Friday, May 18, 2012

UDHAIFU wa CCM!


Leo Nimeona nitafakari kuhusu Udhaifu wa Chama cha Mapinduzi - Chama ambacho kimeitawala Tanzania tangu kilipoundwa hadi leo. Kwa maana hiyo, ndio chama pekee ambacho kimekuwa na fursa ya kuweka mipango ya kuiendeleza hii na kuitekeleza huku kikiwa na mamlaka kubwa ambayo haiathiriwi na upinzani (katika kufanya maamuzi makuu ya kitaifa). Pamoja na makubwa na Mazuri yote ya Chama hiki hakijapungukiwa udhaifu na mapungufu. Baadhi yake ni pamoja na haya:

"Kukosa Uongozi"

Nadhani hakuna tatizo kubwa ambalo linakikabili Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka kadhaa mfululizo sasa kama kutokuwa na Uongozi. Ni muhimu kuelewa tofauti ya mtu kushika nafasi ya Uongozi na mtu huyo kuwa kiongozi. Kiongozi hapimwi kwa nafasi anayoishikiria  katika taasisi - bali kwa yale anayoyafanya kwa kuitumia hiyo nafasi.

Katika ngazi ya kitaifa, CCM imekuwa na Ombwe la Kiuongozi tangu Mkapa aondoke Madarakani - jambo ambalo ndilo limechangia kwa kiasi kikubwa sana mitikiiko mingi ambayo imekikumba chama katika miaka zaidi ya 6 iliyopita!


Viongozi wa CCM Kikaoni

 Matatizo na misuko-suko mingi ambayo imeipata CCM na taifa kwa ujumla katika miaka kama 6 iliyopita imechangiwa kwa kiasi kikubwa sana na kukosekana kwa Uongozi wenye uwezo wa kufanya yale yanayotakiwa katika Chama hicho (na hatimaye taifa - kwa sababu Chenyewe ndicho kina dhamana ya kuongoza Serikali na taifa pia).


Matatizo hayo mengi yamekua na kuonekana kuwa na makubwa ndani ya Chama na hata katika taifa pia kutokana na Chama kutokuwa na Uongozi wenye uwezo wa kuona na kupambanua matatizo yakiwa bado madogo na katika hatua zake za awali, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa sana matatizo hayo madogo kuendelea kukua pasipo kushughulikiwa ipasavyo na uongozi wa juu wa chama hivyo mpaka pale yalipotoka nje ya chama na hivyo yakawa makubwa zaidi hata kuyashughulikia ndani ya chama!

Kuwashindwa Maadui wa Taifa!

baba wa taifa Mwl. Nyerere wakati ule alipenda kuelezea kuwa maadui wakubwa wa taifa la Tanzania ni Umaskini, Ujinga na Maradhi. Kwa maana hiyo, jukumu kubwa la Serikali na taifa kwa ujumla ilikuwa ni kupambana na maadui hawa watatu!
Miaka 50 ya Uhuru: Darasa Nchini Tanzania!
Kwa bahati mbaya sana, miaka 35  mfululizo ya CCM kuliongoza hili taifa sio tu kwamba imeshindwa kulisaidia hili Taifa kuwashinda na kuwatokomeza maadui hao, bali wamezidi kuimarika kwa njia tofauti-tofauti. Ahadi nyingi za CCM nyakati za uchaguzi na katika hotuba mbalimbali zimekuwa zikionesha kwamba CCM inatambua changamoto zilizopo na inajua ni nini kinaweza kufanyika ili kukabiliana na changamoto hizo. 

Tatizo limekuwa katika uwezo mdogo wa CCM kuweka mifumo sahihi ya utekelezaji wa mipango na mikakati inayowekwa na kuisimamia ili kuhakikisha kuwa mipango na mikakati hiyo inazaa matunda yanayotakiwa. matokeo yake maadui hao wameendelea kuimarika na kwa Upande wa CCM, Chama kimeendelea kujiimarisha katika kubadilisha ahadi, kauli mbiu na (kwa lugha ya Waziri Mwakyembe) - Ngonjera za kuhalalisha kuendelea kuwepo kwa matatizo hayo!

Kuzalisha / Kulea Maadui wengine wa Taifa!

Kiukweli, sio tu kwamba CCM imeshindwa kuwatokomeza maadui wa Taifa katika miaka 35 ya kutawala kwake, bali uwepo wa CCM madarakani umeshuhudia kuzaliwa na kukua kwa maadui wengine ambao mwanzoni hawakuwepo - kwa viwango vya sasa!
(Maneno yaliongezwa na mwandishi)
UFISADI: Chini ya CCM taifa limeshuhudia kuibuka kwa Ufisadi na uhujumu mkubwa wa Rasilimali za Taifa (Fedha na Mali) kupita katika wakati mwingine. Mbaya zaidi, UOVU huu mkuu ambao unafanyika hadi sasa ndani ya Taifa letu aidha Unafanyika Serikali (Chini ya Dhamana ya CCM) au nje ya Serikali ambapo hata huko, Wanachama wengi na VIONGOZI wa CCM ndio wanaoongoza kwenye Orodha ya Washukiwa wa Maovu hayo!

Kama vile haitoshi, mara kadhaa Chama cha Mapinduzi kimekuwa mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea Washukiwa wa vitendo vya Ufisadi na Uhujumu mwingine wa taifa - japo mwishoni wamekuwa wakibainika kuwa ni wahusika katika maovu husika. Vitendo hivi vimezidi kuongeza hisia miongoni mwa Watanzania wengi kwamba kwamba CCM inaweza kuwa inahusika aidha moja kwa moja au kwa njia nyinginezo!

UJINGA:  Chini ya Serikali ya Awamu ya Nne ya CCM chini ya Kikwete, kwa mara ya kwanza tumeshudia Maelfu ya Wanafunzi wa Shule za Msingi WASIO JUA KUSOMA WALA KUANDIKA ETI wamafaulu kwenda Sekondari! Ufisadi hadi katika Elimu - Chini ya Serikali ya CCM! Zoezi Dogo tu la NIDA mwaka huu limebainisha kuwepi kwa Wanajeshi "FEKI" takribani 1,000 katika majeshi yetu - Chini ya Serikali ya CCM!!!
Jairo akipokelewa kwa shangwe Ofisini!
Kiukweli, hali ikiendelea hivi, CCM itakuja kuwa ni mojawapo ya maadui wa Taifa hili pia!

Chama Cha Mapinduzi sio tu kimeruhusu Ufisadi kulivamia hili na kuliathiri Vibaya bali hata Chama chenyewe pamoja na kuukumbatia Ufisadi, ni wazi kwamba Umekiathiri vibaya. Chaguzi nyingi za ndani ya CCM zimekuwa zimetawaliwa na Ufisadi/Rushwa kiasi kwambani vigumu kupata viongozi bora hata ndani ya Chama hicho. Mbunge wa Nzega CCM alisema hivi: "Mnaotamani Kugiombea nafasi za Uongozi Tanzania andaeni mafungu ya hela kwanza...  somo nililopata kutoka uchaguzi wa East Africa Legislative Assembly. Waliopata bila kutoka hela ni wachache sana!!!"

Kutegemea "Ujinga"

Ni ukweli usiopingika kwamba jamii kubwa sana ya Watanzania - hususan wanaoishi mbali na maeneo ya mijini (vijijini) - ni wajinga sana wa masuala ya siasa na uongozi. Ujinga kwa maana ya kutokuwa na Uelewa na maarifa ya masuala husika.

Wananchi wengi wa vijijini walikifahamu Chama cha Mapinduzi tangu enzi za Nyerere na kwa misingi hiyo, waliamini CCM ndio chama cha Nyerere. Imani waliyokuwa nayo kwa Nyerere imani hiyo hiyo waliiunganisha na Chama cha Mapinduzi - wengi pasipokujua kuwa kuondoka kwa Nyerere kulimaanisha mabadiliko makubwa sana katika Chama hicho. Na wengi hawafahamu bado kwamba CCM ya Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea sio hii CCM ya wawekezaji tuliyo nayo leo. Hayo yote, Achilia mbali wananchi wengi wapiga kura ambao bado wanaamini kuwa Nyerere ndiye Rais wa Nchi hii mpaka sasa au kwamba ndiye kiongozi wa CCM hadi sasa!
CHADEMA ina nguvu zaidi Mijini
Kama kuna chama hapa Tanzania ambacho kinanufaika sana na Ujinga wa wananchi- hususan nyakati za Uchaguzi - ni CCM! Ni kutokana na utegemezi wa "ujinga" wa wananchi ndio maana kila mahali ambapo wananchi wamekuwa wakipata mwangaza wa masuala ya Siasa na Uongozi kutoka kwa vyama vya Upinzani - hususan CHADEMA - wamekuwa wepesi wa kutaka mabadiliko ukilinganisha na katika maeneo ambako vyama vya Upinzani havijajikita sana - hususan vijijini! 

Maana yake ni kwamba Ushindi wa CCM vijijini hautegemei sana Ubora na Kupendwa kwa chama hicho katika maeneo hayo - bali zaidi kwa sababu wakazi wengi wa maeneo hayo bado hawana mwangaza wa maarifa mbadala ya siasa na uongozi. Hii inamaanisha kwamba siku vyama vya Upinzani vikijipenyeza na kujiimarisha sana katika maeneo ya vijijini ambako kwa sasa ndio ngome kuu ya CCM, basi CCM itakuwa katika hali ngumu zaidi kisiasa, kama sio kwamba itapotezza nguvu yake ya kuiongoza nchi. Maelezo zaidi kuhusiana na utegemezi wa CCM kwa wanachi wa vijijini na wale wasio na ufahamu na maarifa ya siasa yapo katika makala ya UDHAIFU wa CHADEMA unayoweza kuisoma hapa: http://msbillegeya.blogspot.com/2011/11/udhaifu-wa-chadema.html
Shule kijijini
Wakati wa Uchaguzi mdogo wa Igunga ambapo CCM ilishinda, Mbunge wa Nzega, Kigwangalla wakati matokeo ya awali ya vituo vya maeneo ya mjini huko Igunga yalipokuwa yanaonesha CHADEMA inaongoza, alieleza kuwa ngome ya CCM iko vijijini na hivyo watu wasubiri matokeo ya Vijijini ndipo wajuo mshindi ni nani - na kweli matokeo ya vijijini yalipoanza kuingia, mwishoni mgombea wa CCM alitangazwa mshindi (Japo kuna kesi ya kupinga matokeo hayo mahakamani hadi sasa)!!

Katika chaguzi kadhaa zilizopita, CCM ilichagua pia kuwakataza wagombea wake kwenda kwenye Midahalo ambako wangekutana na watu weledi na kuhojiwa maswali na kutakiwa kuyajibu hadharanani huku wakikabiliana na wapinzani wao! Badala yake wagombea wa CCM walichagua kwenda TU kwenye mikutano ya hadhara ambako HAWAULIZIWI Maswali na badala yake wanashangiliwa muda wote na mashabiki wao pasipo kuhojiwa! Siasa hizi zitakufa hivi karibuni katika karne hii ya 21!

Kushindwa Kujisafisha!

Changamoto nyingine kubwa ambayo inaikabili CCM kwa sasa ni kutokuwa aidha na UWEZO au NIA ya kujisafisha yenyewe! Pamoja na kwamba suala hili linahusiana na uwezo na nia ya uongozi, lakini lina mapana zaidi ndani ya chama yanayowagusa hata wanachama.
Waliitwa "Mapacha 3": Bado ni Wana-CCM!
Tangu kubadilishwa kwa Uongozi wa juu wa CCM, matarajio ya watu wengi yalikuwa ni Chama kuanza kujipanga vizuri na kujiimarisha kuanzia ndani - lakini hali haijawa hivyo! Kutuhumiana ndani ya Chama na kusimangana kwa wanachama na viongozi majukwaaani kumezidi badala ya kushughulikiwa ndani ya Chama!

Kwa upande mwingine, jitihada nyingi za Viongozi hao - hususan katibu mwenezi - zimelenga katika kulumbana na kujibizana vyama vya Upinzani - Hususan CHADEMA - japo ukweli ni kwamba Tatizo kubwa la CCM kwa sasa SIO CHADEMA wala vyama vya Upinzani - ni Uozo uliomo ndani ya Chama chenyewe!

Chama kilipotoa ahadi wakati fulani ya Kuwaondoa kundini wanachama wanaotuhumiwa kuwa Mafisadi ili kuongeza imani ya wananchi kwa chama, Imani ya wananchi wengi kwa CCM ilianza kuongezeka - kwa kuamini kuwa sasa CCM inaweza kurudia enzi zake za Ubora na Usafi! Ahadi hizo ziliishia kuwa ni "danganya-toto" ya kisiasa, kwani watuhumiwa wanaendelea kuwa ndani ya chama na kushika nafasi zai ndani ya chama. MBAYA ZAIDI, wanachama wanatoa kauli za kutaka mabadiliko au wanaojiondoa kwenye chama kama ishara ya kuonesha kutoridhishwa na kufugwa kwa maovu ndani ya chama ndio wamekuwa wakiitwa "Mzigo" wakati mwingine "magamba"!

Kutegemea "Wazee"

Udhaifu mwingine mkubwa kwa CCM imekuwa ni kutegemea "Wazee". Ukweli ni kwamba watu wengi waliokuwa wanaifahamu CCM enzi za Nyerere iliwawea vigumu kuamini kwamba kuna chama kinaweza kuwa Bora zaidi ya CCM kwa hapa Tanzania.

CCM ililijua hilo na kujenga imani kwamba itaendelea kuwa na wafuasi wengi kwa sabau "wazee" wengi walikuwa katika Chama hicho. Ukweli ilianza kubadilika hivi karibuni baada ya kizazi kipya cha Vijana waliozaliwa au waliopata akili Wakati tayari kuna mfumo wa vyama vingi ambao hawakutaka kuitambua tena CCM kama "godfather" katika Siasa za Tanzania - na badala yake walikiona kama chama kingine tu - na mbaya zaidi - cha wazee na ambacho hakitaki mabadiliko.
Katibu Mkuu CCM
CCM ina kazi kubwa sana kwa sasa kuendelea kujionesha kuwa ni chama ambacho kinaweza kuwa na vijana na kukubali mawazo mapya ya mabadiliko kutoka kwa vijana na SIO kuendelea kukumbatia "ukale" ETI kwa sababu tu ndivyo "wazee" wanataka! Mabadiliko katika Uongozi wa CCM ambayo yamewapatia Vijana nafasi za juu za uongozi zingeweza kuwa ni hatua nzuri kwa chama hicho - iwapo vijana hao wasingekuwa "wanahujumiwa" na Wazee kwenye Utendaji wao ndani ya Chama!

N.B: Uzee sio lazima uwe ni wa Umri, unaweza kuwa ni Uzee wa Fikra (kijana akawa na umri mdogo lakini fikra na aidolojia zake zikawa za kizee)!!

Kuendelea Mbele...

Kiukweli, CCM imekuwa na muda mrefu mno wa kuweza kuongoza nchi na kuonesha kwamba inastahili kweli kuwa na hiyo nafasi muhimu kwa taifa. Kwa bahati mbaya sana Chama hicho kimetumia vibaya sehemu kubwa ya muda huo, na badala ya kulisaidia taifa kukabiliana na Changamoto na matatizo yake - CCM yenyewe kwa sasa inazidi kuonwa na wengi kuwa na yenyewe ni mojawapo ya Matatizo yanayolikabili hili taifa!
Mwenyekiti wa CCM!

No comments:

Post a Comment