Friday, May 25, 2012

KUTOA MIMBA: Daktari Apigwa Faini kwa Kushindwa Kutoa Mimba!

Katika hali iliyowashangaza watu wengi, Daktari mmoja katika kisiwa cha Mallorca nchi Hispania ameshindwa kesi iliyokuwa inamkabili katika mahakama mjini humo. Katika Kesi hiyo, Daktari huyo alikuwa anakabiliwa na shitaka la kushindwa kutoa mimba ya binti mmoja miaka kama miwili iliyopita.

Tukio Lilikuwa hivi

Miaka kama miwili iliyopita, binti mmoja alienda kwenye hospitali ya daktari huyo kwa minadhiri ya kutoa mimba aliyokuwa nayo yenye umri wa majuma saba. Baada ya daktari kumfanyia “upasuaji” wa kutoa kiumbe (mtoto) kilichokuwa tumboni mwake.
Wiki mbili baadaye binti huyo alirudi hospitali kwenda kufanyiwa vipimo na daktari huyo huyo ili kuona afya yake inaendeleaje ambapo daktari  huyo alimwambia kuwa mimba ilikuwa imetoka kama kawaida na kwamba afya yake ilikuwa inaendelea vyema. Binti huyo aliondoka na kurudi nyumbani kuendelea na maisha yake ya kila siku.

Kwa nini alitaka kutoa Mimba

Binti huyo alitaka kutoa mimba kwa sababu alikuwa bado anaishi na wazazi wake nyumbani na ambao ni wakali sana kwake hivyo alikuwa na wasiwasi kuwa wangetambua kwamba ni mjamzito wangeweza kumkaripia na hata kumuadhibu kwa kupata mimba kabla ya kuolewa na akiwa anaishi na wazazi wake.

Nini kilitokea

Miezi (5) tano baadaye, baada ya kuendelea kuona mabadiliko katika mwili wake – ambayo alidhani yalitokana na kutoa mimba, binti huyo alienda tena kwenye hospitali nyingine kupima afya yake na ndipo alipogundulika kuwa alikuwa na mimba ya zaidi ya miezi sita!

Mimba “mpya” ilitoka wapi?

Baada ya kuwaeleza madktari kuwa alikuwa ametoa mimba kabla ya hapo, walipofuatilia wakakuta umri wa ile mimba ulikuwa unaendana ile mimba “iliyotolewa”. Hata hivyo, yeye baada ya kutoa ile mimba ya kwanza hakuwahi kujihusisha tena na kufanya mapenzi kwa sababu alikuwa anaogopa kufanya makosa tena kama yale ya kwanza.

Hofu ikazidi mara mbili

Baada ya kugundulika kuwa mjamzito, binti huyu sasa alikuwa na wasiwasi mara mbili. Kwanza, ule wasiwasi wa kwanza wa kuwajulisha wazazi na familia yake kwamba amepata mimba wakati bado hajaolewa na anaishi na wazazi wake nyumbani – na pili – hali ya kiafya ya motto huyo ambaye alishawahi kujaribiwa kutolewa kwa oparesheni!

Binti huyu ilibidi akabiliane na hofu  nzote kwa wakati mmoja sasa – kwanza kwa kuwa mimba ilikuwa tayari imeshakuwa kubwa, asingeruhusiwa kuitoa – hivyo ilibidi aikabili hofu ya kwanza ya kuwaambia wazazi na jamii yake kwa ujumla – aliwaambia!

Baada ya hapo akabaki na ile hofu ya pili! Binti huyu alikuwa na wasiwasi kwamba lile jaribio la kwanza la kuitoa ile mimba kwa oparesheni yawezekana lilihusisha kukata sehemu ya “mwili” au “viungo” vya mtoto aliyekuwa tumboni hivyo kuwa na wasiwasi kwamba kama angezaliwa akiwa hai basi angekuwa mlemavu na hata kuwa upungufu mkubwa wa kimaumbile. Mimba iliendelea kukua na muda wa kujifungua ukafika – binti akajifungua MTOTO WA KIUME salama salimini!!!

Binti afungua Kesi

Baada ya kujifungua salama, binti huyu alimfungulia kesi ya madai daktari na hospitali waliomfanyia ule “upasuaji” wa kutoa mimba! Madai ya huyo binti yalikuwa makuu mawili:

Kwanza: Kudanganywa kwamba mimba yake ilitolewa salama na kwa usahihi wakati sio kweli. Pili: Makosa hayo ya daktari yalimsababishia msongo mkubwa wa mawazo (stress) kwa muda wote wa ujauzito wake na hata baada ya kujifungua, na Tatu: Hakuwa na uwezo wa kifedha wa kumlea huyo mtoto wa kiume!

Hukumu

Baada ya jopo la majaji kupitia maelezo na ushahidi wa pande zote mbili, mahakama ilimhukumu daktari huyo na hospitali yake kama ifuatavyo:
i.                     Daktari huyo aliamriwa na mahakama kumlipa mama wa mtoto huyo kiasi cha Dola Elfu Moja (1,000 USD)- Sawa na Shilingi Milioni Moja na Nusu kwa Mwezi za Tanzania – kila mwezi mpaka mtoto huyo atakapofikia umri wa miaka Ishirini na Mitano (25); na
ii.                   Hospitali ya daktari huyo imeamriwa kumlipa binti/mama huyo malipo ya jumla ya Dola za Kimarekani Laki Moja na Elfu Themanini (180,000 USD) – sawa na Shilingi Milioni Mia Mbili Sabini (270,000,000/=) za Tanzania!

Mwitikio wa Mawakili wa Pande husika

Wakili wa Upande wa Mlalakaji (mama wa mtoto) alisema hukumu ni nzuri na inatosha kwa mteja wake. Wakili wa upande wa Mlalamikiwa (daktari na hospitali yake) alisema watakata rufaa maana hukumu haikuwa ya haki.

ONYO: Utoaji wa Mimba ni DHAMBI, Ni Hatari kwa Afya yako na Ni Mbaya kwa Jamii yako Pia – USITOE MIMBA! 

"Kutoa Mimba Hakukufanyi uwe Binti ambaye hajazaa, bali kunakufanya kuwa “Mama wa Mtoto aliyeuawa kwa Amri ya Mama yake!”" Mussa Billegeya

No comments:

Post a Comment