Nyerere: Hakika Namheshim Sana |
Nimesoma sehemu hii hapa Chini ya hotuba ya Nyerere kuhusu kuanzishwa kwa Serikali Mbili katika Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania. Inawezekana ni kweli kwamba maelezo aliyokuwa anayatoa ya ukweli ndani yake, lakini ni ukweli pia kwamba yana Ombwe kubwa sana linaloacha maswali mengi ya msingi bila kujibiwa.
Kwa Ufupi, namaanisha maelezo ya Nyerere kuhusu suala la Serikali Mbili - Ni Majibu Mepesi kwa Maswali Mazito! Inawezekana Nyerere hakuwa na majibu mazuri zaidi ya haya kwa wakati huo, au pia inawezekana kwa sababu alikuwa amezungukwa na watu ambao - aidha hawakuwa na UWEZO wa kuhoji au kurekebisha maamuzi yake binafsi - au HAWAKUWA NA UHURU wa kufanya hivyo. Hivyo matokeo yake ikawa kwamba kila atakalolisema yeye linafutiwa na makof mengi na vigeregere huku mkutano mzima ukiitikia kwa Sauti - ZIDUMU FIKRA ZA MWENYEKITI!
Maswala yangu ya Msingi
Kwanza: Nani aliamua Kuziunganisha Nchi hizi Mbili Zilizo Huru?
Nyerere na Karume Wakisaini Hati ya Muungano |
Kwa maelezo ya Nyerere, Tanganyika na Zanzibar "ZILIAMUA" kuungana! Sijui Nyerere aliposema "ziliamua" alikuwa anamaanisha nini? Kwamba ni Watu wa Wenye Nchi (wananchi) hizi mbili ndio waliamua au Ni VIONGOZI wa Nchi hizi Ndio waliamua?
Kama ni Viongozi Ndio waliamua - Basi Huu ulikuwa MSINGI MBOVU SANA wa kujengea Muunganoa wa Mataifa mawili YALIYO HURU! Muungano wa Nchi ni suala pana sana ambalo haliwezi kuachwa na kufanywa na Viongozi wachache wa KISIASA ambao wanatekeleza Ilani za Vyama vya Kisiasa - katika mataifa ambayo SI KILA RAIA ni mwanachama au hata kama ni "Mwanachama wa Kulazimishwa" - Basi SI Muumini wa vyama hivyo!
Ndio maana LEO, ni muhimu sana suala la Muungano likarudishwa kwa wananchi wao ndio walijadili na kulitolea uamuzi. Kama Serikali ina wasiwasi kwamba wananchi hawatafanya maamuzi ambayo yenyewe inayaona ndiyoo "sahihi" basi ianze kwanza kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maamuzi gani yanaweza kuwa ni sahihi, lakini mwisho wa siku wnanchi ndio waamue wenyewe kipi ni sahihi!
PILI: Kumezwa kwa Zanzibar!
Karume |
Nadhani kati ya hoja nyepesi MNO zilizo katika maelezo ya Nyerere ni suala la "Kumezwa" kwa Zanzibar kwa kisingizio cha Uchache wa Watu! Kwa kawaida, Nchi huendeshwa na MIFUMO, Mifumo ambayo kwa kawaida hutengenezwa kulingana na mahitaji ya Jamii/Taifa husika. Ni hoja nyepesi mno kusema ETI Zanzibar inaweza kumezwa kwa sababu ya Uchache wa Watu!
Nini kingefanyika?
Jambo lililotakiwa ilikuwa ni kuwekwa kwa mifumo mizuri ambayo ingehakikisha uwakilishi mzuri wa pande zote mbili katika ufanyaji wa maamuzi na katika uchangiaji wa gharama za huo Muungano! Taifa likiingia kwenye mahusiano au muungano na taifa lingine haliwezi kumezwa kutokana na Idai ya watu wake - litamezwa na mifumo isiyo mizuri ambayo hailipi nafasi ya kuonekana na kusikika katika hayo mahusiano!
TATU: Gharama za Kuendesha Muungano
Jambo la tatu ambalo halikuwa la Msingi kuliweka kama sababu ya Kuvunja Serikali ya Tanganyika na kuunda ya Muungano tu, lilikuwa ni suala la gharama. Kwa wakati huo (baada ya kuanzishwa kwa Muungano), hoja hii ilionesha mapungufu makubwa wakati wa uanzishaji wa muungano wenyewe. Kauli hii inamaanisha Mambo haya hayakufikiriwa wala kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa Muungano:
- Faida za Muungano: Katika hali ya kawaida, mtu hauwezi kuingia katika mahusiano pasipo kufanya mahesabu ya faida utakayoipata katika mahusiano hayo na iwapo faida hiyo inatosha kugharimikia Uendeshaji wa Mahusiano hayo!
- Gharama za Kuendesha Mifumo itakayoundwa Chini ya Muungano: Suala la Nyerer kusema kwamba kuendesha Serikali ya Tanganyika ingekuwa gharama kubwa linaonesha ni kwa kiasi gani taathimini haikufanyika KABLA YA KUUNGANISHA NCHI kuona ni kwa kiasi gani Mifumo itakayozaliwa na Muungano (ikiwa ni pamoja na Serikali ya Muungano) itaweza kugharimikiwa. Hatua ya kuiua Serikali ya Tanganyika na kulivunja Bunge lake ilikuja kama Zimamoto ambayo ilitokana na kutokufanyika kwa taathimini ya kutosha kuuhusu Muungano husika kabla haujaundwa!
- Maelezo ya Nyerere yanaonesha kwamba haukufanyika Uchunguzi wa kina gharama za uendeshaji wa mifumo itakayoundwa chini ya Muungano - Huu ni upungufu mkubwa mno ambao unaleta matatizo hadi sasa kuhusu gharama za kuendesha muungano na Nani anufaike vipi na mapato yatokanayo na Muungano!
NNE: Hofu
Tayari Zanzibar Kuna Vurugu za Kuupinga Muungano! |
Labla katika hoja zote zilizotumika kufanya maamuzi kuhusu nini kifanyike katika muungano, hakuna hoja isiyofaa kama ya "Hofu". Nyerere alisema ETI maamuzi ya kutengenza muundo uliopo wa Muungano YALITOKANA NA HOFU ya kumezwa kwa Zanzibar! Kama kuna jambo baya ambayo mtu anaweza akalifanya maisha yake basi ni kufanya maamuzi kutokana na hofu inayokuzunguka!
Kwa mara nyingine tena, HOFU hii ilitokana kwa kiasi kikubwa sana na Kutokuwashirikisha Wananchi katika Kufanya maamuzi - hivyo walioyafanya WALIOGOPA iwapo maamuzi yatakuwa mzigo wa gharama kwa wananchi - wananchi wanaweza kuinuka na kuyapinga!
Na kwa upande mwingine, Hofu hii ilitokana na kutokufanyika kwa taathimini ya kina kuhusu gharama, faida na mahitaji mengine ya kuuendesha Muungano. Taathimini hiyo ingefanyika mapema, hakika tusingehitaji kufanya maamuzi kwa "Hofu" ya kitu Chochote!
Kweda Mbele....
Kimsingi, binafsi napenda uwepo wa Muungano, na ningependa uendelee. Tatizo kubwa lilipo ni kwamba Muungano wetu huu wa sasa Umejengwa kwenye MSINGI MBOVU ambao hauwezi kuuhakikishia huu Muungano UENDELEVU wake!
Najua kubomoa ni rahisi kuliko Kujenga, ndio maana wengi hupenda kukimbilia wazo la kuuvunja Muungano kuliko kutumia akili na nguvu zao kufikiria namna ya kuuboresha!
Maoni ya Wananchi zamu hii LAZIMA yatumike Kuamua Hatma ya Muungano |
Binafsi nalishauri taifa - kwa uongozi wa Serikali kubadilisha mawazo yake ya Sasa ya Hofu na Wasiwasi kuhusu maamuzi ya Wananchi. Serikaoli yetu - Iwapo inao uwezo wa kufanya hivyo - Inatakiwa ijipange zivuri na kuliwasilisha hili suala RASMI kwa wananchi kwa ajili ya kulijadilia na kulifanyia maamuzi.
HOTUBA YA NYERERE AKIFAFANUA KUUNDWA SERIKALI 2 NA SIO 3 TANZANIA
Nchi mbili zinapoungana na kuwa nchi
moja mifumo ya kawaida ya katiba ni miwili;
Muungano wa serikali moja, au
shirikisho la serikali tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali
yake,na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika
mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka Fulani ambayo yatashikwa na serikali
ya shirikisho na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo
yaliyobaki.
Mambo yatakayoshikwa na serikali ya
shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi
kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, basi zinaendelea kuwa
nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo Fulani Fulani. Nchi za Afrika
Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa jumuiya ya
Afrika ya Mashariki. Zilikuwa ni nchi tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini
hazikuwa nchi tatu zilizoungana kuwa Nchi moja yenye muundo wa shirikisho.
Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu,
serikali ya shirikisho, na serikali mbili za zile nchi mbili za awali
zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.
Tanganyika na zanzibar zilipoamua
kuungana na kuwa Nchi moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya
kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na
ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa ina watu laki tatu (300,000) na
Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000).
Muungano wa serikali moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya! Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa serikali Moja na Shirikisho la serikali tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha serikali ya shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha serikali ya shirikisho.
Muungano wa serikali moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya! Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa serikali Moja na Shirikisho la serikali tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha serikali ya shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha serikali ya shirikisho.
Kwa hiyo Tanganyika
ingeendesha serikali yake ya watu 12,000,000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa
ya kuendesha serikali ya shirikisho la watu 12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi
zao wanaodhani kuwa gharama ya serikali yoyote kati ya
hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo,
(waulizeni wazanzibari) na wala ya serikali ya shirikisho isingekuwa ndogo,
hata bila gharama za mambo yasiyo ya shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli
zingebebwa na Tanganyika.
Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa
nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini
tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika,
bila kuwa na serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni
kwamba tukiwa na serikali moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar.
Basi na tutafute muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila
kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha serikali mbili zenye uzito
unaolingana.
Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa
muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu,
tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo utakaotufaa zaidi.
No comments:
Post a Comment