Tuesday, May 8, 2012

UWAZIRI: Rais Analihujumu Bunge!

Mbunge apewao Uwaziri Huacha Majukumu Mengi sana ya Ubunge!

Katika wakati huu ambao taifa linaanza mchakato wa kupitia upya katiba yetu, ni muda ambapo watu na makundi mbalimbali yamekuwa yakitoa maoni yao mbalimbali kuhusiana na masuala gani yawemo na yasiwemo kwenye katiba. jambo mojawapo ambalo leo nalifikisha kwa wananchi wote tulisemee ni matakwa ya katiba kwamba Rais ateue Mawaziri kutoka Miongoni mwa wabunge - NAPINGA SANA utaratibu huu na katiba ijayo ikataze kabisa utaratibu huu. Kuna sababu nyingi za msingi:

Kwanza, ni muhimu kutambua kuwa Mbunge huchaguliwa na Wananchi au kuteuliwa na chama chake kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi katika Bunge - ambalo ni chombo cha kitaifa cha wananchi kuongea na serikali yao, kuihoji, kuishauri, kutunga sheria na sera, na hata kufanya maamuzi ya kuiwajibisha serikali. Kwa hiyo, Mbunge huchaguliwa mahsusi kwa ajili ya majukumu hayo!

Waziri, kwa upande mwingine, ni msaidizi wa Rais katika kutekeleza majukumu ya Dola, dola ambayo ndiyo hutakiwa kwenda kutoa maelezo na "hesabu" ya matendo yake kwa wananchi kupitia bunge! Kwa maana hiyo, Waziri huwa hawafanyi kazi za Mbunge za kuwawakilisha wananchi katika kuihoji na kuiwajibisha serikali, badala yake huwa anavuliwa hayo majukumu na kuvishwa majukumu mengine ambayo ni kinyume cha Ubunge - Yaani kuilinda na kuitetea Serikali machoni pa wawakilishi wa wananchi!

Kutokana na tofauti kuu hiyo ya kazi za Wabunge na Mawaziri, maana yake ni kwamba Wabunge wanatakiwa ni watu makini, wenye uelewa, upeo na ufahamu mkubwa wa masuala na majukumu ya mawaziri na serikali kwa ujumla ili waweze kuiwajibisha serikali ipasavyo.

Nafasi ya Rais hutumiwa Vibaya
Bunge huweza kugawanywa na Kuvunjwa nguvu na Rais
Tunapokuja kwenye uteuzi wa Mawaziri, hapo ndipo tatizo kubwa huanzia. Kwa kawaida, rais yeyote anapoteua Mawaziri, huwangalia na kuchagua watu wenye uelewa, upeo na ufahamu wa kutosha kuweza kumsaidia kufanya kazi zake. Hii inamaanisha kwamba anapokuwa anafanya uteuzi, huwateua wabunge wenye sifa hizo na Kuwaondoa kwenye Kundi na majukumu ya Ubunge (ambayo ni kumuwajibisha yeye na serikali anayoiongoza) na anawaweka upande wake kwa kuwapa Uwaziri!

Kitendo hiki moja kwa moja hulivunja nguvu bunge na kuliathiri kwa kiasi kikubwa sana kwa kuliondolea Nguvu kazi zake ambazo ndizo zingetumika katika kuisimamia na kuiwajibisha serikali ipasavyo! Kwa mfano, kati ya Wabunge, Rais anapoamua kuwa"chomoa" wabunge 60 (sitini) wenye uwezo mkubwa, ni wazi kwamba kunabaki pengo kubwa sana kwa upande wa Bunge!

Hali hii huwa mbaya zaidi kutokana na mfumo wetu kutoweka viwango vya juu ya elimu miongoni mwa wabunge - ambapo hata waliomaliza darasa la Saba tu na wasipate elimu nyingine yoyote wanaweza kuwa  Wabunge. Katika hali kama hiyo, Rais anapowateua Wasomi 60 kutoka bungeni na kuacha kundi kubwa lililobakia likiwa na watu wasio na elimu wala upeo wa uelewa - ni wazi kuwab bunge litapawaya kwa kiasi kikubwa!
Aliwahi kuwa Waziri, leo hana Ujasiri wa Kuongea!

Ebu fikiria, unamchukua mtu kama Profesa Mwandosya na Kumfanya kuwa Waziri wa Mazingira, halafu bunge unaliacha na mtu kama Profesa Majimarefu (mganga wa kienyeji), au Livingstone Lusinde (Darasa la Saba) ndiye aje kumuhoji, kumsimamia na kumuwajibisha Prof. Mwandosya kwenye masuala yahusianyo na Hewa Ukaa, Tabia Nchi, Kaboni Monoksaidi n.k.!!! Ni wazi kuwa bunge litabaki na wapiga makofi na waunga mkono hoja kwa sababu ni wazi kuwa wataburuzwa kwa ujinga wao na kutokujua kwao. Vyama vya Upinzani vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuziba pengo hilo kwa kuwa wasomi wake huwa hawapewi Uwaziri!

Kwa msingi huo, Katiba inampatia Rais mamlaka ya kuweza kulivuruga na kulivunja nguvu bunge huku yeye akijihakikishia kuwa hatakabiliana na shinikizo kubwa kutoka kwa chombo cha wananchi (bunge) kwa kuwa wale ambao wangeweza kumsababishia shinikizo hilo amewatoa bungeni na kuwaapisha kuwa mawaziri kwamba hawatatoa siri yoyote ya serikali - hata kama inawaumiza wananchi waliowachagua!!!

Madhara huwa hayaishii hapo, tatizo huwa linakuwa kubwa zaidi pale Mbunge huyu safi, bora na mwenyewe uwezo anapoteuliwa kuwa waziri - halafu akapatikana na makosa ambayo yakapelekea aondolewe kwenye uwaziri - kwa kawaida anabaki kuwa mbunge jina tu kwa kuwa mara nyingi tayari atakuwa ameshachafuliwa kiasi kwamba hawezi tena kutekeleza majukumu yake kama mbunge ya kuiwajibisha serikali kikamilifu - kwa sababu tayari alikwisha kuchafuka akiwa katika serikali hiyo hiyo!

Kwa mfano, watu kama Mkulo, Maige, Ngeleja ambao walichaguliwa na wananchi wao kwa dhamira nzuri ya kuwawakilisha - leo hii wamechafuka kutokana na kupewa majukumu ya utendaji ambayo hawakuchaguliwa kuyafanya - na wakirudi bungeni kama wabunge hakika watakuwa wabunge majina tu maana hawatakuwa na ujasiri tena wa kusimama na kuihoji au kuiwajibisha serikali iliyowachafua. Kimsingi, wananchi wa majimbo yao watabaki bila wawakilishi halisi bungeni!

Baadhi ya Wabunge ambao hawapewi Uwaziri
Kwa upande mwingine, mabadiliko hayo ni kwa hakika kuwa yatabilisha sana sura ya watu wanaoenda kugombea ubunge majimboni. Kwa utaratibu wa sasa, Watu wengi - hususan wasomi na matajiri - huenda kugombea ubunge majimboni SIO kwa nia ya kuwatumikia wananchi katika nafasi za Ubunge - bali kwa kuamini kuwa kutokana na Elimu zao au sifa zao nyingine - watateuliwa kuwa mawaziri! Kwa maana hiyo, wanaenda kuomba kazi ya ubunge kwa wanachi huku wakujiua kabisa SIO NIA YAO kuifanya hiyo kazi, na badala yake wanamalengo ya kufanya kazi nyingine - ambayo wao wanaiona kubwa na yenye heshima na maslahi zaidi - japo siyo waliochaguliwa kuifanya!

Utaratibu huu ukibadilishwa, tutashuhudia watu wenye dhamira moja na ya wazi ya kuwatumikia wananchi ndio wakienda majimboni kugombea ubunge na sio wale wanatamani uwaziri lakini wanautumia ubunge kama daraja la kufikia matamanio yao.

Mwaziri Watatoka wapi?
Kuna nchi duniani ambapo kuna mfumo wa namna hii pia. Katika mfumo mbadala, Rais na Waziri Mkuu wake watawajibika kukaa na kuteua watu kutoka sehemu mbalimbali (nje ya Bunge) ambao watawapatia dhamana za Uwaziri na kufanya nao kazi katika dola. Hawa ndio watakuwa wanaiwakilisha serikali bungeni kwenye kukabiliana na wawakilishi halisi wa wananchi na kutoa majibu kwao!

Mgawanyo huu sio tu kwamba utahakikisha bunge litakuwa "focused" kwenye majukumu yake bila kuathiriwa na hisia au woga wa kupata au kukosa uwaziri - bali pia serikali itajikuta ikitakiwa kuwajibika sana kwa sababu kiongozi wake ambaye ni rais atakuwa hana nafasi ya kuliingilia bunge na kulivunja nguvu kwa kipindi chote cha utawala wake.

Madhara ya Utaratibu wa Sasa
Utaratibu wa sasa huathiri kwa kiasi kikubwa sana Utendaji na uwajibikaji wa wabunge wengi - hususan wa chama tawala ambao wengine aidha walishawahi kuwa mawaziri wakashindwa kazi hiyo na kuondolewa - na hivyo wanakosa ujasiri wa kuwakosoa wale waliopo - lakini pia huathiri kwa namna mbalimbali utendaji wa wabunge ambao hawajateuliwa kuwa mawaziri kwa vile wanavyokuwa wanafikiria uwezekano wa wao pia kuteuliwa kuwa mawaziri - iwapo watajionesha kuwa nao wanafaa. Hali kama hii huweza kuibua hisia za Unafiki na Kujipendekeza au Kuzushiana uongo na Kuchafuliana majina ili mmoja aonekane hafai na nafasi yake apewe mwingine.
Wabunge wenye uwezo huweza kupewa Uwaziri na Kuathiri Utendaji wao Kama Wabunge

Wabunge wanatakiwa kuelewa kuwa tangu siku anapochaguliwa na wananchi kuwa mbunge - aelewe kuwa miaka yote ya kuwepo kwake kwenye hiyo nafasi atakuwa mbunge na muwakilishi wa wanachi na asiingiwe na wazi la kwamba anaenda bungeni kujitependekeza ili apewe nafasi ya uwaziri.

Kimsingi, utaratibu wa sasa unampatia Rais fursa na mamlaka ya kuweza "kulihujumu"  bunge na kulidhoofisha kwa kuwaondoa wabunge wanaoipa serikali shinikizo kubwa na kuwaacha wale ambao hawana "impact" ambao wao kwao mara nyingi kuitwa mbunge tu ni heshima kubwa hata kama hafanyi lolote - na hawa ni wale ambao miaka yote huweza kukaa na kauli pekee wanayoifahamu wao ni kuunga "mkono hoja".

Baadhi ya Wabunge ambao huwa hawapewi Uwaziri!

Mabadiliko haya yataongeza Uwajibikaji katika pande zote mbili - Bunge na Dola - ambapo rais yeyote ajaye atakuwa anafahamu kabisa kuwa hana namna ya kulidhoofisha bunge kwa kuwaondoa wale "wanaoongea sana", litaongeza ubora wa wabunge watakaokuwa wanachaguliwa (watachaguliwa wale tu wenye nia ya kweli ya kufanya kazi ya ubunge na sio wale wanaotaka kuutumia ubunge kama daraja la kujipatia uwaziri na kuachana na majukumu ya msingi ya Ubunge) na zaidi ya yote - litadumisha dhana muhimu katika taif letu ya Mgawanyo wa Madaraka katika Nguzo kuu tatu za Nchi - Bunge, Dola na Mahakama.

2 comments:

  1. Ni kweli... ubunge ubaki kuwa ubunge. Uwaziri uwe tofauti.
    Nadhani kuna haja ya kufanya mabadiliko, tuwe na mfumo wa uongozi kuanzia ngazi ya Rais hadi vingozi wa nyumba kumi ambao utaendana na hali ya nchi yetu na matakwa ya watu wake. Si lazima kuendelea kutumia mfumo tuliorithi kwenye nchi nyingine.
    Tunaweza kutengeneza Serikali mpya kwa namna ambayo inatufaa waTanzania.
    Tatizo tunaiga kila kitu. Demokrasia ya Marekani si lazima iwe sawa na Demokrasia ya Tanzania. Tunaweza kutengeneza jinsi mpya kabisa ya uongozi na uendeshaji nchi

    ReplyDelete