Idd Simba |
Tausi Ally na James Magai MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) Ltd, Iddi Simba, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka manane, likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh2.4 bilioni.Mbali na Simba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, washtakiwa wengine ni Meneja Mkuu wa Uda, Victor Milanzi na Mkurugenzi wake Salim Mwaking’inda ambaye pia aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Sinza (CCM).
Baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Benny Lincoln kumaliza kuwasomea mashtaka yanayowakabili, aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na wanaomba kesi ipangiwe tarehe ya kutajwa kabla ya kupangiwa tarehe ya maelezo ya awali. Wakili Said El- Maamry anayemtetea Simba na mwenzake, Alex Mgongolwa waliiomba Mahakama impatie dhamana mteja wao hoja ambayo haikuwa na pingamizi kutoka kwa Lincoln ambaye alisema mashtaka yanayowakabili washtakiwa yanadhaminika.
Ili kujidhamini, Hakimu Mfawidhi, Ilvin Mgeta aliwataka washtakiwa kutoa hati ya nyumba na kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika, kila mmoja wao asaini bondi ya Sh500 milioni.
Baada ya kutolewa kwa masharti hayo, Simba aliwasilisha hati ya nyumba yenye thamani ya Sh8 bilioni na kuridhia wenzake waitumie kupata dhamana.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hati hiyo ya nyumba ni ya kiwanda cha Kays Hygiene Products Ltd, kilichoko Mikocheni eneo la Viwanda, Plot namba 23, kinachomilikiwa na Simba na mkewe Khadija.
Simba ni Mwenyekiti wa Taasisi ya mikopo kwa Wajasiriamali ya Pride (T) Ltd na Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam. Akisoma hati ya mashtaka jana Lincoln alidai kuwa Septemba 2, 2009 Dar es Salaam, Simba na Milanzi walikula njama ya kuchepusha fedha kinyume na Kifungu cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 11 ya 2007.
Lincoln alidai kuwa Simba na Milanzi walighushi barua wakionyesha kuwapo kwa kiwango zaidi cha fedha kwenye akaunti zote za benki za Uda wakati wakijua kuwa si kweli. Aliongeza kuwa siku hiyo hiyo, Simba na Milanzi kwa pamoja, walichepusha Sh320 milioni wakijifanya ni malipo ya awali ya mauzo ya hisa katika shirika hilo fedha ambazo walijipatia kutokana na nyadhifa zao.
Aidha, kati ya Septemba 3, 2009 na Machi 31, 2010, Simba na Milanzi wanadaiwa kujipatia Sh320 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Robert Simon Kisena wakijifanya ni sehemu ya malipo ya hisa za Uda. Lincoln alidai kuwa washtakiwa Simba na Mwaking’inda kati ya Septemba 2009 na Februari 2011, wakati wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya nafasi zao waliharibu hisa milioni 7,880,330 zisizotumika za Uda ambalo ni shirika linalomilikiwa kati ya Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh1,142,643,935 bila kufuata taratibu za zabuni kitendo ambacho ni uvunjwaji wa masharti ya Kanuni ya 63 (1) ya Ununuzi ya umma.
Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 9 na Februari 11, 2011 wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kugawanya hisa 7,880,330 zisizotumika za UDA kitendo ambacho ni uvunjwaji wa masharti ya vifungu vya ushirikiano katika kampuni na Kifungu cha 74 cha Sheria ya Makampuni Sura ya 212 iliyorekebishwa mwaka 2002.
Mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru, alidai kuwa Februari 11, 2011 washtakiwa hao walishindwa kuchukua tahadhari zinazostahili, walimuuzia Simon hisa milioni 7,880,303 zisizotumika za Uda kwa bei ya Sh1,142,643,935 bila kufuata utaratibu wa zabuni ambao ungeweza kutoa nafasi kwa mnunuzi kutoa ofa ya bei inayolingana na thamani ya hisa hizo, jambo ambalo liliisababishia Uda hasara ya Sh2,378,858,878.80.
No comments:
Post a Comment