Friday, May 25, 2012

GHARAMA za Matibabu MOI Zapanda MARA TATU!

Hospitali ya Taifa Muhimbili

KATIKA hali inayoashiria mwendelezo wa mfumuko wa bei nchini, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), imepandisha gharama za huduma zake kati ya asilimia 80 na 300.Ongezeko hilo la gharama za matibabu limekuja katika kipindi ambacho tayari, kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za maisha katika bidhaa muhimu za chakula yakiwemo mazao ya nafaka.

Kutokana na ongezeko hilo, wapo wagonjwa walioshindwa kupata huduma ya matibabu kwasababu hawakuwa na fedha zinazotosheleza kupata huduma walizokuwa wakizihitaji.

Jana, Ofisa Uhusiano msaidizi wa Moi  Frank Matua alithibitisha kupanda kwa gharama hizo na kwamba jambo hilo ni utekelezaji wa sera za huduma za afya katika hosipitali hiyo. “Kweli gharama zimepanda, lakini, mchanganuo halisi bado haujapangwa,” alisema Matua alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake jana.

Matua alisema kwa sasa taarifa bado hazijawa rasmi na unahitajika muda zaidi wa kuandaa takwimu za kuonyesha mchanganuo halisi wa gharama hizo zitakavyotozwa. Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa ongezeko hilo linahusisha huduma zote zinazotolewa na taasisi hiyo.

Miongoni mwa huduma hizo ni kumwona daktari ambazo zimeongezeka kutoka Sh2,000 za awali hadi Sh8,000, huduma ya X - ray kutoka Sh5,000 hadi Sh9,000 wakati gharama za matibabu zimepanda kwa viwango tofauti kwa kuzingatia aina ya ugonjwa.

Kabla ya kupanda kwa gharama hizo za matibabu, uongozi wa Moi ulitoa tangazo ambalo limebandikwa kwenye ukuta ofisini kwa muhasibu likieleza kupanda kwa gharama hizo, lakini bila kuonyesha viwango vya ongezeko hilo. "Kuanzia Mei 21 mwaka huu gharama za matibabu zitapanda," inasomeka sehemu ya tangazao hilo lililopo kwenye ofisi ya mhasibu.  Taarifa hii Imetoka http://www.mwananchi.co.tz/habari/-/23268-gharama-za-matibabu-moi-juu-mara-tatu-zaidi

No comments:

Post a Comment