Monday, May 28, 2012

Muungano: TUUZUNGUMZE au TUUVUNJE!


Ni hivi majuzi tu mwezi uliopita Muungano wetu umetimiza miaka 48, kama kawaida tulifanya Sherehe. Lakini ukweli ni kwamba kwa Sasa Muungano wetu unahitaji kuadhimishwa kwa kitu kingine zaidi ya Maonesho kwenye viwanja vya mipira, magwaride ya majeshi na hotuba zilizojaa nukuu za Nyerere na za Karume.
Kuzaliwa kwa Muungano
Muungano wetu umedumu kwa miaka yote hii katika mazingira ya usiri na ulinzi mkuwa mkubwa wa "mada" hiyo. Lakini ukweli ni kwamba, zama hizo zimepita.

Maswali kuhusu Muungano

Sheikh Karume
Muungano huu ni wa nchi mbili ambazo kabla ya kuungana zilikuwa huru. Katika mazingira ambayo hayafahamiki vizuri kwa Watu wa Nchi hizi mbili mpaka sasa - hususan vijana - nchi hizi ziliungana na kuunda Nchi Moja iliyokuja kuitwa Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania. Maswali mengi yaliyobaki tangu kuundwa kwa Muungano huu hadi leo ni pamoja na:
  1. Majadiliano baina ya Nchi hizi mbili ili ziungane yalifanyika wakati gani na kwa muda gani?
  2. Ni wajumbe wapi na wapi walioziwakilisha nchi hizi mbili katika majadiliano hayo?
  3. Ni yapi yaliyokuwa makubaliano ya mwisho baina ya pande hizi mbili?
  4. Makubaliano ya majadiliano ya pande hizo mbili yalijadiliwa na Wananchi wa Nchi husika (moja kwa moja au kupitia mabunge yao) na kuridhia kuunganishwa kwa Nchi zao?
  5. Nakala ya Mkataba/Makubaliano baina ya nchi hizi mbili yalifikishwa kwa wananchi na kusambazwa kwa uwazi ili waelewe misingi ya kuunganishwa kwa nchi zao?
  6. Nani anayenufaika Zaidi na Nani anayepoteza Zaidi kwenye huu Muungano?
Maswali haya yote - pamoja na mengine mengi - inawezekana katika nchi hii kuna watu wana majibu yake, lakini ukweli unabakia kuwa walio na hayo majibu ni wachache (kama wapo kweli). Kwa misingi hiyo Muungano tangu zama hizo mpaka leo umebakia ni kama kitendawili ambacho wananchi wengi hawawezi kukitegua. Na wengine wamefikia hatua ya kuamini kuwa Siri ya Muungano alikuwa nayo Nyerere na Karume (ambao walikuwa marais wa Tanganyika na Zanzibar kwa wakati huo) na sio Watanzania wote!

Mwisho wa Zama Umefika

Wanasiasa na viongozi wa Serikali kwa ujumla walijitihidi sana kwa miaka kuutunza, kuudumisha na kuulinda Muungano kwa njia mbali - kubwa ikiwa ni kutoruhusu ujadiliwe - na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini ni wazi kwamba Zama hizo za "Giza" kuuhusu Muungano zinapita kwa kasi - kama sio kwamba zimeshapita kabisa mpaka sasa!
Zanzibar: Wanawake Barabarani kutaka Muungano Upigiwe Kura!
Zama za kuulinda na Kuudumisha Muungano kwa kutumia mbinu ya kuuficha usijadiliwe waziwazi zimefikia mwisho wake sasa.

Mapinduzi ya Uarabuni Yamewaamsha Watanzania!

Watanzani wa leo - hususan baada ya kushuhudia "Mapinduzi ya Umma" katika nchi kadhaa za Kaskazini mwa Afrika na Uarabuni - leo hii wengi wao nao wanaamini kwamba jambo lolote linawezekana kwa nguvu za Umma, hata hapa Tanzania - NA INAWEZEKANA WAKO SAHIHI! Na huu ni ukweli usiopingika kwamba Hakuna Nguvu Duniani hapa inayoweza kuishinda Nguvu ya Umma - hata Serikali na Majeshi haziwezi kuzima nguvu ya Umma - Umma uliojiunga na Kusimama pamoja!


Mubaraka: nguvu ya Umma ilimng'oa


Ukiwa unaongoza watu kama hao, ni wazi kwamba unapaswa kuwa makini sana na mambo ambayo wao wanayataka au kuyaona ni ya kipaumbele na kuyapatia nafasi stahiki - badala ya kudhani unaweza kuwanyamazisha kwa "kujifanya" unashughulikia mambo mengine ambayo kwako ndiyo ya muhimu zaidi - UTAKUWA UNAJIDANGANYA!

Maswali yanayobaki

Utaratibu huu wa sasa wa "kuulinda na kuudumisha" Muungano unaweza kudumu iwapo tu Nchi ingeendelea kutawaliwa na CCM kwa Asilimia 100 siku zote (kutokana na sababu zinazojulikana). Lakini hilo kwa sasa hilo halipo tena! CCM Inazidi kupoteza majimbo na Ushawishi miongoni mwa raia kwa kasi kubwa kila kunapokucha. Vyama vyenye Upinzani vilivyojawa na hamu ya kuhoji kila Sera ya CCM ndivyo vinazidi kupata mvuto na kusikilizwa zaidi Nchini!

Sera za CHADEMA zinamaswali mengi kuhusu Muungano!
MOJA: Kwa Mfano, Iwapo CHADEMA Itachukua dola mwaka 2015 na ikaamua kuigawa nchi katika Majimbo kama sera yake inavyoelekeza kwa sasa, ZANZIBAR Itakuwa katika jimbo Lipi? Je, Itabakia ba hadhi yake ya Sasa ambayo hata hivyo haijulikani Vizuri - au kutakuwa na Badiliko?

PILI: Iwapo Jumuiya ya Afrika Mshariki Itaanzisha Shirikisho la Kisiasa (kuwa na rais Mmoja wa AM), Zanzibar itakuwa mgeni wa Nani chini ya huo Mfumo? (maana muundo wa Muungano wa Sasa hauko wazi katika hilo pia)!... na mengine mengi!


Dalili kutoka Zanzibar

Zanzibar Leo! - Tatizo ni Muungano!
Mambo yanayoendelea kwa sasa visiwani Zanzibar - kwa hakika ni ishara kubwa sana kwamba zama za kuulinda na kuudumisha Muungano kwa mbinu ya Ukimya imepitwa na wakati. Vurugu zinazoendelea kwa sasa huko Zanzibar - hususan zinapoanza kuhusisha hisia za Ubaguzi dhidi ya "wabara", ni wazi kwamba Siku sio nyingi zitaweza kuigia bara, na kundi la kwanza kutafutwa wanaweza kuwa Makamu wa Rais na Mawaziri kutoka Zanzibar - kabla ya kuingia mitaani na kuwageukia wapenmba waliojazana kwenye miji ya Tanganyika!


Katiba Mpya SIO Jibu!

Wakati vuguvugu la kudai katiba mpya lilipoanza kushika kasi mwishoni mwa mwaka juzi (wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu) na hatimaye Serikali ikazidiwa nguvu na Upinzani na kukubali Madai ya CHADEMA ya kuundwa kwa katiba mpya (ikumbukwe CCM haikuwa na Mpango wa Kuunda Katiba Mpya Tanzania wakati wa Awamu ya Pili ya Kikwete Madarakani), binafsi nilidhani kwamba hii ndiyo ingekuwa fursa muhimu sana kwa Serikali "kujivua lawama" za usiri na tatizo la Muungano kwa kuruhusu wananchi waujadili Muungano huu wakati wanajadili katiba mpya na kuutolea majibu! HAIKU WA HIVYO!

Uundaji wa Sheria ya Katiba Mpya bado ulighubikwa na "WOGA" ule ule wa miaka neda rudi, na hatimaye Suala la Muungano kuondolewa kwenye masuala yatakayojadiliwa! Ukweli ni kwamba hili NI KOSA, na kuna "mtu" atalilipia hili kosa!

Nini Kifanyike?

Ushauri wangu kwa Rais Kikwete na Serikali kwa ujumla ni kutambua na kufanya yafuatayo:
  1. Kwanza, ni muhimu kwa Kikwete na Serikali yetu ya leo kutambua kwamba Watanzania wa leo sio wa miaka ile ya Uhuru - au enzi za Nyerere! Watanzania wa leo sio watu unaoweza kuwaridhisha kwa "maneno mepesi" huku ukikwepa kujibu maswali yao Magumu?  Watanzania wengi wanataka waelezwe - kabla hawajashawishiwa kuendelea nao au kuuvunja - ni nani anayenufaika zaidi na huu Muungano na Nani anayepunjwa zaidi kwenye huu Muungano. Hili ni swali gumu ambalo linahitaji majibu magumu, zaidi ya zile hotuba ambazo tumezoea kuzisikia za kuuremba na kuupamba Muungano pasipo takwimu na Vielelezo!
  2. Serikali itafute njia nzuri ya kulileta Suala la Muungano katika mjadala wa Wazi wa Kitaifa. Kama nilivyosema hapo juu - Fursa kubwa ya kufanya hivyo ilikuwa ni Mjadala wa Katiba. Ninaposema "njia nzuri" ninamaanisha kwamba iwapo Serikali tayari ina mtazamo wake ambao isingependa ubadilishwe - hata na "wenye nchi" wenyewe (wananchi), basi ijipange kuuleta huu mjadala kwa namna ambayo itawavuta Watanzania wengi kuunga mkono matakwa ya Serikali ya kuudumisha!
Kinyume cha Hapo, kuendelea kuuficha-ficha na kuutetea Muungano kwenye Hotuba pasipo kujibu maswali ya Msingi ya Wananchi, kutazidi kuongeza idadi ya watu wanaotaka kujua kiini hasa cha "Usiri"huo, na hapo ndipo tatizo litakuwa kubwa zaidi hata ya hapa lilipo leo!


Watanzania kwa Sasa wanahitaji Majibu magumu Zaidi
 Kuendelea kukwepa kuujadili Muungano SIO kuulinda wala kuudumisha kama ambavyo wanasiasa wetu wengi wanaweza kuwa wanajidanganya kwa sasa. Kitendo hicho ni kuzidi kuongeza watu wanaouhoji na wale wanaotaka majibu mazidi. Kwa kadri idadi ya watu wanaouhoji na kuutilia mashaka Muungano itakavyoongezeka ndivyo Uwezekano wa Kuwapa Majibu Sahihi na kuwaridhisha utakavyozidi kuwa mgumu - NA HUO NDIO UTAKUWA MWISHO WA MUUNGANO!

The Union: It's Now or Never!

No comments:

Post a Comment