Tuesday, May 22, 2012

UDINI Unavyowagawa Waarabu!


Nchi za kiarabu zimekuwa zikikabiliwa na migogoro mingi ya ndani kwa miaka mingi sasa – hata kabla ya kuanza kwa vuguvugu la mapinduzi la mwaka juzi. Lakini kuna sura moja kuu ya migogoro hiyo ambayo huwa haijulikani kwa watu wengi – udini ndani ya dini moja ya Kiislam!
Mgawanyiko wa ki-Madhehebu katika Nchi za Kiarabu!

Nchi za kiarabu zimegawanyika katika makundi makuu mawili – zile zinazotawaliwa na Waislamu wa Shia na wa Sunni. Tofauti na migawanyiko hii iko katika nchi karibu zote – hususan ambako kuna idadi kubwa ya waumini wa madhebu yote mawili.
Nasrallah (Shia) - Kiongozi wa Hezbollah, Lebanon

Nchi za kiarabu kwa sasa zimegawanyika katika kambi mbili kuu – upande wa kwanza ni zile zinazotawaliwa na wa Sunni ambazo zinongozwa na kuitegemea Saud Arabia na zile zinazoongozwa na wa Shia ambazo zinaongozwa na kuitegemea sana Iran. Mgawanyiko huu umekuwa ni msingi wa mashindano na mivutano mingi sana kati ya nchi na nchi na hata kati ya makundi mbalimbali na serikali za nchi zao huko uarabuni.

Mgogoro wa Syria
Mfano mmoja mzuri unaweza kutumika kuonesha namna gani Udini ndani ya Uislamu unavyowagawa waarabu ni mgogoro unaoendelea kwa sasa nchini Syria. Kimsingi, mgogoro unaoendelea kwa sasa nchini Syria ni vita dhidi ya Waislam wa madhehebu ya Sunni walio wengi nchini humo wanaopambana na serikali ya Assad ambaye ni muumin madhehebu ya Shia. 
Al-Assad (Shia) - Rais wa Syria

Tatizo limekuwa kubwa zaidi kutokana na mgawanyiko wa mataifa ya kiarabu yanayounda Jumuiya ya Nchi za Kiarabu – ambazo na zenyewe kimsingi zimegawanyika kutokana na mlengo wake wa kiimani!

Nchi zinazoongozwa na wa Shia – kwa maana ya Iran na Iraqi ndizo zilikuwa msitari wa mbele kuilinda na kuitetea serikali ya Syria na kimsingi, ndizo zinampatia sana rais Assad ujasiri wa kuendelea kuwepo madarakani na kufanya yale anayoyafanya! Kwa upande mwingine, nchi zinazoongozwa na wa Sunni – kama Saud Arabia na Qatar ndizo zimekuwa mstari wa mbele katika kupinga kuendelea kuwepo madarakani kwa rais Assad na hata zikafikia hatua ya kutaka kutumia nguvu za kijeshi kumuondoa!

Mgogoro wa Syria ndani ya Lebanon!
Rafik Hariri wa Lebanon, (Sunni) aliyeuawa kwa Njama za Syria (Shia)
Hivi karibuni yameibuka mapigano makali hadi mauaji nchini Lebanon! Mapigano haya – tofauti na yale ya nchi nyingine za Kiarabu, hayalengi kuipindua Serikali wala kutaka mabadiliko yoyote ndani ya Lebanon! NI mapigano kati ya makundi ya mawili ya Raia wa Lebanon – moja ni lile la waumin wa Alawite (tawi la Shia) ambao wanaiunga mkono Serikali ya Syria (Rais Assad) na kundi la pili ni lile la waumin wa Madhehebu ya Sunni wanaowaunga mkono Waasi wa Syria!!

Mgogoro nchini Iraq
Migogoro inayoendelea nchi Iraqi – vivyo hivyo – imejengwa sana katika tofauti za kidhehebu ndani ya Uislam. Waumin wa madhehebu ya Shia walifurahia sana uvamizi wa jeshi la Marekani ambao ulilenga kumuondoa madarakani Rais Saddam Hussein ambaye alikuwa muumini wa Sunni – kundi ambalo ni la watu wachache nchini Iraqi! 
Nour Al-Malik - Waziri Mkuu wa Iraq (Shia)

Tofauti hizo ziliimarika zaidi na kuwaingiza kwenye vita Wasunni na Washia baada ya vita hiyo – mapigano ambayo yameua raia wengi Waislam wa Iraq kuliko wale waliouawa na majeshi ya Marekani moja kwa moja!

Mivutano hiyo nchini Iraqi inachagizwa na ushawishi  mkubwa wa Iran – ambayo ndiyo inamuunga mkono Waziri Mkuu wa Iraq kwa upande mmoja na Uingilizi na Ushawishi mkubwa wa Saudi Arabia – ambayo inamuunga mkono Makamu wa Rais wa Iraqi – Hashim – ambaye kwa sasa ameikimbia nchi kwa kuwa anatafutwa na serikali ya Wasuni afikishwe mahakamani kwa tuhuma za kuongoza kundi la mauaji ambalo huwalenga na kuwaua viongozi Washia nchini Iraqi! Saud Arabia imesema haitamkabidhi kwa Iraq makamu huyo wa rais – ambaye ni Msunni – pamoja na Interpol kutaka akamatwe na arejeshwe Iraq!

NOTE: Katika Uchaguzi Mkuu uliopita Nchini Iraq, Chama kilichoshinda Uchaguzi wa Bunge uliopita mwaka 2010 (kwa Kupata viti vingi - 91)  kilikuwa Al-Iraqiya - Chama kinachoongozwa na Ayad Alawi (Sunni) - Lakini kwa Ushawishi wa Iran (Shia) katika Siasa za Iraq, kiongozi wa Chama hicho alinyimwa nafasi ya kuunda Serikali na badala yake akapewa Al-Maliki (Shia) ambaye chama chake cha State of Law Coalition kilipata viti 89!
Matokeo ya Uchaguzi Iraq - March 2010

Mgogoro wa Bahrain!
Baada ya vuguvugu la mapinduzi kuanza katika nchi za kiarabu – mojawapo ya nchi zilizovamiwa haraka sana na maandamano hayo ilikuwa Bahrain. Hii ni nchi ndogo sana ambayo ni kisiwa iliyo karibu na Saud Arabia. Nchi hii ina idadi kubwa sana ya waumin wa Shia lakini inaongozwa na Mfalme na serikali yake ambao ni wa Sunni. 
King Abdul wa Saud (Suni) aliwazima Washia Bahrain

Baada ya kuonekana wazi kwamba serikali ile ingepinduliwa na wananchi walio wengi ambao ni wa Shia, Serikali ya Saud Arabia (ambao ni wa Sunni) walipeleka jeshi haraka sana na kuyakandamiza na kuyapoteza yale maandamano na upinzani haraka sana! Ni wazi kwamba Saud Arabia haikuwa tayari kuona Serikali nyingine ya ki Sunni – tena iliyo jirani – ikiangushwa na wa Shia wanaoungwa mkono na Iran! Viongozi wa mapinduzi yale mara moja walikimbilia Iran kukwepa kukamatwa na kuteswa na serikali ya wa Sunni.

Tangu kuibuka kwa mgogoro huu ndani ya Bahrain – nchi hiyo imekuwa na mahusiano mabaya sana ya kidiplomasia na Iran – nchi ambayo ndiyo inatuhumiwa kwa kuchochea uasi na kuwasaidia waasi ambao ni wa madhehebu ya Shia ili kuweza kuipindua serikali yao – ambayo inaongozwa na familia ya kifalme ambao ni wa Sunni!

Al-Qaeda na Udini
"Mtu Mzima" (Sunni)
Kundi la Al-Qaeda lilianzishwa na kuongozwa na Osama Bin Laden, raia wa Saud Arabia, mpaka alipouawa na majeshi ya Marekani huko Pakistan. Kimsingi, kundi hilo SIO LA WAISLAM, bali la wa Sunni. Mara zote limekuwa likifanya kazi na wa Sunni na katika nchi ambako kuna waumin wengi wa Sunni. Ndio maana watu huwa wengi huwaelewi ni kwa nini hawasikii uwepo wa Al-Qaeda katika nchi kama Iran na Syria ambazo zinaongozwa na wa Shia!

Baada ya Marekani kumuondoa rais Msunni wa Iraq – Saadam Hussein, gaidi mmoja, Abu Musab Al-Zarqaw – raia wa Lebanon – Msunni – alienda nchini Iraqi na kuanzisha rasmi kundi la Al-Qaeda tawi la Iraqi. Lengo lake kuu na kazi yake kubwa ya kwanza HAIKUWA kuwashambulia na kuwaua Wamarekani – Bali kupanga mashambulizi na kuwaua wa Shia! Mpaka mwaka 2011 mwishoni, kundi hilo lilikuwa limekwisha kuwaua wanajeshi 400 wa Marekani na rais 12,000 wa Iraqi – ambao ni waumin wa Shia! Na hii ni katika mashambulizi yale tu ambayo kundi hilo lilithibitisha kuyafanya!

Abu Musab Al-Zarqaw (Sunni)
Ndio maana hata Al-Qaeda hawakuingilia mgogoro kati ya Israeli na kundi la kiislam la Hezbollah la Lebanon pale Israeli ilipoingia nchini Lebanon na kushambulia vituo vyote vya kundi hilo kwa siku zaidi ya 15 mfululizo! Jambo hili liliwashangaza watu wengi – lakini msingi uko kwenye tofauti ya kiitikadi ya kiimani ndani ya Uislam – Al-Qaeda ni kundi la wa Sunni na Hezbollah ni kundi la wa Shia – ambalo linaungwa mkono na Iran na Syria.

Vurugu zinazoendelea kwa sasa nchi Syria pia zimeanza kuonesha ushiriki wa hali ya juu wa kikundi cha Al Qaeda (cha wa Sunni) ambacho kimeungana na makundi ya wananchi na wanajeshi katika kupambana na serikali ya Assad (wa Shia). Hadi sasa kimeshafanya mashambulizi kadhaa makubwa nchini humo ambayo inalenga kuihujumu serikali ya wa Shia na hatimaye kuwaondoa.

Nafasi ya Marekani na Nchi za Magharibi
Obama: Marekani hutumia Migawanyiko kujinufaisha
Watu wengi wamekuwa wakizilaumu nchi za kimagharibi – hususan Marekani – kwa kuingilia na kuvuruga hali na mahusiano ya kisiasa katika nchi za kiarabu. Lakini ukweli ni kwamba Marekani hutumia mianya iliyopo tayari – ya tofauti baina ya nchi – ili kuweza kupenyeza ajenda na matakwa yake. Lakini ukweli ni kwamba hata pasipo uingilizi wa nchi za magharibi – tofauti za kimaslahi na mielekeo ya kidini zimeshazigawa mno nchi za kiarabu na zitaendelea kwa miaka mingi sana kuzigawanya nchi hizo.

… wasiliana na mwandishi wa makala hii kwa msbillegeya@hotmail.com

No comments:

Post a Comment