Wiki iliyopita niliandika makala moja kuhusu mauaji ya kisiasa yanayozidi kushika kasi hapa Nchini. Tangu mwaka jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kuwa Viongozi na Wananchama wake 15 wameshambuliwa na kuuawa kikatili katika maeneo mbalimbali ya Tanzania!
Siku moja tu baada ya kuandka makala hiyo, Kiongozi wa CUF mkoani Pwani aliuawa kikatili nyumbani kwake - mbele ya familia yake - katika mauaji mengine ambayo yaliripotiwa pia kuwa ni ya kisiasa!
Tabia hii ya kutumia vitisho na mauaji kama njia ya kueneza propaganda za kisiasa inaonekana kuzidi kushika kasi hapa nchini, hususan katika wakati huu ambapo Chama cha Mapinduzi kinapitia wakati mgumu sana wa kisiasa - katika historia yake miaka 35!
Wakati ukweli ni kwamba vyama au watu wanatunga na kuratibu mauaji wanaweza kuwa wanafurahia vitendo hivyo na kudhani kuwa vitawafanikisha katika matakwa yao ya kisiasa, napenda kutoa tahadhari kuwa sidhani kama kuna, kikundi au watu ambao wako tayari kuendelea kuvumilia kunyanyaswa na kuuawa kisiasa katika nchi ambayo ni ya kwao!
Tukiendelea kufumbia macho mauaji haya katika hatua hizi za awali, siku sio nyingi yatazidi kujenga hofu na hatimaye chuki mioyoni mwa wananchi na wanasiasa walio wengi na hapo ndipo Kisasi kitakapoanza. Napenda kuwatahadharisha wale wanaotumia njia za vitisho na mauaji kuwa mafanikio wanayodhani kuwa wanayaona kwa sasa yanaweza yasidumu muda mrefu sana kabla waathirika kwa sasa hawajageuka nao kuwa washambuliaji!
Uwezo wa kudhibiti Uovu tunao tukiwa na Nia! |
Hali itakapofikia katika hatua hiyo ni wazi kuwa taifa litakuwa limepoteza mwelekeo kabisa sio tu kisiasa - bali kijamii na kiuchumi! Hata hivyo, kuna watu ambao wanapaswa kuchukua hatua SASA ili kuzuia wimbi hili la Uharibifu wa Kisiasa! Siku kisasi cha mauaji haya kitakapoanza, hawatalaumiwa watakaokuwa wakiyfanya mauaji hayo kwa kulipiza kisasi, bali Lawama NA LAANA zetu sote zitawaelekea wale walioacha kuchukua hatua mapema kukomesha uhalifu huo wa kisiasa!
Wito wangu kwa Kikwete na Serikali yako ni kwamba hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wauaji hawa na wote wanaoratibu mauaji hayo (japo hata wanunuaji wa viungo vya albino hawakukamatwa wala kuchukuliwa hatua yoyote)! Ninaamini kwa asilimia zote kwamba Serikali kwa kutumia vyombo vyake IKIWA NA NIA inaweza kuwabaini wote wanaofanya mauaji hayo na kuwadhibiti mapema!
Na Serikali ikiamua kuwaacha waendelee kufanya na kufanikisha uovu huo, basi isidhani kwamba wanaouawa leo wataendelea kuwa Wauliwa tu, kuna siku wataamka na kuanza kujibu. Wenye uwezo wa kuzuia hayo watalaumiwa iwapo hawatakuwa wamechukua hatua SASA!
No comments:
Post a Comment