Tuesday, May 29, 2012
Zanzibar: KANISA Lininge LACHOMWA MOTO!
BAADA ya Kanisa la Assemblies of God kuchomwa moto katika vurugu zilizoanza mwishoni mwa wiki iliyopita, jana Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae nalo limechomwa moto.
Akizungumzia hali hiyo jana, kiongozi wa Kanisa hilo, Ambaros Mkenda, alidai kwamba Kanisa hilo lilichomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha uharibifu mkubwa.
Alidai Kanisa hilo lilichomwa moto jana saa 8.30 mchana na watu wanaohisiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, waliokuwa wakitoka katika Mahakama ya Mwanakwerekwe kusikiliza kesi ya wenzao waliokamatwa juzi.
Mkenda alidai kuwa watu hao waliwazidi nguvu walinzi wawili wa Kanisa hilo na kuvunja lango kuu la kuingilia ndani ya Kanisa na kuchoma moto na waliharibu madirisha na vifaa kadhaa vyenye thamani ya Sh milioni 20.
“Tunasikitika sana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika Kanisa letu ambalo lilikuwa tegemeo kubwa kwa wafuasi wapatao 2,000 wa eneo la Parokia ya Mpendae na jirani,” alisema Mkenda.
Mkenda alidai kuanzia juzi, viongozi wa makanisa mbalimbali waliwasilisha maombi yao Polisi kuhusu kupewa ulinzi katika nyumba za ibada, baada ya kupokea vitisho. Hata hivyo, Mkenda alidai ombi lao hilo halikutekelezwa na Polisi na uharibifu mkubwa ukatokea katika Kanisa la Assemblies of God la Kariakoo.
Wafuasi na waumini wa Kanisa hilo walikusanyika nje ya jengo hilo, huku vijana wakishikwa na hasira wakitaka kwenda kulipiza kisasi katika maeneo ya jirani wakidai wanawatambua vijana waliofanya vitendo hivyo.
Mmoja wa waumini wa Kanisa hilo ambaye ni mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Susan Kunambi alilazimika kuwatuliza wafuasi vijana wa Kanisa hilo waliopandwa na jazba wakitaka kulipa kisasi.
“Hakuna sababu ya kupandisha jazba na kutaka kufanya vitendo ambavyo vitasababisha hasara na uharibifu ... Kanisa siku zote linahimiza amani na upendo na si chuki,” alisema Kunambi.
Polisi walifika haraka katika eneo la tukio na kurusha mabomu ya machozi ili kutawanya makundi ya vijana waliojikusanya na wengine kurusha mawe.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alithibitisha kuchomwa moto Kanisa hilo na kusema ulinzi umeimarishwa katika baadhi ya maeneo ya nyumba za ibada yakiwamo makanisa. Baadhi ya mitaa ya Jang’ombe na Mwanakwerekwe njia zimewekwa mawe na vikundi vya vijana waliochoma mipira ya gari na kusababisha moshi mkubwa.
Vikundi marufuku Wakati huo huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepiga marufuku maandamano, mihadhara ya kidini na mikusanyiko isiyo na kibali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema hayo wakati akitoa taarifa rasmi ya SMZ baada ya vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Uamsho baada ya kukamatwa kwa viongozi wao wa kidini.
Aboud alisema Serikali haitakubali kuona kikundi cha watu wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kuvuruga utulivu wa nchi kwa kisingizio cha kudai mabadiliko ya Katiba na imani ya dini.
“Wapo watu wanataka kuona tunarudi nyuma katika kipindi cha fujo na vurugu za kisiasa...wakati huo umepita,” alisema Aboud. Kutokana na hatua hiyo ya Serikali, mihadhara na maandamano kuanzia sasa italazimika kupata kibali kutoka taasisi husika ikiwamo Polisi. Alitaka wazazi wakataze watoto wao kujishughulisha na ushawishi wa kufanya vitendo vitakavyohatarisha amani na utulivu wa nchi.
Utulivu wajirudia mjini Jana hali ya utulivu ilirejea kisiwani hapa ikiwamo Mji Mkongwe na sehemu za mitaa ya Ng’ambo, huku wananchi wakifanya shughuli zao za maendeleo na biashara bila matatizo.
Maduka na huduma za usafiri viliendelea kama kawaida huku wafanyakazi wa Manispaa wakifanya usafi ikiwa ni pamoja na kuondoa matairi ya magari yaliyochomwa barabarani katika vurugu za juzi.
“Tunasafisha barabara zilizoharibiwa na waandamanaji kwa kuchoma moto mipira ya magari,” alisema Ali Juma mfanyakazi wa Manispaa ya Mji wa Unguja. Kamishna Mussa alisema Polisi waliendelea kuweka doria katika maeneo mbalimbali ya mji kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ.
“Tutaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ikiwamo nyumba za ibada ili kuhakikisha hakuna vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema Mussa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alionya kuwa suala la amani na ulinzi wa raia na mali zao halina mjadala na kuvihadharisha vikundi vinavyohatarisha amani, kwamba vitapambana na mkono wa Dola.
Dk Nchimbi aliyekuja hapa ili kukutana na viongozi wa vikundi vya dini na mihadhara na Polisi, alisema athari ya kuvunja amani na utulivu ni kubwa na wananchi wa Zanzibar wanafahamu vizuri mazingira yalivyokuwa miaka ya nyuma.
Alitaka viongozi wa dini wajifunze sheria za nchi na kuzifuata na kuwataka wasihusishe Uislamu na vurugu na fujo kiasi cha kuhatarisha amani ya nchi.
Pia alitaka wananchi walioharibiwa mali zao kwenye vurugu na fujo kutoa taarifa Polisi kwa hatua zaidi.
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, alisema Polisi itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya nchi.
Watu 30 wakiwamo wafuasi wa Uamsho walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe kujibu mashitaka yakiwamo ya kuandamana kinyume cha sheria na ukorofi wa kuwashambulia polisi kwa mawe.
Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka katika makundi matatu tofauti; kundi la kwanza likiwa la viongozi wawili wa jumuiya hiyo; Mussa Juma Issa (57) na Mbarouk Said Khalfan (45). Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mohamed Ali Sheni ya kujikusanya kinyume cha sheria na kufanya maandamano ambayo yalianzia Uwanja wa Lumumba kupitia Msikiti wa Kwabiziredi na kumalizia uwanjani hapo.
Watuhumiwa hao walikana mashitaka na kupewa dhamana ya masharti ya Sh 300,000 kila mmoja kwa kiasi hicho hicho; walitimiza masharti na wako nje kwa dhamana hadi Juni 11 kesi yao itakapotajwa. Kundi la pili la watuhumiwa wengine sita walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Janet Sekihola ambayo ni ya uzembe, ukorofi na kushambulia polisi waliokuwa doria.
Watuhumiwa hao ni Abdulrahman Simai Khatib, Hashim Juma Issa, Martar Said Ramadhan, Mbwana Hamad Juma, Masoud Hamad Mohamed na Mohamed Juma Salum.
Kesi ya watuhumiwa hao iliahirishwa hadi Juni 11 itapotajwa huku baadhi yao wakitafuta wadhamini na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja kwa Sh 500,000.
Maimamu wawakana Jumuiya ya Maimamu na Mihadhara ya Jumaza, imesema waliofanya fujo na vurugu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi si wafuasi wao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Muhidin Zubeir Muhidin ambayo pamoja na jumuiya hiyo ndizo taasisi zinazojishughulisha na mihadhara ya dini ya Kiislamu ambayo hutoa elimu kuhusu marekebisho ya Katiba.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Shehe Zubeir alisema jumuiya hiyo haijatuma watu kufanya fujo, kwa sababu katika dini hiyo ni makosa mtu kuharibu mali ya mwenzake. “Tunataka Waislamu wote na wafuasi wa Jumaza na Uamsho kuacha fujo na kurudi nyumbani kusubiri hatma ya viongozi wao,” alisema Shehe Zubeir.
Serikali ya Marekani imesema matukio yaliyotokea kwa siku mbili Zanzibar yanaweza kuchafua taswira nzuri iliyowekwa na visiwa hivyo, katika uchaguzi mkuu uliosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutokana na ghasia zilizotokea visiwani humo na kusababisha Kanisa na gari la kiongozi wa Kanisa kuchomwa moto.
“Kudumisha mazingira ya amani visiwani Zanzibar ambayo yanaruhusu utalii na maendeleo kuna maslahi kwa Wazanzibari wote na hata wageni waingiao visiwani humo,” alisema Balozi Lenhardt katika taarifa yake iliyotolewa jana Dar es Salaam.
Alisema ni muhimu kwa kila mtu kujizuia na kulinda maisha na mali za watu wasio na hatia na aliunga mkono waliozitaka pande zinazozozana kushirikiana kuleta amani na utulivu katika visiwa hivyo.
“Tunatambua umuhimu wa mjadala wa kisiasa unaoendelea lakini tunavitaka vyama vyote kuendelea kuufanya kwa njia ya amani na kidemokrasia zaidi,” alisema Balozi huyo.
Aliongeza kuwa anakubaliana na anaunga mkono hatua za haraka zilizochukuliwa na viongozi waandamizi wa kisiasa waliojitokeza kushughulikia masuala yaliyosababisha matukio hayo ya kusikitisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment