hii ni kwa sababu mtu anapondika, msomaji yeyote huelewa kwamba huyu mwandishi ametafakari kwanza jambo la kuandika, kisha akaliandika, kisha akalisoma tena na kujiridhisha na ubora wa kile alichokiandika kabla ya kuki-share na umma kwa ujumla. Hivyo kauli nyepesi ambayo ingeweza kuchukuliwa kwa wepesi katika mazungumzo, huweza kuchukuliwa kwa uzito mkubwa inapokuwa imetolewa kwa umma - hususan kwa maandishi!
Pili, Kuelewa Umuhimu wa Nafasi yake kwa Chama na kwa taifa kwa ujumla. Kama nilivyoelezeahapo juu, Wasomi na viongozi wanaowajibu wa kuwasaidia wananchi walio wengi wasio na ufahamu na maarifa ya siasa na uongozi kuelewa ni yapi masuala sahihi na ya muhimu katika taifa letu - na yapi ni masuala ya kishabiki tu ambayo hana nafasi wala tija katika kulisaidia taifa na vyama vya siasa kwa ujumla.
Wananchi wasio na uelewa na maarifa ya uongozi na siasa wanapoona kauli nyepesi na zisizo na tija kwa taifa zinatoka kwa viongozi wakubwa kitaifa, na wao huingiwa na hisia kwamba kumbe yale waliyokuwa wanadhani sio ya msingi - ndiyo ya msingi hata kwa taifa - HUU NI UPOTOSHAJI! Taifa lenye changamoto na umaskini mkubwa kama Tanzania linahitaji Viongozi walio serious zaidi na Masuala nyeti ya Kitaifa na sio watu wanaotafuta umaarufu kwa "Cheap Politics" (umaarufu wa dezo / gharama nafuu)!
Kuendelea Mbele
Wakati Ole Millya anaondoka CCM, Nape alielezea kuwa kitendo hicho ni kizuri kwa sababu Millya alikuwa MZIGO MKUBWA kwa CCM! Nachelea kwamba Nape asipoangalia vizuri mwenendo wake Kisiasa, atajikuta na yeye ANAKUWA MZIGO MKUBWA pia kwa CCM!
CCM kwa sasa inakabiliwa na Changamoto kubwa sana ya Sura yake machoni pa wananchi. Kashfa nyingi za Viongozi na Wanachama wake kuhusiana na vitendo vya Ufisadi na kuhujumu serikali na uchumi wa taifa zimekichafua sana Chama cha Mapinduzi machoni pa watanzania wengi.
CCM kwa sasa inahitaji kuweka mbele viongozi wanaoweza kuongea na kuwasiliana na wananchi kwa hekima busara ya hali ya juu, ili kurejesha imani ya wananchi walio wengi kwamba Chama hicho bado kina viongozi wenye Hekima, Busara na Dhamira safi ya kiuongozi, na hivyo waendelee kukiamini kama chama kinachoweza kuendelea kuliongoza taifa hili. Tofauti na hapo chama kitazidi kudidimizwa na mwisho wake utakuwa mbaya zaidi kuliko hata sasa!
Nape asipokuwa makini atakuja kuwa MZIGO kwa CCM hivi Karibuni! |
point noted
ReplyDeleteNape ni mzigo ccm na anakimaliza chama chake,
ReplyDeleteto a wise only a word is enough
ReplyDeleteAnaaibisha vijana kwa kujiingiza kwenye siasa za kishabiki
ReplyDeleteNimeipenda sana hii makala mwandishi alitulia sana,tatizo la huyu jamaa ni sifa tu
ReplyDelete